Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Gileadi—Mkoa wa Watu Wenye Moyo Mkuu
Muda mfupi kabla ya Israeli kuvuka Mto Yordani kuingia lile Bara Lililoahidiwa, Musa aliwahimiza hivi: “Iweni hodari na moyo wa ushujaa . . . BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe.”—Kumbukumbu la Torati 31:6.
Makabila ya Reubeni na Gadi na lile kabila nusu la Manase yalitiwa ndani katika himizo la Musa. Walikuwa wameona ‘kwamba nchi ya Gileadi ilikuwa mahali pa kuwafaa wanyama,’ kwa hiyo walikuwa wameomba wapewe mgawo wa kuishi katika mkoa wa Gileadi.—Hesabu 32:1-40.
Mkoa wa Gileadi ulikuwa kwenye upande ule mwingine, upande wa mashariki, wa Yordani. Ulitia ndani hasa upande wote wa mashariki, kutoka sehemu ya kaskazini mwa Bahari ya Chumvi hadi Bahari ya Galilaya. Mkoa huo uliinuka kutoka katika Bonde la Yordani hadi nyanda za juu au vilima vya mviringo vyenye maji mengi. Kwa hiyo Gileadi ulikuwa mkoa mzuri wa kupanda nafaka na wa kulisha mifugo. Picha iliyo juu yakutolea wazo fulani juu ya jinsi sehemu ya Gileadi ilivyokuwa. Lakini kwa nini moyo mkuu uhusianishwe na eneo lenye kupendeza sana hivyo?
Kwa wazi makabila yaliyochagua kuishi katika Gileadi hayakufanya hivyo kwa sababu ya hofu. Kumbuka kwamba yalikubali kuvuka Yordani ili kupigana vita dhidi ya adui katika Bara Lililoahidiwa. Na yaliporudi Gileadi, yalihitaji moyo mkuu zaidi. Kwa nini? Yalikuwa mpakani, yakiweza kushambuliwa kwa urahisi na Waamoni waliokuwa kusini mashariki na Wasiria kaskazini. Nao walishambuliwa.—Yoshua 22:9; Waamuzi 10:7, 8; 1 Samweli 11:1; 2 Wafalme 8:28; 9:14; 10:32, 33.
Mashambulio hayo yalikuwa pindi maalumu ambapo moyo mkuu ulihitajiwa. Kwa kielelezo, baada ya Yehova kuwaruhusu Waamoni wadhulumu Gileadi, watu wa Mungu walitubu wakageukia uongozi wa “mtu shujaa sana,” ambaye baba yake pia aliitwa Gileadi. Mtu huyo shujaa, au mwenye moyo mkuu, alikuwa Yeftha. Anajulikana sana kwa ajili ya kiapo fulani kilichoonyesha kwamba, hata ingawa alikuwa na moyo mkuu, alitafuta mwelekezo na utegemezo wa Mungu. Yeftha aliweka nadhiri kwamba ikiwa Mungu angemwezesha kuwashinda wale Waamoni wadhalimu, wa kwanza kutoka katika nyumba yake kumlaki angetolewa kuwa ‘toleo la kuteketezwa,’ au angetolewa dhabihu kwa Mungu.a Kumbe ikatokea kuwa ni mtoto pekee wa Yeftha, binti yake, ambaye baadaye alikwenda kutumikia kwenye patakatifu pa Mungu. Naam, Yeftha na pia binti yake walionyesha moyo mkuu, kwa njia tofauti.—Waamuzi 11:1, 4-40.
Wonyesho mmoja wa moyo mkuu ambao labda haujulikani sana kadiri hiyo lilitukia wakati wa Sauli. Ili uweze kuwazia kikao hicho, kumbuka kwamba Sauli alipopata kuwa mfalme, Waamoni walitisha kung’oa jicho la kulia la wanaume wa Yabesh-gileadi, mji ambao huenda ikawa ulikuwa katika bonde la kijito lililoteremka kupitia vilima hadi Yordani. Upesi Sauli alikusanya jeshi ili kuimarisha Yabeshi. (1 Samweli 11:1-11) Tukikumbuka hayo, acheni tufikirie mwisho wa utawala wa Sauli na kuona jinsi moyo mkuu ulivyoonyeshwa.
Huenda ukakumbuka kwamba Sauli na wana wake watatu walikufa katika vita dhidi ya Wafilisti. Adui hao walikata kichwa cha Sauli na kwa ushindi wakatundika miili ya Sauli na wana wake kwenye ukuta wa Beth-shani. (1 Samweli 31:1-10; kulia, waona kilima cha Beth-shani kilichochimbwa.) Habari hiyo ilifika Yabeshi, katika vilima vya Gileadi ng’ambo ya Yordani. Wagileadi wangefanya nini wakiwa wanakabili adui mwenye nguvu sana hivi kwamba angeweza kumshinda mfalme wa Israeli?
Fuatia kwenye ramani. “[Mara hiyo] wakainuka mashujaa wote, wakaenda usiku kucha, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, na kuiondoa ukutani kwa Beth-shani; nao wakaja Yabeshi, na kuiteketeza huko.” (1 Samweli 31:12) Naam, walivamia ngome ya adui wakati wa usiku. Unaweza kuelewa ni kwa nini Biblia huwaita wenye ushujaa, au wenye moyo mkuu.
Baadaye, yale makabila kumi yalijitenganisha yakafanyiza ufalme wa Israeli wa kaskazini, na huo ulitia ndani Gileadi. Mataifa yaliyokuwa kando-kando, kwanza Wasiria kisha Waashuru, yalianza kunyakua sehemu-sehemu za eneo hilo kwenye upande wa mashariki mwa Yordani. Kwa hiyo zijapokuwa pindi fulani-fulani za kuonyesha moyo mkuu, watu wa Gileadi walilipa bei ya kuwa katika eneo la mpakani.—1 Wafalme 22:1-3; 2 Wafalme 15:29.
[Maelezo ya Chini]
a Kuchunguza rekodi hiyo kwa uangalifu kwakanusha lile shtaka kwamba Yeftha alitoa dhabihu ya kibinadamu ya mtoto wake. Ona Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 27-8, lililotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Ramani katika ukurasa wa 8]
BAHARI YA GALILAYA
BAHARI YA CHUMVI
Mto wa Yordani
Beth-shani
Ramoth-gileadi
Yabeshi
GILEADI
[Hisani]
Inategemea ramani iliyo haki ya Pictorial Archive (Near Eastern
History) Est. na Survey of Israel.