Maswali Kutoka kwa Wasomaji
■ Je! Farao wa Kutoka alikufa wakati jeshi la Misri lilipoharibiwa katika Bahari Nyekundu?
Ndiyo, alikufa, ingawa kitabu cha Kutoka hakisemi uhakika huo moja kwa moja. Kinasema:
“Wale Wamisri wakawafuatia [Waisraeli], wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake.. .. [Yehova] akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. Musa akaunyosha mkono wake . . . Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.”—Kutoka 14:23-28.
Masimulizi hayo yanataja wapanda farasi na majeshi, lakini hayasemi waziwazi kama Farao alikufa. Wala wimbo wa ushindi wa Waisraeli, ambao katika huo walisema: “Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini maakida yake wateule wamezama katika Bahari ya Shamu.”—Kutoka 15:4.
Lakini, Zaburi 136:1-15 inaonyesha kwamba Farao aliangamia. Hapo tunasoma watu wakimtolea shukrani ‘Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao, na Yeye aliyewatoa Waisraeli katikati yao kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa, yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu, akawavusha Israeli katikati yake, na akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu.
Kwa hiyo kitabu cha Zaburi kinakamilisha Kutoka na kuonyesha kwamba Farao mwenye kimbelembele, aliyewaonea Waisraeli, alikufa ndani ya Bahari ya Shamu (Nyekundu).