Furiko Lisilosahaulika
KARIBU miaka 4,300 iliyopita, gharika iliyosababisha msiba mkuu iligharikisha dunia. Kwa kumbo moja kubwa, ilifutilia mbali karibu kila kitu chenye uhai. Ilikuwa kubwa mno hivi kwamba iliachia ainabinadamu alama isiyofutika, na kila kizazi kimepitisha hadithi hiyo kwa kile kinachofuata.
Miaka 850 hivi baada ya hilo Furiko, mwandikaji Mwebrania Musa aliandika usimulizi huo wa lile Gharika ya duniani pote. Umehifadhiwa katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo, ambamo twaweza kusoma maelezo ya waziwazi katika sura 6 hadi 8.
Usimulizi wa Biblia Juu ya Furiko
Mwanzo kinatoa maelezo haya, kwa wazi yakiwa ni yale ya mtu aliyejionea mwenyewe: “Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu [Noa, NW], mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa.”—Mwanzo 7:11, 17, 19.
Kuhusu jinsi Furiko lilivyoathiri vitu vyenye uhai, Biblia husema hivi: “Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu.” Hata hivyo, Noa na watu wengine saba waliokoka, pamoja na namna ya kila hayawani, kiumbe arukaye, na kitu kitambaacho chini. (Mwanzo 7:21, 23) Wote walikuwa wamehifadhiwa katika safina kubwa yenye kuelea iliyokuwa na urefu yapata meta 133, upana wapata meta 22, na kimo cha yapata meta 13. Kwa kuwa kazi ya safina hiyo ilikuwa kwamba iwe isiyovuja maji tu na kubaki ikielea, haikuwa na sehemu ya chini iliyo bapa, gubeti yenye ncha, mtambo wa kuiendesha, wala vifaa vya kuielekeza njia. Safina ya Noa ilikuwa chombo cha kimstatili tu, kilichokuwa kama sanduku.
Miezi mitano baada ya kuanza Gharika, safina ilitua kwenye milima ya Ararati, iliyo mashariki mwa Uturuki ya leo. Noa na familia yake waliondoka safinani kwenye bara kavu mwaka mmoja baada ya kuanza Furiko kisha wakaanza upya utaratibu wa kawaida wa maisha. (Mwanzo 8:14-19) Baadaye, wanadamu walikuwa wameongezeka vya kutosha kuweza kujenga mji wa Babeli na mnara wayo wenye sifa mbaya karibu na Mto Eufrate. Kutoka hapo watu walitawanywa polepole kuelekea sehemu zote za dunia wakati Mungu alipochafua lugha ya ainabinadamu. (Mwanzo 11:1-9) Lakini ni nini kilichokipata safina hiyo?
Kuitafuta-tafuta Safina
Tangu karne ya 19, kumekuwako jitihada nyingi za kupata safina kwenye milima ya Ararati. Milima hiyo ina vilele viwili maarufu, kimoja chenye kimo cha meta 5,165 na kile kingine cha meta 3,914. Kile cha juu zaidi kati ya hivyo viwili huwa kimefunikwa kwa theluji daima. Kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya anga yaliyofuata Furiko, safina ingalifunikwa kwa theluji upesi. Wachunguzi fulani huamini kwa uthabiti kwamba safina ingali ipo hapo, ikiwa imezikwa chini sana katika barafuto. Wanadai kwamba kumekuwako vipindi ambavyo barafu iliyeyuka vya kutosha kuruhusu sehemu ya safina ifunuliwe kwa muda.
Kitabu In Search of Noah’s Ark chamnukuu George Hagopian, Mwarmenia, aliyedai kwamba alikwea Mlima Ararati na kuona safina katika 1902 na tena katika 1904. Kwenye ziara ya kwanza, alisema, alipanda juu ya safina hasa. “Nilisimama wima na kuangalia kotekote melini. Ilikuwa ndefu. Kimo chayo kilikuwa yapata meta 12.” Kuhusu maono yake kwenye ziara yake iliyofuata, alisema hivi: “Sikuona kombo zozote za kweli. Ilikuwa tofauti na mashua nyingine yoyote ambayo nimepata kuona wakati wowote. Ilionekana sana sana kama mashua kubwa yenye sehemu ya chini iliyo bapa.”
Kutoka 1952 hadi 1969, Fernand Navarra alifanya jitihada nne za kupata ushuhuda wa safina. Kwenye safari yake ya tatu kwenda Mlima Ararati, alifanya jitihada ya kwenda chini ya mwanya katika barafuto, ambapo alipata kipande cha mbao nyeusi ndani ya barafu. “Ni lazima iwe ilikuwa ndefu sana,” akasema, “na labda ilikuwa bado imefungamana na sehemu nyingine za kiunzi cha meli. Niliweza tu kukata kwenye nyuzi za mbao mpaka nilipopasua kipande cha urefu wapata meta 1.5.”
Profesa Richard Bliss, mmoja wa wastadi kadhaa waliochunguza mbao hiyo, alisema hivi: “Kipande cha mbao cha Navarra kilikuwa muundo wa boriti na kupakwa lami ya bitumeni. Kina mashimo ya kuunganisha mabao mengine na viungo vya kupachika. Na bila shaka kimechongwa na kufanyizwa umbo kwa mkono.” Umri wa kukadiriwa wa mbao hiyo uliwekwa kwenye yapata miaka elfu nne au tano.
Ingawa juhudi zimefanywa za kupata safina kwenye Mlima Ararati, uthibitisho wa kweli kwamba ilitumiwa kuokoka gharika iliyosababisha maafa makuu umo katika rekodi iliyoandikwa ya tukio hilo katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo. Uthibitisho wa rekodi hiyo yaweza kuonwa katika hekaya za furiko miongoni mwa watu wa kale kotekote ulimwenguni. Angalia ushuhuda wao katika makala inayofuata.
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Safina ilikuwa na nafasi ya kubeba iliyo sawa na magari-moshi 10 ya mizigo kila moja likiwa na mabehewa ya Kiamerika kama 25!