Kwa Nini Kuna Kutamauka Kwingi?
TUMAINI la kupata maisha bora zaidi—limetimizwa hatimaye! Watu wengi walioishi katika ile iliyokuwa Ujerumani Mashariki waliamini hivyo wakati Ukuta wa Berlin ulipobomolewa katika Novemba 1989. Hata hivyo, baada ya muda uliozidi kidogo mwaka mmoja, walilalamika juu ya “kuona ulimwengu mgumu wa demokrasia ya ubepari kuwa mgumu wa kukabiliana nao kuliko maisha yaliyolindwa na Ukuta wa Berlin.” Tokeo likawa nini? Kukata tamaa na kutamauka kwenye kuongezeka.
Jeuri ya kinyumbani na ya kijamii huenda ikasababisha watu waondoke nyumbani kutafuta usalama, lakini ni wachache wanaoupata. Wengine hata huenda hatimaye wakawa miongoni mwa wale wasio na makao wanaoishi kwenye barabara za mji. Katika nchi fulani wengi wao hulazimika kufuata taratibu za kiserikali zinazochukua muda mrefu ili kuweza kufanikiwa. Kwa sababu hawawezi kulipia nyumba kwa kukosa kazi, hawawezi kupata kazi ya kuajiriwa kwa sababu hawana anwani ya makao. Mashirika ya serikali ya kutunza hali njema za watu hujaribu kusaidia, lakini inachukua wakati mwingi kusuluhisha matatizo hayo. Kwa hiyo kufadhaika na kutamauka hufuata.
Wanawake wengi husukumwa na kutamauka wakafanye mambo ya ajabu kweli kweli. Katika ripoti Women and Crime in the 1990s, mhadhiri wa sheria Dakt. Susan Edwards aeleza hivi: “Kuhusika kwa wanawake wachanga zaidi [katika umalaya] ni tokeo la moja kwa moja la uhitaji wa kiuchumi, si ukosefu wa kujitia nidhamu au malezi ya kifamilia.” Vivyo hivyo, wanaume wachanga wanaoondoka nyumbani ili kutafuta kazi mara nyingi hukosa kupata kazi yoyote. Wengine, kwa kutamauka, huwa hatimaye ‘wavulana wa kukodishwa,’ wakitoa miili yao kwa wanaume wanaofanya ngono ya jinsia moja ili wapate chakula na makao, wakiwa vibaraka vya vikundi vya wahalifu wenye ufisadi.
Mambo mabaya yanayoletwa na siasa, jeuri, hali ngumu za kiuchumi, mambo hayo yote huenda yakachochea kadiri fulani ya kutamauka. Hata watu walio na kazi za elimu ya juu hawaepuki kutamauka wanapojaribu kudumisha mitindo-maisha yao ya hali ya juu huku wakikabiliana na matatizo ya kifedha yenye kuongezeka. Tokeo ni nini? “Jeuri [uonevu, New World Translation of the Holy Scriptures] humpumbaza mwenye hekima,” kama alivyosema Mfalme Sulemani wa zamani!a (Mhubiri 7:7) Kwa kweli, kutamauka huongoza idadi ya watu yenye kuongezeka wachukue hatua ya kupita kiasi ya kusuluhisha tatizo—kujiua.
Hatua ya Kupita Kiasi ya Kusuluhisha Tatizo
Visa vingi vya kujiua miongoni mwa vijana huonyesha kwamba hata wao huathiriwa na pigo la kutamauka. Mwandishi-safu wa habari Mwingereza aliuliza hivi: “Ni jambo gani katika wakati huu wetu linalosababisha kutamauka kwingi sana kwa matineja?” Katika uchunguzi wa watoto kati ya miaka 8 na 16 waliokuwa wamelazwa hospitalini baada ya kujaribu kumeza sumu, Dakt. Eric Taylor wa Taasisi ya London ya Tiba ya Magonjwa ya Akili aripoti hivi: “Jambo moja lenye kutokeza lilikuwa ni kwamba wengi wa watoto hao walikuwa wakitamauka na kukata tamaa juu ya mambo.” Uingereza huripoti kadirio la visa 100,000 kila mwaka vya kumeza sumu kimakusudi kusikosababisha kifo ambako huonyesha jinsi watu wanavyohitaji msaada.
Shirika moja la Uingereza la kutoa msaada lilianzisha kampeni ya kuwasikiliza kwa huruma wenye kutamauka. Kwa njia hiyo washauri walo walidai kutoa “vibadala vya kifo.” Ingawa hivyo, wanakiri kwamba hawawezi kusuluhisha matatizo yanayosababisha watu watamauke.
Kadiri ya wanaojiua huonyesha “hali ya upweke na ukosefu wa ushirikiano wa kijamii katika jumuiya,” laeleza gazeti la habari The Sunday Correspondent. Kwa nini kuna ongezeko kubwa la kadiri ya wanaojiua leo? Gazeti hilo la habari lilitaja “ukosefu wa makao, ongezeko la kunywa vileo, tisho la Ukimwi na kufungwa kwa hospitali za kutibu magonjwa ya akili” kuwa visababishi vinavyofanya watu mmoja mmoja wapatwe na kutamauka kwingi sana hivi kwamba wafikirie kujiua ndiko suluhisho la pekee kwa matatizo yao.
Je! kuna tumaini lolote la kuondoa kutamauka? Ndiyo! “Changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu,” ndio mwito wa Yesu wenye kutia moyo! (Luka 21:28) Yeye alimaanisha nini? Kuna tumaini gani?
[Maelezo ya Chini]
a Kulingana na Theological Wordbook of the Old Testament, kilichohaririwa na Harris, Archer, na Waltke, msingi wa lugha ya awali ya neno lililotafsiriwa “uonevu” huhusiana na “kulemezwa, kukanyagwa-kanyagwa kwa miguu, na kupondwa kwa wale wenye cheo cha chini.”