Kutoa Je, Hutazamiwa?
HUENDA ukajua vizuri kwamba kutoa zawadi mara nyingi hufuata desturi. Katika tamaduni nyingi kuna vipindi ambavyo zawadi hutazamiwa. Zawadi hizo huenda zikawa ishara za staha au maonyesho ya upendo. Nyingi zazo hazitumiwi kamwe na wenye kuzipokea; nyingine husaidia kutimiza mahitaji ya kweli nazo huthaminiwa kwelikweli.
Katika Denmark mtoto anapozaliwa, marafiki na watu wa ukoo huzuru na kuleta zawadi ambazo wanatumaini kwamba zitakuwa zenye manufaa kwa kitoto hicho. Katika nchi nyinginezo, marafiki waweza kufanya sherehe ambapo zawadi kama hizo hutolewa kwa kutazamia kuzaliwa kwa mtoto.
Mara nyingi, pindi ambazo zawadi hutazamiwa, ni katika sherehe za mwaka. Ingawa sherehe kama hizo hazikuwa zoea miongoni mwa Wakristo wa mapema, zimekuja kupendwa sana miongoni mwa wengi wanaojiita Wakristo na wasio Wakristo vilevile. Katika tamaduni nyinginezo, zoea la kutoa zawadi za siku ya kuzaliwa huenda likafifia watoto wanapoendelea kuwa wakubwa, lakini desturi miongoni mwa Wagiriki ni kinyume cha hilo. Katika Ugiriki siku za kuzaliwa hutiliwa mkazo mwingi. Wao pia hutolea mtu zawadi “siku [yake] ya kupewa jina.” Hiyo ni nini? Desturi za kidini huunganisha “mtakatifu” fulani kwa kila siku ya mwaka, nao watu wengi hupewa jina la “watakatifu” hao. Siku ya “mtakatifu” ifikapo, waitwao kwa jina hilo hupokea zawadi.
Kuongezea sherehe za siku ya kuzaliwa kwa watoto wao, Wakorea wana sikukuu ya kitaifa iitwayo Siku ya Watoto. Huo ni wakati ambapo familia huenda kutembea na ambapo zawadi zinapewa watoto bila kujali tarehe zao za kuzaliwa. Wakorea pia wana Siku ya Wazazi, ambapo watoto huwapa wazazi wao zawadi, na Siku ya Walimu, ambapo wanafunzi huwaonyesha heshima walimu wao na kuwapa zawadi. Kulingana na desturi ya Wakorea, mtu afikapo umri wa miaka 60, sherehe kubwa hufanywa. Familia na marafiki huungana katika kutakia maisha marefu na furaha yule aliyefikia umri huo, naye hupokea zawadi.
Arusi ni tukio jingine ambapo wengi wana desturi ya kutoa zawadi. Katika Kenya watu wanapooana, familia ya bwana-arusi hutazamiwa kutolea zawadi familia ya bibi-arusi. Wageni pia huleta zawadi. Ikiwa hawa bwana-arusi na bibi-arusi watafuata vile desturi isemavyo, wataketi jukwaani, huku wageni wakiwapelekea zawadi mbele. Kila zawadi itolewapo, tangazo litafanywa kwamba “Fulani na fulani wameletea maarusi zawadi.” Watu wengi wenye kutoa zawadi waweza kuhisi vibaya sana ikiwa hawakutambuliwa hivyo.
Miongoni mwa Walebanoni, mtu anapojitayarisha kuoa au kuolewa, marafiki na majirani, hata watu wasiowajua vizuri hao watakaooana, huanza kufika siku nyingi kabla ya siku ya arusi wakibeba zawadi. Tangu utotoni, wao hufundishwa kwamba kutoa zawadi ni daraka, kama vile kulipa deni. “Usipofanya hivyo, huhisi vizuri,” akasema mtu mmoja Mlebanoni. “Hilo ni pokeo.”
Hata hivyo, katika pindi zote ambapo zawadi hutazamiwa, Krismasi ndiyo ya kwanza katika nchi nyingi. Je, sivyo ilivyo unakoishi? Hivi majuzi katika 1990, ilikadiriwa kwamba kila mwaka Wamarekani hutumia zaidi ya dola bilioni 40 kwa zawadi za Krismasi. Kwa uchangamfu mwingi sikukuu hiyo husherehekewa na Wabuddha na Washinto katika Japani, na aina mbalimbali za sherehe zapatikana katika Ulaya, Amerika Kusini, na sehemu za Afrika.
Krismasi ni pindi ambayo watu hutazamia kufurahi, lakini wengi hawafurahi. Na walio wengi huona kwamba ununuzi mwingi mno wa zawadi na masumbufu ya kulipa gharama ya vitu hivyo huwa mengi kupita dakika zozote zile za raha wazipatazo.
Hata hivyo, Biblia husema kwamba kuna furaha katika kutoa. Kwa kweli ipo, ikitegemea roho ya kutoa.—Matendo 20:35.