Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 11/1 kur. 4-7
  • Ulimwengu Usio na Dhambi—Jinsi Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulimwengu Usio na Dhambi—Jinsi Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Dhambi Ni Nini?
  • Chanzo cha Dhambi
  • Jitihada za Binadamu za Kufuta Mbali Dhambi
  • Uhuru Kutoka Katika Dhambi
  • Wakati Dhambi Haitakuwapo Tena
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Dhambi
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Kuondoa Doa la Dhambi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Kwa Nini Watu Hufa?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 11/1 kur. 4-7

Ulimwengu Usio na Dhambi—Jinsi Gani?

VILIO vya sauti kubwa nyembamba vya kuomba msaada viliharibu utulivu wa saa za mapema za asubuhi moja ya kipupwe katika ujirani mmoja wa Tokyo wenye amani. Kwa muda wa dakika tano hadi kumi watu wengi walisikia mayowe ya kuhitaji msaada ya mwanamke mmoja mpelekea watu magazeti ya habari akiwa anafukuzwa akidungwa kisu tena na tena. Hakuna hata mmoja aliyejali vya kutosha kujaribu kujua lililokuwa likiendelea. Alikufa kutokana na kupoteza damu nyingi mno. “Kama mmoja wa watu hao angaliripoti tukio hilo kwa polisi mara aliposikia mwanamke huyo akipiga yowe,” akasema mpelelezi mmoja, “uhai wake ungaliokolewa.”

Ingawa wale waliokuwa wamemsikia mwanamke huyo aliyekuwa akifa hawakufanya jambo baya zaidi ya kumpuuza tu, je, wangeweza kudai kwa haki kwamba hawakuwa na hatia? “Dhamiri yangu ilinisumbua siku yote ya Ijumaa baada ya mimi kupata habari ya uuaji huo,” akasema mwanamume mmoja aliyekuwa amesikia vilio vya mwanamke huyo. Hilo latufanya tutake kujua, Kwa kweli dhambi ni nini?

Dhambi Ni Nini?

Akielekeza kwenye ufahamu wa udhambi, Hideo Odagiri, mhakiki wa fasihi na aliye profesa aliyestaafu kwenye Chuo Kikuu cha Hosei, Japani, alisema, kama ilivyonukuliwa katika gazeti la habari la Asahi Shimbun: “Siwezi kufuta mbali zile kumbukumbu dhahiri nilizo nazo za ufahamu wa dhambi, kama vile kule kujiona kubaya kuliko ndani ya mto-to, wivu wenye aibu, usaliti wa kichini-chini. Utambuzi huo ulikaziwa kikiki akilini mwangu nilipokuwa katika shule ya msingi na ungali ukinisumbua.” Je! umepata kupatwa na hisia hizo wakati wowote? Je! una sauti ya ndani inayokushutumu ukifanya jambo unalojua ni kosa? Labda hakuna uhalifu wowote ambao umefanywa, lakini hisia ya kutostarehe hukwamilia-kwamilia na kulemea akili yako. Hiyo ni dhamiri yako ikifanya kazi, na Biblia huitaja katika fungu la maneno lifuatalo: “Watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.” (Warumi 2:14, 15) Naam, kwa asili watu walio wengi husumbuliwa na matendo kama vile uzinzi, wizi, na kusema uwongo. Dhamiri yao inashuhudiza dhambi.

Hata hivyo, sauti ya dhamiri inapopuuzwa tena na tena, haitumiki tena ikiwa mwongozo salama. Yaweza kuwa sugu na kuchafuka. (Tito 1:15) Uwezo wa kuhisi lililo baya hupotezwa. Kwa kweli, dhamiri ya watu wengi leo imekufa kwa habari ya dhambi.

Je! dhamiri ndicho kipimio pekee cha dhambi, au kuna jambo fulani liwezalo kutumika kama kiwango kamili kuhusu dhambi na ni nini kisicho? Zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, Mungu aliwapa watu wake wateule mpangilio wa sheria, na kupitia Sheria hiyo, dhambi ilikuja “kutambuliwa kuwa dhambi.” (Warumi 7:13, New International Version) Hata mwenendo uliokuwa umekubalika kwa kadiri fulani hapo kwanza ulifunuliwa sasa kuwa jinsi ulivyokuwa—dhambi. Watu wa Mungu wateule, Waisraeli, walifunuliwa kuwa watenda dhambi na kwa hiyo walikuwa chini ya laana.

Ni zipi zile dhambi ambazo dhamiri yetu hutujulisha na ambazo Sheria ya Musa ilitaja mahususi na kuorodhesha? Katika utumizi wa Kibiblia wa neno hilo, dhambi humaanisha kukosa shabaha kwa habari ya Muumba. Lolote lisilopatana na utu, viwango, njia, na mapenzi yake ni dhambi. Hawezi kuendeleza uhai wa kiumbe chochote kinachoshindwa kufikia shabaha ambayo ameweka. Kwa hiyo mstadi mmoja wa sheria katika karne ya kwanza aliwaonya Wakristo Waebrania hivi: “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.” (Waebrania 3:12) Naam, ukosefu wa imani katika Muumba ni dhambi kubwa. Hivyo, mweneo wa dhambi kama inavyoelezwa katika Biblia ni mpana zaidi ya yale ambayo kwa kawaida huonwa kuwa dhambi. Biblia hufikia hatua ya kusema hivi: “Wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”—Warumi 3:23.

Chanzo cha Dhambi

Je! hilo lamaanisha kwamba mwanadamu aliumbwa akiwa mtenda dhambi? La, Yehova Mungu, Mwanzilishi wa uhai wa kibinadamu, alimfanya mtu wa kwanza akiwa kiumbe kikamilifu. (Mwanzo 1:26, 27; Kumbukumbu la Torati 32:4) Hata hivyo, wenzi wa ndoa wa kwanza wa kibinadamu walikosa shabaha walipokaidi lile katazo la pekee ambalo Mungu alikuwa ameweka, walipokula kutoka kwa ule “mti wa ujuzi wa mema na mabaya” uliokatazwa. (Mwanzo 2:17) Ingawa waliumbwa wakiwa wakamilifu, sasa walikosa shabaha ya utii kamili kwa Baba yao, wakawa watenda dhambi, na kwa hiyo wakahukumiwa kufa.

Historia hiyo ya kale inahusuje dhambi leo? Biblia hueleza hivi: “Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.” (Warumi 5:12) Sisi sote kabisa ni watenda dhambi kwa kurithi; kwa hiyo, tumekuja chini ya hukumu ya kifo.—Mhubiri 7:20.

Jitihada za Binadamu za Kufuta Mbali Dhambi

Adamu alipitisha dhambi kwa wazao wake, lakini alipitisha pia uwezo wa kupewa na Mungu wa dhamiri. Dhambi yaweza kusababisha hisia ya kutostarehe. Kama ilivyotajwa mbeleni, watu wamebuni njia mbalimbali za kuondosha hisia hizo. Hata hivyo, njia hizo ni zenye mafanikio?

Mashariki na Magharibi, watu wamejaribu kushughulika na matokeo ya dhambi kwa kubadili viwango vyao au kwa kukanusha kuwako kwenyewe kwa dhambi. (1 Timotheo 4:1, 2) Hali ya ainabinadamu yenye dhambi yaweza kufananishwa na ile ya mgonjwa mwenye homa. Dhambi yaweza kufananishwa na vairasi inayosababisha dalili za ugonjwa, hali dhamiri iliyosumbuliwa yaweza kufananishwa na homa hiyo isiyostarehesha. Kuvunja chombo cha kupimia joto hakubadili uhakika wa kwamba mgonjwa huyo ana homa kali. Kutupilia mbali viwango vya kiadili, kama vile wengi katika Jumuiya ya Wakristo wamefanya, na kupuuza ushuhuda wa dhamiri ya mtu mwenyewe hakutasaidia kufuta mbali dhambi yenyewe.

Mtu aweza kutumia kifuko chenye barafu ili kutuliza homa yake. Hiyo ni kama kujaribu kutuliza maumivu ya dhamiri kwa kufanya desturi za utakasaji kijuujuu tu. Kifuko chenye barafu chaweza kumfanya mwenye homa awe na baridi kwa muda mfupi, lakini hakiondoi kisababishi cha homa. Makuhani na manabii katika siku ya Yeremia walijaribu njia iyo hiyo ya kuponya Waisraeli wa wakati huo. Waliponya “vyepesi” majeraha ya watu ya kiroho na ya kiadili, wakisema, “Yote ni sawa, yote ni sawa.” (Yeremia 6:14; 8:11, An American Translation) Kufanya desturi za kidini kijuujuu tu na kukariri jambo kama vile “yote ni sawa” hakukuponya haribiko la kiadili la watu wa Mungu, na sherehe za utakasaji hazibadili kanuni za watu za kiadili leo.

Kwa kunywa dawa zinazopunguza homa huenda mtu akasababisha homa yake ipungue, lakini vairasi ingali mwilini mwake. Hivyo ndivyo ilivyo na njia ya Dini ya Confucius ya kushughulikia uovu kupitia elimu. Yaweza kusaidia watu kijuujuu wageuke kutoka uovu, lakini kuzoea li hukandamiza tu mwenendo wenye dhambi na hakumwondolei mtu mwelekeo wake wa udhambi aliozaliwa nao, ambao ndio kisababishi hasa cha mwenendo mwovu.—Mwanzo 8:21.

Namna gani fundisho la Dini ya Buddha la kuingia Nirvana ili kujiondolea mwenyewe mielekeo ya dhambi? Hali ya Nirvana, inayosemwa humaanisha “kuzima kwa kupulizia,” yadhaniwa kuwa haiwezi kufafanulika, ikiwa kuzimiwa kwa harara na tamaa yote. Wengine hudai kwamba ni kukoma kwa kuwako kwa mtu mmoja mmoja. Je! hilo halisikiki kana kwamba ni kumwambia mtu mgonjwa mwenye homa afe ili apate kitulizo? Isitoshe, kufikia hali ya Nirvana huonwa kuwa jambo gumu sana, hata lisilowezekana. Je! fundisho hilo lasikika kuwa lenye msaada kwa mtu mwenye dhamiri inayosumbuka?

Uhuru Kutoka Katika Dhambi

Ni wazi kwamba falsafa za kibinadamu kuhusu maisha na mielekeo ya dhambi zaweza, kwa kufaa zaidi, kutuliza tu dhamiri ya mtu. Haziondoi hali ya dhambi. (1 Timotheo 6:20) Je! kuna njia yoyote ya kuondoa hali hiyo? Katika Biblia, kitabu cha kale kilichoandikwa katika Mashariki ya Karibu, tunapata ufunguo wa uhuru kutoka katika dhambi. “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji . . . Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi.” (Isaya 1:18, 19) Hapo Yehova alikuwa akisema na Waisraeli, ambao, ingawa walikuwa watu wake wateule, walikuwa wamekosa shabaha ya uaminifu-maadili kwake. Hata hivyo, kanuni iyo hiyo huhusu ainabinadamu kwa ujumla. Kuonyesha nia ya kusikiliza maneno ya Muumba ndio ufunguo wa kufanya dhambi za mtu mwenyewe zisafishwe, kuoshwa kabisa.

Neno la Mungu hutuambia nini kuhusu kuoshwa kabisa kwa dhambi za ainabinadamu? Kama vile kupitia mtu mmoja ainabinadamu yote ilikuwa yenye kutenda dhambi, kupitia utii mkamilifu kwa Mungu wa mtu mwingine, ainabinadamu tiifu itaachiliwa huru kutoka huzuni yayo, Biblia husema. (Warumi 5:18, 19) Jinsi gani? “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8) Yesu Kristo, aliyezaliwa akiwa mwanamume mkamilifu asiye na dhambi, aliye sawa na Adamu wa hapo kwanza kabla ya yeye kutenda dhambi, alikuwa na uwezo wa kuchukua kabisa dhambi za ainabinadamu. (Isaya 53:12; Yohana 1:14; 1 Petro 2:24) Kwa kuuawa kwenye mti wa mateso kana kwamba alikuwa mhalifu, Yesu aliachilia huru ainabinadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na kifo. “Kwa maana,” akaeleza Paulo kwa Wakristo katika Roma, “hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. . . . Kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.”—Warumi 5:6, 21.

Kufa kwa Kristo kwa ajili ya ainabinadamu yote na kusawazisha mizani iliyopinduliwa na Adamu huitwa mpango wa “fidia.” (Mathayo 20:28) Yaweza kufananishwa na dawa inayofanya kazi dhidi ya vairasi inayosababisha homa. Kwa kutumia thamani ya fidia ya Yesu kwa ainabinadamu, hali ya ainabinadamu ya ugonjwa iliyosababishwa na dhambi—kutia na kifo chenyewe—yaweza kuponywa. Taratibu hiyo ya kuponya inaelezwa kitamathali katika kitabu cha mwisho cha Biblia: “Na upande huu wa mto na upande ule kulikuwa na miti ya uhai ikifanyiza mazao kumi na mawili ya tunda, ikitoa matunda yayo kila mwezi. Na majani ya miti yalikuwa kwa ajili ya kuponeshwa kwa mataifa.” (Ufunuo 22:2, New World Translation) Ebu wazia! Mto wa kitamathali wenye maji ya uhai ukitiririka kati ya miti ya uhai pamoja na majani yayo, yote kwa ajili ya kuiponesha ainabinadamu. Ishara hizo zilizopuliziwa roho kimungu huwakilisha uandalizi wa Mungu wa kuirudisha ainabinadamu kwenye ukamilifu kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu.

Njozi za kiunabii za kitabu cha Ufunuo zitakuwa mambo halisi hivi karibuni. (Ufunuo 22:6, 7) Ndipo, kwa utumizi kamili wa thamani ya dhabihu ya fidia ya Yesu kwa ainabinadamu, wote wenye mioyo ifaayo watakuwa wakamilifu na ‘watawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata waingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.’ (Warumi 8:21) Utimizo wa unabii mwingi wa Biblia huonyesha kwamba uhuru huo mtukufu u karibu. (Ufunuo 6:1-8) Hivi karibuni Mungu ataliondolea tufe uovu, na wanadamu watafurahia uhai wa milele kwenye dunia-paradiso. (Yohana 3:16) Huo kwa kweli utakuwa ulimwengu usio na dhambi!

[Picha katika ukurasa wa 7]

Dhabihu ya fidia ya Yesu itawezesha familia nyingi kama hii zionee shangwe furaha ya milele

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki