Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w93 4/1 kur. 13-18
  • Ni Nani Wanaoifuata Nuru ya Ulimwengu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nani Wanaoifuata Nuru ya Ulimwengu?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wapendao Giza
  • Huruma ya Yesu
  • Kuwakusanya Wachukuaji Nuru
  • Kuiangaza Nuru ya Ufalme
  • Ulimwengu Mpya Uliotiwa Nuru
  • Ni Jambo la Muhimu Kufuata Nuru
  • Fuata Nuru ya Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • “Nuru Imekuja Ulimwenguni”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • “Kuzivaa Silaha Za Nuru”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Wachukuaji Nuru—Kwa Kusudi Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
w93 4/1 kur. 13-18

Ni Nani Wanaoifuata Nuru ya Ulimwengu?

“Mnang’aa kama wamulikaji ulimwenguni.”—WAFILIPI 2:15, NW.

1. Biblia husema nini juu ya nuru bandia za kidini?

BIBLIA humtambulisha Yesu kwa wazi kuwa “nuru kuu,” “nuru ya ulimwengu.” (Isaya 9:2; Yohana 8:12) Hata hivyo, ni wachache kwa kulinganisha waliomfuata alipokuwa duniani. Walio wengi walichagua kufuata nuru bandia, watu ambao kwa uhalisi walikuwa wachukuaji giza. Neno la Mungu husema hivi juu yao: “Watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”—2 Wakorintho 11:13-15.

2. Ni nini ambacho Yesu alisema kingekuwa ndio msingi wa kuwahukumu watu?

2 Hivyo, si wote wanaotaka nuru, hata ingawa hiyo ni nzuri ajabu. Yesu alisema hivi: “Hili ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, ili matendo yake yasije yakakemewa.”—Yohana 3:19, 20.

Wapendao Giza

3, 4. Viongozi wa kidini katika siku ya Yesu walionyeshaje kwamba hawakutaka kuifuata nuru?

3 Fikiria jinsi hilo lilivyokuwa kweli Yesu alipokuwa duniani. Mungu alikuwa amemwezesha Yesu afanye miujiza yenye kusisimua ikiwa njia ya kuthibitisha kwamba Yesu alikuwa Mesiya. Kwa kielelezo, katika siku moja ya Sabato, alirudisha uwezo wa kuona wa mtu aliyezaliwa kipofu. Jinsi lilivyokuwa tendo la ajabu la rehema! Mtu huyo alishukuru kama nini! Yeye angeweza kuona kwa mara ya kwanza maishani mwake! Lakini itikio la viongozi wa kidini lilikuwa nini? Yohana 9:16 husimulia hivi: “Baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato.” Jinsi mioyo yao ilivyokuwa imepotoka! Ponyo la kustaajabisha lilikuwa limetokea, lakini badala ya kuonyesha shangwe kwa yule mtu aliyekuwa kipofu hapo kwanza, na kuonyesha uthamini kwa mponyaji wao walimshutumu Yesu! Kwa kufanya hivyo, bila shaka walitenda dhambi dhidi ya wonyesho dhahiri wa roho takatifu ya Mungu, dhambi isiyosameheka.—Mathayo 12:31, 32.

4 Baadaye, wakati wanafiki hao walipomhoji yule mtu aliyekuwa kipofu hapo kwanza juu ya Yesu, mtu huyo alisema hivi: “Hii ni ajabu! kwamba ninyi hamjui atokako [Yesu], naye alinifumbua macho! Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo. Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.” Viongozi wa kidini waliitikiaje? “Wakajibu, wakamwambia, Ama! wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje.” Walikosa huruma kama nini! Walikuwa na mioyo migumu. Kwa hiyo Yesu aliwaambia kwamba ingawa wangeweza kuona kwa macho yao ya kimwili walikuwa vipofu kiroho.—Yohana 9:30-41.

5, 6. Viongozi wa kidini wa karne ya kwanza walifanya nini kingine kilichoonyesha kwamba walipenda giza?

5 Jambo la kwamba wanafiki hao wa kidini walikuwa wakitenda dhambi dhidi ya roho ya Mungu laweza kuonekana wazi kwenye pindi nyingine, wakati Yesu alipomfufua Lazaro kutoka kwa wafu. Kwa sababu ya muujiza huo, watu wengi wa kawaida walimwamini Yesu. Hata hivyo, ona kile ambacho viongozi wa kidini walifanya. “Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu.” (Yohana 11:47, 48) Walikuwa wakihangaikia vyeo na umashuhuri wao. Yajapokuwa matokeo, wao walitaka kuwapendeza Warumi, si Mungu. Kwa hiyo, walifanya nini? “Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua [Yesu].”—Yohana 11:53.

6 Je! yalikuwa ni hayo tu? La. Kile walichofanya baada ya hapo chaonyesha jinsi walivyopenda giza sana: “Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.” (Yohana 12:10, 11) Huo ni uovu mkubwa jinsi gani! Ingawa walifanya yote hayo ili kulinda vyeo vyao, ni nini kilichotukia? Katika kizazi hichohicho, waliasi dhidi ya Warumi, waliokuja dhidi yao katika 70 W.K. wakachukua mahali pao, taifa lao, na uhai wao pia!—Isaya 5:20; Luka 19:41-44.

Huruma ya Yesu

7. Kwa nini wapendao kweli walimiminika kwa Yesu?

7 Kwa hiyo katika wakati wetu pia, si wote wanaotaka kutiwa nuru kiroho. Lakini wale wanaopenda kweli wanataka kuijia nuru. Wao wanataka Mungu awe Mwenye Enzi Kuu wao, nao wanamgeukia Yesu kwa hamu, yule ambaye Mungu amemtuma kueleza nuru ni nini, na wanamfuata. Ndivyo watu wanyenyekevu walivyofanya wakati Yesu alipokuwa duniani. Walimiminika kwake. Hata Mafarisayo walilazimika kukubali hilo. Walilalamika hivi: “Ulimwengu umekwenda nyuma yake.” (Yohana 12:19) Watu wenye mfano wa kondoo walimpenda Yesu kwa sababu alikuwa tofauti na wale viongozi wa kidini wenye ubinafsi, wafidhuli, na wenye hamu ya uongozi, ambao Yesu alisema hivi juu yao: “Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu.”—Mathayo 23:4, 5.

8. Tofauti na wanafiki wa kidini, Yesu alikuwa na mtazamo gani?

8 Kwa kutofautisha, ona mtazamo wa Yesu wenye huruma: “Alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.” (Mathayo 9:36) Naye alifanya nini juu ya hilo? Alisema hivi kwa wale waliokuwa wamenyonywa na mfumo wa Shetani: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” (Mathayo 11:28-30) Yesu alifanya yale yaliyotabiriwa juu yake kwenye Isaya 61:1, 2, linalosomwa hivi: “Roho ya Bwana MUNGU [Yehova, NW] i juu yangu; kwa sababu BWANA [Yehova, NW] amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA [Yehova, NW] uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao.”

Kuwakusanya Wachukuaji Nuru

9. Ni mambo gani yenye kutokeza yaliyotukia katika 1914?

9 Baada ya kupaa kwake mbinguni, Yesu alihitaji kungojea mpaka wakati ulipowadia wa Mungu kumpa yeye mamlaka ya Ufalme. Kisha angewagawanya “kondoo” kutoka kwa “mbuzi.” (Mathayo 25:31-33; Zaburi 110:1, 2) Wakati huo ulifika wakati “siku za mwisho” zilipoanza katika 1914. (2 Timotheo 3:1-5) Yesu, akiwa amepewa mamlaka awe Mfalme wa Ufalme wa Mungu wa kimbingu, alianza kukusanya kwenye mkono wake wa kuume wa upendeleo wale waliotaka kuifuata nuru. Baada ya Vita ya Ulimwengu 1, kazi hiyo ya kugawanya iliendelea kwa mwendo wenye kuongezeka.

10. Ni swali jipi liwezalo kuulizwa juu ya wale ambao Yesu anatumia katika kazi ya kukusanya?

10 Chini ya uongozi wa Kristo Yesu, kazi ya kukusanya imethawabishwa na mafanikio makubwa. Katika historia yote hakujapata kuwako watu wengi hivyo kutoka kwa mataifa mengi tofauti-tofauti wanaoshirikiana pamoja katika ibada ya kweli iliyotiwa nuru. Na ni nani leo wanaoifuata ile nuru inayotoka kwa Mungu na Kristo? Ni nani wanaofanya kama Wafilipi 2:15 (NW), lisemavyo, ‘kung’aa kama wamulikaji ulimwenguni,’ wakiwaalika wengine ‘waje na wayatwae maji ya uzima bure’?—Ufunuo 22:17.

11. Msimamo wa Jumuiya ya Wakristo ni nini kuhusiana na nuru ya kiroho?

11 Je! Jumuiya ya Wakristo inafanya hivyo? Jumuiya ya Wakristo, pamoja na dini zayo zenye migawanyiko, kwa hakika haing’ai ikiwa kimulikaji. Kwa kweli, makasisi wako kama wale viongozi wa kidini katika siku ya Yesu. Hawaiangazi nuru ya kweli kutoka kwa Mungu na Kristo. Miaka 33 iliyopita, gazeti Theology Today lilisema hivi: “Kwa kusikitisha ni lazima ikubaliwe kwamba nuru hiyo haiangazi Kanisani kwa uangavu wa kutosha. . . . Kanisa limeelekea zaidi na zaidi kufanana na jumuiya zinazolizunguka. Kuliko kuwa nuru ya ulimwengu Kanisa huziangaza nuru zinazotoka katika ulimwengu wenyewe.” Na hali ya Jumuiya ya Wakristo ni mbaya hata zaidi leo. Ile iitwayo eti nuru ambayo inaangaza kutoka kwa ulimwengu kwa kweli ni giza kwa sababu hilo tu ndilo jambo ambalo Shetani na ulimwengu wake waweza kutoa. La, hakuna nuru ya kweli inayotoka kwa dini za Jumuiya ya Wakristo zinazopingana na zilizo za kilimwengu kabisa kabisa.

12. Ni nani hufanyiza tengenezo la kweli linalochukua nuru leo?

12 Inaweza kusemwa kwa uhakika kwamba ni Jamii ya Ulimwengu Mpya ya Mashahidi wa Yehova ambayo ndiyo tengenezo la kweli linalochukua nuru leo. Katika njia ya umoja, washiriki wayo wote—wanaume, wanawake, na watoto pia—huacha nuru yao kutoka kwa Yehova na Kristo iangaze mbele ya ainabinadamu yote. Mwaka uliopita, katika makundi karibu 70,000 ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote, wachukuaji nuru waliozidi sana milioni nne walikuwa wakiwaambia wengine kwa bidii juu ya Mungu na makusudi yake. Na kila mwaka sasa, tunaona ukusanyaji mkubwa unaoendelea wa watu wanaotaka kuelimishwa kiroho. Mamia ya maelfu wanabatizwa baada ya kujifunza Biblia na kupata ujuzi sahihi wa kweli. Kwa kweli, mapenzi ya Mungu ni kwamba “watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.”—1 Timotheo 2:4.

13. Twaweza kulinganisha na nini ile nuru inayotoka kwa Yehova?

13 Tunaweza kulinganisha mnurisho unaotoka kwa Yehova sasa na yale yaliyotukia wakati watu wa Mungu wa nyakati za kale walipoondoka Misri: “BWANA [Yehova, NW] naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku.” (Kutoka 13:21, 22) Wingu wakati wa mchana na moto wakati wa usiku kutoka kwa Mungu ilikuwa miongozo yenye kutegemeka. Ilikuwa yenye kutegemeka kama vile jua lililoumbwa na Mungu ili kutuandalia saa za mchana. Vivyo hivyo, tunaweza kumtegemea Yehova kuendelea kuwaangazia njia kiroho watafutaji kweli katika siku hizi za mwisho zilizo mbovu. Mithali 4:18 hutuhakikishia hivi: “Njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu.”

Kuiangaza Nuru ya Ufalme

14. Ni nini lazima liwe ndilo kusudi kuu la wachukuaji nuru?

14 Ingawa Yehova ndiye Chanzo cha mnurisho, na Kristo ndiye Mwangazi Mkuu wa nuru hiyo, ni lazima wafuasi wa Yesu waiangaze pia. Yeye alisema hivi kuhusu wao: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. . . . Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:14, 16) Na ni nini kilichokuwa kichwa kikuu cha nuru hiyo ambayo wafuasi wake wangeangaza mbele za ainabinadamu? Walipaswa wafundishe nini katika upeo huu wa historia ya ulimwengu? Yesu hakusema kwamba wafuasi wake wangehubiri demokrasia, udikteta, muungano wa Kanisa na Serikali, au itikadi nyingineyo yote ya kilimwengu. Badala yake, kwenye Mathayo 24:14 alitabiri kwamba kujapokuwa na upinzani kutoka ulimwenguni pote, “habari njema ya ufalme [ingehubiriwa] katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho [ungekuja].” Hivyo, wachukuaji nuru leo huwaambia wengine kuhusu Ufalme wa Mungu, utakaoleta mwisho wa ulimwengu wa Shetani na kuleta ulimwengu mpya wenye uadilifu.—1 Petro 2:9.

15. Wale wanaoipenda nuru watageukia wapi?

15 Wale wapendao nuru hawatakengeushwa na madai na miradi ya ulimwengu huu. Madai hayo na miradi hiyo yote itapotelea mbali hivi karibuni, kwa kuwa ulimwengu huu unakaribia mwisho wao. Badala yake, wapendao uadilifu watageukia habari njema zinazotangazwa na wale wanaoacha nuru ya Ufalme wa Mungu iangaze hadi kwenye miisho ya dunia. Hao ndio waliotabiriwa kwenye Ufunuo 7:9, 10, ambalo husema: “Nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi [cha Mungu] na mbele za Mwana-Kondoo [Kristo] . . . Wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.” Mstari wa 14 husema: “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu.” Naam, wanaokoka mwisho wa ulimwengu huu kuingia katika ulimwengu mpya usio na mwisho chini ya Ufalme wa Mungu.

Ulimwengu Mpya Uliotiwa Nuru

16. Ni nini kitakachoupata ulimwengu wa Shetani kwenye dhiki kuu?

16 Ulimwengu huo mpya utajawa na nuru nyangavu ya kweli. Kwa kweli, fikiria jinsi hali itakavyokuwa siku itakayofuata baada ya Mungu kukomesha mfumo huu wa mambo. Shetani, roho waovu, na mifumo yake ya kisiasa, kibiashara, na kidini itakuwa imeondoshwa—kila moja yayo! Mfumo wote wa Shetani wa kutokeza propaganda utakuwa umeondoshwa pia. Hivyo, baada ya dhiki kuu, hakutakuwa tena kamwe na nyusipepa, gazeti, kitabu, kijitabu, au kikaratasi chochote kilichochapishwa kinachounga mkono ulimwengu huu mbovu. Hakutakuwako mavutano yenye kufisidi yanayoenezwa na vituo vya televisheni au redio. Mazingira yote yenye sumu ya ulimwengu wa Shetani yatafagiliwa mbali kwa pigo moja kubwa!—Mathayo 24:21; Ufunuo 7:14; 16:14-16; 19:11-21.

17, 18. Ungefafanuaje hali ya kiroho baada ya mwisho wa ulimwengu wa Shetani?

17 Hicho kitakuwa kitulizo kikubwa jinsi gani! Kuanzia siku hiyo na kuendelea, ni nuru ile tu ya kiroho ifaayo na yenye kujenga itokayo kwa Yehova na Ufalme wake itakayokuwa na uvutano juu ya ainabinadamu. Isaya 54:13 hutabiri hivi: “Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA [Yehova, NW]; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.” Utawala wa Mungu ukiwa unamiliki dunia nzima, ahadi yake ni kwamba, kama Isaya 26:9 lisemavyo, ‘watu wakaao duniani watajifunza uadilifu.’

18 Upesi, hali nzima ya kiakili na ya kiroho itabadilika kuwa bora zaidi. Mambo yenye kujenga ndiyo yatakayokuwa ya kawaida badala ya mambo yenye kushusha moyo, na yasiyo ya kiadili ambayo yameenea sana leo. Kila mtu aishiye wakati huo atafundishwa kweli kuhusu Mungu na makusudi yake. Katika maana kamili, unabii wa Isaya 11:9 utatimizwa, ambao husema: “Dunia itajawa na kumjua BWANA [Yehova, NW], kama vile maji yanavyoifunika bahari.”

Ni Jambo la Muhimu Kufuata Nuru

19, 20. Kwa nini wale wanaotaka kuifuata nuru wanahitaji kuwa chonjo?

19 Sasa, katika miaka ya mwisho-mwisho ya mfumo huu mbovu, ni jambo la muhimu kuifuata nuru ya ulimwengu. Na tunahitaji kuwa chonjo, kwa kuwa kuna vita kali inayopigwa dhidi yetu ili kutufanya tusitembee nuruni. Upinzani huo huja kutoka kwa mamlaka za giza—kutoka kwa Shetani, roho waovu wake, na tengenezo lake la kidunia. Hiyo ndiyo sababu mtume Petro aonya hivi: “Mwe na kiasi [zitunzeni akili zenu, NW] na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”—1 Petro 5:8.

20 Shetani ataweka kila kikwazo njiani mwa wale wanaopata nuru, kwa sababu anataka kuwafanya waendelee kuwa gizani. Huenda ikawa ni msongo kutoka kwa watu wa ukoo au marafiki wa zamani wanaopinga kweli. Huenda ikawa ni kutilia shaka Biblia kwa sababu ya mtu kuwa amepofushwa na mafundisho ya dini bandia au propaganda za wasioamini kuwako kwa Mungu na waagnosti. Huenda ikawa ni mibetuko yenye dhambi ya mtu mwenyewe inayofanya iwe vigumu kuishi kupatana na matakwa ya kimungu.

21. Ni hatua gani ipasayo kuchukuliwa na wote wanaotaka kuishi katika ulimwengu mpya wa Mungu?

21 Vikwazo viwe ni nini, je! wewe wataka kufurahia maisha katika ulimwengu mpya usio na umaskini, uhalifu, ukosefu wa haki, na vita? Je! wewe wataka kufurahia afya kamilifu na uhai wa milele katika dunia-paradiso? Basi kubali na umfuate Yesu Kristo kuwa ndiye nuru ya ulimwengu, na usikilize ujumbe wa wale wanaolishika kwa imara “neno la uzima” na ‘wanaong’aa kama wamulikaji katika ulimwengu.’—Wafilipi 2:15, 16.

Ungejibuje?

◻ Viongozi wa kidini huonyeshaje kwamba wao ni wapendao giza?

◻ Yesu alikuwa na mtazamo gani kuwaelekea watu?

◻ Kukusanywa kwa wachukuaji nuru kumeendeleaje?

◻ Ni mabadiliko gani yenye kutokeza yatakayotukia hivi karibuni?

◻ Kwa nini ni jambo la muhimu kuifuata nuru ya ulimwengu leo?

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Mafarisayo wenye mioyo migumu walimtupa nje yule mtu ambaye macho yake yalikuwa yamefunguliwa na Yesu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki