Kumtumikia Yehova Katika Majira Yenye Kupendeleka na Katika Yenye Matata
Kama ilivyosimuliwa na Hal Bentley
MATAYARISHO yalikuwa yamefanywa kwa ajili ya kusanyiko la mzunguko la Mashahidi wa Yehova katika kijiji kidogo cha Nyasaland (sasa Malawi). Waangalizi wa mzunguko na wilaya walikuwa wakifanya ukaguzi wao wa mwisho kwenye lile jukwaa la nyasi na mianzi na kwenye vijumba vya nyasi vya kutumiwa kwa malazi. Kwa ghafula, wakazungukwa na wafanya ghasia waliokuwa wamejificha katika kichaka cha hapo karibu. Wafanya ghasia hao waliviwasha moto vijumba hivyo na jukwaa na kulazimisha ndugu hao wawili kuelekea kwenye nyumba ambako walikuwa wakikaa.
Mke wa mwangalizi wa wilaya, Joyce Bentley, alikuja mbio aone lililokuwa likitukia. Yeye pia akasukumwa arudi alikotoka. Kiongozi wa wafanya ghasia hao alipaaza sauti kwamba ni lazima mzungu aondoke mara iyo hiyo. Wafanya ghasia hao hawakutaka kuturuhusu tuchukue mali zetu na walitulazimisha kuingia katika Land-Rover yetu. Wakasongamana kuzunguka gari hilo—wanaume, wanawake, na watoto—wakipiga makelele kwamba “Pitani mzungu” (Nenda, mzungu) na “Kwacha” (Uhuru). Tuliwatarajia waipindue Land-Rover na kwa hiyo tukasali kwa Yehova kwa ukimya. Lakini umati huo ukapungua-pungua, nasi tukaenda zetu kwenye kituo cha polisi cha karibu zaidi, kule Mzimba, umbali upatao kilometa 50.
Baadaye tulirudi, tukiandamana na ofisa mmoja tu wa polisi. Kwa sababu ya matata mahali pengine pengine, yeye peke yake ndiye angeweza kuachwa aje. Tulipowasili mahali tulipokuwa tumeghasiwa, tulikuta bendera ya Malawi Congress Party (Chama cha Kongresi cha Malawi) ikiwa inapeperuka na herufi M.C.P. zikiwa zimekwaruzwa kwenye ukuta wa matope. Hata hivyo, baada ya polisi huyo kusema na watu wa hapo, walituruhusu tupakie mali zetu katika ile Land-Rover.
Pia tulimkuta mwangalizi wa mzunguko, Rightwell Moses, na pia mke wake. Mke wake alikuwa amekimbia kichakani wakati wa ghasia hiyo. Lakini Rightwell alinusurika kuzamishwa katika mto wa hapo karibu. Pia wafanya ghasia walikuwa wamechukua chakula chote cha kusanyiko. Halafu wakawafanya akina ndugu wapige miguu kuelekea upande mmoja huku akina dada na watoto wakielekea upande ule mwingine kwa kilometa kadhaa mpaka wafanya ghasia hao walipochoka na kuwaacha.
Kituko hiki kilikuwa kimoja cha vingi ambavyo vilifikia upeo katika kupigwa marufuku kwa kazi katika Malawi, nayo ikaongoza kwenye mnyanyaso mkali wa Mashahidi wa Yehova, kutia na visa vya kuuawa, kupigwa kikorofi, kuingilia wanawake kinguvu, na kutiwa gerezani.
Kwa Nini Tulikuwa Malawi?
Siku ya Juni 28, 1916, mimi nilizaliwa katika jiji la Leeds, katika Yorkshire, Uingereza, nikiwa ndimi mtoto mchanga zaidi wa familia ya watoto watano. Hatukuwa familia ya kidini na hatukuhudhuria kanisa.
Kufikia 1939, Vita ya Ulimwengu 2 ilipotokea, wazazi wangu wote wawili wakawa wamekufa. Katika Juni 1940, nilipokuwa na miaka 24 tu, nikawa nimevaa mavazi ya jeshi, na kwa miaka mitano iliyofuata, nikatumikia katika vikosi mbalimbali vyenye kuhusika na mashine. Wakati wa miaka hiyo, nilipokuwa nimeketi katika vituo vya bunduki za kumimina risasi katika pwani ya kaskazini-mashariki ya Uingereza na kutazama juu kwenye anga lenye nyota, mara nyingi nilipata pindi ya kufikiria Mungu na kushangaa ni kwa nini Mfanyi wa uzuri huu wa kuvutia angeruhusu jeuri, umwagaji damu, na mteseko wa jinsi hiyo miongoni mwa ainabinadamu. Haikuwa mpaka niliporuhusiwa kutoka jeshini kwamba nikapata jibu la maswali mengi yaliyokuwa yamenitatanisha kwa muda mrefu.
Jioni moja ya kipupwe chenye baridi mwaka huo, mtu fulani alibisha hodi mlangoni pangu. Nilipofungua nikakuta mwungwana mzee-mzee aliyeanza kuongea juu ya Biblia. Hiyo ikaongoza kwenye funzo la Biblia na muda si muda kwenye ubatizo wangu katika Aprili 1946. Katika 1949 niliacha kazi yangu nikawa mhudumu painia wa Mashahidi wa Yehova.
Ndipo nikatumikia kwenye Betheli ya London kwa miaka zaidi ya mitatu, na katika 1953 nikaalikwa kuhudhuria darasa la 23 la Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi katika South Lansing, New York, nikazoezwe kuwa misionari. Baada ya muda, nilianza mgawo wa kimisionari katika ile iliyokuwa Nyasaland wakati huo. Baadaye nikatumwa nje katika kazi ya wilaya. Kwa miaka mitano niliyasafiri mapana na marefu ya nchi hiyo nzuri nikiwa kijana mseja. Nikaja kuwapenda watu wa huko, waliokuwa wenye furaha na wakaribisha-wageni sana hata ingawa walio wengi hawakuwa na vitu vingi vya kimwili isipokuwa vishamba vyao vya mahindi, kuku wachache, na mbuzi au nguruwe. Baadhi yao walikuwa wavuvi hodari. Nilikaa nao katika makao yao yaliyojengwa kwa miti na matope na kutembea nao katika kazi ya kuhubiri kijiji kwa kijiji. Pia niliuonea shangwe ushirika wao kwenye makusanyiko ya nje peupe, ambapo wao wangeketi pamoja na familia zao huku wakielekeza uangalifu wa makini kwa wasemaji, hata ingawa nyakati fulani mvua ilikuwa ikimwagika kweli kweli!
Nilipokaa katika kijiji, kila mtu, wachanga kwa wazee, walikuwa wakija na kila mmoja kunisalimu, akisema: “Moni, muli bwanji?” (Habari, u mzima?) Hata nilipotembea kijiji kwa kijiji, watu walikuwa wakiacha kulima mashamba kwa majembe yao na kupaaza sauti kunisalimu.
Kila kundi nililozuru pamoja na mwangalizi wa mzunguko lingejenga nyumba kwa ajili yangu hasa. Nyakati fulani ingekuwa imara ikiwa imefanyizwa kwa miti yenye paa iliyoezekwa nyasi, nami nilithamini sana hilo. Lakini nikagundua kwamba muda fulani hupita kabla paa iliyoezekwa nyasi karibuni kuwa isiyovuja maji!
Wakati mmoja akina ndugu walinijengea nyumba iliyofanyizwa kwa nyasi-tembo nene bila kuongezea kitu kingine chochote. Ilikuwa ya pande tatu, huku Land-Rover yangu ikiwa ndio upande wa nne. Hiyo ilikuwa katika bonde la Mto Shire, ambako huwa kwenye joto mwaka wote, nao mbu hupokezana zamu ya kazi, kwa usemi wa kitamathali, bila kupumzisha mtu sio mchana sio usiku! Kwa maana sikuwa na neti ya mbu wala dawa ya kuwafukuza, ilikuwa ni kama haiwezekani kuendelea.
Mwenzi wa Maisha Ajiunga Nami
Katika 1960 mke mgeni, Joyce Shaw, aliyekuwa amekuwa akitumikia akiwa misionari katika Ekwadori alijiunga nami. Ndiyo, baada ya kuionea shangwe zawadi ya useja kwa miaka kadhaa, nilibarikiwa kwa zawadi nyingine—ndoa—ambayo ningali naithamini sana baada ya miaka 30. Joyce na mimi tumebarikiwa kwa maono mengi ya kusisimua tukiwa pamoja.
Katika pindi moja, kwa kutumia miti na nyasi, akina ndugu walijenga daraja la kuvuka kijito. Hilo lilifanywa ili niweze kuvuka kwenda kwenye kijiji ambako walinitaka nionyeshe filamu ya Sosaiti “Sosaiti ya Ulimwengu Mpya Katika Kitendo.” Lakini trela (sehemu yenye kukokotwa nyuma) ya Land-Rover yangu ilikwamishwa na mti fulani darajani. Bila kutishika, akina ndugu wakaifungashua trela, hiyo ikiniruhusu niendeshe gari kuondoka darajani, halafu wakafanya maarifa kuvusha trela ng’ambo. Tulifanikiwa kuonyesha filamu.
Nyakati fulani mito ilikuwa mipana mno isiweze kujengewa daraja. Hapo akina ndugu wangeondoa kila kitu kwenye Land-Rover—jenereta ya kubebwa, projekta, filamu, kitanda—na kwa shida nyingi tukapasua mwendo mtoni, huku mimi nikisafirishwa juujuu kwenye mabega imara ya mmoja wa akina ndugu. Dada wawili wangebeba Joyce kumvusha ng’ambo. Mito fulani ilikuwa na kina kirefu mno. Tuliivuka kwa kivuko cha utumizi wa muda kilichofanyizwa kutokana na jukwaa la magogo likiwa juu ya mapipa makubwa manane hadi kumi. Ndipo wanaume wawili wa kuvuta kivuko wangetuvusha ng’ambo kwa kamba.
Ndugu wa Malawi walikuwa wenye msaada na wafadhili kabisa na walitutendea kwa staha ya kina kirefu. Mahali pamoja watu wa huko walikuwa wametisha kuteketeza nyumba tulimokuwa tukikaa, kwa hiyo akina ndugu wakakesha usiku kucha ili kuhakikisha usalama wetu. Hata kabla ya marufuku kupigwa juu ya Mashahidi wa Yehova katika 1967, kulikuwako hali zenye hatari, kutia na ile iliyosimuliwa mwanzoni mwa hadithi hii. Wengi wa ndugu na dada wa Malawi wangalitoa uhai wao kwa ajili yetu.
Katika pindi moja mimi nilifanya kazi nyumba kwa nyumba pamoja na ndugu mmoja aliyekuwa na uvimbe mkubwa kwenye kipaji cha uso. Alikuwa amepigwa vibaya sana siku chache mapema. Kwenye nyumba moja alimtolea mwenye nyumba ushahidi mzuri kwa utulivu. Baada ya kuondoka, ndugu huyo akasema hivi: “Jamaa huyo ndiye aliyenipiga vibaya hivi!” Mimi nikakumbuka maneno ya Paulo: “Msimlipe mtu ovu kwa ovu . . . Uushinde ubaya kwa wema.”—Warumi 12:17-21.
Kupanua Utumishi Wetu
Tukiwa bado Malawi, Joyce na mimi tulifanya ziara za mara kwa mara kwenda Msumbiji iliyo hapo karibu. Maarifa ya Joyce ya Kihispania, aliyojipatia akitumikia katika Ekwadori, yalisaidia, kwa kuwa Wareno wa huko wangeweza kumwelewa. Baada ya muda sisi wawili tuliweza kuongea katika Kireno. Tuliendelea kuzuru Msumbiji tukiwa kwenye mgawo wetu uliofuata, Zimbabwe. Kanisa Katoliki lilipinga vikali kazi ya kuhubiri na likachochea matata. Lakini katika miaka kumi iliyofuata, tulijionea mara nyingi utunzi na ulinzi wenye upendo wa Yehova tulipokuwa tukitafuta huko watu walio kama kondoo.
Wakati wa moja ya ziara zetu za kwenda Msumbiji, tulizuru bibi mmoja mwenye kupendezwa kaskazini ya bandari ya Beira. Dada yake katika Ureno alikuwa amemwandikia na kusimulia baadhi ya mambo mazuri ajabu aliyokuwa amejua kwa kujifunza na Mashahidi wa Yehova. Bibi huyo akawa ameyachunguza katika Biblia yake na hata akaanza kuambia jirani zake juu yayo. Hata hivyo anwani pekee tuliyokuwa nayo ilikuwa jina la gereji ambako mume wake alifanya kazi.
Tulipokuwa tukikaribia mwingilio wa karakana hiyo, mwanamume mmoja akauliza kama angeweza kutusaidia. Tukasema tungependa kuona mume wa yule bibi. Akaelekeza kidole kwenye mekanika mwenye kutengeneza gari fulani na akatuacha kwa ghafula. Sisi tukajijulisha kwa mekanika huyo na kusema tungependa kuzuru mke wake. Alibabaika sana. Alipokuwa akitusindikiza kwenye nyumba yake, akaeleza kwamba mwanamume tuliyekuwa tumesema naye kwanza alikuwa ameshika njia ili akaripoti kwa chifu wa hapo wa P.I.D.E. (polisi wa siri) kwamba tumewasili. Kumbe tulikuwa tumeingia mtegoni! Pia akaeleza kwamba mke wake, kwa sababu ya utendaji wake wa kuhubiri, alikuwa amekuwa chini ya uchungulizi wa polisi kwa muda fulani na kwamba wao walikuwa wameinasa barua yenye kumwambia kwamba sisi tunakuja kumzuru. Wakawa wamechukua Biblia yake, lakini kwa hekima akawa ameficha mbali Biblia nyingine! Pia wakawa wamemleta askofu Mkatoliki ajaribu kumsihi mke wake aache kuongea juu ya Yehova na Ufalme!
Tulipomkuta bibi huyo mwenye kupendezwa, alizongwa na hisia akajitupa kumkumbatia Joyce. Alimsihi sana mume wake aturuhusu tukae nao, lakini yeye akakataa na kurudi kazini. Tulitumia ziara hiyo fupi kwa faida nyingi kabisa, tukimpa kitia-moyo kutoka katika Biblia na kumpongeza kwa kuchukua msimamo imara hivyo. Ili kuepuka kumsababishia matatizo zaidi, tuliondoka lakini tukaahidi kurudi baadaye hali ikiisha kuwa nafuu. Tulipokuwa tukiondoka kwenye nyumba hiyo na pia kujaza petroli katika tangi la gari letu kwenye gereji, tukaona kwamba tulikuwa tukitazamwa, lakini hatukukamatwa. Halafu tukasonga mbele kwenda Beira na kuzuru kundi dogo la huko kabla ya kurudi Zimbabwe. Miezi kadhaa baadaye tulirudi na tukaweza kuwa na shangwe ya kula mlo mmoja pamoja na bibi yule mwenye kupendezwa na mume na binti yake. Mwishowe bibi huyo alibatizwa wakati wa ziara moja ya kwenda Ureno na akawa mhubiri wa Ufalme mwenye bidii.
Mbali zaidi kaskazini tulifanya mara nyingi ziara za kwenda mahali mbalimbali kama vile Quelimane, Nampula, na Nacala, bandari ndogo. Huko Nacala tulizuru mara nyingi familia ya akina Soares. Bw. Soares alikuwa kwanza amesikia juu ya ukweli katika Ureno. Lakini alipohamia Msumbiji, akina ndugu katika Lourenço Marques (sasa Maputo), mji mkuu wa Msumbiji, walijifunza pamoja naye na familia yake. Wao walithamini sana kwamba sisi tulikuwa tayari kusafiri mamia ya kilometa kuzuru jamaa iliyo peke yayo. Walifanya maendeleo mazuri. Baadaye wakahamia Afrika Kusini, ambako yule binti, Manuela, anatumikia Betheli akiwa mtafsiri wa Kireno.
Tulizuru kundi la huko Lourenço Marques mara nyingi. Hiyo ilihusisha ndani safari ya kilometa zaidi ya 1,100 kutoka Blantyre kwa kupita katika barabara mbaya-mbaya. Mara mbi-li tulipata matatizo makubwa ya gari na kulazimika kukokotwa hadi Salisbury (sasa Harare). Hata hivyo ilikuwa shangwe kubwa kuona kile kikundi kidogo katika Lourenço Marques kikikua kikawe kundi zuri wajapofanya kazi chini ya marufuku. Makusanyiko ya mzunguko madogo yalifanywa kwa ukawaida. Lakini ilikuwa lazima yaendeshwe vichakani kana kwamba akina ndugu walikuwa kikundi kikubwa chenye shangwe ya kufanya mandari (pikniki) tu. Katika pindi kadhaa kusanyiko lilipangwa ng’ambo ya mpaka kule Nelspruit katika Afrika Kusini. Hiyo ilisaidia ndugu wa Maputo kuthamini tengenezo la Yehova na kukua kiroho.
Kundi la Beira pia liliimarika. Kwa sababu ya misukosuko ya kisiasa katika Msumbiji, akina ndugu kutoka nchi hiyo sasa wametapakaa katika Ureno, Afrika Kusini, Kanada, Brazili, United States, na mahali penginepo. Sifa yote yamwendea Yehova, ambaye ‘aliikuza mbegu.’ (1 Wakorintho 3:6, 7) Ndiyo, kwa miaka kumi tulikuwa na pendeleo la kutoa usaidizi kwa akina ndugu katika Msumbiji wakiwa chini ya utawala wa Kireno. Tunapotazama nyuma, twastaajabia jinsi Yehova alivyotufungulia mlango ili tufanye hivyo.
Katika pindi moja, tulipokuwa tukizuru Nampula kule kaskazini, tulikamatwa na mshiriki wa P.I.D.E. Fasihi zetu zote, kutia na Biblia, zilichukuliwa, nasi tukaambiwa hatungeruhusiwa kamwe kurudi Msumbiji. Ijapokuwa hivyo, kwa msaada wa Yehova tuliweza kufanya ziara nyingi zaidi ndani ya nchi hiyo. Kila wakati tulipofika mpakani, tulikuwa tukiomba msaada na mwongozo wake ili tuweze kutimiza mapenzi yake na kuwapa ndugu zetu kitia-moyo na mazoezi yaliyohitajiwa sana katika bara hilo.
Katika 1979 tulihamishwa tukapelekwa Botswana. Ina eneo kubwa la bara, karibu nusu ya ukubwa wa Afrika Kusini. Kwa kuwa eneo kubwa sana ni jangwa, lile la Kalahari, wakaaji ni wachache kuliko milioni moja. Hapa sisi tumekuwa na mapendeleo ya kusaidia kujenga Jumba la Ufalme moja na makao ya kimisionari katika Gaborone, mji mkuu. Pendeleo jingine limekuwa kusaidia wakimbizi wenye kusema Kireno waliotoka Angola na kujifunza Biblia pamoja nao.
Pia tuliweza kusaidia vijana kadhaa wa kutoka Zimbabwe. Yaonekana kwamba katika nchi hii jirani, Mashahidi wa Yehova, kwa mpango maalumu, waliruhusiwa kufundisha Maandiko katika shule fulani-fulani. Hiyo iliamsha upendezi katika vijana hawa. Walipohama baadaye kwenda Botswana, tuliwafikia, nao wakatuomba funzo la Biblia. Hata hivyo, wazazi wao walipinga na kwa hiyo wao wakalazimika kuja kwenye makao ya wamisionari ili kujifunza. Walifanya maendeleo mazuri wakawa Mashahidi waliobatizwa.
Mimi nitazamapo nyuma kwenye miaka 41 ya utumishi wa wakati wote katika nchi nane, nahisi shukrani za kina kirefu kwa Yehova kwa ajili ya baraka nyingi nilizozionea shangwe. Imekuwa si rahisi, lakini imekuwa shangwe kubwa kwa Joyce na mimi kusaidia wengi wachukue msimamo imara kwa ajili ya Ufalme na kuona maendeleo yale mazuri kujapokuwako matatizo mengi na upinzani mgumu. Kwa kweli kimekuwa ni kisa cha ‘kulihubiri neno, na kufanya hima kuwa kwenye hilo katika majira yenye kupendeleka na katika majira yenye matata.’ Ndiyo, utumishi wa wakati wote ni maono yenye manufaa nyingi na pendeleo kubwa ambalo sisi twalipendekeza kwa moyo kwa wale wawezao kurekebisha maisha zao ili walionee shangwe.—2 Timotheo 4:2, NW.
[Ramani katika ukurasa wa 21]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
AFRIKA KUSINI
ANGOLA
ZAMBIA
MALAWI
BAHARI KUU YA HINDI
MSUMBIJI
Mzimba
Blantyre
Nacala
Beira
Maputo
ZIMBABWE
Harare
NAMIBIA
BOTSWANA
Gabarone
600 km
400 mi
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Mito ilipokuwa na kina kirefu mno, wanaume wawili wa kuvuta kivuko wangetuvusha ng’ambo kwa kamba