Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w87 5/1 kur. 22-30
  • Kutazama Nyuma Kwenye Miaka 93 ya Kuishi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutazama Nyuma Kwenye Miaka 93 ya Kuishi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Shule ya Sekondari na Chuo Kikuu
  • “Huo Ndio Ukweli!”
  • Kupata Kumjua Ndugu Russell
  • “Fumbo Lililokwisha”
  • Kualikwa Betheli
  • Mapendeleo ya Redio na Mikusanyiko
  • Mabadiliko Katika Usimamizi wa Sosaiti
  • Maisha Yangu Katika Tengenezo la Yehova Lenye Kuelekezwa kwa Roho
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Tangazeni Mfalme na Ufalme! (1919-1941)
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • Kujulisha Habari Njema Bila Kuacha (1942-1975)
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • Wakati wa Kutahini (1914-1918)
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
w87 5/1 kur. 22-30

Kutazama Nyuma Kwenye Miaka 93 ya Kuishi

Kama ilivyosimuliwa na Frederick W. Franz

KATIKA Septemba 12, 1893, mtoto mvulana alizaliwa katika Covington, Kentucky, katika upande wa kusini wa mto wenye kukabiliana na Cincinnati, Ohio. Baba yake mwenye furaha, Edward Frederick Franz, na mama mwenye kung’aa furaha, Ida Louise née Krueger, wali-mwita mwana huyo wao Frederick William Franz.

Huo ulikuwa ndio mwanzo wa miaka yangu 93 ya kuishi. Baba yangu, aliyezaliwa Ujeremani, alidai kuwa wa Kanisa la Kilutheri na kwa hiyo akanibatizisha kwa kuweke-ewa mkono wenye unyevu-unyevu wa kiongozi wa kidini juu ya kipaji cha uso wangu. Cheti cha ubatizo kilijazwa, na kikatiwa fremu na kuangikwa juu ya ukuta wa nyumba yetu, pamoja na vyeti vya ubatizo vya kaka zangu wawili, Albert Edward na Herman Frederick. Miaka 20 tu baadaye ndipo mimi nilipojifunza jinsi desturi hiyo ya kidini isivyopatana na Maandiko.

Ulikuwa wakati ambao tulikuwa tumehamia Barabara ya Greenup kwamba nikaona kwa mara ya kwanza mkokoteni usio na farasi wa kuukokota, motakaa yenye viti viwili isiyofunikwa juu ikiendeshwa barabarani. Miaka mingi baadaye ningeona eropleni. Wakati huo tuliishi karibu na mahali pa kuokea mikate pa Krieger, ambako baba yangu alifanya kazi nyakati za usiku akiwa mwokaji. Alikuwa akija nyumbani asubuhi na kwenda kulala. Ndipo alasiri angekuwa huru kutumia wakati fulani akiwa pamoja nasi wavulana.

Nilipokuwa na umri wa kwenda shule, nilipelekwa kwanza kwenye shule ya parokia na mikutano ya kidini ya Kanisa Katoliki la Roma la Mt. Yusufu, kwa kuwa ilikuwa karibu kwenye Barabara ya 12 na Barabara ya Greenup. Bado naweza kukumbuka darasa la shule. Pindi moja “ndugu” wa kidini mwenye kutenda kama mwalimu aliniagiza nije mbele ya darasa na kunyosha kiganja changu cha mkono uliokunjuliwa nipokee mipigo kadha kwa rula ya inchi 12 kwa sababu ya kikosa kidogo kwa upande wangu.

Nakumbuka pia kuingia katika sanduku la maungamo la kanisa lisilowashwa taa, nikisema na muungamiwaji aliyekuwa nyuma ya ukuta uliogawanya sehemu mbili, na nikisema sala ya kukariri na kuungama jinsi nilivyokuwa mvulana mbaya. Baada ya hapo, nilishuka kwenye kiegemeo cha madhabahu nikapiga magoti pale huku padri mmoja akiingiza kipande cha mkate kinywani mwangu, hivyo akanipa mkate wa Komunio kama ilivyofundishwa na kanisa, huku yeye akijiwekea akiba divai ainywe baadaye. Huo ulikuwa ndio mwanzo wa mazoezi yangu rasmi ya kidini na heshima yangu kwa Mungu ambayo ingeongezeka katika miaka ya baadaye.

Baada ya kumaliza mwaka mmoja katika shule ya parokia katika 1899, jamaa yetu ilihamia ng’ambo ya Mto Ohio katika Cincinnati, kwenye Barabara Mary ya 17 (ambayo sasa inaitwa Barabara Mashariki ya 15). Safari hii nilipelekwa shule ya hadharani nikawekwa katika darasa la tatu. Nilithibitika kuwa mwanafunzi asiyetega masikio, nami ninakumbuka kwamba, katika pindi moja, mimi na mwanafunzi mmoja aliyekuwa katika dawati iliyokuwa mkono wangu wa kuume tulipelekwa kwenye afisi ya mkuu wa shule kwa sababu ya mwenendo wetu usiofaa., Nikiwa kule Mkuu wa Shule Fitzsimmons alituagiza sisi wote wawili tuiname kwa kuangalia chini na kugusa ncha za viatu vyetu kwa vidole huku akifikiliza mipigo kadha matakoni kwa kifimbo kirefu cha mtende. Kama unavyoweza kutazamia, mimi nilianguka mtihani.

Lakini baba yangu hakuwa na nia ya kutaka nitumie miaka miwili nikiwa katika darasa lile lile, kwa hiyo wakati muhula ule mwingine wa shule ulipoanza, yeye alinipeleka kwenye shule ya Barabara ya Uhuru, kwenye afisi ya mkuu wa shule, Bw. Logan. Akamwomba Bw. Logan aniandike katika darasa la nne. Bw. Logan alikuwa na mwelekeo wa fadhili kwangu, naye akasema: “Basi, acha tuone kijana huyo amejua nini.” Baada ya mimi kujibu maulizo kadha ya kunichungua-chungua huku akionekana kuwa ameridhika, akasema: “Basi, inaonekana ni kama anastahili kuwa katika darasa la nne.” Kwa njia hiyo yeye binafsi alinisogeza mbele kwenye darasa la juu zaidi ya lile nililokuwa nimeanguka. Kuanzia wakati huo na kuendelea nikatulia na kujitoa kwa uzito nifanye masomo yangu ya shuleni, nami sikuanguka kamwe tena.

Pande za kidini za maisha yangu ya ujana zilibadilika pia. Kwa njia fulani, wawakilishi wa Kanisa Presbiteri la Pili la Cincinnati waliwasiliana na mama yangu, naye akaamua kuwapeleka Albert, Herman, na mimi kwenye shule ya Jumapili ya kanisa hilo. Wakati huo, Bw. Fisher alikuwa ndiye msimamizi wa shule ya Jumapili, naye Bessie O’Barr akawa mwa-limu wangu wa shule ya Jumapili. Kwa njia hiyo, mimi nilipata kuijulia Biblia Takatifu yenye roho ya Mungu. Nilishukuru kama nini wakati mwalimu wangu wa shule wa Jumapili aliponipa nakala ya kibinafsi ya Biblia Takatifu iwe zawadi ya Krismasi!

Nilipiga moyo konde nifanye iwe lazima katika maisha yangu kusoma kisehemu kimoja cha Biblia ki-i-la siku. Jambo hilo lilifanya nikijulie sana kitabu hicho kitakatifu. Na mavutano yacho yenye mafaa yalinizuia nisihusike na usemi na mwenendo usio wa adili wa wanadarasa wenzangu. Si ajabu kwamba wao walinitazama kuwa mtu tofauti.

Shule ya Sekondari na Chuo Kikuu

Baada ya mimi kuhitimu kutoka shule ya tatu ya masomo ya kiwango cha katikati katika 1907, wazazi wangu waliniruhusu niendelee na elimu yangu na kuingia Shule ya Sekondari ya Woodward ambako Albert, kaka yangu mkubwa zaidi, alikuwa amehudhuria kwa mwaka mmoja. Kama yeye, mimi niliamua kuchukua Somo la Kivitabu. Kwa hiyo nikachukua funzo la lugha ya Kilatini​—funzo ambalo nilifuatia kwa miaka saba iliyofuata.

Ndipo ukaja wakati wa kuhitimu katika masika ya mwaka 1911. Mimi nilichaguliwa niwe mhutubu mwenye kuwakilisha Shule ya Sekondari ya Woodward kwenye mazoezi ya kuhitimu ambayo yangefanywa katika jumba lililo kubwa zaidi katika Cincinnati, lile Jumba la Muziki.

Wakati huo, shule zote tatu za sekondari za Cincinnati​—Shule ya Sekondari ya Woodward, Shule ya Sekondari ya Hughes, na Shule ya Sekondari ya Walnut Hills—​zilikutana pamoja kwa ajili ya mazoezi ya kuhitimu. Wanadarasa wa kuhitimu shule ya sekondari waliketi juu ya jukwaa lile kubwa wakielekeana uso kwa uso na jumba lililojaa watu pomoni. Hotuba ya kufungua iligawiwa mhutubu mwenye kuwakilisha Shule ya Sekondari ya Woodward. Habari niliyochagua kwa pindi hiyo ilikuwa “Shule na Uraia.” Wasemaji wote watatu walipigiwa makofi ya kufurahisha sana. Sasa mimi nilikuwa katika mwaka wa 18 wa maisha yangu.

Wazazi wangu waliniruhusu niendelee na shughuli yangu ya kufuatia maisha ya kielimu, kwa hiyo nikaingia Chuo Kikuu cha Cincinnati, nikichukua Somo la Mafunzo ya Kilugha na Vitabu. Sasa nilikuwa nimeamua kwamba ningekuwa mhubiri Mpresbiteri.

Nikaongezea funzo la Kigiriki kwenye funzo nililokuwa nikiendelea nalo la kujifunza lugha ya Kilatini. Ilikuwa baraka kama nini kujifunza Kigiriki cha Biblia chini ya Profesa Arthur Kinsella! Chini ya Dakt. Joseph Harry, mtungaji-vitabu fulani vya Kigiriki, nilijifunza pia Kigiriki cha hali ya juu. Nilijua kwamba kama nilitaka kuwa kiongozi wa kidini Mpresbiteri, ilinipasa kuwa na ujuzi mwingi wa Kigiriki cha Biblia. Kwa hiyo nilijitoa jasho kweli kweli katika kujifunza nami nikapata maksi za kupita mtihani.

Kuongeza kujifunza Kigiriki na lugha ya Kilatini shuleni, nilipendezwa na kujifunza Kihispania, ambacho nilikiona kuwa chenye kufanana sana na Kilatini. Sikutambua wakati huo ni kwa kadiri kubwa namna gani ningeweza kutumia Kihispania baadaye katika huduma yangu ya Kikristo.

Tukio kubwa katika maisha yangu ya masomo lilikuwa wakati Dakt. Lyon, msimamizi mkuu wa chuo kikuu, alipotangazia kusanyiko la wanafunzi kwenye jumba la shule kwamba mimi nilikuwa nimechaguliwa kwenda Chuo Kikuu cha Mkoa wa Ohio nikafanye mtihani wa kushindana na wengine ili niipate zawadi ya Uanachuo wa Cecil Rhodes ya kunistahilisha kuingizwa katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza. Mmoja wa washindani wangu alinipita kwa habari ya michezo ya uanariadha uwanjani, lakini kwa sababu ya maksi zangu zilizolinganika na zake walitaka kunipeleka mimi pamoja naye, kwenye Chuo Kikuu cha Oxford. Nilithamini kwamba nilikuwa nimeyatimiza matakwa ya kuupata uanachuo, na, kwa kawaida, hilo lingalikuwa jambo la kuridhisha sana.

“Huo Ndio Ukweli!”

Tunakumbuka kwamba katika pindi moja Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” (Yohana 8:32) Mwaka uliotangulia, 1913, ndugu yangu Albert aliupata “ukweli” katika Chicago. Albert aliupataje “ukweli”?

Usiku mmoja wa Jumamosi katika masika ya 1913, Albert alikuwa ameenda kulala mapema katika bweni la Ushirika wa Vijana Wanaume Wakristo [YMCA], alikokuwa akiishi alipokuwa akifanya kazi Chicago. Baadaye, mwanachumba mwenzake aliingia chumbani kwa kishindo kueleza tatizo fulani. Yeye alialikwa usiku huo kwenye nyumba ya Bw. na Bi. Hindman, na Nora binti yao angekuwa na rafiki msichana katika nyumba hiyo. Mwanachumba mwenzi wa Albert aliona hangeweza kuelekeana na wasichana wawili akiwa peke yake. Kwa shauku nyingi, Albert alijikaza atumie pindi hiyo vizuri. Jioni hiyo ilipokuwa ikiendelea, mwanachumba mwenzi wa Albert alikuwa akiendelea vizuri sana katika maongezi na wasichana wale wawili. Lakini Bw. na Bi. Hindman walikaza fikira juu ya Albert, wakimjulisha mafundisho ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi Biblia na Trakti.

Ndipo Albert aliponipelekea kijitabu chenye kichwa Wafu Wako Wapi? kilichoandikwa na daktari Mskoti, John Edgar, mshiriki wa Kundi la Glasgow la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa. Kwanza, mimi nilikiweka kijitabu hicho kando. Halafu jioni moja, nilipokuwa na wakati mchache kabla ya kwenda kufanya mazoezi ya kwaya, nilianza kukisoma. Nilikiona kuwa chenye kupendeza sana hata nikashindwa kukiweka chini. Niliendelea kukisoma huku nikitembea karibu maili moja kwenda kwenye kanisa la Kipresbiteri. Kwa kuwa mlango wa kanisa ulikuwa umefungwa kwa kufuli, mimi nilikalia vipandio vile vya mawe vyenye baridi na nikaendelea kusoma. Mwenye kupiga ki-anda akaja na, alipoona jinsi fikira zangu zilivyo-kuwa katika kusoma, akasema: “Lazima hicho kiwe kitu cha kupendeza.” Nikajibu: “Hakika ndivyo!”

Kwa kuwa nilifurahia sana kweli mpya nilizokuwa nikijifunza, wazo lilikuja kwangu kumwuliza mhubiri, Dakt. Watson, alivyofikiri juu ya kijitabu hicho. Kwa hiyo jioni ile ile, mimi nilimpokeza kijitabu kile na kuuliza: “Dakt. Watson, wewe unajua nini juu ya hiki?”

Alikichukua kijitabu, akakifungua, halafu akakunja midomo: “Oh, bila shaka huo ni baadhi ya ule upuzi wa Russell. Yeye anajua nini juu ya eskatolojia?” Niligutushwa kweli kweli na mwelekeo huo wake wenye madharau. Nilipokuwa nikichukua kijitabu kile na kugeuka niende zangu, nikafikiri hivi nikijiambia mwenyewe: “Sijali analofikiri kuhusu jambo hili. Huu ndio UKWELI!”

Kabla ya muda mrefu, Albert alipokuwa katika moja ya ziara zake za kurudi nyumbani, aliniletea mabuku matatu ya kwanza ya Studies in the Scriptures, yaliyoandikwa na Charles Taze Russell. Albert alinifanya pia nijuliane na kundi la kwetu la Wanafunzi wa Biblia, lililokuwa likikutana pale pale tu karibu na mlango wa kanisa la Kipresbiteri. Nilifurahishwa sana na mambo niliyokuwa nikijifunza na karibuni nikaamua kwamba wakati ulikuwa umekuja ili mimi nikatize uhusiano wangu na Kanisa la Kipresbiteri.

Kwa hiyo baadaye, wakati Albert alipokuwa akitutembelea tena, tulienda kwenye moja ya hotuba za mausiku ya Jumapili za Dakt. Watson. Baada ya hapo, Albert na mimi tulitembea kwenda mahali alipokuwa akisalimiana na wanakanisa waliokuwa wakiondoka. Mimi nikamwambia: “Dakt. Watson, mimi naliacha kanisa.”

Yeye akasema: “Nilijua tu! Nilijua tu!” Mara tu nilipokuona ukiusoma ule upuzi wa Russell. Mtu huyo, Russell, mimi singemruhusu akanyage ndani ya mlango wangu!” Ndipo akao-ngezea hivi: “Fred, hufikiri kwamba inafaa tuingie katika chumba changu cha kanisa cha kuvalia tusali pamoja?” Mimi nikamwambia: “Hapana, Dakt. Watson, mimi nimekata mane-no.”

Basi ikawa kwamba, Albert na mimi tulitembea tukatoka kanisani. Ilikuwa hisia tukufu kama nini kuwa huru kutoka utumwa wa kidini uliokuwa ukifundisha mambo ya uwongo! Lilikuwa jambo jema kama nini kuingizwa katika kundi la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, waliokuwa washikamanifu sana kwa Neno la Mungu! Katika Aprili 5, 1914, katika Chicago, Illinois, mimi nilionyesha utakatisho wangu​—kama vile tulivyokuwa tukiita wakfu—​kwa ubatizo wa maji.

Sijapata kamwe kujuta juu ya jambo hilo, muda mfupi kabla ya matangazo yaliyotolewa na wenye mamlaka wa kielimu kuhusu matokeo ya mitihani ya kujipatia Uanachuo wa Cecil Rhodes, niliandikia wenye mamlaka barua nikawaeleza kwamba sikuwa nikipendezwa tena na uanachuo wa Chuo Kikuu cha Oxford na kwamba inawapasa waniondoe katika orodha ya wenye kushindania uanachuo huo. Nilifanya hivyo hata ingawa profesa wangu wa Kigiriki kwenye Chuo Kikuu, Dakt. Joseph Harry, alinijulisha kwamba mimi nilikuwa nimechaguliwa nipokee uanachuo.

Miezi miwili baadaye, au katika Juni 28, 1914, Duki-mkuu Ferdinand wa Austria-Hungari na mke wake waliuawa kule Sarajevo katika Bosnia. Katika tarehe iyo hiyo, Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa walikuwa katika siku ya tatu ya mkusanyiko mkuu wao kwenye Jumba la Ukumbusho, Columbus, Ohio. Mwezi mmoja tu baadaye, au katika Julai 28, 1914, vita ya ulimwengu ya kwanza ya historia yote ya kibinadamu ilitokea kwa ghafula. Sisi Wanafunzi wa Biblia tulikuwa tukiutazamia mwisho wa Nyakati za Mataifa zenye miaka 2,520 uwe umekuja kufikia Oktoba 1 mwaka huo.

Mimi nilikuwa nimekiacha Chuo Kikuu cha Cincinnati katika Mei 1914, kwa ruhusa ya baba yangu, majuma kadha tu kabla ya kumalizika kwa muhula wangu wa tatu nikiwa mwa-nafunzi wa mwaka wa tatu huko. Nilipanga mara hiyo na Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ya Biblia na Trakti niwe mwuza-vitabu, au painia, kama anavyoitwa mhudumu wa wakati wote leo. Kufikia wakati huo nilikuwa nimeshirikiana kwa bidii na Kundi la Cincinnati la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa.

Baadaye nikawa mzee wa Kundi la Cincinnati. Kwa hiyo wakati United States ya Amerika ilipohusika katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ikiwa upande wa Walioungana, na vijana wanaume wakaandikishwa jeshini, mimi niliepushwa na jambo hilo kwa kuonwa kuwa mhudumu wa Injili.

Kupata Kumjua Ndugu Russell

Miongoni mwa visa ninavyofurahia sana kutazama kule nyuma katika maisha yangu ni nyakati ambazo nilikuwa na furaha ya kukutana na msimamizi wa kwanza wa Sosaiti, Charles Taze Russell. Kwa mara ya kwanza nilijuliana naye kibinafsi iliyotangulia onyesho lile mashuhuri la Mchezo wa Kuigiza Wenye Picha za Uumbaji kwenye Jumba la Muziki siku ya Jumapili, Januari 4, 1914. Jumamosi hiyo mzee mmoja wa Kundi la Cincinnati alinikuta nje ya Jumba la Muziki na kusema: “Hei, Ndugu Rus-ell yumo ndani mle, nawe ukienda nyuma ya jukwaa unaweza kumwona.” Nilienda nikiwa na shauku nyingi na nikajikuta nikiongea naye uso kwa uso. Alikuwa amekuja kukagua mipango ya onyesho hilo la kwanza Mchezo wa Kuigiza Wenye Picha za Uumbaji.

Ndipo katika 1916, ikawa kwamba alikuwa akingojea gari-moshi la kumwelekeza mahali pengine akiwa katika Cincinnati na akakaa pale muda wa saa kadha. Dada mmoja na mimi, tulipoelezwa jambo lile, tulifanya haraka kwenda kwenye kituo cha reli, tukamkuta akiwa pamoja na mwandishi wake. Yeye alikuwa amekuja pamoja na chakula chake cha mchana, na wakati wa chakula ulipofika, akatugawia sisi chakula.

Tulipomaliza chakula cha mchana, yeye aliuliza kama mtu ye yote alikuwa na ulizo la Biblia. Mimi nikauliza juu ya uelekeo wa Adamu kufufuliwa kwa sababu yeye alikuwa mtenda dhambi asiyetubu, wa kukusudia. Kwa kupepesa jicho moja akajibu: “Ndugu, wewe unauliza ulizo na kulijibu wakati ule ule mmoja. Sasa, ulizo lako lilikuwa nini hasa?”

“Fumbo Lililokwisha”

Siku ya Jumanne, Oktoba 31, 1916, Charles Taze Russell alikufa, bila ya kuweza kutokeza buku la saba kwenye mfululizo wake wa Studies in the Scriptures. Alipokuwa akikaribia, kufa akiwa katika gari-moshi lililokuwa lirudi kutoka Kalifornia, mwandishi wake alimwuliza juu ya buku lile la saba, yeye alijibu: “Mtu mwingine atapaswa kuliandika.”

Katika mwaka uliofuata, 1917, buku la saba lilitokea likiwa na maelezo juu ya vitabu vya kiunabii kuhusu Ezekieli na Ufunuo, pamoja na maelezo ya kupendeza sana ya kitabu cha Biblia cha Wimbo wa Sulemani. Sosaiti ilipanga kuwe na mwenezo mkubwa ajabu wa kitabu hicho. Kwa hiyo, wao walipelekea watu fulani katika makundi vibweta vya buku hilo la saba katika sehemu zote za United States. Vibweta vingi vilipelekwa kwenye nyumba yangu katika 1810 Baymiller Street, Cincinnati, Ohio, na kuwekwa akibani huku sisi tukingojea maagizo zaidi juu ya jinsi vitabu vilivyokuwamo vingegawanywa.

Kulikuwa na kurasa nane za The Finished Mystery (“Fumbo Lililokwisha”) zilizokuwa na mitajo ya maneno yaliyokuwa yametangazwa na watu mashuhuri kwa njia isiyofaa kuhusu vita. Kwa kuchochewa na matengenezo ya kidini ya Jumuiya ya Wakristo, ya Kikatoliki na Kiprotestanti, serikali ya United States ilitokeza vipingamizi, kwa hiyo kurasa 247-254 zikakatwa na kuondolewa. Baada ya hapo, wakati The Finished Mystery kilipotolewa kwa watu, walipewa elezo kuhusu sababu iliyofanya kurasa hizo zisiwepo. Serikali ya United States haikubaki ikiwa imeridhishwa na hatua hiyo na kwa kuchochewa zaidi na matengene-zo ya kidini ya nchi hiyo, ilipiga marufuku buku zima la saba la Studies in the Scriptures.

Mimi nakumbuka kwamba asubuhi moja ya Jumapili nilikuwa nikifanya kazi kwenye mla-ngo wa nyuma wa nyumba yetu. Wanaume fulani walikuja wakitembea kwenye kijia kili-chokuwa kando ya nyumba, na kiongozi wao akavuta shavu la koti yake na kunionyesha beji yake ya chuma na kudai aingie ndani ya nyumba. Kwa hiyo nililazimika kuwapeleka ndani na kuwaonyesha vibweta vile vyenye nakala za The Finished Mystery. Siku chache baadaye, walileta lori wakavichukua vyote.

Baadaye tulipata habari kwamba Joseph F. Rutherford, msimamizi wa pili wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, na sita kati ya washirika wake wenye kutumikia kwenye makao makuu ya Brooklyn walishitakiwa kimakosa juu ya kuvuruga jitihada ya kivita ya United States. Walihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwenye Gereza Kuu la Taifa la Atlanta kuhusu kila moja ya mashtaka yale manne. Hata hivyo, vifungo vya mashtaka yote hayo vingeendelea wakati ule ule mmoja. Vita ilikwisha Novemba 11, 1918, na ndipo katika Machi 25, 1919, Ndugu Rutherford na washirika wake wakaachiliwa kwa dhamana. Baadaye waliondolewa hatia kabisa. Kitabu The Finished Mystery kiliondolewa pia chini ya marufuku na kikapewa mamlaka ya kuenezwa kwa uhuru kwa mara nyingine tena.

Roho zetu zilirudiwa na nguvu kama nini wakati Sosaiti ilipopanga mkusanyiko wetu wa kwanza baada ya vita katika Cedar Point, iliyo kwenye ncha ya peninsula yenye kute-mbelewa na wanalikizo, karibu na Sandusky, Ohio, ufanyike katika Septemba 1-8, 1919! Lilikuwa pendeleo lenye kufurahisha sana kwangu kuhudhuria mkusanyiko huo.

Kualikwa Betheli

Katika mwaka uliofuata wa 1920, Msimamizi Rutherford aliukubali mwaliko wa kuhutubia wasikilizaji wa peupe katika Cincinnati, Ohio. Mimi nilikuwa nikifanya kazi ya mwuza-vitabu, na Ndugu Rutherford alinialika nimwandikie barua nikiomba utumishi kwenye makao makuu ya Betheli ya Brooklyn.

Niliipeleka barua, na baada ya kupokea jibu la kukubaliwa, nikapanda gari-moshi kuelekea Mji wa New York. Usiku wa Jumanne, Juni 1, 1920, nilifika kule na nikalakiwa na Leo Pelle, rafiki mmoja wa zamani kutoka Louisville, Kentucky, naye akanielekeza kwenye makao ya Betheli. Kesho yake, Jumatano, nilipewa mgawo rasmi niwe nikikaa chumba kimoja na Hugo Riemer na Clarence Beatty katika chumba cha juu cha nyumba, nikawa mtu wa 102 wa jamaa ya Betheli ya Brooklyn.

Sosaiti ilikuwa imeanzisha karakana yake ya kwanza kwenye 35 Myrtle Avenue, katika orofa ya chini ambapo mashine-rotari yetu ya kwanza ya uchapaji iliwekwa, ambayo tuliiita Meli ya Kivita kwa sababu ya ukubwa wayo. Tulikuwa tukichapa gazeti jipya la Sosaiti lenye kichwa The Golden Age​—ambalo baadaye liliitwa Consolation na sasa ni Amkeni! Wakati magazeti yalipotokea kupitia nafasi-wazi sakafuni na kupitishwa juu ya mfumo wa waya kupanda juu ya ubao ulioinama, mimi niliyakusanya, nikiyatikisa kidogo yalaliane vizuri na kuyapanga pamoja yakatwe baadaye na kushughulikiwa.

Asubuhi ya Jumamosi, wakati mashine ya uchapaji ilipokuwa haichapi magazeti, hesabu fulani kati yetu ndugu tulikuwa tukiyafunga magazeti katika karatasi za rangi kahawia zenye majina na anwani za waandikishaji. Halafu tulikuwa tukiyafunga yashughulikiwe na afisi ya posta. Niliendelea kufanya kazi hiyo kwa miezi kadha mpaka Donald Haslett, aliyekuwa akitumikia katika Dawati ya Wauza-Vitabu, alipoondoka akamwoe Mabel Catel. Halafu nikahamishwa kutoka 35 Myrtle Avenue kwenda kwenye afisi ya Sosaiti katika 124 Columbia Heights nikatumikie kwenye Dawati ya Wauza-Vitabu.

Pia, nikiwa mshiriki wa Kundi la New York, nilipewa mgawo wa kuongoza funzo la kitabu nyumbani kwa jamaa ya akina Afterman katika eneo la Ridgewood la Brooklyn.

Mapendeleo ya Redio na Mikusanyiko

Niliendelea kutumikia kwenye Dawati ya Wauza-Vitabu mpaka 1926. Muda huo ulipokuwa ukiendelea, Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ya Biblia na Trakti ilikuwa imeanzisha katika Kisiwa cha Staten kituo cha redio chao cha kwanza, WBBR. Hiyo ilikuwa katika 1924. Mimi nilikuwa na pendeleo la kufurahisha la kutumikia katika programu za Sosaiti, si kutoa hotuba tu bali kuimba pia sauti ya tenor nikiwa peke yangu na hata kupiga mandolini kwa kufuatana na mwenye kupiga piano. Zaidi ya hilo, niliimba sauti ya pili ya tenor katika kikundi chetu cha waimbaji wanne wanaume wa kituo cha WBBR. Bila shaka, Ndugu Rutherford, akiwa ndiye msimamizi wa Sosaiti, alikuwa ndiye msemaji mkuu katika WBBR na alikuwa na wasikilizaji wengi sana.

Lilikuwa katika mwaka wa 1922 ndipo mkusanyiko mkuu wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ya Biblia na Trakti ulipofanywa kwa mara ya pili katika Cedar Point, Ohio. Hapo tulihimizwa kwa uthabiti mwingi na Ndugu Ruther-ord kwamba “tangazeni, tangazeni, tangazeni, Mfalme na ufalme wake!”

Moja la mapendeleo yangu ninalothamini sana katika miaka ya 1920 lilikuwa kutumikia pamoja na Ndugu Rutherford kwenye mkusanyiko wa kimataifa katika London, Uingereza, katika 1926. Kule yeye alitoa hotuba ya watu wote katika Royal Albert Hall ya London mbele ya wasikilizaji wengi baada ya mimi kuimba sauti ya tenor nikiwa peke yangu kwa kufuatana na kinanda chenye sifa kubwa cha jumba lile.

Usiku uliofuata yeye aliwahutubia wasikilizaji Wayahudi juu ya “Faraja kwa Wayahudi ​—kwa Sababu Gani?,” nami nikaimba sauti ya solo nikiwa peke yangu kwa kutumia wimbo Masihi uliotungwa na Handel, “Wafarijini, Watu Wangu.” Maelfu kadha ya Wayahudi walihudhuria ibada hiyo ya pekee. Wakati huo, sisi tulikuwa tukitumia mambo ya unabii kimakosa kutokana na Maandiko ya Kiebrania ili yawahusu Wayahudi wa kimwili, waliotahi-riwa. Lakini katika 1932 Yehova aliyafungua macho yetu tuone kwamba mambo hayo ya unabii yalitumika kwa Israeli wa kiroho.

Nalo lilikuwa jambo la kusisimua kama nini kuwa kwenye mkusanyiko kwenye Columbus, Ohio, katika 1931 wakati Ndugu Rutherford alipolitokeza “jina jipya” Mashahidi wa Yeho-va, na sisi sote tukalichukua kwa shauku! Mara tu baada ya hapo, makundi yote ya watu wa Yehova kuzunguka dunia walilichukua ‘jina jipya’ hilo.​—Linganisha Isaya 62:2.

Ijumaa, Mei 31, 1935, ilinikuta nikitumikia nikiwa kiongozi wa okestra katika mahali palipoteremka kando ya kinara cha jukwaa ambalo Ndugu Rutherford alitoa hotuba yake maarufu juu ya Ufunuo 7:9-17, akitutambulishia kwa usahihi ni akina nani wangekuwa washiriki wa “umati mkubwa” ulioonyeshwa humo. Hasa ile inayoitwa jamii ya Yonadabu ilialikwa iwepo, na sababu ikaonekana wazi wakati Ndugu Rutherford alipoonyesha kwamba “umati mkubwa,” au “mkutano mkubwa” (New World Translation), ungekuwa wa “kondoo wengine” wa “mchungaji mwema” Yesu Kristo. (Yohana 10:14, 16, KJ) Ilikuwa pindi ya kusisimua. Mimi nilichangamka moyo kama nini wakati kesho yake, Juni 1, wakusanyikaji 840 walipozamishwa katika maji kuonyesha wakfu wao kwa Mungu kupitia Kristo wakiwa na tazamio la paradiso ya kidunia! Tangu wakati huo na kuendelea, hesabu ya “kondoo wengine” wa Kristo ilizidi kusonga mbele na kuipita, kwa mbali, hesabu ya washiriki wanaopungua-pungua wa “kundi dogo” la wanafunzi wazaliwa-kwa-roho walio mfano wa kondoo wa mchungaji mzuri sana, Yesu Kristo.​—Luka 12:32.

Hata hivyo, wakati Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipotokea kwa ghafula katika 1939, ilione-kana kama kwamba hilo lilimaanisha mwisho wa kukusanywa kwa “mkutano mkubwa.” Mimi nakumbuka Ndugu Rutherford akiniambia siku moja: “Haya basi, Fred, inaonekana kama kwamba ‘umati mkubwa’ hautakuwa mkubwa sana kama ilivyotazamiwa.” Hatukujua sana kwamba kumbe kulikuwa bado na mkusanyo mkubwa mbele.

Sosaiti ilianzisha kinanda chenye kubebeka katika 1934, na maneno yaliyorekodiwa katika sahani za santuri kuhusu hotuba za Msimamizi Rutherford yalitumiwa kuwa utangulizi wa kutolea vitabu vya Kibiblia. Wakati maneno hayo yalipotafsiriwa katika Kihispania, mimi nilikaza fikira kuyatumia katika kufikia watu wenye kusema Kihispania katika ujirani wa kiwanda chetu kwenye 117 Adams Street. Ndipo, kwa ziara za kurudia, nikawasaidia watu wenye kupendezwa wajifunze kweli za Biblia, na kwa njia hiyo hatimaye nilipendezwa kulitengeneza kundi la kwanza lenye kusema Kihispania katika Brooklyn. Nilikuwa wa Kundi la Kihispania la Brooklyn, namba moja, tangu wakati lilipofanyizwa.

Mabadiliko Katika Usimamizi wa Sosaiti

Ndugu Rutherford alipokufa Januari 8, 1942, Nathan H. Knorr alimfuata katika usimamizi wa Sosaiti. Ijapokuwa vita ya ulimwengu ya pili iliyokuwa ikiwaka moto, hotuba ya watu wote aliyotoa katika kiangazi cha 1942 juu ya habari “Amani​—Je! Inaweza Kudumu?” ilipindua tazamio letu kuhusu mambo ambayo yangetukia karibuni sana. Upesi baada ya hapo, Ndugu Knorr alifungua Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi kwenye Shamba la Ufalme siku ya Jumatatu, Februari 1, 1943, huku wanafunzi mia moja wakiwa ndilo darasa la kwanza. Mimi nilikuwa na pendeleo la kutumikia katika programu kwa kipindi cha mzinduo. Ndugu Eduardo Keller, Maxwell G. Friend, Victor Blackwell, na Albert D. Schroeder walitumikia wakiwa walimu.

Katika hotuba yake ya kufungua, Ndugu Knorr alitujulisha kwamba Sosaiti ilikuwa na pesa za kutosha kuendeleza shule hiyo kwa miaka mitano. Lakini kumbe, leo Yehova Mungu Mwenye Nguvu Zote ameiendeleza shule hiyo kwa wakati wenye urefu ulio mara tisa ya huo!

Lilikuwa pendeleo kubwa sana kushirikiana na Nathan H. Knorr. Sikuweza kutambua wakati yeye alipozamishwa baada ya hotuba ambayo mimi nilitolea wenye kubatizwa siku ya Julai 4, 1923, kando ya Mto wa Little Lehigh nje ya mji wa nyumbani kwao wa Allentown, Pennsylvania, kwamba yeye angekuwa ndiye msimamizi wa tatu wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ya Biblia na Trakti.

Chini ya usimamizi wa Ndugu Knorr, nilisafiri sana, nikihutubia makusanyiko makubwa ya akina ndugu kuzunguka ulimwengu ​—kutia ndani Latini Amerika na Australia—​nikiwatia moyo wabaki waaminifu. Katika pindi moja ya namna hiyo, katika 1955, kulipokuwa na marufuku juu ya kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Hispania, nilitumikia kusanyiko la siri mwituni nje ya Barcelona. Kusanyiko letu la ndugu Wahispania lilizingirwa na polisi wa siri wenye silaha, na wanaume waliokuwapo wakachukuliwa katika magari makubwa kuelekezwa kwenye makao makuu ya polisi. Huko tukafungwa na kuulizwa-ulizwa maswali. Kwa kuwa mimi nilikuwa raia Mwamerika, nilijifanya sijui Kihispania. Pia, dada wawili walikuwa wameponyoka na kuujulisha Ubalozi wa Amerika juu ya kukamatwa kwangu, nao wakawasiliana na polisi. Kwa sababu ya kutaka kuepuka kisa kile kisitangazwe katika mataifa na habari mbaya zisiandikwe, mwishowe wakatuachilia sisi wageni-wageni na, baadaye, hata akina ndugu. Baada ya hapo, hesabu fulani kati yetu tulikusanyika pamoja kwenye nyumba ya akina ndugu walioitwa Serrano, nasi tukafurahia sana ukombozi wa Yehova juu ya watu wake. Katika 1970 Hispania iliwapa Mashahidi wa Yehova utambuzi wa kisheria. Leo sisi tuna afisi ya tawi karibu ya Madrid, na mwaka huu uliopita tengenezo katika Hispania lilitia ndani wahubiri wa Ufalme zaidi ya 65,000 kukiwa na makundi katika sehemu zote za nchi ile.

Katika Juni 8, 1977, Nathan H. Knorr alikufa, akimaliza mwendo wake wa kidunia, nami nikamfuata katika cheo cha msimamizi wa Sosaiti. Ndugu Knorr alikuwa ametumikia kwa miaka zaidi ya 35 katika usimamizi, huo ukiwa ni muda mrefu kuliko ule wa ye yote wa wale wasimamizi wawili waliotangulia wa Sosaiti, Russell na Rutherford. Nikiwa mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova, nimepewa mgawo wa kutumikia katika Halmashauri ya Uchapishaji na katika Halmashauri ya Waandikaji ya Baraza Linaloongoza.

Ni pendeleo kubwa na furaha kuu kweli kweli kuendelea kutumikia katika afisi za Sosaiti kwenye 25 Columbia Heights. Jambo hilo linanihitaji nitembee kwa ukawaida siku za kazi kati ya afisi kuu na makao ya Betheli ​—mazoezi ya kimwili bora kabisa kwa mtu mwenye mwili unaozeeka. Ingawa mimi ni mwenye umri wa miaka 93 na nguvu za macho yangu zinaendelea kupungua, ninafurahi sana kwamba Yehova amenibariki kwa afya njema, hivi kwamba sijakosa hata siku moja ya kazi kwa sababu ya ugonjwa muda wa miaka 66 nikiwa Betheli, nami ningali naweza kutumikia wakati wote. Limekuwa pendeleo la kimungu kweli kweli kwa mimi kuwa hapa tangu 1920 na kuuona ukuzi na mpanuko wa tengenezo kwenye makao makuu ya Brooklyn na kuzunguka ulimwengu.

Nikiwa na uhakika kamili katika Mwenye Enzi Kuu wa Ulimwengu Mzima Wote, Yehova Mungu na Jemadari Mkuu wake Yesu Kristo, anayesimamia vikosi visivyohesabika vya maserafi, makerubi, na malaika watakatifu wa mbinguni, mimi natazama mbele, wakati wa uandikaji wa habari hii, pamoja na mamilioni ya Mashahidi wenzangu, kwenye kile ambacho Biblia inaonyesha kingali mbele: uharibifu wa Babuloni Mkuu, milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo, na “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” kwenye Har–Mage-doni, itakayofikia upeo katika ushindi wa ushindi wote kwa upande wa Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Mzima Wote, Yehova Mungu, ambaye ni wa “kutoka umilele mpaka umilele.” Haleluya!​—Zaburi 90:2, Byington.

[Picha katika ukurasa wa 23]

[Picha katika ukurasa wa 24]

Nikiwa katikati pamoja na wafanya kazi wenzangu wa Betheli 1920

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nikiwa pamoja na N. H. Knorr 1961

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nikihutubia mkusanyiko katika Japani 1978

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki