Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 11/15 kur. 29-31
  • Alipewa Neema na Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Alipewa Neema na Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Pendeleo Lake la Ajabu
  • Awa Mke wa Yusufu
  • Mariamu Alikuwa na Watoto Wengine
  • Mama Mhofu-Mungu
  • Mariamu Akiwa Mwanafunzi wa Yesu
  • Mapendeleo ya Milele
  • “Tazama! Kijakazi wa Yehova!”
    Igeni Imani Yao
  • Mfano wa Maria Unatufundisha Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • “Tazama! Kijakazi wa Yehova!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Alikabiliana na Upanga wa Majonzi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 11/15 kur. 29-31

Alipewa Neema na Yehova

“SALAMU, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.” Salamu ya ajabu kama nini! Msemaji si mwingine ila malaika Gabrieli. Anaongea na mwanamke mchanga mwenye moyo wa unyenyekevu—Mariamu, binti ya mwanamume aitwaye Heli. Ni mwaka wa 3 K.W.K., na mahali ni jiji la Nazareti.—Luka 1:26-28.

Mariamu ameposwa na Yusufu yule seremala. Kulingana na sheria na desturi za Kiyahudi, yeye aonwa kama mke aliyeozwa. (Mathayo 1:18) Kama Mariamu, Yusufu ni wa maisha ya hali ya chini. Kwa nini basi, malaika anamsalimu kuwa yule aliyepewa neema?

Pendeleo Lake la Ajabu

Gabrieli aongeza: “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”—Luka 1:29-33.

Kwa kustaajabu na kufadhaika, Mariamu auliza: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” Gabrieli ajibu: ‘Roho takatifu itakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.’ Kuondoa shaka lolote, malaika aongeza: “Tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”—Luka 1:34-37.

Mara hiyo Mariamu akubali pendeleo hili la utumishi la ajabu. Kwa utayari, lakini kwa unyenyekevu, aitikia: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha Gabrieli aondoka. Mariamu akaondoka haraka-haraka kuenda katika eneo lenye milima la Yuda. Alipofika nyumbani mwa kuhani Zekaria na mkeye, Elisabeti, anakuta hali zikiwa sawa na vile malaika alivyozieleza. Mariamu ajawa na furaha moyoni kama nini! Midomo yake yabubujika maneno ya kumsifu Yehova.—Luka 1:38-55.

Awa Mke wa Yusufu

Bikira atatoa mwili wa kibinadamu wa Yesu, kwa kuwa kuzaliwa huko kulikuwa kumetabiriwa. (Isaya 7:14; Mathayo 1:22, 23) Lakini kwa nini bikira aliyechumbiwa ahitajiwa? Ili aandae baba mlezi ambaye aweza kumkabidhi mtoto huyo uhalali wa kiti cha enzi cha Mfalme Daudi. Yusufu na Mariamu ni wa kabila la Yuda nao ni wazao wa Mfalme Daudi. Hivyo haki ya urithi ya Yesu itaimarishwa maradufu. (Mathayo 1:2-16; Luka 3:23-33) Hii ndiyo sababu malaika baadaye amhakikishia Yusufu kwamba hapaswi kusitasita kumchukua Mariamu akiwa mke wake halali, ingawa yeye ni mja mzito.—Mathayo 1:19-25.a

Amri ya kutoza kodi iliyotolewa na Kaisari Augusto yawalazimisha Yusufu na Mariamu kujiandikisha katika Bethlehemu. Wakiwa huko, amzaa mwanaye wa kwanza. Wachungaji waja kuona kitoto hicho, nao wamsifu Baba yake, Yehova. Baada ya siku 40 za kutakaswa kulingana na Sheria ya Kimusa, Mariamu aenda hekaluni katika Yerusalemu kufanya ufuniko kwa dhambi zake. (Mambo ya Walawi 12:1-8; Luka 2:22-24) Ndio, kwa sababu hakuzaliwa bila dhambi, na hivyo kuwa na alama ya dhambi, kutokamilika kwake kwa kiasili lazima kufunikwe na matoleo ya upatanisho.—Zaburi 51:5.

Mariamu na Yusufu wakiwa hekaluni, Simeoni mzee-mzee na Ana nabii-mke aliyezeeka wapendelewa kumwona Mwana wa Mungu. Si Mariamu anayepata uangalifu wa watu. (Luka 2:25-38) Baadaye, mamajusi wamsujudia Yesu.—Mathayo 2:1-12.

Baada ya kukimbilia Misri na kukaa huko hadi Herode mwovu afe, wazazi wa Yesu warudi na kukaa katika kijiji kidogo cha Nazareti. (Mathayo 2:13-23; Luka 2:39) Ni huko ambako Yusufu na Mariamu wamlea Yesu katika hali za familia za kimungu.

Mariamu Alikuwa na Watoto Wengine

Baada ya muda, Mariamu na Yusufu wamwandalia Yesu ndugu na dada wa kimwili. Huduma ya Yesu imrudishapo kwenye mji wa nyumbani kwao Nazareti, watu waliomjua akiwa mchanga wamtambua. “Huyu si mwana wa seremala?” wao wauliza. “Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu?” (Mathayo 13:55, 56) Wanazareti hao wanarejezea familia ya kimwili ya Yusufu na Mariamu, kutia ndani wanawe na binti zake wawajuao kama ndugu na dada wa kimwili wa Yesu.

Hawa ndugu na dada si binamu wa Yesu. Wala si wanafunzi wake, au ndugu na dada wa kiroho, maana Yohana 2:12 hutofautisha wazi kati ya vikundi hivyo viwili kwa kusema: “[Yesu] akashuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake.” Miaka mingi baadaye katika Yerusalemu, mtume Paulo alimwona Kefa, au Petro, akasema: “Sikumwona mtume mwingine; ila Yakobo, ndugu yake Bwana.” (Wagalatia 1:19) Zaidi ya hayo, usemi wa kwamba Yusufu ‘hakumjua kamwe Mariamu hata alipomzaa mwanawe’ waonyesha kwamba baba mlezi wa Yesu alimjua Mariamu kimwili baadaye na kumzalia watoto wengine. (Mathayo 1:25) Hivyo, Luka 2:7 humwita Yesu “kifungua mimba.”

Mama Mhofu-Mungu

Akiwa mama anayemhofu Mungu, Mariamu ashirikiana na Yusufu katika kuwaagiza watoto wake katika uadilifu. (Mithali 22:6) Kuwa kwake mwanafunzi mwenye bidii wa Maandiko kwaonyeshwa na usemi uliojaa mambo ya kiroho aliposalimiwa na Elisabeti. Wakati huo mama ya Yesu arudia semi za wimbo wa Hana na aonyesha ujuzi wa zaburi, maandishi ya kihistoria na ya kiunabii, na vitabu vya Musa. (Mwanzo 30:13; 1 Samweli 2:1-10; Mithali 31:28; Malaki 3:12; Luka 1:46-55) Mariamu alikuwa ameweka akilini matukio na semi za kiunabii kuyahifadhi ndani ya moyo wake, na kuyatafakari akilini. Hivyo amejiandaa vema kushiriki katika maagizo ya kimzazi kwa kivulana Yesu.—Luka 2:19, 33.

Yesu aliyefundishwa vema akiwa na umri wa miaka 12 aonyesha ujuzi wa Kimaandiko uliowastaajabisha wanaume wenye elimu katika hekalu. Kwa sababu amejitenga na wazazi wake katika pindi hiyo ya Pasaka, mama yake amwambia: “Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.” Yesu akawaambia: “Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?” Akikosa kuelewa maana ya jibu hili, Mariamu aliweka moyoni mwake. Arudipo Nazareti, Yesu azidi “kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”—Luka 2:42-52.

Mariamu Akiwa Mwanafunzi wa Yesu

Ni jambo linalofaa kama nini kwamba mwishowe Mariamu akawa mwanafunzi aliyejitoa wa Yesu! Ijapokuwa pendeleo lake lisilo na kifani la mgawo aliopewa na Mungu, yeye ni mnyenyekevu na hana tamaa ya kutaka kujitokeza. Mariamu anayajua Maandiko. Ukiyachunguza wewe mwenyewe, hutapata yakimweleza kuwa na utukufu, akiwa ameketi kwenye kiti cha enzi kama “mama-malkia” mwenye kung’aa kwa utukufu wa Kristo. Badala ya hivyo, utafahamu kwamba yeye ni wa kawaida bila mng’ao wowote.—Mathayo 13:53-56; Yohana 2:12.

Yesu alikatiza mapema heshima yoyote kama hiyo ya Kumtukuza Mariamu kati ya wafuasi wake. Pindi moja alipokuwa akisema, “mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.” (Luka 11:27, 28) Kwenye sherehe ya harusi, Yesu alimwambia Mariamu: “Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.” (Yohana 2:4) Tafsiri nyinginezo husema: “Acha jambo hili mikononi mwangu.” (Weymouth) “Usijaribu kuniongoza.” (An American Translation) Ndiyo, Yesu alimheshimu mamaye, lakini hakumtukuza.

Mapendeleo ya Milele

Mariamu alifurahia mapendeleo yaliyoje! Alimzaa Yesu. Halafu akamlea na kumfundisha mtoto huyo. Mwishowe, akawa na imani, akija kuwa mwanafunzi na dada wa kiroho wa Kristo. Katika uchunguzi wetu wa mwisho wa Kimaandiko juu ya Mariamu, twamwona katika orofa ya juu katika Yerusalemu. Yuko huko pamoja na mitume wa Yesu, wanawe wengineo, na wanawake fulani waaminifu—wote wakiwa waabudu wa Yehova.—Matendo 1:13, 14.

Baada ya muda, Mariamu akafa na mwili wake ukarudi mavumbini. Kama vile wafuasi wengine wa mapema waliotiwa mafuta wa mwanaye mpendwa, alilala katika kifo hadi wakati uliowekwa wa Mungu wa kumfufua akiwa kiumbe wa roho akiwa na uhai usioweza kufa katika mbingu. (1 Wakorintho 15:44, 50; 2 Timotheo 4:8) Lazima huyu “aliyepewa neema” awe mwenye furaha nyingi sasa katika kuwapo mbele ya Yehova Mungu na Yesu Kristo!

[Maelezo ya Chini]

a Ikiwa Mariamu hangalikuwa bikira, ni nani angalitaka kumwoa? Wayahudi walisisitiza msichana awe bikira.—Kumbukumbu la Torati 22:13-19; linganisha Mwanzo 38:24-26.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Mariamu alipewa neema kuwa mama ya Yesu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki