Kwa Nini Umpende Jirani Yako?
UHAI wa milele wategemea kumpenda kwetu Mungu na jirani. Jambo hilo lilielezwa katika mazungumzo yaliyofanywa karibu miaka 2,000 iliyopita.
Mwanamume mmoja wa Kiyahudi aliyezoeleana na Sheria ya Kimusa alimuuliza Yesu Kristo hivi: “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Yesu alijibu hivi: “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Akiinukuu ile Sheria, mwanamume huyo alisema hivi: “Mpende Bwana [Yehova, New World Translation] Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.” “Umejibu vema,” akasema Yesu. “Fanya hivi nawe utaishi.”—Luka 10:25-28.
Kisha, huyo aliyemsaili Yesu akauliza hivi: “Na jirani yangu ni nani?” Badala ya kujibu moja kwa moja, Yesu alitoa hadithi yenye kielezi juu ya mwanamume wa Kiyahudi aliyekuwa amenyang’anywa mali, akapigwa, na kuachwa akiwa karibu kufa. Ndipo Wayahudi wawili wakaja—kwanza kuhani kisha Mlawi. Wote wawili walitazama hali ya yule Myahudi mwenzao lakini hawakufanya lolote kumsaidia. Halafu Msamaria akaja. Akisukumwa na huruma, alifunga majeraha ya Myahudi huyo aliyeumia, akampeleka kwenye nyumba ya wageni, na kufanya maandalizi ili atunzwe zaidi.
Yesu alimuuliza hivi, huyo aliyemsaili: “Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?” Kwa wazi, alikuwa yule Msamaria mwenye rehema. Hivyo Yesu alionyesha kwamba kumpenda jirani kikweli hupita vizuizi vya kikabila.—Luka 10:29-37.
Ukosefu wa Kumpenda Jirani
Leo uadui unakua kati ya watu wa makabila tofauti-tofauti. Kwa mfano, hivi karibuni wale wenye kuunga mkono kanuni za Wanazi katika Ujerumani walimwangusha mtu mmoja chini, wakamkanyaga-kanyaga kwa buti zao nzito, wakivunja karibu mbavu zake zote. Kisha wakamwagilia kinywaji chenye kileo kingi sana, wakamwasha moto. Mtu huyo aliyeachwa kufa alishambuliwa kwa sababu alidhaniwa kuwa Myahudi. Katika kisa kingine tofauti, nyumba moja karibu na Hamburg ilirushiwa bomu la moto, likiwachoma watu watatu Waturuki hadi kufa—mmoja wao akiwa msichana wa miaka kumi.
Katika nchi za Baltiki na mashariki ya mbali zaidi, maelfu ya watu waliuawa katika vita vya kikabila. Wengine walikufa katika mapigano kati ya watu wa malezi mbalimbali katika Bangladesh, India, na Pakistan. Na katika Afrika, watu wengine bado walikufa katika mapigano ya kikabila na ya kirangi.
Watu wengi huchukizwa sana na jeuri ya jinsi hiyo na hawangefanya kamwe jambo lolote ili kumdhuru jirani yao. Kwa kweli, maandamano makubwa katika Ujerumani yamelaumu jeuri ya kikabila huko. Lakini, The New Encyclopædia Britannica yasema: “Washiriki wa karibu tamaduni zote za ulimwengu huona njia yao wenyewe ya maisha kuwa bora zaidi ya ile ya hata majirani wa karibu zaidi.” Maoni hayo huzuia kumpenda jirani. Je! jambo lolote laweza kufanywa juu ya hilo, hasa kwa kuwa Yesu alisema kwamba uhai wategemea kumpenda Mungu na jirani?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Cover: Jules Pelcog/Die Heilige Schrift
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Yule Msamaria Mwema/The Doré Bible Illustrations/Dover Publications, Inc.