Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w96 2/15 kur. 5-7
  • Mwisho Wenye Kudumu wa Jeuri—Utakujaje?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwisho Wenye Kudumu wa Jeuri—Utakujaje?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kiwezacho Kufanywa?
  • Nguvu ya Neno la Mungu
  • Kampeni Imalizayo Jeuri
  • Somo Muhimu
  • Kutembea Pamoja na Mungu Katika Ulimwengu Wenye Jeuri
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Je, Inawezekana Kuishi Katika Ulimwengu Usio na Jeuri?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2016
  • Maoni ya Mungu Ni Nini Kuhusu Jeuri?
    Amkeni!—2002
  • Jeuri
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
w96 2/15 kur. 5-7

Mwisho Wenye Kudumu wa Jeuri—Utakujaje?

ILI kukomesha ongezeko la jeuri, majiji kadhaa katika Marekani yalifanya majaribio ya wazo jipya—kutoa pesa au bidhaa kwa bunduki zinazoletwa, bila kuuliza maswali yoyote. Tokeo likawa nini? Kwa gharama ya dola 341,000, jiji la St. Louis, kwa kielelezo, lilipata bunduki 8,500. Mpango kama huo katika New York City ulitokeza zaidi ya silaha elfu moja.

Mipango hiyo ilikuwa na tokeo gani kwa uhalifu? Kwa kusikitisha, hakuna. Mauaji yenye kuhusiana na bunduki yalivunja rekodi mwaka uliofuata katika St. Louis. Katika New York City, kungali kuna bunduki za watu wa kawaida zinazokadiriwa kuwa milioni mbili. Katika Marekani, kuna bunduki zipatazo milioni 200 za watu binafsi, karibu bunduki moja kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto. Katika nchi nyinginezo, jeuri yenye kuhusika na bunduki inaongezeka kwa kiwango cha kutisha. Katika Uingereza “kati ya 1983 na 1993, hesabu ya makosa yaliyorekodiwa na polisi ambayo kwayo bunduki zilitumiwa iliongezeka karibu maradufu kufikia 14,000,” lasema The Economist. Ingawa kiwango cha mauaji ni kidogo kwa kulinganisha, kuna silaha haramu zipatazo milioni moja katika nchi hiyo.

Kwa hakika, upungufu wowote wa idadi hizo zenye kuhofisha za bunduki ni maendeleo. Hata hivyo, hatua kama zile ambazo zimefafanuliwa hapo juu hazisuluhishi hata kidogo visababishi vya msingi vya jeuri. Visababishi hivyo ni nini? Mambo mengi yametajwa, lakini machache kati yayo ni ya msingi. Ukosefu wa uthabiti wa familia na mafundisho ya kiadili umefanya vijana wengi wajiunge na magenge ili wajihisi kuwa washiriki wa kikundi fulani. Uvutio wa kupata faida kubwa huchochea wengi kuingia katika jeuri. Ukosefu wa haki husukuma wengine wasuluhishe mambo kwa kutumia jeuri. Kuonea fahari nchi, jamii, au tabaka maishani hufanya watu wapuuze mateseko ya wengine. Hivyo ni visababishi vya ndani sana visivyo na masuluhisho rahisi.

Ni Nini Kiwezacho Kufanywa?

Je, ni kuongeza polisi wengi zaidi, vifungo vikali zaidi vya gereza, kudhibiti ununuzi wa bunduki, adhabu ya kifo—hayo yote yamependekezwa na kujaribiwa kuwa njia za kupunguza uhalifu na jeuri. Hizo zimeleta mafanikio ya kadiri mbalimbali, lakini uhakika wenye kuhuzunisha ni kwamba jeuri ingali sehemu kubwa ya maisha yetu. Kwa nini? Ni kwa sababu hatua hizo zinazochukuliwa hazisuluhishi tatizo lenyewe.

Kwa upande mwingine, wastadi wengi huhisi kwamba njia ya kumaliza jeuri ni elimu. Ingawa wazo hilo ni zuri, ni lazima tutaje kwamba jeuri haipatikani tu katika mataifa ambayo hayana fursa nyingi za elimu. Kwa hakika, inaonekana kwamba mataifa yenye jeuri zaidi ni yale yenye viwango vya juu zaidi vya elimu. Basi si vigumu kuona kwamba kile kinachohitajika si elimu tu, bali elimu ifaayo. Hiyo ni elimu ya aina gani? Je, kuna mtu anayeweza kufundisha watu kuwa wapenda amani na wanyoofu?

“Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako [“uadilifu wako,” “New World Translation”] kama mawimbi ya bahari.” (Isaya 48:17, 18, italiki ni zetu.) Yehova Mungu hufundishaje watu kuwa wapenda amani na waadilifu? Hasa kupitia Neno lake, Biblia.

Nguvu ya Neno la Mungu

Hakika Biblia si mkusanyo tu wa hadithi na misemo ya kale ambayo haitumiki sikuhizi na haituhusu. Hiyo ina kanuni na mawazo kutoka kwa Muumba wa wanadamu, ambaye, kutoka mahali pake pa juu zaidi, ajua asili ya kibinadamu kuliko mtu yeyote. “Kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu,” asema Yehova Mungu.—Isaya 55:9.

Kwa sababu hii mtume Paulo atoa ushuhuda kwamba “Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake.” (Waebrania 4:12) Ndiyo, Neno la Mungu lina nguvu ya kufikia na kugusa moyo wa mtu na kubadili kufikiri kwake na tabia yake. Je, si jambo hili linalohitajiwa kubadili njia za watu zenye jeuri leo?

Mashahidi wa Yehova, sasa wakiwa wapatao milioni tano katika nchi zaidi ya 230, ni uthibitisho uonekanao kwamba kwa kweli Neno la Mungu, lina nguvu ya kubadili maisha kuwa mazuri zaidi. Miongoni mwao mna watu kutoka kila taifa, lugha, na jamii. Wao pia hutoka kwa kila aina ya maisha na malezi ya kijamii. Mbeleni wengine wao walikuwa na maisha zenye jeuri na zenye usumbufu. Lakini badala ya kuacha mambo hayo kuchochea uhasama, upinzani, ubaguzi, na chuki kati yao, wao wamejifunza kushinda vizuizi hivyo nao wamekuwa wapenda amani wenye muungano ulimwenguni pote. Ni nini kimefanya jambo hili liwezekane?

Kampeni Imalizayo Jeuri

Mashahidi wa Yehova wamejitoa kusaidia wengine kupata ujuzi sahihi wa kusudi la Mungu kama lifunuliwavyo katika Neno lake, Biblia. Katika kila pembe ya dunia, wanatafuta wale wanaotaka kujifunza njia za Yehova na kufundishwa naye. Jitihada zao zinazaa matunda. Tokeo la hii kampeni ya kuelimisha ni kwamba unabii mzuri ajabu unatimizwa sasa.

Miaka ipatayo 2,700 iliyopita, nabii Isaya alipuliziwa kuandika: “Na itakuwa katika siku za mwisho . . . mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake.”—Isaya 2:2, 3.

Kufundishwa na Yehova na kutembea katika njia zake kwaweza kutokeza mabadiliko ya ajabu katika maisha za watu. Mojawapo mabadiliko hayo linatabiriwa katika unabii uo huo: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” (Isaya 2:4) Watu wengi wamesoma andiko hili. Hata limechorwa kwenye ukuta mmoja katika Jengo la Umoja wa Mataifa katika New York City. Hilo ni kikumbusho cha matamanio ya Umoja wa Mataifa ambayo limeshindwa kutimiza. Kuondolewa kabisa kwa vita na jeuri hakuwezi kutimizwa na tengenezo la kisiasa lililoanzishwa na mwanadamu. Hilo ni jambo ambalo ni Yehova Mungu pekee awezaye kutimiza. Atalitimizaje?

Bila shaka si kila mtu ataitikia mwaliko wa ‘kwenda juu mlimani kwa BWANA’ na ‘kufundishwa njia zake’ na ‘kwenda katika mapito yake’; wala si wote watakaokubali ‘kufua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu.’ Yehova atawafanyia nini watu kama hao? Hatafungua milele mlango wa fursa au kuwangoja wabadilike. Ili kuondoa jeuri, Yehova pia atawaondoa wale wanaodumu katika njia zao zenye jeuri.

Somo Muhimu

Kile alichofanya Mungu katika siku ya Noa hutupa somo lenye kuonya leo. Rekodi ya Biblia yaonyesha aina ya ulimwengu uliokuwapo wakati huo: “Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma [“jeuri,” NW].” Kwa sababu hiyo, Mungu alimwarifu Noa: “Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma [“jeuri,” NW], basi nitawaharibu pamoja na dunia.”—Mwanzo 6:11, 13.

Ni lazima tuone jambo moja muhimu. Alipoleta Gharika dhidi ya kizazi hicho, Mungu alimhifadhi Noa na familia yake. Kwa nini? Biblia yajibu: “Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu.” (Mwanzo 6:9; 7:1) Ingawa si lazima kwamba kila mtu aliyeishi wakati huo alikuwa mjeuri, ni Noa pekee na familia yake ‘waliokwenda pamoja na Mungu.’ Kwa sababu hiyo wao waliokoka ulimwengu huo wenye jeuri ulipoharibiwa.

Kadiri tuonavyo dunia ‘ikijaa jeuri’ tena, twaweza kuwa na hakika kwamba Mungu anaiona hali hiyo. Kama alivyofanya tu katika siku ya Noa, ndivyo atakavyochukua hatua ya kumaliza jeuri karibuni—kwa kudumu. Lakini pia ataandaa usalama kwa wale ambao sasa wanajifunza ‘kwenda pamoja na Mungu,’ wale wanaoitikia kampeni yake kubwa ya kielimu ya amani.

Kupitia mtunga-zaburi, Yehova atoa uhakikisho huu: “Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:10, 11.

Mashahidi wa Yehova watafurahi kujifunza Biblia pamoja na wewe ili uweze kujiunga na wale wasemao: “Twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake.” (Isaya 2:3) Kwa kufanya hivyo, unaweza kuwa miongoni mwa wale ambao wataona mwisho wa uovu wote na jeuri zote. Unaweza ‘kufurahia wingi wa amani.’

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 5]

Reuters/Bettmann

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki