Yule Amiri-Mia Mroma Mwenye Fadhili
MAAMIRI-MIA Waroma hawakuwa na sifa ya kuwa wenye fadhili. Akiwa amegawiwa kuongoza kikosi cha askari-jeshi mia wenye kuzoea vita, amiri-mia alipaswa awe sajini mkali mwenye kufunza mazoezi ya kijeshi, mwenye kutia nidhamu, na, nyakati nyingine, hata kuwa mtekeleza kifo. Hata hivyo, Biblia yatuambia juu ya amiri-mia Mroma wa kikosi cha Augusto aliyemwonyesha mtume Paulo ukarimu na huruma ya kweli. Jina lake? Yulio.
Biblia yajulisha mwanamume huyo kwetu katika Matendo sura ya 27. Mtume Paulo alikuwa amekata rufani kwa Kaisari huko Roma. Hivyo, Paulo, pamoja na wafungwa wengine kadhaa, alitiwa mikononi mwa “akida [amiri-mia, NW] mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto.” Walisafiri baharini kutoka Kaisaria, mji wenye bandari kaskazini-magharibi mwa Yerusalemu uliotumika kuwa makao makuu ya vikosi vya Waroma. Mhistoria Luka asema hivi: “Siku ya pili tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa.”—Matendo 27:1-3.
Sababu hasa kwa nini Yulio alisukumwa kuonyesha fadhili ya jinsi hiyo haitaarifiwi katika Biblia. Angaliweza kuwa chini ya maagizo kutoka kwa Gavana Festo kumpa Paulo utunzi wa pekee. Au labda akiwa amefahamu hali zilizosababisha kukamatwa kwa Paulo, huenda Yulio alipendezwa tu na moyo mkuu na uaminifu wa kimaadili wa Paulo. Kwa vyovyote vile, yaonekana Yulio alijua kwamba Paulo hakuwa mfungwa wa kawaida.
Hata hivyo, Yulio alichagua kutosikiliza onyo la Paulo dhidi ya kusafiri baharini kutoka Bandari Nzuri. Upesi merikebu ikashikwa katika upepo wa dhoruba uliotisha kuipandisha merikebu funguni kwenye pwani ya kaskazini mwa Afrika. (Matendo 27:8-17) Katika dhoruba hiyo, Paulo alisimama na kuwahakikishia maabiria wenye kuogopa kwamba ‘hapana hata nafsi mmoja miongoni mwao angepotea, ila merikebu tu.’ Hata hivyo, baadhi ya mabaharia walijaribu kutoroka baadaye. Paulo kisha akamwambia Yulio: “Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka.”—Matendo 27:21, 22, 30, 31.
Wakati huu, Yulio akachagua kumsikiliza Paulo, na kutoroka kwa mabaharia hao kukazuiwa. Sawa na utabiri wa Paulo, merikebu ilipanda funguni na ikavunjwa. Wakihofu kwamba wafungwa wangetoroka, askari-jeshi waliokuwa merikebuni waliazimia kuwaua wote. Lakini, kwa mara nyingine, Yulio aliingilia na kuwazuia watu wake, hivyo akiuokoa uhai wa Paulo.—Matendo 27:32, 41-44.
Biblia haituambii lililompata amiri-mia huyo mwenye fadhili au kama alipata kuikubali imani ya Kikristo kwa wakati wowote. Fadhili yoyote ile aliyoonyesha ilikuwa wonyesho wa utendaji wa dhamiri yenye kupewa na Mungu. (Warumi 2:14, 15) Hata hivyo, Wakristo huonyesha zaidi ya fadhili ya kibinadamu tu na huonyesha fadhili ya kimungu inayotokana na kuwa na roho ya Mungu. (Wagalatia 5:22) Kwa hakika, ikiwa askari-jeshi mpagani asiyemjua Mungu angeweza kuonyesha fadhili, watu wa Mungu wapaswa kusukumwa kufanya hivyo kwa kadiri kubwa zaidi kama nini!