Kukawia Kulifisha!
FAMILIA tatu, watu wazima saba na watoto sita, walipiga mbio kufa na kupona ili kuokoa uhai wao. Yaonekana walikuwa wamesongamana katika himaya ya nyumba ya mtu fulani, wakitumaini kuokoka mvua ya mawe yenye kuogofya. Lakini ngurumo ya mawe yenye kuanguka ilipopungua, ogofyo jipya likaja—wingu jeusi la majivu yenye kusonga pumzi. Sasa hakukuwa na la kufanya ila kupiga mbio.
Mwenye kuongoza alikuwa mwanamume, labda mtumishi, aliyepiga mbio akiwa na mfuko wenye maandalizi begani pake. Alifuatwa na wavulana wawili, mmoja akiwa na karibu miaka minne, na yule mwingine akiwa na miaka mitano, wakipiga mbio wakiwa wameshikana mikono. Wale wengine wakafuata—wakiwa wameshikwa na woga mkuu, waking’ang’ana, wakijikwaa, wakijaribu kuponyoka kwa kila njia. Walijaribu kupumua, lakini badala ya hewa, walipumua majivu yenye unyevunyevu. Mmoja baada ya mwingine, wote 13 wakaanguka na kutulia tuli na hatimaye wakazikwa na majivu yaliyokuwa yakianguka. Mabaki yao yenye kusikitisha yalifichwa mpaka wanaakiolojia waliyafukua karibu miaka 2,000 baadaye wakapata kujua habari zote zenye kuhuzunisha juu ya dakika zao za mwisho.
Wale 13 wenye kupatwa na msiba huo walikuwa wachache tu miongoni mwa karibu 16,000 walioangamia katika jiji la kale la Pompeii, Italia, katika Agosti 24, 79 W.K. Wengi waliokoka kwa kulikimbia jiji hilo wakati Mlima Vesuvius ulipolipuka kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, wale waliokawia—hasa matajiri ambao hawakutaka kuacha makao na mali zao—walizikwa chini ya meta 6 ya miamba na majivu.
Lile lililotukia katika Pompeii miaka karibu 2,000 iliyopita huenda ikawa historia ya kale. Lakini linalingana katika njia nyingi na hali inayoipata jamii nzima ya wanadamu leo. Ishara ya duniani pote, yenye kuogofya zaidi ya zile ngurumo za Mlima Vesuvius, inaonya kwamba utaratibu wa ulimwengu huu uliopo unakabili uharibifu ulio karibu sana. Ili kuokoka, ni lazima tutende mara ii hii. Kukawia kunafisha. Kujua ishara hiyo ni nini hasa na jinsi sisi tunavyoweza kuiitikia kwa hekima ndiyo habari ya makala yetu inayofuata.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Picha ya Jalada ni ya National Park Service
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Soprintendenza Archeologica di Pompei