Neno la Mungu Li Hai
Sababu Inayofanya Watu Watende Mabaya
HUYU mwanamume aliye hapa mbele akifanya pigano karibu na ukuta ni Uria. Mfalme Daudi wa Israeli alikuwa amemwandikia barua Yoabu, jemadari wa jeshi lake, akamwambia: “Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe, akafe.”—2 Samweli 11:15.
Uria alikuwa mwanamume mwema, mshikamanifu. Basi, kwa sababu gani Daudi, ambaye pia alikuwa mtumishi wa Yehova, aagize kwa makusudi Uria auawe?
Linaloweza kutusaidia tufahamu jambo hilo ni kusoma mistari inayofuata ya Biblia: “Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”—Yakobo 1:13-15.
Lakini huenda ukauliza, ni kwa njia gani habari hizi zinatusaidia tufahamu sababu iliyomfanya Daudi aagize Uria auawe? Ili kupata jibu tunahitaji kuchunguza hali zilizosababisha Daudi atake Uria auawe.
Siku moja, Uria alipokuwa ameenda zake, Daudi alikuwa akitazama akiwa kwenye dari ya nyumba yake kisha akamwona Bath-sheba mke mrembo wa Uria akioga. Daudi alifanya nini? Aliendelea kutazama. Kwa kufanya hivyo aliacha tamaa ya kufanya ngono na Bath-sheba ikue ndani ya moyo wake. Si Mungu aliyekuwa akimjaribu au kumshawishi Daudi. Hapana, Daudi alivutwa na kushawishwa na tamaa yake mwenyewe.
Mwishowe, tamaa mbaya iliyokuwa ndani ya Daudi ikawa yenye nguvu sana hata akaagiza Bath-sheba aletwe kwenye jumba la kifalme lake. Humo akafanya ngono naye. Baadaye, kwa sababu Bath-sheba alikuwa amechukua mimba na Daudi alishindwa kuficha uzinzi huo, alipanga Uria auawe katika pigano.
Ni kweli kwamba dhambi ya Daudi haikumwongoza apoteze milele upendeleo wa Mungu na kupokea hukumu Yake ya kifo. Hiyo ni kwa sababu Daudi alitubu kwa weupe wa moyo, na Yehova akamwonyesha rehema. (Zaburi 51:1-14) Hata hivyo, tukio hilo linatusaidia kufahamu kwamba mara nyingi watu wanatenda mabaya kwa sababu wanaweka tamaa mbaya katika moyo wao. Kwa hiyo imetupasa sisi tujifunze kutokana na lililompata Daudi kuwa tunaepuka hali, na pia utendaji na tafrija, ambazo zinachochea “hamu ya ngono.”—Wakolosai 3:5, NW; 1 Wathesalonike 4:3-5, UV.