Je, Wafundisha Kama Alivyofanya Yesu?
“Makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.”—MATHAYO 7:28, 29.
1. Ni nani waliomfuata Yesu alipokuwa akifundisha katika Galilaya, na Yesu aliitikiaje?
KOKOTE alikoenda Yesu, umati ulimmiminikia. “Alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.” Ripoti za utendaji wake mbalimbali zilipoenea, “makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani.” (Mathayo 4:23, 25) Alipowaona, “aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.” Alipowafundisha wao wangeweza kuhisi huruma na shauku nyororo aliyokuwa nayo kwao; yalikuwa kama mafuta katika majeraha yao yaliyowafanya wamkaribie.—Mathayo 9:35, 36.
2. Zaidi ya miujiza ya Yesu, ni nini kilichovutia umati mkubwa?
2 Yesu alifanya miujiza ya kuponya watu kimwili kama nini—alitakasa wenye ukoma, alifanya viziwi kusikia, vipofu kuona, wenye ulemavu kutembea, wafu kurudia uhai! Kwa kweli maonyesho hayo ya ajabu sana ya uwezo wa Yehova ukifanya kazi kupitia Yesu yalikuwa yakivutia idadi kubwa ya umati! Lakini wao hawakuvutiwa na miujiza tu; umati mkubwa ulikuja pia kwa ajili ya ponyo la kiroho walilopata wakati Yesu alikuwa akifundisha. Kwa mfano, ona jinsi walivyoitikia baada ya kusikia Mahubiri yake ya Mlimani yaliyo maarufu sana: “Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.” (Mathayo 7:28, 29) Marabi wao walinukuu kutoka kwa mapokeo ya mdomo ya marabi wa kale ili kutegemeza mafundisho yao. Yesu aliwafundisha akiwa na mamlaka kutoka kwa Mungu: “Hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.”—Yohana 12:50.
Mafundisho Yake Yalifika Moyoni
3. Njia ya Yesu ya kutoa ujumbe yatofautianaje na njia ya waandishi na Mafarisayo?
3 Tofauti kati ya mafundisho ya Yesu na yale ya waandishi na Mafarisayo haikuwa tu mambo yaliyofundishwa—kweli kutoka kwa Mungu kwa kutofautishwa na mapokeo ya mdomo ya watu yenye kulemeza—lakini vilevile jinsi yalivyofundishwa. Waandishi na Mafarisayo walikuwa wenye kiburi na wakali, wakidai kwa kiburi kupewa majina makubwa ya kuwatukuza huku wakiwadharau sana umati kuwa ‘walaaniwa.’ Lakini, Yesu alikuwa mnyenyekevu, mpole, mwenye fadhili, mwenye huruma, na mara nyingi mwenye usikivu, naye aliwahurumia sana. Yesu hakufundisha tu kwa maneno yaliyo sahihi bali pia kwa maneno yenye kuvutia yatokayo moyoni mwake, yaliyoingia moja kwa moja katika mioyo ya wasikilizaji wake. Ujumbe wake wenye furaha ulivuta watu kwake, ukiwasukuma kwenda mapema hekaluni kumsikiliza, na kuwafanya washikamane sana naye na kumsikiliza kwa furaha. Walikuja kwa wingi kumsikiliza, wakitangaza: “Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.”—Yohana 7:46-49; Marko 12:37; Luka 4:22; 19:48; 21:38.
4. Ni nini hasa kilichovutia watu wengi katika mahubiri ya Yesu?
4 Bila shaka, mojapo sababu zilizowafanya watu wavutiwe na mafundisho yake ni matumizi yake ya vielezi. Yesu aliona yale ambayo wengine waliona, lakini alifikiria mambo ambayo hawakupata kufikiri. Maua ya mayungiyungi yanayokua katika mashamba, ndege wanaojenga vioto vyao, watu wanaopanda nafaka, wachungaji wanaoleta wana-kondoo waliopotea, wanawake wanaoshona viraka katika mavazi makuukuu, watoto wanaocheza sokoni, wavuvi wanaovuta nyavu zao—vitu vya kawaida vilivyoonwa na kila mtu—havikuwa vya kawaida machoni pa Yesu. Kila mahali alipotazama, aliona kitu ambacho angetumia kutoa kielezi juu ya Mungu na Ufalme Wake au kukazia jambo fulani juu ya jamii ya wanadamu aliokuwa nao.
5. Yesu alitegemeza vielezi vyake juu ya nini, na ni nini kilichofanya mifano yake ifanikiwe?
5 Vielezi vya Yesu vyategemea mambo ya kila siku ambayo watu wameona mara nyingi, na kweli ziunganishwapo na mambo hayo ya kawaida, hizo hukaziwa kikiki kwa haraka ndani ya akili za watu wanaosikiliza. Kweli hizo hazisikiwi tu; hizo zaonwa na macho ya akili nazo zakumbukwa kwa urahisi baadaye. Mifano ya Yesu ilikuwa na mambo rahisi, isiyojaa mambo yasiyo ya maana ambayo huenda yangezuia kuelewa kwao kweli. Kwa kielelezo, fikiria mfano wa Msamaria mwenye ujirani. Unaona vizuri jirani mwema kuwa wa namna gani. (Luka 10:29-37) Kisha kulikuwa na wale wana wawili—mmoja aliyesema angefanya kazi katika shamba la mzabibu lakini hakuenda, na yule aliyesema kwamba hangeenda lakini akaenda. Waona upesi jambo muhimu la utii kamili—kufanya kazi uliyopewa kufanya. (Mathayo 21:28-31) Hakuna akili zilizochoka au kutangatanga wakati wa mafundisho ya Yesu yaliyochangamsha. Akili hizo zilikuwa na shughuli zikisikiliza na kuona mambo.
Yesu Alikuwa Msikivu Upendo Uliporuhusu
6. Kuwa mwenye ukubalifu au mwenye usikivu kwafaa hasa wakati gani?
6 Mara nyingi Biblia inapozungumzia kuwa mwenye ukubalifu, kielezi-chini huonyesha kwamba maneno hayo yamaanisha kuwa msikivu. Hekima itokayo kwa Mungu ni yenye usikivu wakati ambapo kuna hali zinazopunguza hatia ya mtu. Nyakati nyingine sisi huhitaji kuwa wenye ukubalifu, au wenye usikivu. Wazee wapaswa kuwa tayari kuwa wasikivu upendo na toba ziruhusupo. (1 Timotheo 3:3; Yakobo 3:17) Yesu aliacha vielelezo vizuri ajabu vya usikivu, akiachilia sheria za kawaida wakati rehema au huruma iliporuhusu.
7. Ni nini baadhi ya vielelezo vya Yesu akiwa mwenye usikivu?
7 Pindi moja Yesu alisema hivi: “Mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” Lakini hakumkataa Petro, Petro ajapomkana mara tatu. Kulikuwa na hali zilizopunguza hatia zake, ambazo kwa wazi Yesu alifikiria. (Mathayo 10:33; Luka 22:54-62) Pia kulikuwa na hali zenye kupunguza hatia wakati mwanamke asiye safi aliyekuwa akitiririka damu alipovunja Sheria ya Kimusa kwa kuingia katika umati. Yesu naye hakumshutumu. Alielewa hali yake mbaya. (Marko 1:40-42; 5:25-34; ona pia Luka 5:12, 13.) Yesu alikuwa amewaambia mitume wake wasimtambue kuwa Mesiya, lakini hakushikilia sana sheria hiyo alipojitambulisha hivyo kwa mwanamke Msamaria kisimani. (Mathayo 16:20; Yohana 4:25, 26) Katika hali hizo zote, upendo, rehema, na huruma ziliruhusu usikivu ufae.—Yakobo 2:13.
8. Waandishi na Mafarisayo wangevunja sheria wakati gani, nao hawangezivunja wakati gani?
8 Hiyo ilikuwa tofauti na waandishi na Mafarisayo wasiokuwa wasikivu. Wao wenyewe wangevunja mapokeo yao ya Sabato ili kuwaongoza fahali zao kwenda majini. Au fahali yao au mwana wao aangukapo kisimani, wangevunja Sabato ili kumwondoa. Lakini kwa watu wa kawaida, hawangekuwa wasikivu hata kidogo! Wao hawakutaka “kuigusa [matakwa hayo] kwa kidole chao.” (Mathayo 23:4; Luka 14:5) Kwa Yesu, watu walikuwa wenye umaana kuliko sheria zilizo nyingi; kwa Mafarisayo, sheria zilikuwa za maana kuliko watu.
Kuwa “Mwana wa Amri”
9, 10. Baada ya kurudi Yerusalemu, wazazi wa Yesu walimpata wapi, na umaana wa maswali ya Yesu ulikuwa nini?
9 Watu fulani hulalamika kwamba kuna tukio moja tu katika maisha ya ujana ya Yesu lililotajwa. Lakini wengi hukosa kuona umuhimu wa tukio hilo. Laripotiwa kwetu kwenye Luka 2:46, 47: “Baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.” Theological Dictionary of the New Testament cha Kittel chatoa wazo kwamba katika hali hiyo neno la Kigiriki la ‘kuuliza maswali’ halikuwa udadisi tu wa utoto. Neno hilo laweza kurejezea kuuliza maswali katika kikao cha hukumu, uchunguzi, mahoji, na hata larejezea “maswali ya kindani na yenye ujanja ya Mafarisayo na Masadukayo,” kama yale yatajwayo kwenye Marko 10:2 na 12:18-23.
10 Kamusi iyo hiyo yaendelea kusema: “Kwa sababu ya matumizi hayo, yaweza kuulizwa kama . . . [Luka] 2:46 yaonyesha, si maswali mengi yenye udadisi ya mvulana huyo, bali ni hoja Zake zenye mafanikio. [Mstari] 47 waweza kupatana sana na maoni hayo ya mwisho.”a Tafsiri ya Rotherham ya mstari 47 yaonyesha tukio hilo kuwa kabiliano lenye kutazamisha: “Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.” Word Pictures in the New Testament cha Robertson chasema kwamba ustaajabu wao wa daima wamaanisha kwamba “walisimama kando yao wenyewe kana kwamba macho yao yalikuwa yakitoka.”
11. Mariamu na Yosefu waliitikiaje yale waliyoona na kusikia, na kamusi moja ya kitheolojia yadokeza nini?
11 Hatimaye wazazi wa Yesu walipokuja, “walishangaa.” (Luka 2:48) Robertson asema kwamba neno la Kigiriki katika semi hiyo lamaanisha “kupiga, kuondosha kwa kupiga.” Yeye aongezea kwamba Yosefu na Mariamu “walipigwa” kwa yale waliyoona na kusikia. Kwa maana fulani, tayari Yesu alikuwa mwalimu mwenye kustaajabisha. Na kwa kufikiria tukio hilo katika hekalu, kitabu cha Kittel chadai kwamba “tayari Yesu ameanza katika ujana Wake upinzani ambao maadui Wake hatimaye watasalimu amri.”
12. Ni jambo gani lilitokea katika mazungumzo ya baadaye ya Yesu pamoja na viongozi wa kidini?
12 Nao walisalimu amri! Miaka ya baadaye, ilikuwa ni kwa kuuliza maswali kama hayo kwamba Yesu alishinda Mafarisayo mpaka “hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.” (Mathayo 22:41-46) Masadukayo vilevile walinyamazishwa juu ya swali la ufufuo, nao “hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.” (Luka 20:27-40) Waandishi nao hawakufanikiwa. Baada ya mmoja wao kuwa na mazungumzo pamoja na Yesu, “hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.”—Marko 12:28-34.
13. Ni nini kilichofanya lile tukio katika hekalu liwe la maana katika maisha ya Yesu, nalo ladokeza uelewevu gani?
13 Kwa nini tukio hili lililohusu Yesu na walimu hekaluni ndilo linalotajwa katika kumbukumbu? Ulikuwa ni wakati wa mabadiliko katika maisha ya Yesu. Alipokuwa na umri upatao miaka 12, alikuja kuwa kile ambacho Wayahudi walikiita “mwana wa amri,” akiwa na daraka la kutii sheria zayo zote. Mariamu alipomlalamikia Yesu kuhusu mkazo wa kiakili aliomsababishia yeye na Yosefu, jibu la mwana wake laelekea lilionyesha kwamba alijua jinsi alivyozaliwa kimwujiza na wakati wake ujao wa Kimesiya. Jambo hilo ladokezwa kwa kutaja kwake kwamba kwa njia ya moja kwa moja, Mungu alikuwa Baba yake: “Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?” Hayo nayo yalikuwa maneno ya kwanza ya Yesu yaliyoandikwa katika Biblia, nayo yaonyesha kujua kwake kusudi la Yehova la kumtuma duniani. Kwa hiyo, tukio hilo lote lina umaana sana.—Luka 2:48, 49.
Yesu Apenda na Kuwaelewa Watoto
14. Ni mambo gani yapendezayo ambayo simulizi hilo la Yesu mchanga akiwa hekaluni laweza kukazia vijana?
14 Simulizi hilo lapasa hasa kusisimua vijana. Laonyesha jinsi lazima iwe Yesu alisoma kwa bidii alipokuwa akikua mtu mzima. Marabi katika hekalu walistaajabishwa na hekima ya “mwana wa amri” huyo mwenye umri wa miaka 12. Na bado alifanya kazi pamoja na Yosefu katika duka la useremala, ‘akaendelea kumtii’ yeye na Mariamu, akaendelea ‘kupendeza Mungu na wanadamu.’—Luka 2:51, 52.
15. Yesu alikuwaje mwenye utegemezo kwa vijana wakati wa huduma yake duniani, na jambo hilo lamaanisha nini kwa vijana leo?
15 Yesu alitegemeza vijana sana katika huduma yake ya duniani: “Wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?” (Mathayo 21:15, 16; Zaburi 8:2) Leo, yeye hutegemeza vivyo hivyo mamia ya maelfu ya vijana wanaoshika ukamilifu wao wa maadili na kutoa sifa, wengine wao wakifanya hivyo kwa gharama ya uhai wao!
16. (a) Yesu alifundisha mitume wake somo gani kwa kusimamisha mtoto mchanga katikati yao? (b) Ni katika pindi gani iliyo muhimu sana maishani mwa Yesu ambayo bado alikuwa na wakati kwa ajili ya watoto?
16 Mitume walipobishana juu ya ni nani aliyekuwa mkuu zaidi, Yesu aliwaambia hivi wale 12: “Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.” (Marko 9:35-37) Isitoshe, alipokuwa akienda Yerusalemu kwa mara ya mwisho, ili akabili maono ya kuogofya na kifo, yeye alichukua fursa ya kuwa na watoto: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.” Kisha “akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.”—Marko 10:13-16.
17. Kwa nini ilikuwa rahisi kwa Yesu kushughulika na watoto, na ni lazima watoto wakumbuke nini kumhusu?
17 Yesu ajua jinsi ilivyo kuwa mtoto katika ulimwengu wa watu wazima. Yeye aliishi na watu wazima, alifanya kazi pamoja nao, akawa na ono la kuwatii, naye alipata hisia changamfu ya usalama itokanayo na kupendwa nao. Watoto, Yesu uyu huyu ni rafiki yenu; alikufa kwa ajili yenu, nawe utaishi milele ukitii amri zake.—Yohana 15:13, 14.
18. Ni wazo gani zito tupaswalo kuweka akilini, hasa katika nyakati za mikazo na hatari?
18 Kufanya kama aamuruvyo Yesu si vigumu kama huenda ikaonekanavyo. Vijana, yeye yupo kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wengine wote, kama tusomavyo kwenye Mathayo 11:28-30: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, [au, “Ingieni ndani ya nira yangu pamoja nami,” kielezi-chini, NW] mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” Ebu wazia, utumiapo maisha yako kumtumikia Yehova, Yesu atumika kando yako, akifanya nira iwe laini na mzigo kuwa mwepesi. Hilo ni wazo lenye kutusisimua sisi sote!
19. Ni maswali gani kuhusu njia za Yesu za kufundisha tunayoweza kupitia pindi kwa pindi?
19 Baada ya kupitia baadhi tu ya njia ambazo Yesu alitumia kufundisha, je, twaona kwamba tunafundisha kama alivyofanya? Tuonapo wale ambao ni wagonjwa kimwili na wenye njaa kiroho, je, sisi husukumwa na huruma tufanye yale tuwezayo ili kuwasaidia? Tufundishapo wengine, je, tunafundisha Neno la Mungu, au, kama Mafarisayo, twafundisha mawazo yetu wenyewe? Je, tu macho kuona mambo ya kawaida yatuzungukayo ambayo yanaweza kutumiwa kuelewesha, kuwazia, kudhihirisha, ili kuongeza uelewevu wa kweli za kiroho? Je, sisi huepuka kushikilia sana sheria fulani, wakati ambapo kwa sababu ya hali, inakuwa bora zaidi kuonyesha upendo, na rehema kwa kuachilia matumizi ya sheria kama hizo? Na vipi juu ya watoto? Je, tunawaonyesha hangaiko lenye uanana na upendo wenye fadhili kama alivyoonyesha Yesu? Je, wewe huwatia moyo watoto wako kujifunza kama alivyofanya Yesu akiwa mvulana? Je, utatenda kwa uthabiti kama alivyofanya Yesu lakini ukiwa tayari kupokea watu wenye toba kwa uchangamfu, kama kuku awakusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake?—Mathayo 23:37.
20. Twaweza kujifariji na wazo gani lenye kupendeza tumtumikiapo Mungu wetu?
20 Tukijitahidi kufanya yote tuwezayo katika kufundisha kama alivyofanya Yesu, kwa hakika ataturuhusu ‘tuingie chini ya nira yake pamoja naye.’—Mathayo 11:28-30.
[Maelezo ya Chini]
a Bila shaka, tuna sababu za kuamini kwamba Yesu alionyesha staha ifaayo kwa wale waliokuwa na umri mkubwa kumliko, hasa wenye mvi na makuhani.—Linganisha Mambo ya Walawi 19:32; Matendo 23:2-5.
Je! Wakumbuka?
◻ Kwa nini umati ulimmiminikia Yesu?
◻ Kwa nini nyakati nyingine Yesu alikuwa msikivu kwa sheria fulani?
◻ Twaweza kujifunza nini kutokana na vile Yesu alivyowauliza maswali walimu wa hekalu?
◻ Twaweza kujifunza masomo gani kutokana na uhusiano wa Yesu pamoja na watoto?