Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 8/1 kur. 3-4
  • Uhai Zawadi Kutoka kwa Mungu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uhai Zawadi Kutoka kwa Mungu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Habari Zinazolingana
  • Kuwa na Watoto— Daraka na Thawabu
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Uhai wa Mwanadamu Unaanza Wakati Gani?
    Amkeni!—2009
  • Kuingia Katika Ulimwengu Usio na Huruma!
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 8/1 kur. 3-4

Uhai Zawadi Kutoka kwa Mungu

MUDA wa saa ishirini na nne kila siku, moyo wetu hupiga na kusukuma damu yenye thamani kubwa kupitia mwili wetu. Tunalala usingizi, na mapafu yetu huendelea kutanuka na kupungua. Tunakula mlo, na chakula humeng’enyeka chenyewe. Yote hayo hutukia kila siku, kwa bidii kidogo au bila bidii yoyote kwa upande wetu. Taratibu hizo za kifumbo na za ajabu, zinazopuuzwa kwa urahisi, ni sehemu ya ile zawadi tunayoita uhai. Kwa maana fulani hiyo ni zawadi iwezayo kuitwa ya kimuujiza.

Fikiria ile taratibu ya utungaji mimba na kuzaliwa kwa kibinadamu. Ingawa mwili kwa kawaida hukatalia mbali tishu ya kigeni, tumbo la uzazi hukubali hali tofauti kwa ajili ya yai lililotungishwa. Badala ya kukatalia mbali kile kiinitete kinachokua kuwa ni tishu ya kigeni, linakilisha na kukilinda mpaka kinapokuwa tayari kutoka kikiwa kitoto. Bila uwezo wa tumbo la uzazi kuikubali hali iliyo tofauti na ile kanuni ya kukatalia mbali tishu ya kigeni, kuzaliwa kwa kibinadamu kusingewezekana.

Hata hivyo, uhai wa kitoto kilichozaliwa hivi karibuni ungekuwa mfupi ikiwa kusingekuwa lile jambo linalotukia katika tumbo la uzazi wakati kijusi kinapokuwa na umri wa miezi minne hivi. Wakati huo kinaanza kunyonya kidole chake, kikiyazoeza misuli itakayokiwezesha kujilisha kwenye matiti ya mama yake. Na hilo ni mojawapo tu ya yale mambo mengi ya kufa na kupona yanayosuluhishwa kabla ya kuzaliwa kwa kitoto.

Kijusi kinapokuwa katika tumbo la uzazi, kuna shimo katika ukuta wa moyo wake. Hata hivyo, shimo hilo hufungika lenyewe wakati wa kuzaliwa. Kwa kuongezea, mshipa mkubwa wa damu upitao kando ya mapafu hubanika wakati wa kuzaliwa; sasa damu huingia mapafuni, mahali iwezapo kupata oksijeni kitoto kianzapo kupumua.

Yote hayo ni mwanzo tu. Maishani mwote, mfululizo wa mifumo iliyobuniwa vizuri (kama vile mifumo ya kupumua, ya uzungushaji damu, ya neva, na ya tezindani) utafanya na kupatanisha kazi zao kwa uhodari wa kazi unaoduwaza ufahamu wa kibinadamu—yote ni kwa ajili ya kuendeleza uhai. Si ajabu kwamba mwandishi wa zamani alisema hivi kwa kumrejezea Mungu: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, na nafsi yangu yajua sana.”—Zaburi 139:14.

Kwa wazi, mwandishi wa maneno hayo yenye kupendeza hakuamini kwamba uhai ni tokeo tu lisiloongozwa, la mageuzi ya nasibu au aksidenti. Ikiwa ingekuwa hivyo, tusingekuwa na wajibu au madaraka yoyote ya kweli kuhusu jinsi tunavyopaswa kutumia uhai wetu. Hata hivyo, taratibu za uhai kwa wazi huonyesha ubuni, na ubuni huhitaji mbuni. Biblia hutoa kanuni hii: “Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.” (Waebrania 3:4) Kwa hiyo ni muhimu ‘kujua kwamba Yehova ndiye Mungu; ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake.’ (Zaburi 100:3) Naam, uhai ni zaidi ya kuwa aksidenti njema tu; ni zawadi itokayo kwa Mungu mwenyewe.—Zaburi 36:9.

Hali ikiwa hivyo, sisi tuna wajibu gani kumwelekea Mpaji wa uhai? Yeye atutarajia tutumie uhai wetu kwa jinsi gani? Maswali hayo na mengine yanayohusu jambo hilo yatazungumziwa katika makala inayofuata.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki