Je, Mfungo Ni Jambo la Kale?
NIMEKUWA nikifunga kila Jumatatu tangu nilipokuwa tineja,” asema Mrudulaben, mwanamke Mhindi aliyefana mwenye umri wa miaka 78. Mfungo umekuwa sehemu ya ibada yake, njia ya kuhakikisha kwamba alikuwa na ndoa nzuri na watoto wenye afya, na vilevile ulinzi kwa ajili ya mumewe. Sasa akiwa mjane, yeye huendelea kufunga siku za Jumatatu kwa ajili ya afya njema, na kwa ajili ya ufanisi wa watoto wake. Sawa na yeye, wanawake Wahindu walio wengi hufanya mifungo ya ukawaida iwe sehemu ya maisha yao.
Prakash, mfanyabiashara wa makamo anayeishi katika kiunga cha Mumbai (Bombay), India, asema kwamba yeye hufunga kila mwaka kwenye Jumatatu za Sawan (Shravan). Huo ni mwezi wenye umaana wa pekee wa kidini kwenye kalenda ya Kihindu. Prakash aeleza hivi: “Nilianza kufunga kwa sababu za kidini, lakini sasa napata kichocheo cha ziada cha kuendelea kwa sababu za kiafya. Kwa kuwa Sawan huja kuelekea mwishoni mwa kuvuma kwa upepo wa monsuni, mfungo huupa mwili wangu fursa ya kuondolea mbali magonjwa ya kawaida ya msimu wa mvua.”
Watu fulani huhisi kwamba mfungo humsaidia mtu kimwili, kiakili, na kiroho. Mathalani, kitabu Grolier International Encyclopedia chataarifu hivi: “Uchunguzi wa juzijuzi wa kisayansi wadokeza kwamba mfungo waweza kuleta afya na, ufanywapo kwa uangalifu, waweza kuleta viwango vya juu vya kuwa macho kiakili na kuwa na maitikio ya kihisia.” Yasemekana kwamba mwanafalsafa Mgiriki Plato aliweza kufunga kwa siku kumi au zaidi na kwamba yule mwanahisabati Pythagoras aliwalazimisha wanafunzi wake wafunge kabla ya kuwafundisha.
Kwa watu fulani, mfungo humaanisha kuepuka chakula na maji kabisa kwa kipindi fulani cha wakati, hali wengine hunywa vinywaji wakati wa mifungo yao. Kukosa milo fulani au kujinyima aina fulani ya chakula kunaonwa na wengi kuwa ni mfungo. Lakini kufunga kwa muda mrefu bila uangalifu kwaweza kuwa hatari. Mwanajarida Parul Sheth asema kwamba baada ya mwili kutumia ugavi wao wa kabohidrati, huanza kubadili protini ya misuli iwe glukosi na kisha huugeukia ugavi wa mafuta ya mwili. Kubadili mafuta yawe glukosi hutokeza sumuvija ziitwazo magimba ya ketoni. Hayo yakusanyikapo, yanasonga kuelekea kwenye ubongo, na kuudhuru mfumo wa neva wa kati. “Huo ndio wakati ambapo mfungo waweza kuwa hatari,” asema Sheth. “Waweza kuchanganyikiwa, kuvurugika, na hata kuwa vibaya zaidi. . . . [waweza kusababisha] kupoteza fahamu na kifo hatimaye.”
Silaha na Desturi
Mfungo umetumiwa kuwa silaha yenye nguvu ya kutimiza makusudio ya kisiasa na kijamii. Mtumiaji maarufu wa silaha hiyo alikuwa Mohandas K. Gandhi katika India. Akiwa anastahiwa sana na mamia ya mamilioni ya watu, alitumia mfungo ili kutokeza uvutano wenye nguvu juu ya matungamano ya Wahindu wa India. Akifafanua matokeo ya mfungo wake ili kusuluhisha bishano kati ya wafanyakazi wa kiwanda na wenye kiwanda, Gandhi alisema hivi: “Tokeo la jumla la mfungo lilikuwa kwamba watu wote waliohusika walikuwa na hali ya nia njema. Mioyo ya wenye kiwanda iliguswa . . . Mgomo ukakomeshwa baada ya mimi kufunga kwa siku tatu tu.” Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alishiriki katika mgomo wa siku tano wa kutokula wakati wa miaka yake akiwa mfungwa wa kisiasa.
Hata hivyo, walio wengi wa wale ambao wamezoea kufunga, wamefanya hivyo kwa sababu za kidini. Mfungo ni desturi maarufu katika Dini ya Hindu. Siku fulani-fulani, chasema kitabu Fast and Festivals of India, “watu hufunga kabisa . . . hata maji hayanywewi hata kidogo. Wanaume na pia wanawake hufunga kabisa-kabisa . . . ili kuhakikisha kuna furaha, ufanisi na msamaha wa ukiukaji-sheria na dhambi.”
Katika dini ya Jain wengi hufunga. Jarida The Sunday Times of India Review laripoti hivi: “Muni [mwenye hekima] wa Jain katika Bombay [Mumbai] alikunywa gilasi mbili tu za maji yaliyochemshwa kila siku—kwa siku 201. Alipoteza uzito wa kilo 33 [pauni 73].” Wengine hata hufunga kufikia kiwango cha kufa njaa, wakiwa na usadikisho wa kwamba hilo litatokeza wokovu.
Kwa watu wazima Waislamu kwa ujumla, mfungo ni lazima wakati wa mwezi wa Ramadhani. Hakuna chakula wala maji yapaswayo kunywewa kuanzia macheo hadi machweo kwa huo mwezi mzima. Yeyote aliye mgonjwa au aliye safarini wakati huo lazima alipie siku za mfungo. Kwaresima, kile kipindi cha siku 40 kinachotangulia Ista, ni wakati wa mfungo kwa watu fulani katika Jumuiya ya Wakristo, na vikundi vingi vya kidini hufunga kwenye siku nyingine hususa.
Bila shaka mfungo haujatoweka. Na kwa kuwa ni sehemu ya dini nyingi, twaweza kuuliza hivi, Je, Mungu hutaka mfungo? Je, kuna nyakati ambapo Wakristo waweza kuamua kufunga? Je, kufanya hivyo kwaweza kunufaisha? Makala ifuatayo itazungumzia maswali hayo.
Picha katika ukurasa wa 3]
Dini ya Jain huona mfungo kuwa njia ya kupata wokovu wa nafsi
[Picha katika ukurasa wa 4]
Mohandas K. Gandhi alitumia mfungo kuwa silaha yenye nguvu ya kutimiza makusudio ya kisiasa na kijamii
[Picha katika ukurasa wa 4]
Katika Uislamu, mfungo ni lazima wakati wa mwezi wa Ramadhani
[Hisani]
Garo Nalbandian