Maisha na Huduma ya Yesu
Yesu Yu Hai!
WANAWAKE wapatapo ziara la Yesu likiwa tupu, Mariamu Magdalene akimbia kuambia Petro na Yohana. Hata hivyo, wanawake wale wengine kwa wazi wabaki kwenye ziara. Muda si muda, malaika atokea na kuwaalika ndani.
Hapa wanawake waona malaika mwingine bado, na mmoja wa malaika hao asema hivi kwao: “Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa [aliyetundikwa mtini, NW]. Hayupo hapa; kwani amefufuka, kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu.” Hivyo basi wakiwa na hofu na shangwe kubwa, wanawake hawa wakimbia kwenda zao.
Kufikia wakati huu, Mariamu amewapata Petro na Yohana, naye aripoti kwao hivi: “Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka.” Mara hiyo wale mitume wawili waondoka mbio. Yohana ni mwepesi zaidi wa miguu—yaonekana kwa kuwa ni mchanga zaidi—naye afika kwanza kwenye ziara. Kufikia wakati huu wale wanawake wameondoka, hivyo basi hapo hapana mtu. Akiinamia chini, Yohana achungulia ndani ya ziara na kuona vile vitambaa vya kufungilia, lakini abaki nje.
Petro awasilipo, hasitisiti bali aingia moja kwa moja. Aona vitambaa vya kufungilia vimelala hapo na pia ile nguo iliyotumiwa kufunga kichwa cha Yesu. Imekunjwa mviringo ikawekwa mahali pamoja. Sasa Yohana pia aingia ndani ya ziara, naye aiamini ripoti ya Mariamu. Lakini wala Petro wala Yohana haelewi kwamba Yesu ameinuliwa, hata ingawa Yeye alikuwa amewaambia mara nyingi kwamba angefanyiwa hivyo. Kwa kushangaa sana, wawili hao warudi nyumbani, lakini Mariamu, ambaye amerudi kwenye ziara, abaki.
Wakati wa sasa, wale wanawake wengine wanafanya haraka kuwaambia wanafunzi kwamba Yesu amefufuliwa, kama vile malaika walivyowaamuru kufanya. Wanapokuwa wakikimbia upesi wawezavyo, Yesu awakuta na kusema hivi: “Salamu!” Wakianguka miguuni pake, wamfanyia ushikamoo. Halafu Yesu asema hivi: “Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
Mapema kidogo, wakati tetemeko la dunia lilipotukia na malaika wakatokea, askari wenye ulinzi waliduwaa wakawa kama wanaume wafu. Waliporudiwa na fahamu, waliingia jijini mara hiyo wakawaambia wakuu wa makuhani yaliyokuwa yametendeka. Baada ya kushauriana na “wazee” wa Wayahudi, uamuzi wafanywa kujaribu kunyamazisha jambo hilo kwa kuwahonga askari. Wao waagizwa hivi: “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.”
Kwa kuwa askari Waroma waweza kuadhibiwa kwa kifo kwa sababu ya kulala usingizi wakiwa kwenye vituo vyao, makuhani waahidi hivi: “Neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi.” Kwa kuwa ukubwa wa hongo hilo ni wa kadiri ya kutosha, askari wafanya kama waagizwavyo. Tokeo ni kwamba, hiyo ripoti bandia juu ya wivi wa mwili wa Yesu yaenea kotekote miongoni mwa Wayahudi.
Mariamu Magdalene, ambaye abaki nyuma kwenye ziara, ashindwa na kihoro. Yesu angeweza kuwa wapi? Akiinamia mbele atazame ndani ya ziara, aona wale malaika wawili waliovaa meupe, ambao wametokea tena! Mmoja ameketi kichwani na mwingine miguuni pa mahali ambapo mwili wa Yesu umekuwa ukilala. “Mama, unalilia nini?” wao wauliza.
“Wamemwondoa Bwana wangu,” Mariamu ajibu, “wala mimi sijui walikomweka.” Halafu ageuka na kuona mtu fulani ambaye arudia swali hilo: “Mama, unalilia nini?” Na huyu pia auliza hivi: “Unamtafuta nani?”
Akiwazia mtu huyu kuwa ndiye mtunzi wa bustani ambamo ziara limo, amwambia hivi: “Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.”
“Mariamu[!]” asema mtu huyo. Naye ajua mara hiyo, kutokana na njia ya kuzoeleana ambayo yeye huongea naye, kwamba ni Yesu. “Raboni!” (maana yake “Mwalimu!”) mwanamke huyo apaaza sauti. Na kwa shangwe isiyo na mipaka, amshika sana Yesu. Lakini Yesu asema: “Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.”
Sasa Mariamu akimbia kwenda mahali ambapo mitume na wanafunzi wenzi wamekusanyika. Aongezea usimulizi wake kwenye ripoti ambayo wale wanawake wengine wametoa tayari juu ya kumwona Yesu mfufuliwa. Hata hivyo, wanaume hawa, ambao hawakuwaamini wale wanawake wa kwanza, yaonekana hawamwamini hata Mariamu. Mathayo 28:3-15; Marko 16:5-8; Luka 24:4-12; Yohana 20:2-18.
◆ Baada ya kupata ziara likiwa tupu, Mariamu Magdalene afanya nini, na wale wanawake wengine wajionea nini?
◆ Petro na Yohana waitikiaje wapatapo ziara likiwa tupu?
◆ Wale wanawake wengine wakuta nini wakiwa njiani kwenda kuripoti kwa wanafunzi juu ya ufufuo wa Yesu?
◆ Ni jambo gani lawapata askari walinzi, na ripoti yao kwa makuhani yapata itikio gani?
◆ Ni jambo gani latendeka Mariamu Magdalene awapo peke yake kwenye ziara, na ni nini itikio la wanafunzi kwa ripoti za wanawake hao?