Alikubali Mwelekezo wa Kimungu
WAZIA ukiwa na mtoto mkamilifu aliyewekwa chini ya utunzaji wako na unatazamiwa umlee vizuri. Ni mwito wa ushindani kama nini! Binadamu yeyote asiyekamilika angewezaje kufanya hivyo? Ni kwa kukubali tu mwelekezo wa kimungu na kuutumia katika maisha ya kila siku.
Jambo lilo hilo lilifanywa na Yusufu, baba mlezi wa Yesu. Kinyume cha elimu yenye kina ya apokrifa kuhusu Yusufu, Biblia husema machache kuhusu fungu lake lenye unyenyekevu katika maisha ya mapema ya Yesu. Twajua kwamba Yusufu na mkeye, Mariamu, walimlea Yesu, wana wengine wanne, na mabinti pia.—Marko 6:3.
Yusufu alikuwa mzao wa Mfalme Daudi wa Israeli kupitia mstari wa Sulemani. Alikuwa mwana wa Yakobo na mwana-mkwe wa Heli. (Mathayo 1:16; Luka 3:23) Akiwa seremala kwenye jiji la Nazareti katika Galilaya, Yusufu alikuwa na mapato ya chini. (Mathayo 13:55; Luka 2:4, 24; linganisha Mambo ya Walawi 12:8.) Lakini alikuwa tajiri kiroho. (Mithali 10:22) Kwa kweli hili lilikuwa kwa sababu alikubali mwelekezo wa kimungu.
Bila shaka, Yusufu alikuwa Myahudi mpole na mnyenyekevu aliyekuwa na imani katika Mungu na kutamani kufanya yaliyokuwa haki. Matukio machache ya maisha yake yaliyorekodiwa katika Maandiko yanaonyesha kwamba alikuwa mtiifu nyakati zote kwa Yehova. Ilikuwa hivyo iwe yalikuwamo ndani ya Sheria au yalipokewa na Yusufu moja kwa moja kupitia kwa malaika.
Mtu Mwadilifu Mwenye Matatizo
Mtu wa kimungu apaswa kufanya nini akabiliwapo na tatizo kubwa? Kwa kweli, apaswa ‘kumtwika BWANA [“Yehova,” NW] mzigo wake’ na kufuata mwelekezo wa kimungu! (Zaburi 55:22) Hivyo ndivyo Yusufu alivyofanya. Alipokuwa amemposa Mariamu, “kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu [“roho takatifu,” NW].” Kwa sababu Yusufu ‘alikuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.’ Baada ya Yusufu kufikiria mambo tena, malaika wa Yehova alimtokea katika ndoto na kusema: “Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu [“roho takatifu,” NW]. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Alipoamka katika usingizi, Yusufu “alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.” (Mathayo 1:18-25) Yusufu alikubali mwelekezo wa kimungu.
Kaisari Augusto aliagiza kwamba watu wajiandikishe katika majiji yao. Kwa utii, Yusufu na Mariamu walienda Bethlehemu katika Yudea. Huko Mariamu alimzaa Yesu na ilimbidi amlaze kwenye hori kwa sababu hapakuwa na mahali pengine pa kulala. Usiku huo wachungaji waliokuwa wamesikia tangazo la kimalaika juu ya kuzaliwa huku kwa pekee walikuja kuona mtoto. Yapata siku 40 hivi baadaye, Yusufu na Mariamu walitii Sheria kwa kumpeleka Yesu kwenye hekalu katika Yerusalemu pamoja na toleo. Wote wawili walishangaa waliposikia maneno ya kiunabii ya Simeoni mzee-mzee kuhusu mambo makubwa ambayo Yesu angefanya.—Luka 2:1-33; linganisha Mambo ya Walawi 12:2-4, 6-8.
Ingawa huenda andiko la Luka 2:39 likaonyesha kwamba Yusufu na Mariamu walienda Nazareti mara tu baada ya kumpeleka Yesu hekaluni, andiko hili ni sehemu ya muhtasari wa andiko. Inaonekana kwamba muda mrefu kadiri fulani baada ya matoleo hekaluni, mamajusi wa Mashariki (Magi) walimzuru Mariamu na Yesu katika nyumba fulani huko Bethlehemu. Mwingilio wa kimungu ulizuia ziara hii isimletee Yesu kifo. Baada ya Mamajusi hao kuondoka, malaika wa Yehova walimtokea Yusufu katika ndoto na kumwambia: “Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.” Kama kawaida, Yusufu alitii mwelekezo wa kimungu na kupeleka familia yake Misri.—Mathayo 2:1-14.
Herode alipokufa, malaika akamtokea Yusufu katika Misri katika ndoto, akisema: “Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli.” Aliposikia kwamba mwana wa Herode Arkelao anatawala mahali pa babaye, Yusufu aliogopa kurudi Yudea. Akitii onyo la kimungu alilopewa katika ndoto, alienda katika eneo la Galilaya na kukaa katika jiji la Nazareti.—Mathayo 2:15-23.
Mtu wa Kiroho
Yusufu alihakikisha kwamba familia yake ilitii sheria ya kimungu nao wakategemezwa kiroho. Kila mwaka alichukua familia yake yote kwenye sherehe ya Sikukuu ya Kupitwa katika Yerusalemu. Katika moja ya pindi hizi, Yusufu na Mariamu walikuwa wakirudi Nazareti na walikuwa wamesafiri mwendo wa siku moja kutoka Yerusalemu walipotambua kwamba Yesu mwenye umri wa miaka 12 anakosekana. Waliporudi Yerusalemu, walimtafuta kwa makini sana na mwishowe wakampata kwenye hekalu, akisikiliza na kuwauliza maswali walimu huko.—Luka 2:41-50.
Yaonekana kwamba Yusufu alimpa mkeye nafasi ya kwanza katika mambo fulani. Kwa kielelezo, waliporudi Yerusalemu na kumpata Yesu hekaluni, ni Mariamu aliyesema na mwanaye mchanga kuhusu jambo hilo. (Luka 2:48, 49) Akiendelea kukua akiwa “mwana wa seremala,” Yesu alipokea maagizo ya kiroho. Yusufu alimfundisha useremala pia, maana Yesu alijulikana kama “yule seremala, mwana wa Mariamu.” (Mathayo 13:55; Marko 6:3) Wazazi wa kimungu leo wanapaswa kutumia kikamili nafasi kama hizo kuwaagiza watoto wao, hasa kuwapa mazoezi ya kiroho.—Waefeso 6:4; 2 Timotheo 1:5; 3:14-16.
Matazamio ya Yusufu
Maandiko hayatoi habari yoyote kuhusu kifo cha Yusufu. Lakini yaonekana kwamba andiko la Marko 6:3 lilimwita Yesu “mwana wa Mariamu,” si wa Yusufu. Hili linaonyesha kwamba wakati huo Yusufu alikuwa amekufa. Zaidi ya hayo, ikiwa Yusufu alikuwa ameishi hadi mwaka wa 33 W.K., Yesu aliyekuwa ametundikwa hangemkabidhi Mariamu chini ya utunzaji wa mtume Yohana.—Yohana 19:26, 27.
Hivyo, Yusufu, atakuwa miongoni mwa wafu watakaosikia sauti ya Mwana wa Adamu na kurudi kwa njia ya ufufuo. (Yohana 5:28, 29) Akijifunza juu ya uandalizi wa Yehova wa uhai wa milele, bila shaka Yusufu atautumia kwa furaha na atakuwa raia mtiifu wa Mfalme, mkuu wa kimbingu, Yesu Kristo, kama vile tu alivyotii mwelekezo wa kimungu zaidi ya miaka 1,900 iliyopita.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Yusufu alimpa Yesu maagizo ya kiroho na pia kumfundisha useremala