Haki kwa Wote—Je! Kuna Wakati Itakuja?
WENYE kuzuru Old Bailey, ambalo ni jengo la kihistoria London lililo Mahakama Kuu Kuhusiana na Uhalifu, wanaona juu sanamu-umbo ya mwanamke anayefananisha haki. Katika mkono mmoja ameshika jozi ya mizani, ikionyesha kwamba ithibati ya mambo itapimwa kwa uangalifu. Mkono ule mwingine umeshika sana upanga, kuwapa himaya wasio na hatia na kuadhibu wenye hatia. Katika mahali pengi penginepo, wewe unaweza kuona maumbo mengine yaliyo kama kifananishi hicho, nyakati nyingine yakiwa yamefunikwa macho kwa kitambaa kinachosema “Haki” ili kuwakilisha kutopendelea kwa mwanamke huyo.a
Ingawa hivyo, wewe ungeweza kuuliza hivi: ‘Je! kinachofananishwa na mwanamke huyo, haki kwa ajili ya wote, kimo kweli katika bara lolote?’ Bila shaka, katika kila bara mna sheria, na pia wenye kuzifikiliza. Kisha kuna mahakimu na mahakama. Kwa uhakika, watu wengi wanaofuata kanuni wamejaribu kutegemeza haki za kibinadamu na kuhakikisha kuna haki ya usawa kwa wote. Na bado, ni wazi kwamba nyingi za jitihada zao zimeshindwa. Karibu kila siku, tunaona, tunasikia, au tunasoma habari za ufisadi, za kutendea watu bila usawa, na za ukosefu wa haki.
Fikiria kisa cha mwanamke mmoja aliyeletwa mahakamani. Kabla hajathibitishwa kuwa ana hatia au hanayo, hakimu alimjulisha kwamba ‘angemtengenezea mambo’ kuhusu shtaka lake ikiwa mwanamke huyo angekutana naye kwenye moteli, kwa uwazi ili wafanye ngono haramu. Ndiyo, wale wanaopaswa kuhakikisha kuna haki wamethibitika mara nyingi kuwa wafisadi au wasioweza mambo. Gazeti Time lilieleza juu ya mkoa mmoja katika United States ambako sehemu tatu kwa tano za mahakimu wa Mahakama walishtakiwa juu ya mwenendo wa kutofuata kanuni bora katika kusaidia hakimu mwenzao.
Waaidha, watu wajuapo kuna wahalifu wanaoendelea kuponyoka adhabu, wengi wanaanza kupuuza sana mambo na kuona ni rahisi zaidi wao wenyewe kuvunja sheria. (Mhubiri 8:11) Twasoma hivi juu ya Uholanzi: “Waholanzi wengi wanalaumu wanasiasa kwa kutia moyo kuwe na uendekevu unaosababisha uhalifu. Wengine wanazishtaki mahakama, sana sana mahakimu . . . wanaoendelea kutoa hukumu ndogo-ndogo tu, nyakati nyingine zikiwa za kupunguza sana adhabu kwa njia ya kushangaza sana.” Lakini haki tunayohitaji haraka sana inatia ndani mengi zaidi ya kusahihisha mashirika ya ufikilizaji sheria na mfumo wa hukumu.
Wewe unajua kwamba katika mabara mengi matajiri wachache wanazidi kuwa matajiri, huku maskini wengi sana wakitendewa isivyo haki kiuchumi. Huo ukosefu wa haki unakuwapo sana wakati watu, kwa sababu ya rangi ya ngozi yao, kabila, lugha, jinsia, au dini, wanapokosa sana fursa ya kuendeleza hali yao au hata kujiruzuku. Tokeo ni kwamba mamilioni wanakumbwa na umaskini, njaa, na ugonjwa. Ingawa watu wengi katika mabara yenye utajiri wananufaika na dawa na matibabu ya hali ya juu, mamilioni wasioelezeka wanateseka na kufa kwa kukosa pesa za dawa zile za kimsingi au hata maji safi. Ebu jaribu kuwaambia mambo ya haki! Wao huzaliwa na kuzikwa katika ukosefu wa haki.—Mhubiri 8:9.
Namna gani yale yaliyo kama matendo ya ukosefu wa haki yanayoonekana kutoweza kudhibitiwa kwa nguvu za kibinadamu? Fikiria vitoto vinavyozaliwa na kasoro za kurithi—upofu, kuzubaa akili, au kasoro za viungo. Je! mwanamke angehisi kuna haki ikiwa kitoto chake kinazaliwa kikiwa kiwete au kimekufa, hali wanawake wengine pale karibu wanakumbatia-kumbatia vitoto vichanga vyenye afya? Kama itakavyoonyeshwa na zungumzo linalofuata, hayo yanayoonekana kuwa matendo ya ukosefu wa haki yatasahihishwa.
Hata hivyo, kufikia hapo, je! wewe hukubaliani na elezo lililo kwenye Mhubiri 1:15? Hapo mfalme mwenye hekima na ujuzi alikiri hivi, kulingana na kituo cha rai ya kibinadamu: “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, wala yasiyokuwapo hayahesabiki.”
Mwanamume mwenye sifa hata zaidi alikuwa Yesu. Kwenye Luka 18:1-5 twasoma kielezi chake cha hakimu ‘asiyemcha Mungu wala kujali watu.’ Basi, mjane mmoja aliendelea kujitetea akimsihi hakimu ampe haki ambayo sheria ilimstahilisha. Lakini Yesu alisema huyo hakimu mwovu alimsaidia kwa sababu tu kujitetea-tetea kwake kulikuwa usumbufu mkubwa. Kwa hiyo unaweza kuona kwamba, Yesu alijua matendo ya ukosefu wa haki yalikuwa tele. Kwa uhakika, baadaye yeye mwenyewe aliumizwa-umizwa na kuuawa kwa shtaka la kutungwa tu, huo ukiwa ni ukosefu mwingine wa haki ulio mbaya sana!
Wengi wanaitikadi kwamba kuna Mungu anayehangaishwa na ukosefu wa haki. Wakati wa Misa katika bara moja la Amerika ya Kati, Papa John Paulo 2 alisema: “Unapokanyaga-kanyaga mtu, unapovunja haki zake, unapotenda dhidi yake madhalimu makubwa kabisa ya ukosefu wa haki, unapomuumiza-umiza, kumvunjia kao lake na kumtorosha au kuvunja haki yake ya kuishi, unatenda uhalifu na kosa kubwa dhidi ya Mungu.” Maneno mazuri hayo. Na bado, matendo ya ukosefu wa haki yanaendelea. Ukosefu wa chakula cha kujenga mwili unasumbua watoto 8 kati ya 10 wa chini ya miaka mitano katika nchi hiyo. Asilimia mbili ya watu wa huko ndio wenye asilimia 80 ya ardhi inayolimika.
Kwa hiyo je! kweli kuna Mungu anayejali kikweli mabaya hayo makubwa sana ya ukosefu wa haki, Mungu atakayehangaishwa hata na matendo ya ukosefu wa haki yanayokuathiri wewe? Je! kuna wakati atakapohakikisha haki imekuja?
[Maelezo ya Chini]
a Picha ya jalada letu inatoka Justitia Fountain katika Frankfurt am Main, Ujeremani. Sanamu iliyo katika ukurasa huu iko juu ya jengo moja la manispaa katika Brooklyn, New York, U.S.A.