Kitabu Chashangaza Ulimwengu
Kitabu: The Origin of Species. “Cha pili kutoka Biblia,” akasema Ashley Montagu msomi wa sayansi ya binadamu, “hakuna kitabu kimepata kuwa chenye kuathiri mno hivyo.”
Mtungaji: Charles Darwin, ambaye wakati huo aliitwa na wengine “mwanamume aliye hatari kupita wote katika Uingereza.”
Habari kuu: Nadharia ya mageuzi. Maneno na semi kama vile “uteuzi wa asilia,” “halisalimika kwa wafaao zaidi,” na “mageuzi” sasa yametia mizizi kabisa. Lakini je, hiyo nadharia imeathiri zaidi ya lugha yako?
KUTOLEWA kwacho katika 1859, The Origin of Species, na Charles Darwin, kuliwasha mjadala motomoto katika nyanja za kisayansi na kidini.a Huo mjadala ulivuka kwenye vizio vya kiuchumi na kijamii na hata waendelea hadi leo hii, yapata miaka 136 baadaye.
Katika A Story Outline of Evolution, C. W. Grimes aliandika kuhusu Origin of Species cha Darwin hivi: “Hakuna kitabu kinginecho kilichopata kuchapwa ambacho kimetokeza mabishano mengi hivyo miongoni mwa watu wenye kufikiri. Hakuna habari nyingine katika historia ya mwanadamu ambayo imeweza kutatiza kwa kiwango kikubwa itikadi za kimapokeo, kubadili Asili ya ulimwengu, na kufanyiza na kugandisha mawazo ya mwanadamu kama ile ya Mageuzi.”
Ni kweli, Darwin hakuanzisha nadharia ya mageuzi; hiyo dhana yaweza kufuatilia nyuma hadi Ugiriki ya kale. Pia kulikuwa na watangulizi kadhaa wa Darwin wa karne ya 18 waliotayarisha njia kwa wengi kukikubali The Origin of Species.
Hata hivyo, kilikuwa kitabu cha Darwin kilichokuja kuwa msingi wa mawazo ya kisasa ya kimageuzi. Kilishangaza, kwa hakika kilishtua ulimwengu, kwani nadharia yacho ya mageuzi ilitokeza zaidi ya mapinduzi katika biolojia. Kilipiga kana kwamba ni dhoruba kwenye misingi yenyewe ya jamii—dini, sayansi, siasa, uchumi, maisha ya kijamii, historia, na mtazamo wa wakati ujao.
Nadharia hiyo imeathirije ulimwengu kwa zaidi ya karne sasa? Imeathirije maisha yako? Kwa kweli matokeo yayo ni yapi? Makala zifuatazo zitachunguza maswali haya.
[Maelezo ya Chini]
a Kichwa kamili cha kitabu cha Darwin ni On the Origin of Species by Means of Natural Selection, or the Preservation of Favoured Races in the Struggle for Life.