Mlo wa Jioni wa Bwana—Huo Wapaswa Uadhimishwe Mara Nyingi Kadiri Gani?
SIKU za Krismasi, Ista, na za “watakatifu.” Sikukuu na karamu nyingi husherehekewa na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Lakini je, wajua Yesu Kristo aliamuru wafuasi wake waadhimishe sherehe ngapi? Jibu ni, Moja tu! Zile karamu nyingine zote hazikuamriwa na Mwanzilishi wa Ukristo.
Kwa wazi, ikiwa Yesu alianzisha sherehe moja tu, hiyo ni ya maana sana. Wakristo wapaswa kuiadhimisha sawasawa na vile Yesu alivyoamuru. Mwadhimisho huo wa pekee ni upi?
Ile Sherehe Moja
Mwadhimisho huo ulianzishwa na Yesu katika siku ile aliyokufa. Yeye alikuwa amekumbuka karamu ya Kiyahudi ya Sikukuu ya Kupitwa akiwa na mitume wake. Halafu akawapitishia mkate usiotiwa chachu wa Sikukuu ya Kupitwa, akisema: “Huu ndio [wamaanisha, New World Translation] mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu.” Halafu, Yesu akapitisha kikombe cha divai, akisema: “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.” Yeye alisema hivi pia: “Fanyeni [endeleeni kufanya, NW] hivi kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22:19, 20; 1 Wakorintho 11:24-26) Mwadhimisho huo unaitwa Mlo wa Jioni wa Bwana, au Ukumbusho. Ndiyo sherehe pekee ambayo Yesu aliamuru wafuasi wake waadhimishe.
Makanisa mengi hudai kwamba hayo hufanya mwadhimisho huo pamoja na karamu zao nyinginezo, lakini makanisa mengi huiadhimisha kwa njia tofauti na ile ambayo Yesu aliamuru. Labda tofauti iliyo wazi zaidi ni mara ambazo mwadhimisho huo hufanywa. Makanisa fulani huusherehekea kila mwezi, kila juma, hata kila siku. Je! hivyo ndivyo alivyokusudia Yesu alipowaambia wafuasi wake: ‘Endeleeni kufanya hivi kwa ukumbusho wangu’? “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” (1 Wakorintho 11:24, 25) Ukumbusho au sherehe ya kila mwaka huadhimishwa mara ngapi? Kwa kawaida, mara moja tu kwa mwaka.
Kumbuka pia kwamba Yesu alianzisha mwadhimisho huu halafu akafa katika tarehe ya kalenda ya Kiyahudi ya Nisani 14.a Hiyo ilikuwa siku ya Sikukuu ya Kupitwa, sherehe iliyokumbusha Wayahudi juu ya ule ukombozi mkubwa waliopata katika Misri katika karne ya 16 K.W.K. Wakati huo, dhabihu ya mwana-kondoo ilitokeza ukombozi wa wazaliwa wa kwanza wa Wayahudi, hali malaika wa Yehova aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri.—Kutoka 12:21, 24-27.
Hilo lasaidiaje uelewevu wetu? Mtume Mkristo Paulo aliandika hivi: “Kristo kupitwa kwetu ametolewa dhabihu.” (1 Wakorintho 5:7, NW) Kifo cha Yesu kilikuwa dhabihu ya Sikukuu ya Kupitwa iliyo kuu zaidi, ikitolea ainabinadamu fursa ya ukombozi ulio mtukufu zaidi. Hivyo, kwa Wakristo, Ukumbusho wa kifo cha Kristo umechukua mahali pa Sikukuu ya Kupitwa ya Kiyahudi.—Yohana 3:16.
Sikukuu ya Kupitwa ilikuwa sherehe ya kila mwaka. Hivyo, kwa kusababu kuzuri, Ukumbusho pia hufanywa kila mwaka. Sikukuu ya Kupitwa—ile siku ambayo Yesu alikufa—ilifanywa sikuzote kwenye siku ya 14 ya mwezi wa Kiyahudi wa Nisani. Kwa hiyo, kifo cha Kristo chapaswa kukumbukwa mara moja kwa mwaka kwenye siku ya kalenda inayolingana na Nisani 14. Katika 1994 siku hiyo ni Jumamosi, Machi 26, baada ya jua kushuka. Hata hivyo, kwa nini makanisa ya Jumuiya ya Wakristo hayajaifanya hiyo kuwa siku ya mwadhimisho wa pekee? Kuchunguza historia kifupi kutajibu swali hilo.
Desturi ya Kimitume Hatarini
Hakuna shaka kwamba wakati wa karne ya kwanza W.K., wale walioongozwa na mitume wa Yesu walisherehekea Mlo wa Jioni wa Bwana sawasawa na alivyoamuru. Hata hivyo, wakati wa karne ya pili, baadhi yao walianza kubadili wakati wa kukumbukwa kwa sherehe hiyo. Waliadhimisha Ukumbusho katika siku ya kwanza ya juma (iitwayo sasa Jumapili), si katika siku ile inayolingana na Nisani 14. Kwa nini hilo lilifanywa?
Kwa Wayahudi, siku ilianza karibu saa 12 jioni na kuendelea hadi wakati uo huo siku iliyofuata. Yesu alikufa katika Nisani 14, 33 W.K., siku iliyoanzia Alhamisi jioni hadi Ijumaa jioni. Alifufuliwa siku ya tatu, mapema Jumapili asubuhi. Watu fulani walitaka kukumbukwa kwa kifo cha Yesu kuadhimishwe katika siku fulani hususa ya juma kila mwaka, badala ya katika siku ile ambayo Nisani 14 ililingana nayo. Wao pia waliiona siku ya ufufuo wa Yesu kuwa ya maana zaidi ya ile ya kifo chake. Kwa hiyo, walichagua Jumapili.
Yesu aliamuru kwamba kifo chake kikumbukwe, si ufufuo wake. Na kwa kuwa Sikukuu ya Kupitwa ya Kiyahudi huangukia siku tofauti kila mwaka kulingana na kalenda ya Gregori tunayotumia sasa, ni jambo la asili tu kwamba Ukumbusho ungeangukia siku tofauti pia. Kwa hiyo wengi walishikilia ule mpango wa awali na kuadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana siku ya Nisani 14 kila mwaka. Baadaye walikuja kuitwa Wakwotodesimi, linalomaanisha “Wa-kumi-na-nne.”
Wasomi fulani walitambua kwamba hao “Wa-kumi-na-nne” walikuwa wakifuata kiolezo cha awali cha kimitume. Mwanahistoria mmoja alisema hivi: “Kwa habari ya siku ya kuadhimisha Pasaka [Mlo wa Jioni wa Bwana], utaratibu wa makanisa ya Kikwotodesimi ya Asia ulikuwa ni mwendelezo wa ule wa kanisa la Yerusalemu. Katika karne ya 2 kwenye Pasaka ya siku ya 14 ya Nisani, makanisa hayo yalikumbuka ukombozi uliotolewa na kifo cha Kristo.”—Studia Patristica, Buku 5, 1962, ukurasa 8.
Bishano Lakua
Ingawa wengi katika Asia Ndogo walifuata utaratibu wa kimitume, Jumapili iliwekwa kando kwa ajili ya mwadhimisho katika Roma. Karibu na mwaka 155 W.K., Polycarp wa Smirna, mwakilishi wa makutaniko ya Asia, alizuru Roma ili kuzungumzia tatizo hilo na mengineyo. Kwa kusikitisha, hawakukubaliana juu ya jambo hilo.
Irenayo wa Lyons aliandika hivi katika barua: “Wala Aniseto [wa Roma] hakuweza kumshawishi Polycarp asiadhimishe kile alichoadhimisha sikuzote na Yohana mtume wa Bwana wetu na mitume wale wengine ambao alishirikiana nao; wala Polycarp hakuweza kumshawishi Aniseto kuiadhimisha, kwani Aniseto alisema kwamba yeye, apaswa kufuata desturi ya wazee waliomtangulia.” (Eusebius, Kitabu cha 5, sura ya 24) Ona kwamba kulingana na ripoti, Polycarp alitegemeza msimamo wake juu ya mamlaka ya mitume, hali Aniseto alitegemea desturi za wazee waliotangulia katika Roma.
Bishano hilo lilizidi kuelekea mwisho wa karne ya pili W.K. Karibu 190 W.K., Victor fulani aliteuliwa kuwa askofu wa Roma. Yeye aliamini kwamba Mlo wa Jioni wa Bwana wapaswa kuadhimishwa Jumapili, na akatafuta kuungwa mkono na viongozi wengine wengi kadiri alivyoweza. Victor aliyakaza makutaniko ya Asia yabadilike na kufuata mpango huo wa Jumapili.
Akijibu kwa niaba ya wale walio katika Asia Ndogo, Polikrato wa Efeso alikataa kufuata mwito huo. Yeye alisema hivi “Sisi twaadhimisha siku hiyo bila kuibadili, hatuongezi, wala kutoa.” Halafu akaorodhesha watu wengi wenye mamlaka, kutia na mtume Yohana. “Hao wote,” yeye akasisitiza, “waliadhimisha siku ya kumi na nne ya Pasaka kulingana na Gospeli, bila kukengeuka kwa njia yoyote kutoka kwayo.” Polikrato aliongeza: “Kwa habari yangu mimi, ndugu zangu, . . . mimi siogopeshwi na vitisho. Kwani wale walio bora kuliko mimi wamesema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”—Eusebius, Kitabu cha 5, sura ya 24.
Victor hakupendezwa na jibu hilo. Kitabu kimoja cha historia husema kwamba “aliyaondoa kwenye ushirika Makanisa yote ya Asia, na kupeleka barua zake za kupokezanwa kwa Makanisa yote yaliyounga mkono maoni yake, kwamba hayapaswi kuwa na ushirikiano wowote na yale yaliyoondolewa.” Hata hivyo, “tendo hilo lisilo la busara na la ujasiri halikupokewa vizuri na watu wote wenye hekima na mioyo myeupe wa kundi lake mwenyewe, watu kadhaa kati yao wakimwandikia kwa hasira, wakimshauri . . . ahifadhi upendo, umoja, na amani.”—Bingham’s Antiquities of the Christian Church, Kitabu cha 20, sura ya 5.
Uasi-Imani Waanzishwa
Kujapokuwa malalamiko hayo, Wakristo katika Asia Ndogo walitatanika zaidi juu ya suala la wakati wa kusherehekea Mlo wa Jioni wa Bwana. Mabadiliko mbalimbali yalikuwa yamefanywa kwingineko. Baadhi yao walisherehekea kipindi chote kuanzia Nisani 14 hadi Jumapili iliyofuata. Wengine walikuwa wakisherehekea pindi hiyo mara nyingi zaidi—kila juma siku ya Jumapili.
Katika 314 W.K. Baraza la Arles (Ufaransa) lilijaribu kulazimisha utaratibu wa Roma ufuatwe na kukandamiza maoni mengineyo. Wakwotodesimi waliobaki walisimama imara. Ili kusuluhisha suala hilo na mambo mengine yaliyokuwa yakigawanya wale waliodai kuwa Wakristo katika milki yake, katika 325 W.K. maliki mpagani Konstantino alitayarisha mkutano wa baraza la makanisa, ile Baraza la Nisea. Hilo lilitoa amri iliyowaagiza wote katika Asia Ndogo wajipatanishe na utaratibu wa Roma.
Inapendeza kuona mojawapo hoja kuu zilizotolewa kuwa sababu za kuacha kuadhimisha Ukumbusho wa kifo cha Kristo kulingana na tarehe ya kalenda ya Kiyahudi. A History of the Christian Councils, cha K. J. Hefele, chasema: “Ilitangazwa kwamba ni jambo lisilostahili hasa kwa hii sherehe iliyo takatifu zaidi ya zote, kufuata desturi (maoni) ya Wayahudi, waliokuwa wamehusika kwa njia ya aibu katika uhalifu wenye kuogopesha sana, na ambao akili zao zilikuwa zimepofushwa.” (Buku 1, ukurasa 322) Kuwa katika hali hiyo kulionwa kuwa “‘ujitiisho wenye kuaibisha’ kwa Sinagogi jambo lililoudhi wenye mamlaka wa Kanisa,” asema J. Juster, aliyenukuliwa katika Studia Patristica, Buku 4, 1961, ukurasa 412.
Huko kulikuwa kukinza Wayahudi! Wale waliosherehekea Ukumbusho wa kifo cha Yesu siku ileile aliyokufa walionwa kuwa Wayuda. Ilisahauliwa kwamba Yesu mwenyewe alikuwa Myahudi na kwamba alikuwa ameipa siku hiyo maana yayo kwa kutoa uhai wake wakati huo kwa ajili ya ainabinadamu. Kuanzia wakati huo na kuendelea, Wakwotodesimi walishutumiwa kuwa wazushi na watu wa mafarakano na kunyanyaswa. Katika 341 W.K., Baraza la Antiokia lilitoa amri kwamba wao walipaswa kuondolewa katika ushirika. Hata hivyo, katika 400 W.K. bado wengi wao walikuwako na waliendelea kuwako wakiwa wachache muda mrefu baadaye.
Tangu siku hizo, Jumuiya ya Wakristo imeshindwa kurudi kwenye utaratibu wa awali wa Yesu. Profesa William Bright alikiri hivi: “Siku ya pekee, Ijumaa Njema, ilipokuja kutumiwa kwa ajili ya mwadhimisho wa Kuteseka kwa Kristo, ilikuwa kuchelewa mno kuifanya isherehekewe tu na vikundi vya ‘pasaka’ ambayo Mt. Paulo alikuwa amehusianisha na kifo cha kidhabihu: vikundi hivyo vilikuwa vimetumiwa waziwazi kwenye sherehe ya Ufufuo yenyewe, na mvurugo wa mawazo ulijiimarisha katika lugha ya kidesturi ya Jumuiya ya Wakristo ya Kigiriki na Kilatini.”—The Age of the Fathers, Buku 1, ukurasa 102.
Vipi Leo?
Baada ya miaka hii yote,’ huenda ukauliza, ‘je, ni jambo la maana Ukumbusho unaadhimishwa wakati gani?’ Ndiyo, ni jambo la maana. Mabadiliko yalifanywa na watu wenye kushikilia maoni yao waliojitakia mamlaka. Watu walifuata mawazo yao wenyewe badala ya kutii Yesu Kristo. Onyo la mtume Paulo lilitimia waziwazi: “Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu [Wakristo], wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.”—Matendo 20:29, 30.
Suala linalohusika ni utii. Yesu alianzisha sherehe moja tu ili Wakristo waiadhimishe. Biblia hueleza wazi ni lini na jinsi gani hiyo yapaswa kuadhimishwa. Ni nani basi, aliye na haki ya kubadili hayo? Wakwotodesimi wa mapema walipatwa na mnyanyaso na kuondolewa katika ushirika badala ya kuridhiana katika jambo hilo.
Huenda ukapendezwa kujua kwamba bado kuna Wakristo duniani wanaostahi mapenzi ya Yesu na kuadhimisha Ukumbusho wa kifo chake katika siku aliyouanzisha. Mwaka huu, Mashahidi wa Yehova watakutana pamoja katika Majumba ya Ufalme yao duniani pote baada ya saa 12:00 jioni, Jumamosi, Machi 26—wakati siku ya 14 ya Nisani ianzapo. Halafu watafanya mambo yaleyale ambayo Yesu alisema yapaswa kufanywa katika wakati huu wa maana sana. Mbona usiadhimishe Mlo wa Jioni wa Bwana pamoja nao? Kwa kuwapo kwako, wewe pia waweza kuonyesha staha yako kwa mapenzi ya Yesu Kristo.
[Maelezo ya Chini]
a Nisani, mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiyahudi, ulianza kwa kuonekana kwa mwezi mpya kwa mara ya kwanza. Hivyo sikuzote Nisani 14 ilifika wakati wa mwezi mpevu.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
“FIDIA HIYO YENYE THAMANI”
Dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo si fundisho tu. Yesu alisema hivi juu yake: “Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:45) Yeye alieleza hivi pia: “Mungu aliupenda ulimwengu [wa ainabinadamu], hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16) Kwa wafu, fidia yafungua njia ya kupata ufufuo na taraja la uhai wa milele.—Yohana 5:28, 29.
Ni kile kifo cha Yesu Kristo chenye umaana mkubwa ndicho kinachokumbukwa kwenye maadhimisho ya Mlo wa Jioni wa Bwana. Dhabihu yake hutimiza mengi sana! Mwanamke mmoja aliyezoezwa na wazazi wenye kumhofu Mungu na ambaye ametembea katika kweli ya Mungu kwa miongo ya miaka alionyesha shukrani zake kwa maneno haya:
“Tunatazamia Ukumbusho kwa hamu. Kila mwaka, huo huzidi kuwa wa pekee. Nakumbuka nikisimama katika mochari miaka 20 iliyopita, nikimtazama baba yangu mpendwa na kuhisi uthamini wa kweli wenye kuhisiwa moyoni kwa ajili ya ile fidia. Hapo mwanzoni fidia ilikuwa imekuwa maarifa ya kichwani tu. Eh, ni kweli nilijua maandiko yote na jinsi ya kuyaeleza! Lakini ni wakati tu nilipohisi uhalisi wa kifo wenye kufadhaisha ndipo moyo wangu uliporuka kwa shangwe juu ya yale yatakayotimizwa kwa ajili yetu kupitia fidia hiyo yenye thamani.”