Abrahamu—Mnabii na Rafiki ya Mungu
MAJESHI yaliyoungana ya wafalme wanne wa Mashariki yanavuka Mto Eufrati. Njia wanayofuata wakipiga miguu ni Njia Kuu ya Mfalme kuelekea upande wa mashariki wa bonde la Mto Yordani. Wakiwa mwendoni wanawashinda Warefaimu, Wazuzimu, Waemimu, na Wahori. Halafu, wavamizi hao wanageuka na kushinda wakaaji wote wa Negebu ya kusini.
Ni nini kusudi la kampeni hii ya kijeshi? Kitu wanachokitaka sana kimo katikati ya majimbo yale yaliyovamiwa ng’ambo ya Yordani na ile Negebu. Kitu chenyewe ni bonde fulani lenye kutamaniwa sana linaloitwa Wilaya ya Yordani. (Mwanzo 13:10) Hapa, wakaaji wa mikoa mitano ambayo ni majiji, Sodoma, Gomora, Adma, Seboimu, na Bela, wanaishi maisha ya kizembe tu yenye starehe za vitu vya kimwili. (Ezekieli 16:49, 50) Wakati mmoja walikuwa wametiishwa chini ya aliyeonekana kuwa kiongozi wa majeshi hayo yaliyounganika, Kedorlaoma, mfalme wa Elamu. Lakini wameasi dhidi yake. Sasa, wanakabiliwa na utozwaji hesabu, bila msaada wa majirani. Kedorlaoma na waungani wake wanashinda pigano linalotokea na kuanza mwendo wao mrefu wa kupiga miguu kwenda nyumbani wakiwa na nyara nyingi.
Miongoni mwa watekwa yumo mwanamume mwadilifu, Loti. Yeye ni mpwa-mume wa Abrahamu, ambaye amepiga hema katika milima ya karibu ya Hebroni. Abrahamu anaposikia habari hizo za kutaabisha sana, mara hiyo anaita watu 318 kati ya wanaume wake. Wakiwa na usaidizi wa majirani fulani, kwa ushujaa wanawafuata mbio wafalme hao wanne na kufumania majeshi yao usiku. Wavamizi hao wanakimbia. Loti na watu wa nyumba yake wanaponyolewa, pamoja na watekwa wengine na bidhaa.
Sisi tuna sababu gani ya kuamini kumbukumbu hili la maandishi yaliyo katika sura ya 14 ya Mwanzo? Je! hadithi hii ilivumbuliwa tu ili kumfanya baba mtangulizi wa mataifa kadhaa, kutia na Wayahudi, awe shujaa wa kitaifa? Namna gani matukio mengine katika maisha ya Abrahamu?
Mambo Ambayo Makasisi Wamesema
Mapema ya karne ya 19, mwanatheolojia Mlutheri Peter von Bohlen alidai kwamba Abrahamu alikuwa mtu wa hadithi tu na kwamba usimulizi wa uvamizi wa Kedorlaoma hauna msingi wa kihistoria. Mwingine, Profesa Julius Wellhausen, alitaarifu hivi: “Sisi hatupati maarifa yoyote ya kihistoria kuwahusu wazee wa ukoo.” Alidokeza hivi: “[Abrahamu] angeweza kuelekea zaidi kuonwa kuwa ubuni tu wa maarifa stadi yasiyo na uhakika.”
Wanatheolojia Waingereza walifuata mwongozo wa wenzao Wajeremani. “Hadithi zenye sifa sana kuhusu wazee wa ukoo katika kitabu cha Mwanzo ni za kabla ya historia, si za kweli kihistoria kama vile zisivyo za kweli hadithi za . . . Mfalme Arthur,” akaandika kasisi Stopford Brooke katika kitabu chake The Old Testament and Modern Life. “Kutokana na . . . Mwanzo . . . sisi tunapata maoni yasiyo kamili na yaliyopotoka juu ya maisha na tabia ya yeyote wa wazee wa ukoo,” anaandika John Colenso, askofu Mwanglikana wa Natal ambalo lilikuwa koloni la Waingereza hapo kwanza. Yeye aliongezea kwamba, “haiwezekani kuwa na uhakika kamili katika yoyote ya kumbukumbu hizi za kimaandishi.”
Uchambuzi huo ulienea kama donda-ndugu. (2 Timotheo 2:17) Leo, mamilioni ya waenda-kanisani wameacha kuyachukua kwa uzito maisha ya wazee wa ukoo. Hata hivyo, jambo la kuaibisha wanatheolojia wa Jumuiya ya Wakristo ni kwamba sasa watu wasioamini kuna Mungu wanataarifu kwamba uchambuzi wa Biblia umeruka mipaka. Kwa kielelezo, Bol’shaia Sovetskaia Entsiklopediia (Ensaiklopedia Kubwa ya Kirusi) inataarifu hivi: “Katika miaka ya majuzi, mfululizo wa mabishano yanayohusu uchambuzi wa kibiblia yalichunguzwa upya kulingana na nuru ya utafiti mpya, hasa kwa kutegemea msingi wa habari za ule unaoitwa uchimbuzi wa vitu vya kale vya kibiblia. Mapokeo fulani ya kibiblia yaliyokuwa yameonwa kuwa hadithi tu . . . yanaonekana kuwa na uthibitifu wa kihistoria.” Fikiria jinsi uchimbuzi wa vitu vya kale umeangaza nuru juu ya kumbukumbu la maandishi yanayohusu Abrahamu.
Uru la Wakaldayo
Kulingana na Biblia, Abrahamu alilelewa katika “Uru la Wakaldayo.” (Mwanzo 11:27-31; 15:7, NW) Kwa karne kadhaa, mahali ambapo jiji la Uru lilikuwa palikuwa fumbo. Wachambuzi waliamini kwamba ikiwa kweli mahali hapo palikuwako, palikuwa mahali pasipo pa maana sana, penye kubaki nyuma kimaendeleo. Ndipo, kwa aibu yao, magofu yaliyo kati ya Babuloni na Ghuba ya Uajemi yakatambulishwa pasipo kukosea kwamba yalikuwa yale ya Uru. Maelfu ya tableti za udongo zilizofukuliwa hapo zilifunua kwamba Uru kilikuwa kitovu cha biashara ya ulimwengu, kikiwa na wakaaji wengi wa kutoka sehemu nyingi za ulimwengu. Wakati wa Abrahamu, jiji hilo hata lilikuwa na shule ambako wavulana walifunzwa kuandika na kufanya hesabu.
Tena, machimbuo huko Uru yalifunua kwamba wasanii wa ujenzi katika jiji hilo walitumia nguzo madhubuti, matao, paa zilizoviringwa zikiwa na maumbo ya matao, na kuba. Mafundi wa Uru walifanyiza majohari ya kupendeza sana, vinubi vilivyoundwa kwa mapambo ya kuvutia, na sime zenye makali ya dhahabu iliyotakata. Katika nyumba kadhaa, wachimbuzi wa vitu vya kale walifukua mitarimbo ya kusafirishia kinyesi, iliyofanyizwa kwa udongo uliookwa, ambayo yalishuka kuingia ndani ya mashimo makubwa ya kufyonzea maji, yenye kina kinachofikia meta 12.
Magunduo haya yaliwapa wanachuo wengi maoni mapya juu ya Abrahamu. “Sisi tulikuwa tumezoea kumfikiria Abrahamu kuwa mkaaji wa kikawaida tu katika mahema, nasi twapata kwamba yawezekana alikuwa mkaaji wa nyumba ya kimaendeleo sana iliyojengwa kwa matofali katika jiji,” akaandika Sir Leonard Woolley katika kitabu chake Digging Up the Past. Mchimbuzi wa vitu vya kale Alan Millard alitaarifu katika kitabu chake Treasures From Bible Times kwamba “Abrahamu aliliacha jiji hilo lenye maendeleo sana, pamoja na usalama na starehe yote yalo, akawe mmoja wa watanga-tangaji wenye kudharauliwa!”
Uvamizi wa Kedorlaoma
Namna gani ushindi wa Abrahamu juu ya Kedorlaoma, mfalme wa Elamu? Mapema katika karne ya 19, ni machache yaliyojulikana juu ya Waelami. Wachambuzi wa Biblia walilikataa wazo la kwamba Elamu alipata kuwa na uvutano juu ya Babuloni, achia mbali Palestina. Sasa, Waelami wanaonwa kwa njia tofauti. Uchimbuzi wa vitu vya kale unawafunua kwamba walikuwa taifa la kivita lenye nguvu. Funk & Wagnalls Standard Reference Encyclopedia inataarifu hivi: “Waelami waliharibu jiji la Uru karibu 1950 K.K. . . . Baada ya hapo walitokeza uvutano wa kadiri kubwa juu ya watawala wa Babulonia.”
Tena, majina ya wafalme Waelami yamepatikana juu ya miandiko iliyochorwa juu ya machimbuo ya kale. Baadhi ya majina hayo yanaanza kwa neno “Kuduri,” linalofanana na “Kedori.” Mungumke Mwelami aliye wa maana alikuwa Lagamari, neno linalofanana na “laoma.” Hivyo, Kedorlaoma anakubaliwa sasa na vyanzo fulani vya kilimwengu kwamba alikuwa mtawala wa kihistoria, kukiwa na uwezekano wa kwamba jina lake lilimaanisha “Mtumishi wa Lagamari.” Fungu moja la miandiko ya Kibabulonia lina majina yanayofanana na watatu kati ya wale wafalme wenye kuvamia—Tudhula (Tidali), Eriaku (Arioki), na Kuduru-lahmili (Kedorlaoma). (Mwanzo 14:1) Katika kitabu Hidden Things of God’s Revelation, Dakt. A. Custance anaongezea hivi: “Zaidi ya majina haya yalikuwako maelezo madogo-madogo yaliyoelekea kutaja matukio yaliyotendeka katika Babulonia wakati Waelami waliposimamisha imara enzi kuu yao juu ya nchi hiyo. . . . Tableti hizi zililithibitisha sana Andiko hata Wachambuzi wa Juu Zaidi wakazirukia na kufanya kila waliloweza ili waugandamize kwa makusudi umaana wazo.”
Namna gani uvamizi uliofanywa na wale wafalme wanne? Je! kuna ushuhuda wowote uliochimbuliwa katika eneo la ng’ambo ya Yordani na ile Negebu kuunga mkono jambo hili? Ndiyo. Katika kitabu chake The Archaeology of the Land of Israel, Profesa Yohanan Aharoni anataja kutoweka kwa utamaduni uliowatangulia Waisraeli ambao ulikuwa na makao “ya kuvutia” ng’ambo ya Yordani na ile Negebu, “karibu 2000 K.W.K.” Wachimbuzi wengine wa vitu vya kale wanasema hii ilitukia karibu 1900 K.W.K. “Vyungu vya kipindi hiki katika mahali pote pawili Negebu na ng’ambo ya Yordani vinafanana na kuonyesha kwamba utamaduni wa hapo ulikomeshwa kwa ghafula, kwa njia ya maangamizi,” anataarifu Dakt. Harold Stigers katika kichapo chake Commentary on Genesis. Hata wachambuzi wa Biblia, kama John Van Seters, wanaukubali ushuhuda wa jambo hili. “Tatizo moja lisilotatuliwa ni mahali ambapo watu hawa walikwenda, ikiwa walikwenda mahali popote, mwishoni mwa kipindi hicho,” anataarifu katika kitabu chake Abraham in History and Tradition.
Mwanzo sura ya 14 inaandaa unaoweza kuwa utatuzi kwa tatizo hilo. Kulingana na orodha ya matukio ya Biblia, Abrahamu aliwasili Kanaani katika 1943 K.W.K. Ni lazima uvamizi wa Kedorlaoma wenye uharibifu uwe ulitokea muda mfupi baada ya hapo. Baadaye, katika karne iyo hiyo, Mungu alileta uharibifu wenye moto juu ya majiji yenye kukosa adili ya Sodoma na Gomora. Hii ikabadili milele mazingira ya Bonde la Yordani ya chini lililokuwa lenye rutuba. (Mwanzo 13:10-13; 19:24, 25) Likawa si kitu cha kutamaniwa tena na wavamizi wa kigeni.
Kuna vielelezo vingi vya jinsi uchimbuzi wa vitu vya kale unavyopatana sana na Maandiko kuangaza nuru juu ya matukio katika maisha ya Abrahamu. Lakini uchimbuzi wa vitu vya kale una mapungukiwa yao. Ushuhuda ambao unaandaa huwa mara nyingi si wa moja kwa moja na unaoweza kufanyiwa fasiri mbalimbali na wanadamu wasiokamilika.
Ushahidi Wenye Kutegemeka Zaidi
Uthibitisho imara zaidi kwamba Abrahamu alikuwako kikweli ni ushahidi wa Muumba wa mwanadamu, Yehova Mungu. Kwenye Zaburi 105:9-15, NW, Mungu alinena kwa kuwakubali Abrahamu, Isaka, na Yakobo kuwa “wanabii” wake. Zaidi ya miaka elfu moja baada ya kifo cha Abrahamu, Yehova Mungu alitaja Abrahamu kupitia kinywa cha angalau wanabii watatu, hata akimwita “rafiki” yake. (Isaya 41:8; 51:2; Yeremia 33:26; Ezekieli 33:24) Vilevile, Yesu Kristo alionyesha wazi kwamba Abrahamu ni kielelezo cha kufuatwa. Wakati Mwana wa Mungu alipokuwa mbinguni kabla hajawa mwanadamu, alikuwa amezishuhudia kwa macho yake binafsi shughuli za Baba yake pamoja na huyo mzee wa ukoo. Hivyo, angeweza kusema hivi kwa Wayahudi:
“ikiwa nyinyi ni watoto wa Abrahamu, fanyeni kazi za Abrahamu. Lakini sasa nyinyi mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye amewaambia nyinyi ukweli ambao nilisikia kutoka kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hivi. Abrahamu baba yenu alishangilia sana lile tazamio la kuona siku yangu, na yeye aliiona na akashangilia.’ Kwa hiyo Wayahudi wakasema kwake hivi: ‘Wewe hujawa na miaka hamsini, na bado umeona Abrahamu?’ Yesu akasema kwao hivi: ‘Kwa ukweli sana mimi nasema kwa nyinyi, Kabla Abrahamu hajapata kuwako, mimi nimekuwako.’”—Yohana 8:39, 40, 56-58, NW.
Tukiwa na ushahidi na kitia-moyo cha Watu wawili walio wakubwa zaidi katika ulimwengu wote mzima, sisi tuna sababu bora kabisa za kukubali kila jambo ambalo Biblia inataarifu juu ya Abrahamu. (Yohana 17:5, 17) Ingawa Biblia inamtokeza Abrahamu kuwa kielelezo cha kufuatwa, haimkwezi isivyofaa kuwa shujaa wa kitaifa. Hii inaweza kuonwa kwa kuchunguza usimulizi wa ushindi wake juu ya wale wafalme wanne wa muungano. Abrahamu aliporudi kutoka kwenye pigano, alilakiwa na Melkizedeki, mfalme wa Salemu, aliyesema hivi: “Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako”! Mwenye kusifiwa naye kwa ukombozi huo alikuwa ni Yehova.—Mwanzo 14:18-20.
Hata hivyo, ushindi mkubwa zaidi u karibu! Muda si muda, Mungu uyu huyu mtukufu atashinda “wafalme wa ulimwengu wote” kwenye vita ya duniani pote inayoitwa Har–Magedoni. (Ufunuo 16:14, 16) Hapo ndipo ahadi ya Mungu kwa Abrahamu, mnabii na rafiki yake, itapata utimizo kamili: “Kwa njia ya mbegu yako mataifa yote ya dunia kwa uhakika yatajibariki yenyewe.” Mamilioni wanaona shangwe kwa kuzionja mapema baraka hizo. Wewe unaweza kutiwa miongoni mwao, kama vile zitakavyoonyesha makala zinazoonekana katika kurasa 18-28 katika gazeti hili.—Mwanzo 22:18, NW.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Great Sea
THE NEGEB
Damascus
Haran
Euphrates River
Tigris River
Ur
ELAM
Persian Gulf
[Map]
Damascus
Dan
REPHAIM
ZUZIM
Shechem
Bethel
District of the Jordan
Salt Sea
Hebron
THE NEGEB
King’s Highway
EMIM
Gomorrah
Sodom
HORITES
[Picha]
Abrahamu alitii, akahama Uru, jiji lenye ufanisi sana
Kiolezo cha vifaa vya kuundwa vilivyotolewa katika Uru:
1. Upanga wa dhahabu na ala
2. ‘Beramu’ ya Uru
3. Kichwa cha ng’ ombe ndume wa dhahabu kutoka sanduku la kukuza mivumo ya kinubi
4. Johari
5. Vao la kichwani lililotiwa johari
[Hisani]
Picha za kupiga Kwa hisani ya Jumba la Makumbusho la Uingereza