Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 9/1 kur. 3-5
  • Mageuzi Yajaribiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mageuzi Yajaribiwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ushuhuda Unaopingana
  • Je, Mageuzi Ni Uchaguzi wa Watu Wenye Akili?
  • Jambo la Imani
  • Mageuzi
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
  • Uumbaji au Mageuzi?—Sehemu ya 2: Kwa Nini Uchunguze Nadharia ya Mageuzi?
    Vijana Huuliza
  • Je, Fundisho la Mageuzi Linapatana na Biblia?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Kanisa Katoliki na Mageuzi
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 9/1 kur. 3-5

Mageuzi Yajaribiwa

Wanamageuzi waliojitolea sana sasa wanataka uchunguzi kamili ufanywe kwa chanzo cha uhai

EBU wazia kwamba wewe ni hakimu katika kesi ya jinai. Mshtakiwa ateta sana akikana kuwa na hatia, na mashahidi wajitokeza kutoa ushahidi kwa niaba yake. Lakini, usikilizapo ushuhuda wao unaona kwamba kila shahidi anapinga wale wengine. Kisha, mashahidi hao wanaomtetea wanapoitwa tena watoe ushahidi, habari zao zabadilika. Ukiwa hakimu, je, ungechukulia ushuhuda wao kwa uzito? Je, ungeelekea kumwachilia huru mshtakiwa? Yaelekea sivyo, kwa sababu mambo yoyote yasiyopatana katika ushuhuda wa mtetezi hudhoofisha kesi ya mshtakiwa.

Ndivyo hali ya mageuzi ilivyo. Mashahidi wengi wamejitokeza kutoa maelezo mengi mbalimbali juu ya chanzo cha uhai, wakitetea nadharia ya mageuzi. Lakini, je, ushuhuda wao waweza kukubalika mahakamani? Je, wale wanaotetea nadharia hiyo wanapatana?

Ushuhuda Unaopingana

Uhai ulianzaje? Labda hakuna suala jingine lililotokeza makisio mengi na kutokeza mijadala mingi zaidi kuliko hilo. Lakini, bishano si baina ya mageuzi na uumbaji tu; pambano kubwa zaidi laendelea kati ya wanamageuzi wenyewe. Karibu kila kijambo kidogo cha mageuzi—jinsi yalivyotokea, mahali yalipotokea, nani au nini kilichoyatokeza, na muda yaliyochukua—kinabishaniwa vikali.

Kwa miaka mingi wanamageuzi walidai kwamba uhai ulianza katika kidimbwi cha “mchuzi” wa karboni kilicho moto kwa kadiri. Wengine sasa waamini kwamba povu la bahari lingetokeza uhai. Wanasayansi wengine wanadokeza kwamba uhai ulianza katika mabubujiko ya maji moto yaliyo chini ya bahari. Wengine nao wanakubali bila uthibitisho kwamba viumbe vilivyo hai vilikuja vikiwa katika vimondo (nyota zipitazo kasi angani) vilivyokuja duniani. Wengine nao wasema kwamba labda vyuma vya angani viligonga dunia na kubadili anga ya dunia, hivyo vikichochea uhai. “Pigisha kipande kikubwa cha chuma cha angani duniani,” asema mtafiti mmoja, “na kwa hakika utapata mambo ya kustaajabisha.”

Jinsi uhai ulivyoanza inafikiriwa vilevile. “Uhai haukuanza katika hali tulivu zilizo shwari, kama ilivyodhaniwa zamani,” ladokeza gazeti Time, “bali ulianza chini ya anga zenye kutisha sana za dunia iliyojawa na milipuko ya volkeno na kutishwa na nyota zenye mikia na vipande vya angani.” Ili uhai upitie mageuzi katikati ya mvurugo huo wote, wanasayansi wengine sasa wasema, ni lazima utaratibu wote huo uwe ulitokea kwa kipindi kifupi zaidi kuliko jinsi kulivyofikiriwa zamani.

Wanasayansi pia wana maoni tofauti-tofauti kuhusu daraka atimizalo Mungu—“iwapo yuko.” Wengine wasema kwamba uhai ulipitia mageuzi bila tendo la Muumba, ilhali wengine wanadokeza kwamba Mungu alianzisha mfumo huo na kuacha mageuzi yaendelee.

Baada ya uhai kuanza, mageuzi yalitokeaje? Maelezo yatofautiana hata kuhusu suala hilo. Mnamo 1958, karne moja baada ya The Origin of Species kutangazwa, mwanamageuzi Bwana Julian Huxley alisema: “Uvumbuzi mkubwa wa Darwin, kanuni ya ulimwenguni pote ya uchaguzi wa asili (viumbe bora kuendelea kuishi na viumbe dhaifu kukwisha), imethibitishwa hatimaye na kuimarishwa kuwa njia ya pekee ya badiliko kubwa la nadharia.” Hata hivyo, miaka 24 baadaye, mwanamageuzi Michael Ruse aliandika: “Idadi inayozidi kuongezeka ya wanabiolojia . . . wanabisha kwamba nadharia yoyote ya mageuzi inayotegemea kanuni za Darwin—hasa nadharia yoyote inayoona kanuni ya uchaguzi wa asili kuwa ule ufunguo wa badiliko la mageuzi—si kamili na inapotosha.”

Ingawa gazeti Time lasema kwamba kuna “mambo mengi ya hakika” yanayounga mkono nadharia ya mageuzi, bado lakiri kwamba mageuzi ni suala gumu sana lenye “mapungufu mengi na nadharia nyingi zinazopingana juu ya jinsi ya kuthibitisha mambo yanayokosekana.” Badala ya kudokeza kwamba kesi hiyo imekwisha, wanamageuzi waliojitolea sana sasa wanataka uchunguzi kamili ufanywe kwa chanzo cha uhai.

Kwa hiyo, kesi ya kutetea mageuzi—hasa kuhusu mwanzo wa uhai kulingana na mageuzi—haitegemei ushuhuda unaopatana. Mwanasayansi T. H. Janabi aonelea kwamba wale wanaounga mkono mageuzi “wametokeza na kuacha nadharia zenye makosa kwa miaka ambayo imepita na kufikia sasa wanasayansi wameshindwa kukubaliana juu ya nadharia yoyote ile.”

Kwa kupendeza, Charles Darwin alitarajia hitilafu kama hiyo itokee. Katika utangulizi wa kitabu The Origin of Species, yeye aliandika: “Ninajua vizuri kwamba karibu kila jambo lililotajwa katika buku hili ambalo haliwezi kuthibitishwa, mara nyingi hutokeza uamuzi tofauti kabisa na ule nilioufikia.”

Kwa kweli, ushuhuda kama huo unaopingana huzusha maswali juu ya ustahili wa nadharia ya mageuzi.

Je, Mageuzi Ni Uchaguzi wa Watu Wenye Akili?

Tangu mwanzo wayo, chasema kitabu Milestones of History, nadharia ya mageuzi “ilivutia watu wengi kwa sababu ilionekana kuwa ya kisayansi sana kuliko nadharia ya uumbaji hususa.”

Na zaidi, taarifa za wanamageuzi fulani zenye kushikilia mambo sana zaweza kukutisha. Kwa kielelezo, mwanasayansi H. S. Shelton asisitiza kwamba wazo la uumbaji hususa ni “la kipumbavu sana hata halipasi kufikiriwa kwa uzito.” Mwanabiolojia Richard Dawkins asema hivi waziwazi: “Mtu akidai kwamba haamini mageuzi, basi yeye ni mjinga, mpumbavu, au amerukwa akili.” Profesa René Dubos asema hivi: “Watu wengi walioelimika sasa wanakubali kwamba kila kitu kilicho katika ulimwengu wote mzima—kuanzia viumbe vya angani hadi wanadamu—kimesitawi na kinaendelea kusitawi kupitia hatua za mageuzi.”

Kutokana na taarifa hizo ingeonekana kwamba kila mtu aliye na akili kiasi fulani angekubali mara moja nadharia ya mageuzi. Kwani, kufanya hivyo kungemaanisha kwamba mtu huyo ‘ameelimika’ badala ya kuwa “mpumbavu.” Lakini, kuna wanaume na wanawake wenye elimu ya juu sana ambao hawatetei nadharia ya mageuzi. “Nilipata wanasayansi wengi walio na shaka zao binafsi,” aandika Francis Hitching katika kitabu chake The Neck of the Giraffe, “na wale wachache ambao hata walisema kwamba nadharia ya mageuzi ya Darwin haikuonekana kuwa nadharia ya kisayansi hata kidogo.”

Chandra Wickramasinghe, mwanasayansi mmoja Mwingereza aliye mashuhuri sana, ana msimamo kama huo. “Hakuna uthibitisho wowote wa mafundisho ya msingi ya mageuzi ya Darwin,” yeye asema. “Ni kani ya kijamii iliyodhibiti ulimwengu katika 1860, na nafikiri imetokeza msiba sana kwa sayansi tangu wakati huo.”

T. H. Janabi alichunguza hoja zilizotolewa na wanamageuzi. “Nilipata kwamba hali ilikuwa tofauti sana na kile tunachoambiwa tuamini,” yeye asema. “Uthibitisho ni mchache sana nao haupatani ili utegemeze nadharia tata hivyo kama chanzo cha uhai.”

Kwa hiyo, wale wakataao nadharia ya mageuzi wasionwe tu kuwa ‘wajinga, wapumbavu, au kuwa wamerukwa akili.’ Kuhusu maoni ya watu yanayopinga mageuzi, hata mwanamageuzi shupavu George Gaylord Simpson alilazimika kukiri hivi: “Kwa hakika lingekuwa kosa kupuuza maoni hayo bila kuyafikiria kwa uzito au kuyadhihaki. Wale waliopinga mageuzi walikuwa (na wangali ni) wasomi wa hali ya juu sana na ni werevu sana.”

Jambo la Imani

Watu wengine hufikiri kwamba itikadi katika mageuzi yategemea mambo hakika, huku itikadi katika uumbaji ikitegemea imani. Ni kweli kwamba hakuna mtu amepata kumwona Mungu. (Yohana 1:18; linganisha 2 Wakorintho 5:7.) Lakini, nadharia ya mageuzi haishindi kwa habari hiyo, kwa kuwa inategemea matukio ambayo hakuna wanadamu wowote wamepata kushuhudia wala kutokeza.

Kwa kielelezo, wanasayansi hawajapata kushuhudia migeuko-papale (mabadiliko ya ghafula ya kiumbe) ikitendeka—hata ile inufaishayo—itokezayo aina mpya za uhai; lakini wao wajua kwa uhakika kwamba ndivyo aina mpya za uhai zilivyoanza. Wao hawajaona uhai ukianza kutoka kwa kitu kisicho na uhai; na bado wao wasisitiza kwamba uhai ulianza hivyo.

Ukosefu wa uthibitisho kama huo wamfanya T. H. Janabi aiite nadharia ya mageuzi kuwa “‘imani’ tu.” Mwanafizikia Fred Hoyle aiita “Gospeli kulingana na Darwin.” Dakt. Evan Shute atumia hata maneno makali zaidi. “Nadhani yule asemaye kwamba ulimwengu uliumbwa kwa muda mfupi tu hatatiziki sana kueleza mambo kama yule ashikiliaye sana mageuzi,” yeye asema.

Wastadi wengine wakubali hivyo. “Nifikiriapo jinsi binadamu alivyo,” akiri mwaastronomia Robert Jastrow, “kutokea kwa binadamu aliye wa kipekee sana kutokana na kemikali zilizoyeyuka ndani ya kidimbwi cha maji yasiyo moto sana kwaonekana kwangu kuwa muujiza kama tu yale masimulizi ya Biblia juu ya chanzo cha binadamu.”

Kwa nini basi watu wengi bado wanakataa wazo la kwamba uhai uliumbwa?

[Picha katika ukurasa wa 3]

Taarifa za watu fulani zenye kushikilia mambo sana zaweza kutisha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki