Hati-kunjo Za Baharifu Hazina Isiyo na Kifani
CHINI ya Wadi Qumrani, upande wa kaskazini-magharibi wa Baharifu, kuna magofu ya kale. Yakiwa yamedhaniwa kwa muda mrefu kuwa mabaki ya ngome ya Kirumi, yalikuwa yamepata uangalifu mdogo sana kutoka kwa waakiolojia. Hata hivyo, uvumbuzi wa hati-kunjo ya Baharifu ya Isaya katika 1947, ulichochea kufikiria tena juu ya mahali hapo.
Upesi wanachuo walitambulisha majengo hayo kuwa mali ya jumuiya ya kidini ya Wayahudi. Dhana ya mara moja ilikuwa kwamba watu hawa walikuwa wamezificha hati-kunjo hizo katika pango miongoni mwa magenge yaliyokuwa karibu. Lakini mavumbuzi ya baadaye yalionekana kuwa yalitilia shaka jambo hilo.
Pato Lisilo na Kifani
Mabedui walikuwa macho kwa thamani ya hati walizokuwa wamepata tayari. Kwa hiyo, katika 1952, utafutaji mpya ulianza wakati mwanamume mzee mmoja aliposimulia kwamba akiwa kijana alikuwa amefuata kwale ambaye alikuwa ameumia hadi alipotoweka ndani ya shimo katika uso wa mwamba, ambamo alipata vyombo vya udongo na taa ya kale ya mafuta.
Yule mwanamume mzee bado aliweza kutambulisha mwingilio wa pango miongoni mwa nyufa zenye kina kirefu za genge lenye miteremko ya ghafula. Lilipatikana kuwa pango lililotengenezwa na wanadamu, linalojulikana sasa kuwa Pango 4. Hapo Mabedui walipata sehemu za hati-mkono meta moja hivi chini ya usawa wa sakafu iliyokuwako wakati huo. Hakuna yoyote ya sehemu hizo iliyokuwa imewekwa katika mitungi, kwa hiyo nyingi zazo zilikuwa zimeharibika vibaya, zikawa nyeusi, na kuwa dhaifu. Wakati ulipopita vijipande 40,000 hivi vilipatikana, vikiwakilisha hati karibu 400. Vitabu vyote vya Maandiko ya Kiebrania, kutotia cha Esta, viliwakilishwa miongoni mwa hati-mkono za Biblia mia moja. Vifaa vingi vilivyopatikana kutoka Pango 4 havijachapishwa bado.
Moja ya hati-mkono zilizo za maana zaidi ilikuwa ile ya vitabu vya Samweli, iliyonakiliwa katika kunjo moja. Mwandiko wayo wa Kiebrania, uliohifadhiwa katika safu 47 kutoka kwa labda 57, unafanana sana na ule uliotumiwa na watafsiri wa fasiri ya Septuagint ya Kigiriki. Pia kuna vijipande vya Kigiriki vya Septuagint kutoka Walawi na Hesabu vinavyorudi tarehe ya nyuma ya karne ya kwanza K.W.K. Hati ya Walawi inatumia IAO, kwa יהרה, ya Kiebrania, jina la kimungu la Mungu, badala ya Kyʹri·os, “Bwana,” ya Kigiriki.a
Katika kijipande kutoka Kumbukumbu la Torati, mwandiko wa Kiebrania unatia ndani sehemu kutoka sura 32, mstari 43, inayopatikana katika Septuagint na kunukuliwa katika Waebrania 1:6 hivi: “Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.” Huu ndio wakati wa kwanza mstari huu umepatikana katika hati yoyote ya Kiebrania, ikifunua mwandiko ambao kwa wazi ni wenye msingi wa tafsiri ya Kigiriki. Hivyo wanachuo wamepata mwono-ndani mpya ndani ya mwandiko wa Septuagint, ambao unanukuliwa mara nyingi katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.
Hati-kunjo ya Kutoka imewekewa tarehe kuwa ni ya robo ya tatu ya karne ya tatu K.W.K., moja ya Samweli kuwa ni ya mwisho wa karne iyo hiyo, na hati-kunjo ya Yeremia katikati ya 225 na 175 K.W.K. Mambo ya kutosha kutoka karne ya tatu hadi karne ya kwanza K.W.K. yamepatikana ili kufuatisha mabadiliko katika mitindo ya kuandika na herufi moja moja ya herufi za Kiebrania na Kiaramu, jambo lenye maana sana katika kupa hati tarehe.
Mshangazo wa Pango 11
Hatimaye, eneo zima kuzunguka Qumrani lilikuwa limechunguzwa kikamili, na Mabedui na waakiolojia pia. Hata hivyo, siku moja katika 1956, Mabedui fulani waliona popo wakitokea kwenye nyufa ndogo katika magenge kaskazini mwa Pango 1. Walipanda juu na kupata pango jingine, ambalo mwingilio walo ulikuwa umezibwa. Tani mbili za miamba iliyokuwa imeanguka zilipasa ziondolewe ili kulifunua. Mapato yaliyokuwa ndani yalistaajabisha—hati-mkono kamili mbili na sehemu kubwa tano za nyinginezo.
Pato lenye maana zaidi lilikuwa hati-kunjo ya Zaburi yenye kupendeza. Unene wa ngozi unadokeza kwamba labda ni ngozi ya ndama wa ng’ombe badala ya ngozi ya mbuzi. Jumla ya kurasa tano, kurasa mbalimbali nne, na vijipande vinne, vinaipa urefu wa zaidi ya meta 4. Ingawa sehemu ya juu ya hati-kunjo hiyo imehifadhiwa vizuri, sehemu ya chini kabisa imeharibika sana. Tarehe yayo ilikuwa kutoka nusu ya kwanza ya karne ya kwanza W.K. na ina sehemu za zaburi 41. Tetragramatoni imeandikwa mara 105 hivi katika herufi za zamani za Kiebrania, hiyo ikiifanya itokeze kati ya mwandiko wa Kiebrania ya mfano wa mraba yanayoizunguka.
Hati-mkono nyingine ya Walawi, imeandikwa kabisa katika mwandiko wa kale wa Kiebrania, lakini sababu ya hilo bado haijaelezwa vya kutosha. Hiyo ndiyo hati yenye urefu mkubwa zaidi iliyoko yenye mtindo huu wa kuandika, uliotumiwa wakati Wayahudi walipokwenda uhamishoni katika Babuloni mwisho wa karne ya saba K.W.K.
Nakala ya Targumu, ufafanusi wa Kiaramu wa kitabu cha Ayubu, ilipatikana pia. Hiyo ni miongoni mwa Targumu za mapema zaidi zilizoandikwa. Baadhi ya maelezo ya vitabu vinginevyo vya Biblia yalipatikana katika pango jingine tofauti. Hati-kunjo zote hizo zilikujaje kufichwa vizuri sana hivyo katika mapango hayo?
Kama ilivyotajwa mapema, huenda nyingine zilifichwa na jumuiya ya Kiqumrani. Lakini kutokana na ushuhuda, inaonekana sana kwamba nyingi ziliwekwa humo na Wayahudi wenye kukimbia ukaribio wa Waroma kwenye Yudea katika mwaka wa 68 W. K., kabla ya uharibifu wa mwisho wa Yerusalemu miaka miwili baadaye. Jangwa la Yudea lilikuwa mahali asili pa usalama kwa ajili ya hati hizo zenye thamani si katika mapango yaliyo karibu na Qumrani tu bali pia katika kilometa nyingi kuelekea kaskazini, kuzunguka Yeriko, na kuelekea Kusini, karibu na Masada. Tuna shukrani kama nini kwa ajili ya kuhifadhiwa kwazo! Zinatoa uthibitisho zaidi juu ya kutokubadilika kwa Neno la Yehova lenye kupuliziwa roho. Kikweli, “neno la Mungu wetu litasimama milele.”—Isaya 40:8.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Reference Bible, Nyongeza [Appendix] 1C (5) na kielezi-chini cha Walawi 3:12, ambapo hati hiyo inatambulishwa kuwa 4Q LXX Lev/b.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
ZAIDI YATAKUJA KARIBUNI?
Ingawa vijipande vya hati-kunjo za Baharifu viligunduliwa miongo mingi iliyopita, vingi havijatangazwa kwa kuchapishwa. The New York Times ya Desemba 23, 1990, lililaumu hivi: “Hata mifano ya kupigwa picha” ya vijipande hivyo “imeshikwa mateka na kikundi cha wanachuo wenye kushikamana sana ambao huepuka washirika wao na hukataa kutangaza vingi vya vifaa walivyo navyo kwa kuchapisha.” Hata hivyo, gazeti hilo liliripoti kwamba badilisho la wafanya kazi katika kundi hilo la wahariri wa gazeti limefanywa karibuni, ambalo huenda likawa mwanzo wa kuvunja “ule ushikamano unaozunguka zile hati-kunjo . . . , na ulimwengu utajua zaidi juu ya wakati usio na kifani katika historia.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.