Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 9/15 kur. 3-7
  • Kwa Nini Watu Wazuri Huteseka?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwa Nini Watu Wazuri Huteseka?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuteseka kwa Ayubu
  • Mungu Si Mwenye Kulaumiwa
  • Wazuri na Wabaya Pia Huteseka
  • Sababu Kwa Nini Watu Wenye Kumcha Mungu Huteseka
  • Karibuni—Kuteseka Hakutakuwapo Tena!
  • Ikiwa Muumba Anajali, Mbona Wanadamu Wanateseka Sana?
    Je, Kuna Muumba Anayekujali?
  • Ayubu—Mtu Mvumilivu na Mtimilifu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
  • Kuteseka Kuteseka
    Amkeni!—2015
  • Ukamilifu wa Ayubu—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 9/15 kur. 3-7

Kwa Nini Watu Wazuri Huteseka?

ULIKUWA ni mwaka wa 1914, na ulimwengu ulikuwa vitani. Kwa ghafula, ikatokea homa iletwayo na chawa katika kambi ya wafungwa wa vita katika Serbia. Lakini huo ulikuwa mwanzo tu. Ugonjwa huo wenye kuhofiwa ulienea hadi kwa raia na kusababisha vifo vya watu 150,000 katika miezi sita tu. Kati ya hali za vita na yale mapinduzi yaliyofuata katika Urusi, watu milioni tatu walikufa kutokana na homa iletwayo na chawa. Waweza kukata maneno kwa usahihi kwamba watu wazuri wengi na washiriki wa familia zao waliofiwa walikuwa miongoni mwa wale waliokufa.

Huo ni mfano mmoja tu wa msiba wa kibinadamu. Huenda ikawa wewe mwenyewe umepatwa na kule kuteseka kunakotokea wakati wapendwa wanapopatwa na magonjwa, aksidenti, na maafa ya aina moja au nyingine. Yaelekea, unataabika wakati mtu mwadilifu anapopatwa na maumivu ya ugonjwa usioponyeka. Yawezekana unahuzunika sana wakati mtu mzuri—labda mwanamume mwenye bidii aliye na familia—anapouawa katika aksidenti. Huzuni ya wale waliofiwa huenda ikafanya moyo wako uwe na uchungu mwingi kwa ajili yao.

Wengi huhisi kwamba mtu anayefanya mema apaswa kuthawabishwa na uhuru kutoka katika kuteseka. Wengine hata huona kuteseka kuwa uthibitisho wa kwamba mtu aliyeathiriwa ni mkosaji. Hiyo ilikuwa ndiyo hoja ya wanaume watatu walioishi miaka 3,600 hivi iliyopita. Waliishi wakati uleule wa mwanamume mmoja mzuri aliyeitwa Ayubu. Acheni turudi hadi siku yao tunapoanza kutafuta jibu la swali, Kwa nini watu wazuri huteseka?

Kuteseka kwa Ayubu

Wakati wale waliokuwa eti marafiki wa Ayubu watatu walipomtembelea, alikuwa akiteseka isivyoelezeka kutokana na maumivu na ugonjwa. Alikuwa amefiwa na watoto wake kumi na alikuwa amepoteza mali zake zote za kimwili. Watu waliokuwa wamemstahi Ayubu sana walimchukia. Hata mke wake aliacha kumwunga mkono na akahimiza kwamba Ayubu amlaani Mungu na kufa.—Ayubu 1:1–2:13; 19:13-19.

Kwa siku na masiku saba, wageni wa Ayubu walitazama kuteseka kwake. Halafu mmoja wao alimshtaki juu ya mwenendo uliokosa uadilifu ambao eti alikuwa akiadhibiwa kwa ajili yao. “Kumbuka, tafadhali,” akasema yule mwanamume Elifazi: “Ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi? Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, na kupanda madhara, huvuna yayo hayo. Kwa pumzi za Mungu huangamia. Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika.”—Ayubu 4:7-9.

Kwa hiyo, Elifazi alitoa hoja ya kwamba Mungu alikuwa akimwadhibu Ayubu kwa ajili ya dhambi zake. Leo pia, wengine hutoa hoja ya kwamba maafa ni vitendo vya Mungu vinavyokusudiwa kuwaadhibu watu kwa ajili ya kutenda mabaya. Lakini Yehova hakuwa akimwadhibu Ayubu kwa ajili ya kufanya vitendo visivyo vya uadilifu. Twajua hilo kwa sababu Mungu alimwambia Elifazi hivi baadaye: “Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.”—Ayubu 42:7.

Mungu Si Mwenye Kulaumiwa

Leo, mamilioni—kwa hakika kutia na watu wazuri wengi—wamepatwa na umaskini na wako karibu kufa kwa njaa. Watu wengine huwa na uchungu na humlaumu Mungu kwa ajili ya kuteseka kwao. Lakini yeye si mwenye kulaumiwa kwa ajili ya njaa. Kwa kweli, yeye ndiye Yule anayeandalia ainabinadamu chakula.—Zaburi 65:9.

Ubinafsi, pupa, na visababishi vingine vya kibinadamu huenda vikazuia utoaji wa chakula kwa wale wenye njaa. Vita ni miongoni mwa visababishi vya njaa. Kwa mfano, The World Book Encyclopedia husema hivi: “Vita huenda ikatokeza njaa ikiwa wakulima wengi wanayaacha mashamba yao na kujiunga na majeshi. Katika visa vingine, jeshi limesababisha njaa kimakusudi ili adui apatwe na njaa kali aweze kujisalimisha. Jeshi huharibu chakula kilichowekwa akibani na mimea inayokua na huzuia kupitishwa kwa chakula cha adui. Vizuizi vilikatiza usafirishaji wa chakula ili kisifike kwenye eneo la Biafra wakati wa Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Niajeria (1967-70). Njaa ilitokea, na Wabiafra zaidi ya milioni moja yaelekea walikufa kwa njaa.”

Wengine walimlaumu Mungu hasa wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, wakati watu wazuri wengi walipoteseka na kufa. Hata hivyo, wanadamu huvunja sheria za Mungu kwa kuchukiana na kupigana. Yesu Kristo alipouli-zwa ni amri gani iliyokuwa “ya kwanza,” alijibu hivi: “Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana [Yehova, New World Translation] Mungu wetu ni Bwana [Yehova, NW] mmoja; nawe mpende Bwana [Yehova, NW] Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”—Marko 12:28-31.

Wanadamu wanapovunja sheria za Mungu kwa kushiriki katika machinjo ya wengi, je, mtu yeyote aweza kumlaumu ikiwa kuteseka kunatokea? Mzazi akiwaambia watoto wake wasipigane miongoni mwao nao wanapuuza shauri lake zuri, je, alaumiwe wanapojeruhiwa? Si daraka la mzazi jinsi lisivyo la Mungu wakati kuteseka kwa kibinadamu kunapotokea kwa sababu ya watu kupuuza sheria za kimungu.

Ingawa kuteseka kwaweza kutokea wakati sheria za Yehova zinapopuuzwa, Biblia haionyeshi kwamba misiba kwa ujumla ni vitendo vya Mungu vinavyokusudiwa kuwaadhibu waovu. Wanadamu wawili wa kwanza walipotenda dhambi, walipoteza baraka na ulinzi wake wa pekee. Visipokuwa vile visa vya mwingilio wa kimungu ili kutimiza kusudi la Yehova, lile ambalo limeipata ainabinadamu kila siku limeongozwa na kanuni hii ya Kimaandiko: “Si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati [tukio lisilotazamiwa, NW] huwapata wote.”—Mhubiri 9:11.

Wazuri na Wabaya Pia Huteseka

Kwa kweli, wanadamu wazuri na wabaya pia huteseka kwa sababu ya dhambi na kutokamilika kulikorithiwa. (Warumi 5:12) Kwa mfano, watu waadilifu na waovu pia hupatwa na magonjwa yenye maumivu. Mkristo mwaminifu Timotheo aliteseka kutokana na ‘magonjwa yaliyompata mara kwa mara.’ (1 Timotheo 5:23) Mtume Paulo alipotaja “mwiba katika mwili” wake mwenyewe, huenda ikawa alikuwa akitaja taabu fulani ya kimwili. (2 Wakorintho 12:7-9) Hata kwa ajili ya watumishi wake waaminifu-washikamanifu, Mungu haondolei mbali wakati huu udhaifu mbalimbali uliorithiwa au wepesi wa kupatwa na magonjwa.

Watu wamchao Mungu huenda pia wakateseka kwa sababu ya kutumia uamuzi mbaya au kushindwa kutumia shauri la Kimaandiko nyakati nyingine. Kutoa kielezi: Mtu akosaye kumtii Mungu na afunga ndoa na asiyeamini huenda akateseka na matatizo ya ndoa ambayo angaliweza kuepuka. (Kumbukumbu la Torati 7:3, 4; 1 Wakorintho 7:39) Mkristo asipokula ifaavyo na kupata pumziko la kutosha, huenda akateseka kwa sababu ya kuiharibu afya yake.

Kuteseka kihisiamoyo huenda kukatokea ikiwa tunashindwa na udhaifu na twashiriki katika mwenendo mbaya. Uzinzi wa Mfalme Daudi pamoja na Bath-sheba ulimletea kuteseka kwingi. (Zaburi 51) Alipojaribu kuficha kosa, aliteseka na kule kutaabika kwingi. “Niliponyamaza,” akasema, “mifupa yangu ilichakaa kwa kuugua kwangu mchana kutwa. . . . Jasho langu likakauka hata nikawa kama nchi kavu wakati wa kaskazi.” (Zaburi 32:3, 4) Uchungu mwingi kwa ajili ya hatia yake ulipunguza nguvu ya Daudi kama mti uwezavyo kupoteza umajimaji wayo wa kutoa uhai wakati wa ukame au katika joto kavu la kiangazi. Yaonekana aliteseka kiakili na kimwili pia. Lakini Zaburi 32 huonyesha kwamba kuteseka huko kwaweza kutulizwa kwa mtu kuungama dhambi kwa kutubu na kupokea msamaha wa Mungu.—Mithali 28:13.

Watu wabaya mara nyingi huteseka kwa ajili ya kufuatia mwendo wenye kukosa maadili, si kwa sababu ya adhabu ya kimungu. Herode Mkuu alikuwa na magonjwa mengi kwa sababu ya mazoea maovu. Katika siku zake za mwisho, Herode “alipatwa na mateso mabaya sana,” akasema mwanahistoria Myahudi Yosefo. “Alitamani sana kujikuna mwenyewe, matumbo yake yalikuwa na vidonda, na viungo vyake vya uzazi vilikuwa vimeoza na vyenye mabuu. Alijaribu bila mafanikio kutuliza kutweta na kutetemeka kwake katika zile chemchemi zenye ujoto katika Kaleroa. . . . Herode sasa alikuwa akiteseka maumivu mabaya sana hivi kwamba alijaribu kujichoma mwenyewe kwa kisu, lakini alizuiwa na binamu yake.”—Josephus: The Essential Writings, kilichotafsiriwa na kuhaririwa na Paul L. Maier.

Kushikamana na sheria ya Mungu huandaa ulinzi fulani dhidi ya mambo kama vile magonjwa yanayoambukizwa kingono. Hata hivyo, ni kwa nini watu wazuri wanaojaribu kupata kibali chake huonekana kana kwamba wanateseka zaidi?

Sababu Kwa Nini Watu Wenye Kumcha Mungu Huteseka

Sababu ya msingi kwa nini watu wenye kumcha Mungu huteseka ni kwamba wao ni waadilifu. Hilo linatolewa kielezi katika kisa cha Yusufu mwana wa mzee wa ukoo Yakobo. Ingawa mke wa Potifa aliendelea kumsihi Yusufu awe na uhusiano wa kingono pamoja na yeye, Yusufu alimwuliza hivi: “Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?” (Mwanzo 39:9) Hilo liliongoza kwenye kifungo cha gerezani kisichokuwa cha haki, na Yusufu aliteseka kwa sababu alikuwa mnyoofu.

Lakini ni kwa nini Mungu huwaruhusu watumishi wake waaminifu wateseke? Jibu limo katika lile suala lililotokezwa na yule malaika aliyeasi Shetani Ibilisi. Suala hilo linahusu uaminifu-maadili kwa Mungu. Tunajuaje hilo? Kwa sababu hilo lilionyeshwa katika kisa cha yule mwanamume mwadilifu Ayubu, aliyetajwa mapema zaidi.

Kwenye mkutano wa wana wa Mungu wa kimalaika mbinguni, Yehova alimwuliza Shetani hivi: “Je! umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu?” Jibu la Ibilisi linathibitisha kwamba kulikuwako na ushindani juu ya kama wanadamu wangedumisha uaminifu-maadili kwa Yehova chini ya jaribu. Shetani alidai kwamba Ayubu alimtumikia Mungu kwa sababu ya baraka za kimwili zilizoonewa shangwe na si kwa sababu ya upendo. Shetani kisha akasema: “Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.” Yehova akajibu: “Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe.”—Ayubu 1:6-12.

Ijapokuwa kila jambo ambalo Shetani angeweza kufanya, Ayubu alidumisha mwendo mwadilifu na akathibitisha kwamba alimtumikia Yehova kwa sababu ya upendo. Kwa kweli, Ayubu aliwaambia wenye kumshtaki hivi: “Hasha! nisiwahesabie ninyi kuwa na haki; hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu.” (Ayubu 27:5) Naam, washika uaminifu-maadili wa jinsi hiyo wamekuwa na nia sikuzote ya kuteseka kwa ajili ya uadilifu. (1 Petro 4:14-16) Biblia hutuambia juu ya wengi ambao wamekuwa wakimpenda Mungu daima na wameishi maisha yenye uadilifu ili kumheshimu na kuthibitisha kuwa bandia lile dai la Shetani kwamba angeweza kuwageuza wanadamu wote kutoka kwa Yehova. Kila mtu anayeteseka kwa sababu ya kudumisha uaminifu-maadili kwa Mungu aweza kufurahi kwamba anamthibitisha Ibilisi kuwa mwongo na anaufanya moyo wa Yehova ushangilie.—Mithali 27:11.

Mungu huhangaikia kuteseka kwa watumishi wake waaminifu. Mtunga zaburi Daudi alisema hivi: “BWANA [Yehova, NW] huwategemeza wote waangukao, huwainua wote walioinama chini.” (Zaburi 145:14) Wale waliojiweka wakfu kwa Yehova huenda wakakosa nguvu ya kibinafsi ya kutosha ili kuvumilia kule kuteseka maishani na ile minyanyaso wanayopata wakiwa watu wake. Lakini Mungu huwaimarisha na huwategemeza na kuwapa hekima inayohitajiwa ili kuvumilia majaribu yao. (Zaburi 121:1-3; Yakobo 1:5, 6) Ikiwa wanyanyasi wanawaua baadhi ya watumishi wa Yehova waaminifu-washikamanifu, watumishi hao wana lile tumaini la ufufuo la kupewa na Mungu. (Yohana 5:28, 29; Matendo 24:15) Hata kwa kadiri hiyo, Mungu aweza kuyapindua matokeo ya kuteseka kokote kunakowapata wale wampendao. Alikomesha kuteseka kwa Ayubu na akambariki sana mwanamume huyo mnyoofu. Na twaweza kuwa na uhakika kwamba Yehova hatawaacha watu wake katika siku yetu.—Ayubu 42:12-16; Zaburi 94:14.

Karibuni—Kuteseka Hakutakuwapo Tena!

Kwa hiyo, basi, kila mtu hupatwa na kuteseka kwa sababu ya kutokamilika kulikorithiwa na maisha katika mfumo huu mbovu wa mambo. Watu wenye kumcha Mungu waweza pia kutazamia kuteseka kwa sababu ya kudumisha uaminifu-maadili kwa Yehova. (2 Timotheo 3:12) Lakini wanaweza kushangilia, kwani Mungu hivi karibuni atakomesha machozi, kifo, maombolezo, kilio, na maumivu. Kwa habari hiyo, mtume Yohana aliandika hivi:

“Nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.”—Ufunuo 21:1-5.

Vivyo hivyo, mtume Petro alitangaza rasmi hivi: “Kama ilivyo ahadi yake [Yehova Mungu], tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.” (2 Petro 3:13) Ni mataraja matukufu kama nini yaliyoko mbele yetu tu! Maisha kwenye dunia-paradiso yaweza kuwa pendeleo lako lenye shangwe. (Luka 23:43) Kwa hiyo, usikuruhusu kuteseka kwa siku za leo kukutie uchungu. Badala ya hivyo, tazamia wakati ujao kwa maoni mazuri. Weka tumaini na uhakika wako katika ulimwengu mpya wa Mungu ulio karibu sana. Fuatia mwendo unaokubaliwa na Yehova Mungu, na unaweza kuishi milele katika ulimwengu ulio huru na kuteseka kote.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Ingawa Ayubu aliteseka, alifuatia mwendo uliokubaliwa na Mungu

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wewe waweza kuishi katika ulimwengu ulio huru na kuteseka kote

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Historia ya picha ya Collier ya Vita ya Ulaya

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki