Kutumikia Msanii Aliye Mkubwa wa Wote
NIKIWA msichana mchanga wa miaka saba, nilianza kujiuliza hivi: ‘Kwa nini itakuwa lazima nife? Je! yawezekana kuepuka kifo?’ Nilikuwa nimeambiwa kwamba Mungu huchukua watu wema kwa sababu huwataka wawe naye mbinguni. Bado nakumbuka mmoja wa wanadarasa wenzangu akipaaza mshangao huu: “Ni afadhali kuwa mtu mbaya kwa sababu watu wema ndio hufa kwanza!”
Nilipenda kuchora, kwa hiyo nikaanza kujifunza sanaa. Shuleni, sikuwa na fursa ya kufikiria mambo ya kidini, wala wakati wa kupendezwa nayo. Kwa uhakika, nilikuwa nikiambia rafiki zangu kwamba ili mtu awe wa kidini, alihitaji elimu ya kiwango cha chini. Nilipomaliza mafunzo yangu ya sanaa, nilipewa cheo cha kuwa mwalimu wa sanaa katika shule ya sekondari.
Nilipenda kazi yangu na kupendezwa pia na Kiitalia na fasihi za kigeni, muziki chemba (wa waimbaji wachache) na simfoni (wa waimbaji wengi), na opera (wa kitamthilia). Jambo moja tu la kidini nililojifunza katika kipindi hicho lilikuwa habari za wanaikonografia (wachoraji taswira za kidini) wa enzi mbalimbali. Ndipo nikapata kujua mtu huhisi namna gani akiwa ndiye mwenye kukaziwa fikira zote, jinsi yeye huhisi anapotandika kazi zake zikaguliwe na watu, jinsi mambo yalivyo katika kustahiwa sana, kusifiwa, na kustaajabiwa ukiwa msanii.
Wakati huo, ulimwengu wa sanaa ulinivutia sana, kwa kuwa humo ndimo nilipata sababu ya sehemu kubwa zaidi ya mimi kuwa hai. Lakini maswali niliyokuwa nimetokeza nilipokuwa na miaka saba yalikuwa yangali katika akili yangu. Niliendelea tu kutafuta kitu cha kina kirefu zaidi, kitu ambacho bado sikukielewa. Nilikuwa msomaji mwenye bidii na niliwaomba wanafalsafa maelezo. Kwa vyovyote, nilitaka jibu hususa kwa shaka zangu.
Nilikuwa bado na mvurugiko huu nilipofunga ndoa. Baada ya kuzaliwa kwa binti yangu, utafutaji wangu wa ukweli ukaongezeka hata zaidi. Nilijaribu kuupata kwa upakaji-rangi picha, uandikaji mashairi, kusikiliza muziki, kusoma vitabu. Wakati wowote nilipohudhuria tumbuizo la muziki na kusikiliza utangulizi wa mitungo ya muziki, moja kwa moja nilifikiria Mungu, Aliye Mkuu Zaidi ambaye sikumjua, nami nikamshukuru. Katika kipindi hicho, nilikuwa nikisifu Mungu mara nyingi kwa vitu vya kupendeza sana nilivyovistaajabia—kitoto changu chenye kulala, rangi za mandhari ya nchi. “Ni vibaya kama nini,” mimi nikawa nikipaaza mshangao, “kwamba sanaa hiyo, ambayo ingeweza kuwa na vitu vingi sana vya kupendeza, hutumiwa sana kusimulia kifo badala ya uhai!” Baadhi ya mashairi na tamthilia zilizotungwa kwa usanifu mkubwa zaidi huwa ama ni nyimbo za huzuni au za tanzia; baadhi ya picha za upakaji-rangi ulio stadi kabisa hutukuza kifo badala ya uhai na urembo wao. Kwa nini?
Mawazo haya yasiyopatana yalinivunja moyo sana, na kidato kwa kidato nikaanza kuingilia hali ya kutojali lolote. Hapo ndipo Mashahidi wa Yehova walikuja mlangoni pangu. Nilipokuwa nikiwasikiliza, ikawa ni kama walikuwa wakiongea nami lugha mpya, Ahadi ya Mungu kufanya dunia iwe paradiso ilisikika kama muziki mtamu kwenye masikio yangu. Nilianza kusoma Biblia. Humo mwishowe nikapata majibu ya maswali ambayo nilikuwa sijaacha kuuliza tangu nilipokuwa na miaka saba. Mungu hataki mwanadamu afe bali madhumuni yake ni kubariki watumishi wake waaminifu kwa kuwapa uhai wa milele duniani!
Hiyo ilikuwa 1973. Mwaka uliofuata nilijiweka wakfu kwa Yehova na kubatizwa. Haikuwa rahisi kukibadili kitabia changu cha kushtukia mambo na kuongozwa na hisia-moyo na badala yake kuwa mwenye roho ya upendo wa kweli wa kidugu, badala ya kuwa mtu asiye na ubinafsi, na badala ya starehe ya kibinafsi kuwa na roho ya kujidhabihu! Ilikuwa lazima nijikane. Mashahidi wa Yehova wamesaidia sana, na ndivyo mikutano ifanywayo katika Jumba la Ufalme.
Msanii Mkuu ameondoa kabisa shaka zangu na mahangaiko. Mimi namshukuru we! Ndiyo sababu, tangu Septemba 1984, nimechukua utumishi wa painia wa kawaida, nikitumia saa 90 kila mwezi katika kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu.
Kutumikia Msanii Mkuu na Muumba, Yehova, pamoja na jamaa yangu ni jambo la kuridhisha kweli kweli. Sisi twaungojea kwa hamu wakati ambapo atachora picha iliyobainika zaidi; wakati ambapo hatimaye ataondoa mfumo wa kale ulio mbovu ambao umetia dosari na kufunika dunia hii. Kifo hakitakuwapo tena, na wakati huo sanaa itahusisha uhai tu. Wakati huo, urembo tu ndiyo utachorwa, kwa maana kwa njia ya mfumo mpya wa Mungu ulio mwadilifu, majonzi na maumivu yatakuwa yamekomeshwa milele.—Imechangwa.