Wema Wapingana na Uovu—Vita Yenye Kudumu Muda Mrefu
KATIKA sinema za zamani, sikuzote mtu mwema ndiye alizishinda kani za uovu. Lakini uhalisi haujawa sahili hivyo. Mara nyingi sana katika ulimwengu halisi, uovu huonekana ndio unaoshinda.
Ripoti kuhusu matendo maovu ni sehemu ya kawaida ya habari za kila usiku. Katika kaskazini mwa United States, mwanamume mmoja wa Milwaukee aua kimakusudi watu 11 na kuweka akiba sehemu zilizobaki za miili yao iliyokatwa-katwa katika chombo chake cha barafu. Kusini mbali na hapo, mtu asiyejulikana aingia kwa kishindo ndani ya mkahawa wa Teksas na kuanza kufyatua bastola vyovyote kwa muda wa dakika kumi, akiwaua watu 23, kutia na yeye mwenyewe. Mpinzani mwenye kuudhika katika Korea awasha moto Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova, akiwaua waabudu 14.
Kuna vituko vya uovu vya mara moja moja na kuna uovu mwingine wenye kuhofisha unaoathiri ulimwengu—uuaji wa kimakusudi wa vikundi vya kijamii. Yakadiriwa kwamba Waarmenia milioni moja, Wayahudi milioni sita, na Wakambodia zaidi ya milioni moja wameangamizwa katika visa vya kijamii na vya kisiasa vya kuondolea mbali watu katika karne hii peke yayo. Ule uitwao eti usafishaji wa kikabila umewaumiza wengi katika iliyokuwa Yugoslavia. Hakuna ajuaye ni mamilioni mangapi ya watu wasio na hatia ambao wameteswa-teswa kikatili kotekote duniani.
Misiba ya jinsi hiyo hutulazimisha tukabili swali hili lenye kusumbua, Kwa nini watu hutenda katika njia hiyo? Hatuwezi kuondosha matendo hayo ya ukatili na kusema kuwa tu tokeo la watu wachache wenye kichaa. Mweneo tu wa uovu uliofanywa katika karne yetu wakanusha elezo hilo.
Tendo ovu lafasiliwa kuwa tendo lisilo sawa kiadili. Ni tendo linalofanywa na mtu anayeweza kuchagua kati ya kufanya mema na kufanya maovu. Kwa njia fulani uamuzi wake wa kiadili wapotoka na uovu unashinda. Lakini kwa nini hilo latokea na kwa jinsi gani?
Mara nyingi maelezo ya kidini kuhusu uovu hayaridhishi. Mwanafalsafa Mkatoliki Thomas Aquinas alidai kwamba “mambo mengi mazuri yangeondolewa ikiwa Mungu asingeruhusu uovu uweko.” Wanafalsafa wengi Waprotestanti wana maoni ayo hayo. Kwa mfano, kama ilivyotaarifiwa katika The Encyclopœdia Britannica, Gottfried Leibniz aliona uovu kuwa “jambo la kusawazisha tu wema uliomo ulimwenguni, ambao uovu unaongeza kwa kutofautisha.” Yaani, aliamini tunahitaji uovu ili tuweze kuthamini wema. Kusababu huko ni kama kumwambia mgonjwa mwenye kansa kwamba ugonjwa wake ni jambo linalohitajiwa tu ili kumfanya mtu mwingineye ahisi akiwa hai na mwenye afya njema kwelikweli.
Ni lazima makusudio maovu yatoke mahali fulani. Je! Mungu ni wa kulaumiwa kwa njia fulani isiyo ya moja kwa moja? Biblia inajibu hivi: “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.” Ikiwa Mungu si wa kulaumiwa, ni nani wa kulaumiwa? Mistari inayofuata hutoa jibu: “Kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” (Yakobo 1:13-15) Hivyo tendo ovu linazaliwa wakati tamaa mbovu inapositawishwa badala ya kukataliwa mbali. Hata hivyo, mengine zaidi yanahusika.
Maandiko yanaeleza kwamba tamaa mbovu zinatokea kwa sababu wanadamu wana kasoro ya msingi—kutokamilika kwa asili. Mtume Paulo aliandika hivi: “Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.” (Warumi 5:12) Kwa sababu ya dhambi iliyorithiwa, ubinafsi waweza kushinda fadhili katika kufikiri kwetu, na ukatili waweza kushinda huruma.
Bila shaka, watu wengi hujua kisilika kwamba mwenendo fulani si sawa. Dhamiri yao—au “torati iliyoandikwa mioyoni mwao” kama vile Paulo anavyoiita—inawazuia wasifanye tendo ovu. (Warumi 2:15) Bado, mazingira yenye ukatili yanaweza kukandamiza hisi hizo, na dhamiri yaweza kufishwa ikipuuzwa tena na tena.a—Linganisha 1 Timotheo 4:2.
Je! kutokamilika pekee kwa mwanadamu kwaweza kueleza sababu ya uovu uliopangwa wa wakati wetu? Mwanahistoria Jeffrey Burton Russell alionelea hivi: “Ni kweli kwamba kuna uovu ndani ya kila mmoja wetu, lakini kujumlisha pamoja hata hesabu kubwa-kubwa za mauovu moja moja hakuelezi sababu ya Auschwitz . . . Uovu wa kadiri hiyo waonekana kuwa wenye hali pamoja na kiasi tofauti.” Si mwingine ila Yesu Kristo aliyeonyesha chanzo cha uovu huo wenye hali tofauti.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yesu alieleza kwamba watu waliokuwa wakipanga kumwua hawakuwa wakitenda kwa hiari yao wenyewe kabisa. Kani isiyoonekana iliwaongoza. Yesu aliwaambia hivi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli.” (Yohana 8:44) Kwa wazi, Ibilisi, ambaye Yesu aliita “mkuu wa ulimwengu huu,” ndiye aliye na fungu mashuhuri katika kuchochea uovu.—Yohana 16:11; 1 Yohana 5:19.
Kutokamilika kwa kibinadamu pamoja na uvutano wa kishetani vimetokeza kuteseka kwingi kwa muda wa maelfu ya miaka. Na hakuna ishara yoyote kwamba mshiko wavyo juu ya ainabinadamu unalegea. Je! uovu upo kwa kudumu? Au kani za wema hatimaye zitaondolea mbali uovu?
[Maelezo ya Chini]
a Watafiti wameona hivi majuzi uhusiano kati ya jeuri inayoonyeshwa waziwazi kwenye televisheni na uhalifu wa vijana. Maeneo yenye uhalifu mwingi na familia zilizovunjika ni visababishi pia vya mwenendo wenye kudhuru jamii. Katika Ujerumani wa Nazi propaganda ya daima ya ubaguzi wa jamii iliongoza watu fulani watetee—na hata kutukuza—matendo ya ukatli dhidi ya Wayahudi na Waslavi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Jalada: U.S. Army photo
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
U.S. Army photo