Maisha na Huduma ya Yesu
Kuzaliwa kwa Yesu—Wapi na Wakati Gani?
KWA kuwa Mariamu anakaribia kuzaa, ni kwa sababu gani Yusufu anafunga safari ndefu? Mtawala wa Milki ya Roma, Kaisari Augusto, ametunga sheria kwamba kila mtu anapaswa kurudi kwenye mji wa kuzaliwa kwake akaandikishwe. Kwa hiyo Yusufu anaenda mahali alipozaliwa, mji wa Bethlehemu.
Watu wengi wameenda Bethlehemu wakajiandikishe, na mahali peke yake ambapo Yusufu na Mariamu wanapata nafasi ya kukaa ni kwenye boma la wanyama wa kufugwa. Humo, mahali ambamo punda na wanyama wengine wanawekwa, ndimo Yesu anazaliwa. Mariamu anamfunga kwa vitambaa na kumlaza juu ya mahali panapowekwa chakula cha wanyama.
Kwa hakika ulikuwa uongozi wa Mungu kwamba Kaisari Augusto akatunga sheria yake ya kuandikisha. Iliwezesha Yesu azaliwe katika Bethlehemu, mji ambao Maandiko yalikuwa yametabiri zamani ungekuwa mahali pa kuzaliwa mtawala aliyeahidiwa.
Huo ni usiku wa maana kama nini! Kule nje kwenye viwanja vya malisho mwangaza mkali unawaka kuwazunguka wachungaji. Ni utukufu wa Yehova! Naye malaika wa Yehova anawaambia: ‘Hivi leo Mwokozi amezaliwa Bethlehemu kwa ajili yenu, ambaye ni Kristo Bwana. Mtamkuta amelala juu ya mahali panapowekwa chakula cha wanyama.’ Kwa ghafula malaika wengine wengi wanatokea na kuimba: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Malaika wanapoondoka, wachungaji wanaambiana: ‘Na tufunge safari ndefu mpaka Bethlehemu tukaone jambo hili ambalo Yehova ametujulisha.’ Wanafunga safari haraka na kumkuta Yesu mahali pale pale ambapo malaika alisema wangemkuta. Wachungaji hao wanaposimulia mambo ambayo malaika aliwaambia, wote wanaosikia wanastaajabu. Mariamu anayatunza maneno hayo yote na kuyaweka hazina moyoni mwake.
Watu wengi leo wanaamini kwamba Yesu alizaliwa Desemba 25. Lakini Desemba ni wakati wa majira yenye mvua na baridi katika Bethlehemu. Wachungaji hawangekuwa usiku kucha nje kwenye mashamba ya malisho wakiwa na mifugo yao wakati huo mwakani, Pia, haielekei Kaisari Mroma angeamuru watu ambao tayari walikuwa na maelekeo ya kumwasi wafunge safari hiyo wakajiandikishe wakati wa baridi kali. Kwa wazi Yesu alizaliwa wakati fulani mwanzoni mwa vuli ya mwakani. Luka 2:1-20; Mika 5:2.
◆ Ni kwa sababu gani Yusufu na Mariamu walifunga safari ya kwenda Bethlehemu?
◆ Ni jambo gani la ajabu lililotokea usiku aliozaliwa Yesu?
◆ Tunajuaje kwamba Yesu hakuzaliwa katika Desemba 25?
[Picha cha ukurasa nzima katika ukurasa wa 25]