Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/8 kur. 22-25
  • Pompeii—Mahali Palipobaki Vilevile

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pompeii—Mahali Palipobaki Vilevile
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mlipuko wa 79 W.K.
  • Hakuna Usalama Katika Herculaneum
  • Mambo Yalibaki Vilevile
  • Maisha ya Kibinafsi
  • Ni Wakati wa Kutenda
  • Huu Ndio Wakati Muhimu Zaidi wa Kukaa Macho!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Kukawia Kulifisha!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1997
  • Kuishi Karibu na Jitu Linalolala
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/8 kur. 22-25

Pompeii—Mahali Palipobaki Vilevile

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

MAJIKO yaliyo na sufuria mekoni, maduka yenye bidhaa za kutosha, chemchemi zisizo na maji, barabara zikiwa sawa—kila kitu kiko vile kilivyokuwa, katika jiji lisilo na wakazi, lililo tupu na lililoachwa. Hilo ni Pompeii, mahali ambapo yaonekana palibaki vilevile.

Kila kitu chabaki vile kilivyokuwa siku hiyo yenye msiba zaidi ya miaka 1,900 iliyopita wakati ambapo Mlima Vesuvius, volkeno inayoelekeana na ghuba ya Naples, ulilipuka. Ukazika Pompeii, Herculaneum, Stabiae, na sehemu za mashambani zilizoyazunguka kwa majivu na lava.

“Wakale hao,” chasema kitabu Pompei, “hawakujua sana kuhusu asili ya kivolkeno ya mlima Vesuvius nao walizoea kuufikiria kuwa mlima wenye mimea mibichi ambapo miti mingi ilichangamana na mashamba yenye kupendeza ya mizabibu.” Lakini mnamo Agosti 24, 79 W.K., baada ya unyamavu wa miaka mingi, mlima huo uliamka kwa mlipuko mkubwa sana.

Mlipuko wa 79 W.K.

Volkeno hiyo ilitokeza safu ya gesi, magima, na takataka zilizotia anga giza na kusababisha mvua mbaya sana ya majivu na lapila (vipande vidogo vya lava). Kwa muda wa siku mbili Pompeii na eneo kubwa sana la mashambani lilifunikwa kwa tabaka nene, kwa kina cha wastani wa meta 2.5. Huku mitetemeko yenye nguvu nyingi ikiendelea kutikisa ardhi, wingu kubwa mno la gesi yenye sumu, lisiloonekana lakini lenye kufisha, lilifunika jiji, likilishika kama kwamba kwa kumbatio la kifo. Pompeii lilipokuwa likizikwa polepole, Herculaneum lilitokomea mara moja. Kulingana na kitabu Riscoprire Pompei (Kuvumbua Pompeii Tena), Herculaneum lilizamishwa katika mtiririko wa “matope na takataka za kivolkeno kwa kina kilichofika meta ishirini na mbili karibu na ufuoni.”

Maitikio ya wakazi wa Pompeii wapatao 15,000 yalitofautiana. Ni wale waliotoroka tu waliofaulu kujiokoa. Hata hivyo, yakadiriwa kwamba wengine wakiwa hawataki kuacha nyumba zao na vitu vilivyokuwamo, walibaki, wakitumaini kuepuka hatari hiyo. Wengine, wakihangaikia kuokoa vitu vyao vya thamani, walisita kabla ya kuamua kuondoka, lakini wakapondwa na paa za nyumba zao, ambazo ziliporomoka kwa sababu ya uzito wa majivu.

