Kuiponyosha Codex Sinaiticus
ILE Codex Sinaiticus imeelezwa kuwa “ndicho kitabu kilicho cha maana, cha kutaharukisha, na chenye thamani kubwa kuliko vyote vilivyoko.” Hiyo si kwa sababu tu ina umri wa angalau miaka 1,600 bali kwa sababu inafanyiza kiunzi muhimu katika orodha yetu ya hati za Biblia. Kugunduliwa kwacho kwa mara nyingine, na Tischendorf muda unaozidi kidogo miaka mia moja iliyopita, ni hadithi yenye kusisimua.
Konstantin von Tischendorf alizaliwa katika Saxony, kaskazini mwa Ulaya, katika mwaka 1815 na alielimishwa Kigiriki kwenye Chuo Kikuu cha Leipzig. Wakati wa machunguzi yake, yeye alifadhaishwa na uchambuzi wa hali ya juu zaidi wa Biblia, uliotamkwa na wanatheolojia mashuhuri Wajeremani wakitafuta kuthibitisha kwamba Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo hayakuwa na unyoofu wa kusema kweli. Hata hivyo, Tischendorf alipata kusadiki kwamba uchunguzi wa hati za mapema ungethibitisha ukweli wa maandishi-awali ya Biblia. Tokeo ni kwamba, yeye alipiga moyo konde ajifanyie mwenyewe utafiti juu ya hati zote zenye kujulikana, akitumainia kugundua nyinginezo wakati wa safari zake.
Baada ya kutumia miaka minne akipekua-pekua katika maktaba za Ulaya zilizo nzuri zaidi, Tischendorf, katika Mei 1844, alifika kwenye Makaowatawa ya St. Catherine, yaliyo kwenye mwinuko wa meta 1,400 juu ya usawa wa Bahari Nyekundu katika Sinai. Njia ya kuingia ndani ya makao yale ya watawa yaliyo kama ngome ilikuwa kwa kutumia kapu lililoning’inizwa kwa kamba kupitia mwanya mdogo ukutani.
MAPATO YENYE KUTHAWABISHA
Kwa siku kadhaa aliruhusiwa apekue-pekue maktaba zao tatu, bila mafanikio. Ndipo, alipokuwa tu karibu kuondoka, akaona kile alichokuwa amekuwa akitafuta—ngozi zilizoandikwa maandishi ya kale! Zilijaza kapu moja lililokuwa katika jumba la maktaba iliyo kuu. Mtunza-maktaba alimwambia kwamba hizo zingechomwa, sawa na vile makapu mawili yaliyojaa yalivyokuwa yamechomwa tayari. Miongoni mwa ngozi hizo zenye maandishi, Tischendorf alistaajabu kupata karatasi 129 za kikurasa za hati ya zamani zaidi aliyokuwa amepata kuona, ikiwa ni tafsiri ya Kigiriki ya sehemu za Maandiko ya Kiebrania. Yeye alipewa karatasi 43, lakini akanyimwa zile nyingine.
Tischendorf alizuru tena makaowatawa hayo katika 1853 lakini alichopata tu kilikuwa ni kisehemu cha Mwanzo kutokana na hati ile ile ya karne ya nne. Yeye alisadiki “kwamba hapo awali hati hiyo ilikuwa na Agano la Kale lote zima, lakini sehemu iliyo kubwa zaidi ilikuwa imeharibiwa muda mrefu uliopita.” Labda hati iliyo kamili ilikuwa na karatasi 730 za kikurasa. Ilikuwa imeandikwa katika herufi kubwa za Kigiriki juu ya ngozi laini za kondoo na mbuzi.
Miaka sita baadaye Tischendorf alifanya ziara yake ya tatu kwenda kwa watawa hao wa Sinai. Alipokaribia kuondoka, alionyeshwa hivi hivi tu si zile tu karatasi za kikurasa alizokuwa ameokoa motoni miaka 15 mapema, bali na nyinginezo pia. Hizo zilikuwa na Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yote mazima, pamoja na sehemu ya tafsiri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania.
Tischendorf aliruhusiwa kupeleka hati hiyo Cairo, Misri, akainakili, na mwishowe ampelekee mmaliki wa Urusi kama zawadi kutoka kwa watawa hao. Leo hati hiyo imewekwa katika Jumba la Makumbusho la Uingereza, ikiwa kwenye wonyesho kando ya Codex Alexandrinus. Zile karatasi za kikurasa 43 za mapema zaidi zimo katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Leipzig, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujeremani.
Sisi tunapaswa kuwa na shukrani kwa Tischendorf kwa kufanya bidii ya kuhusisha sana maisha na vipaji vyake katika utafutaji wa hati za kale za Biblia na hasa kwa kuiponyosha ile Codex Sinaiticus iliyo bora sana kutoka kwenye uharibifu. Lakini asante zetu zilizo nyingi zaidi zinaendea Yehova Mungu, ambaye amehakikisha kwamba Neno lake limehifadhiwa kwa usahihi sana kwa ajili ya manufaa yetu leo.
[Sanduku katika ukurasa wa 30]
Kutumia Kodeksi Hiyo
Kialama kilicho kifananishi cha Codex Sinaiticus ni ile herufi ya Kiebrania א. Kodeksi (kitabu) hiyo inathibitisha usahihi wa hati za majuzi zaidi za Biblia zilizoandikwa katika mafunjo. Pia inasaidia uanachuo wa ki-siku-hizi wa Biblia kwa kuonyesha wazi makosa yasiyoonekana wazi ambayo yalipenya ndani ya nakala za baadaye.
Mathalani, Yohana 1:18, NW, inasomwa hivi: “Hakuna mtu ambaye amemwona Mungu wakati wo wote; yule mungu mzaliwa wa pekee aliye mahali pa kifua pamoja na Baba ndiye ambaye ameeleza juu yake.” Maelezo ya chini ya “New World Translation Reference Bible” yanafunua kwamba “yule mungu mzaliwa wa pekee,” badala ya ile fasiri nyingine “Mwana mzaliwa wa pekee,” ndiyo inayoungwa mkono na Codex Sinaiticus na hati nyingine za zamani. Pia lile rejezeo אc linaonyesha alama ya sahihisho ya kodeski hiyo ili kuthibitisha kwamba ilifaa kurudisha ile nukta-dhihirisho “yule mungu mzaliwa wa pekee.” Cheo cha Yesu Kristo hakina kifani, kama vile andiko linavyoshuhudiza.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Makaowatawa ya St. Catherine kwenye sehemu ya chini ya Mlima Sinai wa tangu hapo. [Kisehemu cha ndani] maktaba yacho ya sasa
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Courtesy of the British Museum, London