Pigano Dhidi Ya Ugonjwa Na Kifo Je! Linashindwa?
HAKUNA tena ugonjwa, hakuna tena kifo! Kwa watu walio wengi huenda hilo likasikika kuwa jambo la kuwazia tu. Ingawaje, kama alivyoandika daktari wa tiba aliye profesa wa elimu ya bakteria, Wade W. Oliver: “Tangu historia ya mapema zaidi iliyoandikwa, ugonjwa umeamulia ainabinadamu mwisho wao kwa kadiri isiyohesabika . . . Magonjwa ya vipuku vikubwa yamekumba binadamu kwa kipigo chenye haraka ya kuhofisha . . . Ugonjwa umenyemelea daima hatua zake.”
Je! kuna sababu yoyote ya kuamini kwamba badiliko kubwa sana liko karibu? Je! sayansi ya kitiba iko karibu kukomesha magonjwa yote na labda hata kifo chenyewe?
Bila shaka, madaktari na watafiti wamefanya kazi nzuri ajabu katika kupigana dhidi ya maradhi. Ni mtu gani mwenye elimu awezaye kukosa shukrani kwa ajili ya matibabu yenye mafanikio juu ya kipindupindu, ambayo yalipatikana hatimaye kuelekea mwisho wa karne ya 19, au kwa ajili ya kutokeza chanjo dhidi ya ugonjwa wa ndui wenye kuogopesha sana? Chanjo hiyo iliendelezwa katika 1796 na Edward Jenner kutokana na kidonda cha ndui ya ng’ombe isiyo hatari kadiri hiyo. Katika 1806, rais wa United States Thomas Jefferson alijieleza kwa maoni yaliyo ya wengi alipomwandikia Jenner hivi: “Wako ni ufikirio usio na wasiwasi kwamba ainabinadamu haiwezi kusahau kamwe kwamba wewe umepata kuishi; vizazi vya wakati ujao vitajua kutokana na historia tu kwamba ule ugonjwa wa ndui wenye kukirihisha ulikuwako.”
Zaidi ya hilo, mafanikio ya utafiti wa kitiba kuhusiana na maradhi kama ule ugonjwa hatari wa kufungika koo na ule wa polio (kupooza) ni lazima pia yatajwe kwa upendelevu na kwa shukrani. Na ni watu wachache leo wasiosifu maendeleo ya majuzi zaidi katika utibabu wa maradhi ya moyo na kansa. Hata hivyo, watu wangali wanakufa kutokana na maradhi ya moyo na kansa. Mradi wa kukomesha maradhi na magonjwa yote umekuwa ukiponyoka sana.
Yale Maradhi “Mapya”
Ajabu ya kinyumenyume ni kwamba, kipindi cha leo ambacho kimeona mtokeo wa michungu-zo-mwili ya kutumia eksirei za kompyuta na upasuaji wa kuunga upya sehemu za mwili kimeona pia uzaliwa wa chipuko la maradhi “mapya,” kama vile maradhi ya Legionnaire, udalili wa mshtuko kutokana na sumu, na yule mwuaji mwenye kutangazwa sana katika habari, UKIMWI.
Ni kweli, wengi wanatia shaka maradhi haya ni mapya kadiri gani hasa. Makala moja katika U.S.News & World Report yaeleza kwamba, katika visa fulani, maradhi ambayo yamekuwapo kwa muda mrefu ni kwamba tu yamechunguzwa kwa usahihi zaidi na kupewa majina mapya. Kwa kielelezo, maradhi ya Legionnaire yalitambuliwa kwanza katika 1976, lakini huenda hapo kwanza yakawa yalichunguzwa yakatajwa kimakosa kuwa ni baridi-mapafu yenye kiini kibaya. Vivyo hivyo, udalili wa mshtuko kutokana na sumu huenda hapo kwanza ukawa ulikosewa kwa kudhaniwa kuwa ni homa nyekundu-nyangavu.
Hata hivyo, idadi fulani ya maradhi yaonekana kuwa mapya pasipo shaka. Bila shaka UKIMWI ndio unaojulikana vizuri zaidi kati ya hayo. Maradhi hayo yenye kulemaza na kuua yalitambuliwa kwanza na kupewa jina katika 1981. Maradhi “mapya” mengine yasiyojulikana kwa kadiri hiyo ni homa-zambarau ya Kibrazili. Ilitambuliwa katika Brazili katika 1984 na kadiri yayo ya vifo yakadiriwa kuwa asilimia 50.
Hakuna Maponyo Yanayotazamiwa Karibuni
Kwa hiyo, binadamu ajapofanya jitihada zilizo bora kabisa, maponyo kamili ya kudumu kwa maradhi ya kibinadamu hayatazamiwi karibuni. Ni kweli kwamba tarajio la maisha ya wastani kwa wanadamu limeongezeka kwa karibu miaka 25 tangu mwaka wa 1900. Lakini badiliko hili limesababishwa sana-sana na mbinu za kitiba ambazo zimepunguza hatari ya kufa wakati wa uchanga au wa utoto. Muda wa maisha ya binadamu wabaki hasa karibu na ile “miaka korija tatu na kumi [70]” ya Kibiblia.—Zaburi 90:10, King James Version.
Hivyo ilikuwa ajabu yenye kutangazwa katika habari wakati Anna Williams alipokufa katika Desemba 1987 akiwa na miaka 114. Akieleza juu ya kifo cha Binti William, mwanasafu wa habari aliandika hivi: “Wanasayansi hufikiri kwamba miaka 115 hadi 120 labda ndio ukomo wa juu wa urefu wa maisha ya kibinadamu. Lakini mbona iwe hivyo? Mbona mwili wa kibinadamu uwe mnyonge sana baada ya miaka 70, 80, au hata 115?”
Katika miaka ya 1960, wanasayansi wa kitiba waligundua kwamba chembe za kibinadamu zaonekana zina uwezo wa kugawanyika karibu mara 50 tu. Ukomo huo ufikiwapo, yaonekana hakuna kitu kiwezacho kufanywa kuendeleza chembe hizo zikiwa hai. Jambo hilo laelekea kupinganisha nadharia ya kisayansi ya mapema zaidi kwamba chembe za kibinadamu zingeweza kuendelea hai kwa wakati usio dhahiri zikipewa hali zifaazo.
Unganisha hilo pamoja na ule ufahamu wa kwamba mteseko mwingi wa kibinadamu ni wa kufanyizwa na binadamu. Kama vile mtafiti mmoja alivyokata shauri kwa kufikiri: “Maradhi hayajashindwa kupitia maponyo ya tiba ya kibayolojia pekee. Historia ya maradhi yafungana kindani na visababishi vya kijamii na kiadili.”
Shirika la Afya Ulimwenguni lilionelea hivi: “Sisi tumejitia majeraha wenyewe, katika imani ya kwamba sayansi, madaktari na hospitali zingepata ponyo, badala ya kuzuia visababishi vyenyewe vya ugonjwa pale mwanzoni. Bila shaka hatuwezi kukaa bila vifaa vya utibabu ambavyo kwa kweli huokoa uhai, lakini na tuseme wazi kwamba haviongezei ‘afya’ yetu—hivyo hutuzuia kufa. . . . Tamaa ya mvutaji sigareti na mnywaji yenye kumwangamiza yeye mwenyewe, matokeo ambayo ukosefu wa kazi ya kuajiriwa huwa nayo juu ya akili na mwili—hayo ni baadhi ya yale ‘maradhi mapya.’ Mbona sisi twaruhusu kile ‘kipuku cha misiba ya barabarani,’ ambacho huangamiza uhai kwa wingi na kukausha mali zetu za kifedha?”
Hivyo, maradhi, ugonjwa, mteseko, na kifo vingali sana pamoja nasi. Hata hivyo, tuna sababu ya kutazama mbele kwa uhakika kwenye wakati ambapo hakutakuwa tena na ugonjwa na hakutakuwa tena na kifo. Zaidi ya yote, kuna kila sababu ya kuamini kwamba wakati huo uko karibu sana.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
“MARADHI YA MISRI”
Kwamba wanadamu wamepigana na ugonjwa kuanzia nyakati za mapema bila kuushinda ni jambo lionwalo hata katika Biblia. Kwa kielelezo, Musa alifanya rejezo la kuvutia juu ya ‘maradhi yo yote mabaya ya Misri.’—Kumbukumbu 7:15.
Yaonekana hayo yalikuwa ni kutia ndani ugonjwa wa matende, kuhara damu, ndui, tauni ya majipu ya kinenani, na kufura kwa gololi la jicho. Watu wa Musa waliponyoka kupatwa na maradhi hayo sana-sana kwa sababu ya mazoea ya hali ya juu ya kufuata kanuni za afya zilizowekwa juu yao na agano la Sheria.
Hata hivyo, uchunguzi wa uangalifu wa maiti zilizohifadhiwa za Kimisri umetokeza kutambuliwa kwa chungu nzima ya ‘maradhi ya Misri’ mengineyo. Hayo yalikuwa ni kutia ndani uyabisi, mwasho wa uti wa mgongo, maradhi ya meno na taya, mchochota wa kidole cha utumbo, na jongo. Andishi la mapema la kilimwengu kuhusiana na tiba, lijulikanalo kuwa Funjo la Ebers, hata hutaja maradhi kama vivimbe, masumbufu ya tumbo na ini, kisukari, ukoma, mchochota wa upande wa ndani wa kope la jicho, na uziwi.
Matabibu Wamisri wa kale walifanya yote waliyoweza kupambana na magonjwa hayo, wengine wao wakipata kuwa wataalamu kabisa katika nyanja zao za kitiba. Mwanahistoria Mgiriki Herodoto aliandika hivi: “Ile nchi [Misri] imejawa na matabibu; mmoja hutibu magonjwa ya jicho tu; mwingine yale ya kichwa, meno, tumbo, au viungo vya ndani.” Hata hivyo, sehemu kubwa ya “tiba” ya Kimisri ilikuwa kwa kweli ni ubandia wa kidini wala si wa kisayansi hata kidogo.
Matabibu wa ki-siku-hizi wamepata shangwe ya kuwa na mafanikio makubwa zaidi katika pigano dhidi ya maradhi. Na bado, mtafiti wa kitiba Jessie Dobson alikata shauri hili lenye kuchochea fikira: “Basi, ni somo gani liwezalo kupatikana kutokana na uchunguzi wa maradhi ya nyakati zilizopita? Shauri la ujumla likatwalo kutokana na kuchunguza ithibati laonekana kuwa kwamba maradhi na magonjwa ya zamani za kale hayatofautiani sana na yale ya sasa . . . Yaonekana kwamba stadi zote na jitihada za utafiti juu ya wagonjwa hazikusaidia sana kukomesha maradhi.”—Disease in Ancient Man.