Kielelezo kimoja ni mwenye “nyumba ya Faun,” ambaye kwa wazi hakuwa tayari kuacha utajiri wake. “Kwa haraka yote,” asema Robert Étienne katika kitabu chake La vie quotidienne à Pompéi (Maisha ya Kila Siku Pompeii), “bibi wa nyumba hiyo alikusanya vito vyake vyenye thamani zaidi—vikuku vya dhahabu vyenye umbo la nyoka, pete, pini za nywele, vipuli, kioo cha fedha, mfuko uliojaa sarafu za dhahabu—na kujitayarisha kutoroka.” Akihofishwa labda na majivu yenye kunyesha, alibaki ndani ya nyumba. “Muda mfupi baada ya hapo.” aendelea Étienne, “paa iliporomoka, ikizika mwanamke huyo wa kuhuzunikiwa na hazina zake.” Wengine walikufa kwa kusongwa pumzi na gesi zenye sumu zilizoenea kila mahali.

Waliositasita walilazimika kukimbia ili kuokoa uhai wao, juu ya tabaka ya majivu ya lava iliyofanyizwa wakati huo. Walikufa mahali walipoanguka, wakiwa wamesongwa pumzi kwa gesi zenye sumu na kufunikwa na mvua yenye kuendelea kunyesha ya majivu mororo. Miili yao yenye kuhuzunikiwa ilipatikana karne nyingi baadaye, vitu vyao vya thamani vikiwa kando yao. Jiji hilo na wakazi walo lilizikwa chini ya tabaka ya jivu ya kina cha meta sita.

Hata hivyo, kwa sababu ya mvua hiyo ya majivu yenye kufisha, hata wakazi wa jiji wameonekana tena. Je, wajua ni kwa jinsi gani? Tazama mifano ya miili yao pichani kwenye ukurasa huu. Ilitokezwaje? Kwa kumwaga plasta katika vishimo vilivyoachwa katika jivu na mnofu uliooza, waakiolojia wametuwezesha kuona ishara za mwili za mwisho zenye maumivu za wahasiriwa hao maskini—“mwanamke kijana anayelala akiwa ameshika kichwa chake; mwanamume, mdomo wake ukiwa umefunikwa kwa kitambaa cha mkono ambacho hakingeweza kuzuia mpumuo wa vumbi na gesi zenye sumu; wahudumiaji wa mahali pa mazoezi na pa kuogea, wakiwa wameanguka katika vikao vya mshtuko na mpindano kwa sababu ya ukosefu wa hewa; . . . mama akimkumbatia binti yake mdogo katika kumbatio la mwisho lenye huruma ambalo ni bure.”—Archeo.

Hakuna Usalama Katika Herculaneum

Katika Herculaneum, kilometa chache kutoka Pompeii, wale ambao hawakutoroka mara moja walijipata wamenaswa. Wengi waliharakisha kuelekea ufuoni, labda wakitumaini kutoroka kwa njia ya bahari, lakini tetemeko kali la bahari lilizuia mashua kuondoka. Uchimbuzi wa hivi majuzi kwenye ufuo wa kale wa Herculaneum umetokeza zaidi ya viunzi vya mwili 300. Walipokuwa wakitafuta kimbilio chini ya pango linaloelekeana na bahari, watu hawa walizikwa wakiwa hai na mtiririko mbaya sana wa matope na takataka za kivolkeno. Hapa, pia, wengi walikuwa wamejaribu kuokoa mali zao zenye thamani zaidi: virembeshi vya dhahabu, vyombo vya fedha, seti kamili ya vifaa vya upasuaji—vyote bado viko hapo, vikiwa haviwezi kusaidia chochote, karibu na miili ya wenye kuvimiliki.

Mambo Yalibaki Vilevile

Pompeii hutoa ushahidi wa wazi wa hali ya kuharibika upesi ya uhai unapokabili kani za asili. Tofauti na mahali penginepo pote pa kiakiolojia ulimwenguni, magofu ya Pompeii na viunga vyalo huandaa wonyesho unaowezesha wasomi wa kisasa na wadadisi kuchunguza maisha ya kila siku katika karne ya kwanza W.K.

Ufanisi wa eneo hilo ulitegemea hasa kilimo, viwanda na biashara. Likiwa na wafanyakazi wengi—watumwa na watu huru walioajiriwa siku kwa siku—eneo la mashambani lenye rutuba lilitokeza mazao kwa wingi. Utendaji mwingi wa jijini ulihusiana na uuzaji wa vyakula. Mtu yeyote anayezuru Pompeii aweza bado kuona vinu vya kusagia mahindi, soko la mboga, na maduka ya wauzaji wa matunda na wafanyabiashara wa divai. Waweza kuona majengo yaliyotumiwa wakati mmoja kwa ajili ya biashara—kwa ajili ya kuchakata sufu na kitani na kwa kusokota na kufuma vitambaa kwa kiwango cha viwanda. Dazani za viwanda vinginevyo vya kiwango kidogo, kuanzia na karakana ya mtengenezaji wa vito hadi duka la vifaa vya chuma, majengo haya, pamoja na nyumba, yalifanyiza jiji.

Barabara nyembamba zilizosongamana watu wakati mmoja zimewekwa matufali ya mawe. Kando yazo kuna vijia vilivyoinuliwa na chemchemi za umma zilizotoa maji katika mfumo wa mfereji wa maji uliotengenezwa kwa busara. Jambo lisilo la kawadia na lenye kupendeza laweza kuonwa kwenye pembe za barabara kuu. Kama vitangulizi vya vivuka-barabara vya kisasa, matufali makubwa ya mawe yaliyowekwa katikati ya barabara yalirahisisha mtiririko wa wenye kutembea na kuwasaidia kutoloa miguu kuliponyesha. Watu wowote walioendesha mikokoteni jijini walilazimika kuwa na ustadi fulani wa akili ili kuepuka matufali hayo yaliyoinuliwa. Bado yapo! Hakuna kilichobadilika.

Maisha ya Kibinafsi

Hata hali ya Wapompeii ya kutotaka maisha yao ya kibinafsi kujulikana haiwezi kuwazuia wasitazamwe na watu wa nyakati za kisasa. Mtu aweza kumwona mwanamke aliyefunikwa kwa vito vyenye fahari amelala akiwa mfu mikononi mwa mpiganaji katika makao yake. Milango ya nyumba na maduka iko wazi kabisa. Majiko yanaonekana wazi, kama kwamba yaliachwa dakika chache zilizopita, kukiwa na sufuria mekoni, mkate usiopikwa bado ukiwa kwenye jiko la kuokea, na mitungi mikubwa ikining’inia ukutani. Kuna vyumba vilivyopambwa kwa kusiribiwa vizuri, michoro ya ukutani, usanii wa mozeiki, ambapo matajiri walifanya karamu kwa ustarehe, wakitumia vikombe vya fedha na vyombo vya ustaarabu. Bustani tulivu za ndani zimezungukwa na safu ya nguzo na kupambwa kwa chemchemi zenye kupendeza ambazo hazifanyi kazi tena. Zinazoonekana pia, ni sanamu za marumaru na shaba zilizotengenezwa kwa njia nzuri sana na madhabahu za miungu ya nyumba.

Hata hivyo, mtindo-maisha wa wengi ulikuwa wa kiasi zaidi. Wengi ambao hawakuwa na vifaa vya kupikia nyumbani walizoea kwenda kwenye mikahawa. Huko, bila kulipa fedha nyingi, waliweza kupiga porojo, kucheza kamari, au kununua chakula na kinywaji. Baadhi ya mahali hapa lazima palikuwa mahali penye sifa mbaya ambapo, baada ya kuandaa vinywaji kwa wateja, wahudumiaji wa kike, ambao mara nyingi walikuwa wasichana watumwa, walifanya kazi ya ukahaba. Licha ya mikahawa mingi sana ya aina hii, uchimbuzi umefunua mahali pengine pengi zaidi penye sifa mbaya, mara nyingi pakiwa na michoro na maandishi machafu sana.

Ni Wakati wa Kutenda

Uharibifu wa ghafula wa Pompeii hufanya mtu afikiri. Bila shaka, maelfu ya waliotokomea huko hawakuitikia kwa uharaka wa kutosha maonyo ya msiba uliotisha kutokea—matetemeko ya dunia yenye kurudia-rudia, milipuko ya volkeno, na mvua mbaya sana ya lapila. Wao walisitasita labda kwa sababu hawakutaka kuacha maisha yao ya starehe na mali zao. Huenda walitumaini kwamba hatari hiyo ingepita au kwamba kungekuwa bado na wakati wa kutoroka ikiwa mambo yangekuwa mabaya. Kwa kuhuzunisha, walikosea.

Maandiko hutuarifu kwamba leo ulimwengu wote uko katika hali kama hiyo. Jamii yenye ufisadi ambayo twaishi ndani yayo imetengwa na Mungu. Iko karibu kufagiliwa mbali kwa ghafula. (2 Petro 3:10-12; Waefeso 4:17-19) Uthibitisho wote huonyesha kwamba wakati huo uko karibu. (Mathayo 24:3-42; Marko 13:3-37; Luka 21:7-36) Na mabaki yenye kuhuzunisha ya Pompeii yabaki yakiwa shahidi aliye kimya kwa kosa la kusitasita.

[Sanduku katika ukurasa wa24]

Misalaba ya Wakristo?

Kupatikana kwa misalaba kadhaa katika Pompeii, kutia ndani mmoja katika kazi ya kusiriba kwenye ukuta wa mahali pa kuokea mikate, kumefasiliwa na wengine kuwa uthibitisho wa kuwapo kwa Wakristo katika jiji hilo kabla ya uharibifu walo katika 79 W.K. Je, hili ni kisio la kweli?

Bila shaka sivyo. Tukitaka kupata “ibada iliyokomaa ya msalaba,” asema Antonio Varone katika kitabu chake Presenze giudaiche e cristiane a Pompei (Kuwapo kwa Wayahudi na Wakristo katika Pompeii), “twahitaji kungojea hadi karne ya nne, wakati ambapo kugeuzwa imani kwa maliki na wapagani wengi kungetokeza kuabudu msalaba kupatana na hali yao ya kiroho.” “Hata katika karne za pili na tatu na hadi wakati wa Konstatino,” aongeza Varone, “ni nadra sana kupata msalaba ukihusiana kwa wazi na Ukristo.”

Ikiwa vyanzo vyayo si Ukristo mifano hiyo ilitoka wapi? Kando na shaka kuhusu utambulisho wa mfano huu uliofikiriwa kuwa msalaba na ugunduzi wa mchoro wa mungu katika namna ya nyoka katika mahali papo hapo pa kuokea mikate, kuna “vitu vilivyopatwa vilivyo vichafu sana ambavyo ni vigumu kuvihusianisha na inayofikiriwa kuwa hali ya kiroho ya Kikristo ya mpangaji wa mahali hapo pa kuokea mikate,” asema Varone. Yeye aongeza: “Inajulikana kwamba tangu mwanzo wa ustaarabu, kabla ya kupata kuwa ishara ya kuokolewa, mfano wenye umbo la msalaba ulitumiwa ukiwa na umaana wa wazi wa kiuchawi na sherehe za ibada.” Katika nyakati za kale, aeleza msomi huyu, msalaba ulionwa kuweza kuwinga au kuharibu uvutano mwovu nao ulitumiwa, zaidi ya kitu kinginecho chote, kuwa hirizi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Tao la Caligula Mlima Vesuvius ukiwa katika mandhari-nyuma

[Picha katika ukurasa wa 23]

Juu: Mifano ya wakazi wa Pompeii iliyofanyizwa kwa plasta

Kushoto: Mwono wa Tao la Nero na sehemu ya hekalu la Sumbula

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Mipaka iliyo wima: Glazier

Picha kwenye kurasa 2 (chini), 22, na 23: Soprintendenza Archeologica di Pompei

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki