Jeuri Ipo Kila Mahali
AKIWA ameketi katika gari lake akingoja taa zimruhusu kupita, kwa ghafula huyo dereva alimwona mtu mwenye mwili mkubwa akimjia, huku akisema matusi kwa sauti kubwa na kutikisa ngumi hewani. Huyo dereva akaharakisha kufunga vizuri milango yake na madirisha yake, lakini yule mtu mwenye mwili mkubwa akaendelea kumjia. Mtu huyo akainama na kutikisa gari kisha akaenda mlangoni mwa gari. Hatimaye, kwa mfadhaiko akainua ngumi yake kubwa na kupiga kioo cha mbele, akakivunja vipande-vipande.
Je, hiyo ni mandhari ya sinema? La! Hilo lilikuwa bishano la wenye magari katika kisiwa cha Oahu, Hawaii, kijulikanacho sana kwa hali yacho tulivu na yenye ustarehe.
Hilo halishangazi. Makufuli milangoni, vyuma madirishani, walinzi kwenye majengo, hata ishara kwenye mabasi zisemazo “Dereva habebi pesa”—zote zaonyesha jambo moja: Jeuri ipo kila mahali!
Jeuri Nyumbani
Kwa muda mrefu nyumbani kumeonwa kuwa maskani salama ya mtu. Hata hivyo, hali hiyo nzuri inabadilika haraka. Jeuri ya familia, ambayo hutia ndani watoto kutendwa vibaya, kumpiga mwenzi wa ndoa, na uuaji, inafanyiza habari kuu ulimwenguni kote.
Kwa kielelezo, “angalau watoto 750,000 katika Uingereza waweza kupatwa na masumbufu ya akili ya muda mrefu kwa sababu walipatwa na jeuri nyumbani,” lasema Manchester Guardian Weekly. Ripoti hiyo ilitegemea uchunguzi ambao pia ulipata kwamba “wanawake watatu kati ya wanne waliohojiwa walisema kwamba watoto wao walikuwa wameona visa vyenye jeuri, na karibu thuluthi mbili ya hao watoto waliwaona mama zao wakipigwa.” Vivyo hivyo, kulingana na U.S.News & World Report, Kamati ya Marekani ya Kutoa Mashauri Juu Ya Kutendwa Vibaya na Kuachwa kwa Watoto yakadiria kwamba “watoto 2,000, wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka 4, hufa kila mwaka mikononi mwa wazazi au watunzi.” Idadi hiyo yashinda ile isababishwayo na aksidenti za magari, kufa maji, au kuanguka, yasema ripoti hiyo.
Jeuri ya nyumbani yatia ndani pia kumtenda mwenzi wa ndoa vibaya, kunakoanzia kusukumwa-sukumwa hadi kupigwa kofi, kupigwa teke, kukabwa-koo, kupigwa mwili, kutishwa kwa kisu au bunduki, au hata kuuawa. Na leo aina hii ya jeuri huathiri wote wanaume na wanawake. Uchunguzi mmoja umepata kwamba kati ya jeuri zilizoripotiwa kutokea kati ya waume na wake, karibu robo ya visa hivyo vilianzishwa na mwanamume, na robo nyingine kuanzishwa na mwanamke, na zinazobaki zilifafanuliwa kuwa magomvi ambayo katika hayo wote wawili wana lawama.
Jeuri Kazini
Mbali na nyumbani, kwa muda mrefu kazini pamekuwa mahali ambapo mtu hupata utengemano, staha na adabu. Lakini haielekei kuwa hivyo tena. Kwa mfano, tarakimu zilizotolewa na Idara ya Sheria ya Marekani zaonyesha kwamba kila mwaka zaidi ya watu 970,000 hupatwa na uhalifu wenye jeuri kazini. Kwa maneno mengine, “kila mfanyakazi mmoja kati ya wanne yumo hatarini mwa kupatwa na aina fulani ya jeuri kazini,” kulingana na ripoti moja katika Professional Safety—Journal of the American Society of Safety Engineers.
Jambo la kufadhaisha zaidi ni kwamba jeuri ya kazini haihusu tu mabishano makali na matukano. “Jeuri ambayo waajiriwa wengine huelekezea hasa waajiri na waajiriwa sasa ndiyo aina ya uuaji yenye kuongezeka kwa kasi zaidi Marekani,” yasema ripoti hiyo. Katika 1992, kifo 1 kati ya kila vifo 6 vyenye kuhusika na kazi kilikuwa uuaji; kwa wanawake, idadi hiyo ilikuwa karibu kifo 1 kati ya kila vifo 2. Hakuna shaka kwamba jeuri nyingi inaenea kazini ambapo zamani palikuwa mahali pa utengemano.
Jeuri Katika Michezo na Vitumbuizo
Michezo na vitumbuizo vimefuatiwa vikiwa njia ya kujifurahisha au kujistarehesha ili viburudishe mtu kwa ajili ya mambo ya maana zaidi maishani. Leo, vitumbuizo ni biashara iletayo mabilioni ya dola. Ili kupata faida kubwa katika biashara hii yenye pesa nyingi, watengeneza-vitumbuizo hawajali kutumia njia yoyote ile ya kuuza vitu vyao. Na njia moja ni jeuri.
Kwa kielelezo, Forbes, ambalo ni gazeti la biashara, liliripoti kwamba watengenezaji fulani wa michezo ya vidio wana mchezo mmoja wa vita upendwao sana ambamo shujaa mmoja hung’oa kichwa na uti wa mgongo wa mpinzani wake huku watazamaji wakipiga kelele, “Mwue! Mwue!” Hata hivyo, aina nyingine ya mchezo uo huo iliyotengenezewa kampuni nyingine yenye kushindana na kampuni hiyo haina umwagikaji mwingi sana wa damu kama ule wa kwanza. Tokeo likawa nini? Ule mchezo wenye jeuri zaidi uliuzwa zaidi kuliko huu mwingine kwa uwiano wa 3 kwa 2. Na hiyo yamaanisha pesa nyingi sana. Aina mbalimbali za michezo ya kuonyeshwa nyumbani zilipotokea, makampuni hayo yalipata dola milioni 65 katika mataifa mengi kwa majuma mawili ya kwanza! Wakati kuna faida, jeuri ni chambo kingine kwa wanunuaji.
Jeuri mchezoni ni jambo jingine baya. Wachezaji hujivunia madhara yoyote wawezayo kutokeza. Kwa mfano, katika mchezo mmoja wa mpira wa magongo katika 1990, kulikuwa na penalti 86—hiyo ikiwa ni rekodi mpya. Mchezo huo ulikatishwa kwa muda wa saa tatu na nusu wa mapigano ya kiholela. Mchezaji mmoja alitibiwa fupa la usoni lililovunjika, sehemu nyeupe ya jicho iliyokwaruzwa, na jeraha la kukatwa. Kwa nini kuwe na jeuri hivyo? Mchezaji mmoja alieleza: “Mshindapo mchezo wenye hisia-moyo nyingi, wenye mapigano mengi, wewe huenda nyumbani ukihisi ukiwa karibu zaidi na wachezaji wa timu yenu. Nafikiri hayo mapigano yalifanya mchezo uwe wa kiroho kwelikweli.” Katika michezo mingi ya leo, inaonekana jeuri haijawa tu njia ya kupata ushindi, bali yenyewe ndiyo ushindi.
Jeuri Shuleni
Sikuzote shule imeonwa kuwa ngome ambamo vijana waweza kusahau mahangaiko yao yote na kukaza akili kwenye kusitawisha akili zao na miili yao. Hata hivyo, leo shule si mahali salama tena. Mahoji ya Gallup katika 1994 yalipata kwamba jeuri na magenge ndiyo tatizo kubwa zaidi katika shule za umma Marekani, zikishinda matatizo ya kifedha, ambayo yalikuwa ya kwanza mwaka uliotangulia. Hali ni mbaya kadiri gani?
Kwa kujibu swali, “Je, umepata kuathiriwa na jeuri iliyofanyika shuleni au karibu na shule?” karibu mwanafunzi 1 kati ya kila 4 waliohojiwa alijibu ndiyo. Zaidi ya mwalimu 1 kati ya kila walimu 10 pia walijibu ndiyo. Uchunguzi uo huo ulipata kwamba asilimia 13 ya wanafunzi, wavulana na wasichana, walikiri kuwa wamepata kubeba silaha shuleni pindi moja au nyingine. Wengi wao walidai kwamba walifanya hivyo ili kuvutia wengine au kujikinga. Lakini mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 17 alimpiga risasi kifuani mwalimu wake wakati mwalimu huyo alipojaribu kumnyang’anya bunduki.
Utamaduni Wenye Jeuri
Hakuna shaka kwamba leo jeuri ipo kila mahali. Nyumbani, kazini, shuleni, na katika vitumbuizo, twakabili jeuri. Kwa kuiona kila siku, wengi wamekuja kuiona kuwa jambo la kawaida—mpaka wanapopatwa nayo. Ndipo wao huuliza, Je, itapata kuisha kamwe? Je, wewe pia ungependa kujua jibu? Basi tafadhali soma makala ifuatayo.