Kanisa Katoliki na Mageuzi
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Italia
APRILI 26, 1882, maziko ya Charles Darwin yalifanywa katika kanisa la Westminster Abbey, London. Huenda ikaonekana kwa wengine kwamba kanisa ni mahali pasipofaa zaidi pa kumzika mtu aliyeshtakiwa ‘kumpindua Mungu’ kwa nadharia yake ya mageuzi ya uteuzi asilia. Lakini, kaburi la Darwin limekuwa hapo kwa zaidi ya karne moja.
Baada ya kitabu cha Darwin Origin of Species kuchapishwa katika 1859, mtazamo wa wanatheolojia ulibadilika polepole na kupendelea mageuzi. Mwanatheolojia Carlo Molari aliandika juu ya jinsi sehemu ya “vita ya wazi” ilivyotokeza “mapatano ya kuacha vita” mapema katika karne hii. Kisha, akasema, kukawa na “mkataba wa muda wa amani” katikati ya miaka ya 1900 na hatimaye “amani” ya sasa.
Kabla ya Darwin
Bila shaka, wazo la mageuzi halikuanzishwa na Darwin. Wanafalsafa wa kale walikuwa wamenadharia kuhusu kugeuzwa umbo kwa kiumbe kutoka namna moja ya uhai hadi nyingine. Tasnifu ya kwanza ya kisasa ya mageuzi yaweza kufuatiliwa nyuma kufikia wanasayansi kadhaa wa karne ya 18 ambao ni watalaamu wa viumbe.
Katika karne za 18 na 19, wasomi wengi walipendekeza nadharia tofauti-tofauti, hata ingawa neno “mageuzi” lilitokea kwa nadra sana. Babu ya Darwin, Erasmus Darwin (1731-1802), alitokeza mawazo kadhaa ya mageuzi katika mojawapo ya vitabu vyake, na kitabu hicho kiliorodheshwa katika faharisi ya Kanisa Katoliki ya vitabu vilivyokatazwa.
Kisababishi cha “Vita ya Wazi”
Wengine wasio wa kidini waliona nadharia ya Darwin kuwa chombo muhimu cha kupunguza nguvu za makasisi. Basi vita kali ikafyatuka. Mwaka wa 1860 maaskofu wa Ujerumani walikariri hivi: “Watangulizi wetu wa kale waliumbwa moja kwa moja na Mungu. Na basi twatangaza kuwa kinyume cha Maandiko Matakatifu na kinyume cha Imani maoni ya wale wathubutuo kusisitiza kwamba mwili wa mwanadamu umetokana na hali ya asili isiyokamilika kupitia mageuzi yanayotokea yenyewe tu.”
Vivyo hivyo, mnamo Mei 1877, Papa Pius wa Tisa alisifu tabibu Mfaransa Constantin James kwa ajili ya kichapo kilichopinga mageuzi na kwa kuunga mkono masimulizi ya Mwanzo kuhusu uumbaji. Sehemu ya kwanza ya pambano hilo ikafikia upeo kwa mfululizo wa barua uliochapishwa na Tume ya Papa ya Biblia kati ya 1905 na 1909. Katika mojawapo ya barua hizo, tume hiyo ilitangaza kwamba sura tatu za kwanza za Mwanzo ni za kihistoria nazo zapaswa kueleweka kuwa “historia halisi.”
“Mapatano ya Kuacha Vita” na “Mkataba wa Muda wa Amani”
Lakini, sifa ya nadharia ya Darwin ilipozidi kuimarika miongoni mwa wasomi, wanatheolojia Wakatoliki, kama vile Myesuiti Mfaransa Teilhard de Chardin, wakaanza kukubali nadharia ya mageuzi. Ingawa mawazo ya Teilhard yalitofautiana na yale ya wanamageuzi wa kawaida, tokea 1921 na kuendelea alifikiria “mageuzi ya kibiolojia . . . akawa na uhakika zaidi na zaidi juu ya uhalisi wake.” Ule ufa uliokuwa kati ya imani ya Kikatoliki na nadharia ya mageuzi ukazidi kupunguka ukielekea kwenye upatano.
Mwaka wa 1948 Myesuiti mwingine alitaarifu: “Kwa zaidi ya miaka 20, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wanatheolojia, walio Wakatoliki kwa dhati, ambao hutangaza kwamba upatano [kati ya mageuzi na imani ya Katoliki] waweza kuwapo iwapo utakuwa na mipaka fulani.” Karibu na wakati huo, Tume ya Papa ya Biblia ilikanusha mengi kati ya yale ambayo ilikuwa imeandika katika mwaka wa 1909 ilipounga mkono masimulizi ya Mwanzo juu ya uumbaji.
Kisha, katika mwaka wa 1950, barua ya Pius wa 12, Humani generis, ilisema kwamba wasomi wa Katoliki wapaswa kufikiria nadharia ya mageuzi kuwa nadharia isiyothibitishwa yenye kuaminika. Lakini, huyo papa akasema: “Imani ya Kikatoliki yatushurutisha tushikilie kwamba nafsi zimeumbwa moja kwa moja na Mungu.”
Kwa Nini Kuna Ile Iitwayo Eti Amani?
Carlo Molari ataarifu kwamba, kwa visa vichache vilivyo tofauti, tangu baraza la makanisa la Vatikani la Pili, “mapingamizi dhidi ya nadharia za mageuzi hayakufua dafu kamwe.” Kwa umuhimu, mnamo Oktoba 1996, Papa John Paul wa Pili alitangaza hivi: “Leo, karibu nusu ya karne baada ya kichapo cha [Pius wa 12], ujuzi mpya watuongoza tutambue kwamba nadharia ya mageuzi ni zaidi ya kuwa nadharia isiyothibitishwa tu. Kwa kweli ni jambo la kutokeza kwamba nadharia hiyo imekubaliwa na watafiti hatua kwa hatua.”
Mwanahistoria Lucio Villari aliitaja taarifa ya papa kuwa “kukubali kabisa.” Kichwa kikuu cha gazeti la habari la kidesturi la Italia Il Giornale chasema: “Papa Asema Huenda Ikawa Tulitokana na Tumbili.” Na gazeti Time lilikata kauli kwamba kukiri kwa papa “kwaonyesha kwamba kanisa limekubali mageuzi.”
Ni kwa nini kumekuwa na kile ambacho kimeitwa “kukubali nadharia ya mageuzi kwa kadiri fulani” kwa upande wa viongozi wa Katoliki? Kwa nini Kanisa Katoliki ya Kiroma limefanya amani na fundisho la mageuzi?
Ni wazi kwamba wanatheolojia wengi Wakatoliki waifikiria Biblia kuwa “neno la wanadamu,” wala si “neno la Mungu.” (1 Wathesalonike 2:13; 2 Timotheo 3:16, 17) Kanisa Katoliki lazingatia zaidi neno la wanamageuzi wa kisasa kuliko neno la Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, ambaye alithibitisha masimulizi ya Mwanzo juu ya uumbaji kwa kusema kwa usahihi: “Je, hamkusoma kwamba yeye aliyewaumba wao kutoka mwanzo aliwafanya wa kiume na wa kike?” (Mathayo 19:4) Wewe wafikiria ni maoni ya nani yanayostahili zaidi?
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Mashahidi wa Yehova na Mageuzi
Mashahidi wa Yehova kwa kudumu wametegemeza fundisho la Kristo kwamba Mungu aliwaumba moja kwa moja wenzi wa kwanza wa kibinadamu ‘akawafanya wa kiume na wa kike.’ (Mathayo 19:4; Mwanzo 1:27; 2:24) Katika mwaka wa 1886, Buku la 1 la Millennial Dawn (ambalo baadaye liliitwa Studies in the Scriptures) lilirejezea nadharia ya Darwin kuwa “nadharia isiyoweza kuthibitishwa,” na katika mwaka wa 1898, kijitabu The Bible Versus the Evolution Theory kilitegemeza masimulizi ya Biblia juu ya uumbaji. Masimulizi ya Biblia juu ya uumbaji pia yalitetewa katika vitabu The New Creation (1904) na Creation (1927) na vilevile katika makala za mapema zilizochapishwa katika The Watch Tower na The Golden Age.
Papa Pius wa 12 alipotangaza wazi barua yake Humani generis, mwaka wa 1950, Mashahidi wa Yehova walikuwa wakichapisha Evolution Versus the New World. Kijitabu hiki kina uthibitisho wa kisayansi na wa kihistoria kuhusu masimulizi ya Biblia juu ya uumbaji nacho chashutumu majaribio ya makasisi fulani ya kufanya “mwafaka kati ya mageuzi na Biblia.” Kitabu Did Man Get Here by Evolution or by Creation? (1967) pia hutegemeza masimulizi ya Biblia ya uumbaji, kama ilivyo na kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation?, kilichochapishwa katika mwaka wa 1985, na makala nyingi ambazo zimechapishwa katika Mnara wa Mlinzi na Amkeni!
Hivyo, wengi wamesaidiwa na Mashahidi wa Yehova kufahamu uthibitisho chungu nzima kwamba Mungu “ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake.”—Zaburi 100:3.