Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 6/15 kur. 28-30
  • Dayoklito Ashambulia Ukristo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dayoklito Ashambulia Ukristo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Upagani kwa Kulinganisha na Ukristo
  • Sheria Mbalimbali
  • Ukristo wa Karne ya Nne
  • Biblia Yashambuliwa
    Amkeni!—2011
  • Jinsi Jumuiya ya Wakristo Ilivyokuja Kuwa Sehemu ya Ulimwengu Huu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Bila Wazo la Kuridhiana!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Ukristo wa Mapema na Serikali
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 6/15 kur. 28-30

Dayoklito Ashambulia Ukristo

KWENYE sherehe ya mungu wa Kiroma Tarminasi katika Februari 23, 303 W.K., iliyofanyiwa katika jiji kuu jipya la milki hiyo liitwalo Nikomedia katika Esia Ndogo, watu walishindana ili kuonyesha uzalendo wao. Lakini ilionekana wazi kwamba jumuiya kubwa ya Wakristo haikuwepo.

Wakiwa katika sehemu ya juu ya jumba la mfalme, Maliki Dayoklito na mdogo wake Kaisari Galiriasi waliweza kuona mahali pa kukutania pa Wakristo. Kwa ishara iliyotolewa, askari na maofisa wa serikali walivunja na kuingia ndani ya jengo hilo la Wakristo, wakiliteka, na kuchoma nakala za Biblia walizopata. Hatimaye, walichoma jengo hilo likawa majivu.

Hivyo kipindi cha mnyanyaso kikaanza kilichotia waa utawala wa Dayoklito. Wanahistoria hukiita “mnyanyaso mkubwa wa mwisho,” “mnyanyaso mkali zaidi,” hata “kufagiliwa kabisa kwa jina la Kikristo.” Kwa kutazama mambo yaliyotangulia matukio hayo yenye kutazamisha, mambo mengi hufunuka.

Upagani kwa Kulinganisha na Ukristo

Dayoklito, aliyezaliwa katika Dalmatia, sehemu ambayo leo ni Yugoslavia, alifikia kuwa maarufu kupita vyeo katika jeshi la Kiroma. Alipowekwa kuwa maliki katika 284 W.K., alipata umaarufu kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kisiasa alipoanzisha utawala wa pamoja wa watu wanne, kuongoza milki. Dayoklito alimteua Maksimiani, aliyekuwa askari mwenzake, afanye kazi pamoja naye akiwa maliki wa pili, na wa pili kwa heshima, akiwa na daraka la pekee katika sehemu ya magharibi ya milki hiyo. Wote wawili Dayoklito na Maksimiani walikuwa na Kaisari mdogo ambaye alipewa haki ya kumiliki. Konstantio Klorasi alitumika kuwa Kaisari wa Maksimiani, hali Galeriasi kutoka Thrace alikuwa na mamlaka chini ya Dayoklito.

Kaisari Galeriasi, kama vile Dayoklito, alikuwa mwabudu mwenye bidii wa miungu ya kipagani. Akiwa anajitakia makuu ya kuchukua mahali pa maliki, Galeriasi alisingizia kuwa alihofia uhaini jeshini. Alichukia uvutano uliozidi kukua wa askari waliodai kuwa Wakristo. Kwa maoni ya maliki huyo, kukataa kwao kushiriki katika ibada ya kipagani kulikuwa ushindani dhidi ya mamlaka yake. Kwa hiyo Galeriasi alimhimiza Dayokilito achukue hatua za kufagilia mbali Ukristo. Hatimaye, katika kipupwe cha 302/303 W.K., maliki alikubaliana na hisi ya Kaisari ya kupinga Wakristo na akakubali kuwaondoa Wakristo wote walio jeshini na nchini. Lakini Dayoklito alipinga umwagaji damu, akihofia kuwa wakifia imani kwa sababu za Kikristo wangewafanya wengine waazimie kuasi.

Bado, akiwa hajaridhika na njia hiyo ya kushughulikia jambo hilo, Dayoklito aliwaona makamanda na maofisa wa jeshi, kutia ndani na Hieroklesi, gavana wa Bithinia. Myunani huyo mwenye bidii aliunga mkono jeuri dhidi ya Wakristo wote. Uungaji mkono wa Dayoklito kwa miungu ya kimapokeo kuliongoza kwenye kuhitilafiana na Ukristo. Tokeo, kulingana na kitabu Diocletian and the Roman Recovery, (Dayoklito na kuhuishwa kwa Roma) cha Stephen Williams, lilikuwa ni “vita isiyozuiwa hadi mwisho wayo kati ya miungu ya Roma na mungu wa Wakristo.”

Sheria Mbalimbali

Ili kutekeleza kampeni yake ya mnyanyaso, Dayoklito alijulisha wazi sheria nne zilizofuatana. Siku iliyofuatia shambulio katika Ni-komedia, aliamuru kuwa mahali pote pa kukutania na mali zote za Wakristo ziharibiwe na akatoa amri kuwa vitabu vyote vitakatifu visalimishwe na kuchomwa. Wakristo walioshikilia nyadhifa za kiserikali walipaswa washushwe vyeo.

Wakati mioto miwili ilipoanza ndani ya jumba la mfalme, Wakristo waliofanya kazi humo ndio waliolaumiwa. Hilo lilitokeza sheria ya pili, iliyoamuru kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa askofu, wapresbiteri, na washemasi wote. Sheria ya tatu ilijaribu kuwafanya watu hawa wawe waasi-imani, ikiruhusu kuteswa ikiwa lazima, wakiwataka watoe dhabihu kwa miungu ya Kiroma. Sheria ya nne ilienda hatua moja mbele kwa kufanya iwe ni kosa la kuadhibiwa kifo kwa mtu yoyote kukiri kuwa Mkristo.

Wimbi hilo la ukatili lilitokeza jamii iliyoitwa traditores (kumaanisha, “wale waliojisalimisha”), wasaliti kwa Mungu na Kristo waliojaribu kulinda maisha zao kwa kusalimisha nakala zao za Maandiko. Kulingana na mwanahistoria Will Durant, “maelfu ya Wakristo walikana imani . . . Lakini wengi wa wale walionyanyaswa walisimama imara; na kuweza kuona au kupata ripoti za kudumisha imani chini ya mateso kuliimarisha imani ya wale walioyumbayumba na kukaleta washiriki wapya kwa makundi yaliyowindwa.” Wakristo katika Frigia, Kapadokia, Mesopotamia, Finishia, Misri, na sehemu nyingine nyingi za Milki ya Roma walifia imani yao.

Eusebio wa Kaisaria aliye mwanahistoria wa kanisa alifikiri kwamba maelfu ya Wakristo walikufa wakati wa mnyanyaso huo. Kwa upande ule mwingine, Edward Gibbon, mbuni wa kitabu The Decline and Fall of the Roman Empire (Kushuka na Kuanguka kwa Milki ya Roma), anadai idadi ya waamini isiyozidi elfu mbili. “Gibbon anaonea mashaka nyingi za hadithi hizo, zikitoka hasa kwa vyanzo vya Kikristo vyenye kutia chumvi mno zikielekea kusifu wafia-imani na kuwaheshimu waaminifu,” aeleza mwandikaji mmoja. “Hakuna shaka lolote,” yeye aendelea, “kutia chumvi kwa waandikaji wanaogeuza kwa urahisi vifo vichache kuwa ‘maelfu,’ ambao hawaonyeshi tofauti yoyote kati ya wafia-imani wasiofanya lolote kustahili kifo na wale wanaokufa kutokana na uchokozi wao wa makusudi; na wanaosimulia juu ya hayawani mwitu kwenye majumba ya michezo waliowala kwa ghadhabu wahalifu wote wengine lakini waliozuiwa na ‘nguvu isiyo ya kawaida’ wasiwaguse Wakristo. Lakini, hata tukiacha nafasi ya kubuniwa kwa hadithi, kile kinachobaki kinahuzunisha vya kutosha.” Kwa kweli mnyanyaso mkatili sana ulitokea kwa vitanda vya kunyoshea watu kwa nguvu, kuchomwa, kuchunuliwa, na vibano vinavyotumiwa kwa kutesa.

Baadhi ya wenye mamlaka huwa na maoni kwamba Galeriasi, badala ya Dayoklito, ndiye aliyeanzisha mnyanyaso huo. “Ni kwa maana kubwa ya kiadili,” adai Profesa William Bright katika kitabu The Age of the Fathers (Kipindi cha Mababa), “kwamba jitihada za mamlaka ya serikali ya kipagani za kufagilia mbali uhai wa Ufalme usio wa ulimwengu huu zapaswa kuwa kwa jina la Dayoklito, badala ya mwanzilishi wazo Galeriasi.” Na bado, hata katika utawala huo wa viongozi wanne, Dayoklito alidumisha udhibiti wote, kama vile mwandikaji Stephen Williams anavyosema: “Hakuna shaka kwamba Dayoklito alikuwa na udhibiti wa kila sheria katika Milki hiyo hadi 304, na yeye ana daraka kuu la mnyanyaso kufikia tarehe hiyo.” Dayoklito alikuwa mgonjwa na hatimaye akapeana uongozi katika 305 W.K. Kwa miaka sita iliyofuata, mnyanyaso uliofuata ulionyesha chuki kubwa ya Galeriasi kuelekea mambo yote yaliyohusu Ukristo.

Ukristo wa Karne ya Nne

Matukio hayo yenye kuhofisha ya mapema mwa karne ya nne yanathibitisha yale yaliyokuwa yametabiriwa na mitume Paulo na Petro, kutia na waandikaji wengine waliopuliziwa roho. “Yule mtu wa kuasi” aliyetabiriwa, ile jamii ya makasisi wenye kuongoza wa wanaodai kuwa Wakristo, alikuwa tayari amesitawi, kama vile sheria za Dayoklito, hasa ya pili, inavyoonyesha. (2 Wathesalonike 2:3, 4; Matendo 20:29, 30; 2 Petro 2:12) Kufikia karne ya nne, mazoea ya waasi-imani yalikuwa tayari mambo ya kawaida. Wengi kadiri fulani waliodai kuwa Wakristo walikuwa washiriki wa jeshi la Roma. Je! wakati huo hakukuwako Wakristo waliokuwa waaminifu kwa “kielelezo cha maneno yenye uzima” yaliyopokewa kutoka kwa mitume?—2 Timotheo 1:13.

Eusebio anataja majina ya baadhi ya wahanga wa mnyanyaso, hata akieleza kwa michoro kuteswa kwao, kutaabika kwao, na hatimaye kufia-imani kwao. Iwe wafia-imani hao wote walikufa kwa kushika uaminifu wa kimaadili kwa ajili ya kweli iliyofunuliwa iliyopatikana wakati huo, hatuwezi kujua kwa sasa. Hakuna shaka kwamba wengine walikuwa wametii onyo la Yesu la kuepuka mafarakano, ukosefu wa adili, na kuridhiana kwa aina yoyote. (Ufunuo 2:15, 16, 20-23; 3:1-3) Kwa wazi, baadhi ya walio waaminifu waliookoka hawakupata kujulikana sana. (Mathayo 13:24-30) Kwa kweli, hatua za kukomesha ibada ya Kikristo ya peupe zilifaulu sana hivi kwamba nguzo ya ukumbusho katika Hispania ya wakati huo humsifu Dayoklito kwa ‘kukomesha ushirikina wa Kristo.’ Hata hivyo, jitihada za kutwaa na kuharibu nakala za Maandiko, zikiwa ndizo sehemu muhimu ya mashambulizi ya Dayoklito dhidi ya Ukristo, zilishindwa kufagilia mbali Neno la Mungu kabisa kabisa.—1 Petro 1:25.

Kwa kushindwa kuondolea mbali Ukristo kabisa, Shetani Ibilisi, mtawala wa ulimwengu, aliendelea na jitihada zake za hila kupitia Maliki Konstantino, aliyetawala kutoka 306 hadi 337 W.K. (Yohana 12:31; 16:11; Waefeso 6:11, kielezi-chini) Konstantino aliyekuwa mpagani hakupigana na Wakristo. Badala yake, aliona kuwa inafaa kuchanganya itikadi za kipagani na Kikristo ziwe dini moja mpya ya Kitaifa.

Ni onyo lililoje kwa sisi sote! Tunapokabiliwa na mnyanyaso mkatili, upendo wetu kwa Yehova utatusaidia kuepuka kuridhiana kwa ajili ya faraja yoyote ya kimwili ya muda mfupi. (1 Petro 5:9) Vivyo hivyo, hatutaruhusu kipindi cha usalama kituondolee bidii yetu ya Kikristo. (Waebrania 2:1; 3:12, 13) Kushikamana kabisa na kanuni za Biblia kutatuweka tukiwa waaminifu-washikamanifu kwa Yehova, Mungu awezaye kuokoa watu wake.—Zaburi 18:25, 48.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 28]

Musei Capitolini, Roma

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki