“Ingawa Hamkumwona Yeye Kamwe, Mwampenda”
“Ingawa hamkumwona yeye kamwe, mwampenda. Ingawa hamwi mkimtazama wakati wa sasa, bado mwadhihirisha imani katika yeye na mnashangilia sana.”—1 PETRO 1:8.
1. Ingawa hakuna yeyote duniani leo ambaye amemwona Yesu, watu fulani wa kidini wanajitahidije kuonyesha ujitoaji kwake?
HAKUNA yeyote aliye hai duniani leo ambaye amepata kumwona Yesu Kristo. Hata hivyo, mamilioni ya watu hudai wanampenda. Kila mwaka Januari 9, katika Manila, Filipino, sanamu yenye ukubwa wa mtu ya Yesu Kristo akibeba msalaba hukokotwa kwenye barabara katika ule ambao umefafanuliwa kuwa udhihirisho mkubwa zaidi na wenye kutokeza zaidi wa dini maarufu katika hiyo nchi. Umati wa watu waliosisimuka husukumana; watu hata hupandana katika jitihada zenye kichaa za kuigusa sanamu. Wengi waliopo ili kuona hilo hasa huvutiwa na maandamano ya kisikukuu. Hata hivyo, baadhi yao bila shaka ni watu wanaohisi wamevutiwa kwa Yesu kwa moyo mweupe. Ukiwa uthibitisho wa hilo, huenda wakavaa kisalaba au waweza kwenda kanisani kwa ukawaida. Hata hivyo, je, ibada ya sanamu kama hiyo yaweza kuonwa kuwa ibada ya kweli?
2, 3. (a) Ni nani miongoni mwa wafuasi wa Yesu waliomwona na kumsikia kihalisi? (b) Ni nani wengine katika karne ya kwanza waliompenda Yesu na kuweka imani kwake, ingawa hawakumwona kibinafsi kamwe?
2 Katika karne ya kwanza, kulikuwa na maelfu mengi ya watu katika mikoa ya Kiroma ya Yudea, Samaria, Perea, na Galilaya ambao wao binafsi walimwona na kumsikia Yesu Kristo. Walisikiliza alipokuwa akifafanua kweli juu ya Ufalme wa Mungu. Walijionea kwa macho miujiza aliyofanya. Baadhi yao wakawa wanafunzi wake wenye ujitoaji, waliosadikishwa kwamba alikuwa “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” (Mathayo 16:16) Hata hivyo, wale ambao Mtume Petro aliandikia barua yake ya kwanza yenye kupuliziwa hawakuwa wamekuwa miongoni mwao.
3 Walioandikiwa na Petro walikuwa katika mikoa ya Kiroma ya Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia, na Bithinia—yote iliyo katika eneo la Uturuki ya siku ya kisasa. Petro aliwaandikia hivi: “Ingawa hamkumwona yeye kamwe, mwampenda. Ingawa hamwi mkimtazama wakati wa sasa, bado mwadhihirisha imani katika yeye na mnashangilia sana kwa shangwe isiyosemeka na iliyotukuzwa.” (1 Petro 1:1, 8) Wao walikuwa wamekuja kumjuaje Yesu Kristo kufikia hatua ya kumpenda na kudhihirisha imani kwake?
4, 5. Watu ambao hawakuwa wamemwona Yesu kamwe walijifunzaje mambo ya kutosha juu yake waweze kumpenda na kuweka imani kwake?
4 Kwa wazi, baadhi yao walikuwa Yerusalemu mtume Petro alipotolea ushahidi umati wa watu waliokuwa wakihudhuria sikukuu ya Pentekoste katika 33 W.K. Baada ya sikukuu hiyo wanafunzi wengi walikaa Yerusalemu ili wapokee maagizo zaidi kutoka kwa mitume. (Matendo 2:9, 41, 42; linganisha 1 Petro 1:1.) Kwenye safari za umishonari za kurudia-rudia, mtume Paulo aliendeleza huduma yenye bidii miongoni pia mwa watu walioishi katika eneo ambalo baadaye Petro alilitumia barua ya kwanza ya Kibiblia yenye jina lake.—Matendo 18:23; 19:10; Wagalatia 1:1, 2.
5 Kwa nini watu hao, ambao hawakumwona Yesu kamwe, walivutiwa kwa nguvu hivyo kwake? Katika siku yetu, kwa nini mamilioni zaidi ya watu, tufeni pote, wanampenda sana?
Mambo Waliyosikia
6. (a) Ikiwa ungalimsikia Petro akitoa ushahidi juu ya Yesu kwenye Pentekoste 33 W.K., ungaliweza kujifunza nini? (b) Hilo liliwaathirije watu wapatao 3,000 waliokuwapo?
6 Ikiwa ungalikuwa Yerusalemu, Petro alipozungumzia umati wa sikukuu katika 33 W.K., ungalijifunza nini juu ya Yesu? Bila shaka yoyote miujiza aliyofanya ilionyesha kwamba alitumwa na Mungu. Kwamba, ingawa watu wenye dhambi walikuwa wamemwua Yesu, hakuendelea kuwa kaburini bali alikuwa amefufuliwa kisha akakwezwa hadi mbinguni kwenye mkono wa kuume wa Mungu. Kwamba kwelikweli Yesu alikuwa Kristo, yule Mesiya ambaye manabii walikuwa wameandika kumhusu. Kwamba kupitia Yesu Kristo, roho takatifu ilikuwa imemwagwa juu ya wafuasi wake hivi kwamba upesi waliweza kutolea watu kutoka mataifa mengi ushahidi juu ya mambo matukufu ambayo Mungu alikuwa akifanya kupitia Mwana wake. Mioyo ya wengi waliomsikia Petro kwenye pindi hiyo ilichochewa sana, na watu wapatao 3,000 wakabatizwa na kuwa wanafunzi Wakristo. (Matendo 2:14-42) Ikiwa ungalikuwako huko, je, ungalichukua hatua hiyo ya kukata maneno?
7. (a) Ikiwa ungalikuwa Antiokia mtume Paulo alipohubiri huko, ungaliweza kujifunza nini? (b) Kwa nini baadhi ya watu katika umati walipata kuwa waamini na kushiriki habari njema na wengine?
7 Ikiwa ungalikuwa miongoni mwa waliokuwapo mtume Paulo alipofundisha katika Antiokia katika mkoa wa Kiroma wa Galatia, ungaliweza kujifunza nini kingine juu ya Yesu? Ungalimsikia Paulo akieleza kwamba kumhukumia kifo Yesu kwa watawala katika Yerusalemu kulikuwa kumetabiriwa na manabii. Pia ungalisikia juu ya uthibitisho wa waliojionea kwa macho ufufuo wa Yesu. Bila shaka ungalivutiwa na ufafanuzi wa Paulo kwamba kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu, Yehova alihakikisha kwamba huyo kwelikweli alikuwa Mwana wa Mungu. Na je, moyo wako usingalichangamshwa huku ulipojifunza kwamba msamaha wa dhambi uliowezeshwa na imani katika Yesu ungeweza kuongoza kwenye uhai udumuo milele? (Matendo 13:16-41, 46, 47; Waroma 1:4) Wakitambua umaana wa yale waliyokuwa wakisikia, baadhi ya watu katika Antiokia wakawa wanafunzi, wakishiriki kwa bidii habari njema pamoja na wengine, hata ingawa kufanya hivyo kulimaanisha kwamba wangekabili mnyanyaso mwingi.—Matendo 13:42, 43, 48-52; 14:1-7, 21-23.
8. Ikiwa ungalikuwa kwenye mkutano wa kutaniko la Efeso barua kutoka kwa Paulo ilipopokewa, ungalijifunza nini?
8 Vipi ikiwa ungalikuwa ukishirikiana na kutaniko la Kikristo katika Efeso, katika mkoa wa Kiroma wa Asia, barua iliyopuliziwa ya Paulo kwa wanafunzi ilipopokewa? Ungaliweza kujifunza nini kutokana nayo juu ya fungu la Yesu katika kusudi la Mungu? Katika barua hiyo Paulo alieleza kwamba kupitia Kristo mambo yote mbinguni na duniani yangepatanishwa pamoja na Mungu tena, kwamba zawadi itokayo kwa Mungu kupitia Kristo ilifikia watu wa mataifa yote, kwamba watu mmoja-mmoja waliokuwa wamekuwa wafu machoni pa Mungu kwa sababu ya makosa yao walikuwa wakihuishwa kupitia imani katika Kristo, na kwamba tokeo la uandalizi huo ni kwamba, ingewezekana tena wanadamu wawe wana wapendwa wa Mungu.—Waefeso 1:1, 5-10; 2:4, 5, 11-13.
9. (a) Ni nini kiwezacho kukusaidia ufahamu ikiwa wewe binafsi waelewa umaana wa yale ambayo Paulo aliwaandikia Waefeso? (b) Ndugu katika mikoa ya Kiroma waliotajwa na Petro waliathiriwaje na yale waliyokuwa wakijifunza juu ya Yesu?
9 Je, uthamini wa yote hayo ungaliongeza kina cha upendo wako kwa Mwana wa Mungu? Je, upendo huo ungalikuwa na uvutano juu ya maisha yako ya kila siku, kama mtume Paulo alivyotia moyo katika sura ya 4 hadi ya 6 ya Waefeso? Je, uthamini huo ungalikusukuma uchunguze kwa uangalifu mambo yako mwenyewe ya kutangulizwa maishani? Kutokana na upendo kwa Mungu na shukrani kwa Mwana wake, je, ungalifanya marekebisho yaliyohitajiwa hivi kwamba kufanya mapenzi ya Mungu kulikuwa kwa kweli jambo kuu maishani mwako? (Waefeso 5:15-17) Kwa habari ya jinsi Wakristo katika Asia, Galatia, na mikoa mingine ya Kiroma walivyoathiriwa na mambo waliyokuwa wakijifunza, mtume Petro aliwaandikia hivi: “Ingawa hamkumwona [Yesu Kristo] kamwe, mwampenda. . . . Mwadhihirisha imani katika yeye na mnashangilia sana kwa shangwe isiyosemeka na iliyotukuzwa.”—1 Petro 1:8.
10. (a) Ni nini ambacho bila shaka kilichangia kumpenda Yesu kwa Wakristo wa mapema? (b) Twaweza kunufaikaje pia?
10 Kuna jambo jingine ambalo bila shaka lilichangia ule upendo wa Mwana wa Mungu uliohisiwa na wale Wakristo wa mapema ambao Petro aliwaandikia. Hilo lilikuwa nini? Kufikia wakati ambapo Petro aliandika barua yake ya kwanza, angalau Gospeli mbili—Mathayo na Luka—tayari zilikuwa zikienezwa. Wakristo wa karne ya kwanza ambao hawakuwa wamemwona Yesu kamwe wangeweza kusoma masimulizi hayo ya Gospeli. Sisi pia twaweza. Hizo Gospeli si masimulizi ya kuwaziwa tu; zina sifa zote za historia yenye kutegemeka zaidi sana. Katika rekodi hizo zilizopuliziwa, twapata mengi ambayo huongeza kina cha upendo wetu kwa Mwana wa Mungu.
Roho Aliyoonyesha
11, 12. Ni nini kuhusu roho aliyoonyesha Yesu kwa wanadamu wengine ambacho hukufanya umpende?
11 Humo katika rekodi iliyoandikwa ya maisha ya Yesu, twajifunza jinsi alivyoshughulika na wanadamu wengine. Roho aliyoonyesha hugusa mioyo ya watu hata leo, miaka zaidi ya 1,960 baada ya kufa kwake. Kila mtu aliye hai analemewa na mzigo wa matokeo ya dhambi. Mamilioni mengi ya watu ni wahasiriwa wa ukosefu wa haki, wanang’ang’ana na magonjwa, au wanahisi kutamauka kwenye kulemea kwa sababu nyingine. Kwa wote hao, Yesu asema hivi: “Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaomenyeka na kulemezwa mizigo, nami hakika nitawaburudisha nyinyi. Chukueni nira yangu juu yenu na mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mwenye tabia-pole na wa hali ya chini moyoni, nanyi mtapata burudisho kwa ajili ya nafsi zenu. Kwa maana nira yangu ni ya fadhili na mzigo wangu ni mwepesi.”—Mathayo 11:28-30.
12 Yesu alionyesha hangaiko lenye hisia nyepesi kwa maskini, wenye njaa, na waliokuwa na majonzi. Hali zilipolazimu, hata alilisha kimuujiza umati mkubwa sana. (Luka 9:12-17) Aliwaweka huru kutoka katika mapokeo yenye kutumikisha. Pia alitia nguvu imani yao katika uandalizi wa Mungu wa kukomesha uonevu wa kisiasa na kiuchumi. Yesu hakuponda roho ya wale ambao tayari walidharauliwa. Aliwainua wasikivu kwa ustadi, akiwa na wororo na upendo. Aliburudisha waliokuwa kama tete lililochubuliwa ambalo limekunjika na wale waliokuwa kama utambi wa kitani-ghafi unaofuka moshi uliokaribia kuzimika. Kufikia wakati wa sasa, jina lake hupulizia tumaini, hata mioyoni mwa wale ambao hawajapata kamwe kumwona.—Mathayo 12:15-21; 15:3-10.
13. Kwa nini njia ambayo Yesu alishughulikia watenda-dhambi huvutia watu?
13 Yesu hakukubali ukosaji, hata hivyo alionyesha uelewevu kuelekea watu waliokuwa wamefanya makosa maishani lakini walioonyesha toba na kumgeukia ili wapate msaada. (Luka 7:36-50) Alikuwa akiketi na kula mlo na watu waliokuwa wamedharauliwa katika jumuiya alipohisi kwamba hilo lingeandaa fursa ya kuwasaidia kiroho. (Mathayo 9:9-13) Tokeo la roho aliyoonyesha ni kwamba, mamilioni ya watu walio katika hali kama hizo ambao hawajapata kamwe kumwona Yesu wamechochewa kupata kumjua na wameweka imani kwake.
14. Ni nini kinachokuvutia juu ya jinsi Yesu alivyowasaidia watu waliokuwa wagonjwa, wasiojiweza, au waliofiwa?
14 Jinsi ambavyo Yesu alishughulika na watu waliokuwa wagonjwa au wasiojiweza hutoa uthibitisho wa uchangamfu wake na huruma yake na pia uwezo wake wa kuwaletea kitulizo. Hivyo, mwanamume mwenye maradhi aliyejawa na ukoma alipomfikia na kuomba msaada, Yesu hakurudi nyuma alipomwona. Naye hakumwambia mtu huyo kwamba, ingawa alimsikitikia, hali yake ilikuwa mbaya sana na hakuna lolote lililoweza kufanywa ili kumsaidia. Mwanamume huyo aliomba sana hivi: “Bwana, ikiwa tu wewe wataka, waweza kunifanya safi.” Bila kukawia, Yesu alinyoosha mkono na kumgusa yule mwanamume mwenye ukoma, akisema hivi: “Mimi nataka. Fanywa safi.” (Mathayo 8:2, 3) Kwenye pindi nyingine mwanamke alijaribu kupata ponyo kwa kugusa kisiri matamvua ya vazi lake. Yesu alishughulika naye kwa njia ya fadhili na yenye kutumainisha. (Luka 8:43-48) Na alipokutana na andamano la mazishi, alisukumwa na sikitiko kwa ajili ya mjane mwenye kihoro ambaye mwana wake pekee alikuwa amekufa. Ingawa Yesu alikuwa amekataa kutumia kimuujiza nguvu alizokuwa amepewa na Mungu ili kujiandalia chakula, alizitumia kwa hiari kumfufua mwanamume huyo mfu na kumrudishia mamaye.—Luka 4:2-4; 7:11-16.
15. Kusoma na kutafakari masimulizi juu ya Yesu hukuathirije?
15 Tusomapo masimulizi hayo na kutafakari juu ya ile roho aliyoonyesha Yesu, kina cha upendo wetu kinaongezeka kwa ajili ya huyo mmoja aliyetoa uhai wake ili tuweze kuishi milele. Ingawa hatujapata kumwona yeye kamwe, twahisi tukivutwa kwake, nasi twataka kufuata hatua zake za miguu.—1 Petro 2:21.
Kutegemea Kwake Mungu kwa Unyenyekevu
16. Yesu alikazia nani uangalifu wa kwanza, naye alitutia moyo tufanye nini?
16 Zaidi ya mengine yote, Yesu alikazia uangalifu wake na wetu kwa Baba yake wa kimbingu, Yehova Mungu. Alitambulisha amri iliyo kubwa zaidi sana katika ile Sheria, kwa kusema hivi: “Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote.” (Mathayo 22:36, 37) Aliwaonya kwa upole wanafunzi wake hivi: “Iweni na imani katika Mungu.” (Marko 11:22) Walipokabili mtihani mzito wa imani yao, aliwasihi sana hivi: ‘Salini kwa kuendelea.’—Mathayo 26:41.
17, 18. (a) Yesu alionyeshaje kumtegemea kwake Baba yake kwa unyenyekevu? (b) Kwa nini lile alilofanya ni la maana sana kwetu?
17 Yesu mwenyewe aliweka kielelezo. Sala ilikuwa sehemu ya maana ya maisha yake. (Mathayo 14:23; Luka 9:28; 18:1) Wakati ulipowadia wa kuwateua mitume wake, Yesu hakutegemea maoni yake tu, ingawa hapo zamani malaika wote mbinguni walikuwa chini ya uangalizi wake. Alitumia kwa unyenyekevu usiku mzima akisali kwa Baba yake. (Luka 6:12, 13) Alipokabili kukamatwa na kifo chenye umivu, kwa mara nyingine Yesu alimgeukia Baba yake, akisali kwa bidii. Hakuwa na maoni ya kwamba alimjua Shetani vema na angeweza kushughulikia kwa urahisi lolote ambalo mwovu huyo angebuni. Yesu alitambua umaana wa kutoshindwa kwake. Kushindwa kwa Yesu kungekuwa suto kama nini kwa Baba yake! Na kungekuwa hasara kama nini kwa jamii ya kibinadamu, ambayo matazamio yayo ya uhai yalitegemea dhabihu ambayo Yesu alipaswa kutoa!
18 Yesu alisali kwa kurudia-rudia—alipokuwa na mitume wake katika chumba cha juu katika Yerusalemu na hata kwa bidii zaidi katika bustani ya Gethsemane. (Mathayo 26:36-44; Yohana 17:1-26; Waebrania 5:7) Alipokuwa akiteseka kwenye mti wa mateso, hakuwatukana waliokuwa wakimdhihaki vikali. Badala ya hivyo, alisali kwa niaba ya wale waliokuwa wakitenda kwa kutojua: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui wanalofanya.” (Luka 23:34) Aliendelea kukazia akili yake Baba yake, ‘akijikabidhi mwenyewe kwa yeye ambaye huhukumu kwa uadilifu.’ Maneno ya mwisho aliyosema kwenye mti wa mateso yalikuwa sala kwa Baba yake. (1 Petro 2:23; Luka 23:46) Sisi tu wenye shukrani kama nini kwamba, kwa kumtegemea Yehova kabisa, Yesu alimaliza kwa uaminifu mgawo aliokabidhiwa na Baba yake! Ingawa hatukumwona Yesu Kristo kamwe, jinsi tunavyompenda kwa kina kwa sababu ya yale aliyofanya!
Kuonyesha Upendo Wetu Kwake
19. Katika kuonyesha upendo kwa Yesu, ni mazoea yapi ambayo tungeepuka kwa kuwa ni yasiyofaa kabisa?
19 Twaweza kutoaje uthibitisho wa kwamba upendo tunaodai kuwa nao si maneno matupu tu? Kwa kuwa Baba yake, ambaye Yesu alimpenda, alikataza kufanyizwa kwa mifano kisha kuitendea ikiwa vitu vyenye kustahili ujitoaji, bila shaka hatungemletea Yesu heshima kwa kuvaa shingoni mfano kama huo au kwa kubeba mfano kama huo barabarani. (Kutoka 20:4, 5; Yohana 4:24) Isingekuwa heshima yoyote kwa Yesu ikiwa sisi tungehudhuria ibada za kidini, hata tukifanya hivyo mara kadhaa kwa juma, ikiwa hatungeishi kwa kupatana na mafundisho yake siku zinazosalia za juma. Yesu alisema hivi: “Yeye aliye na amri zangu na kuzishika, huyo ndiye ambaye hunipenda. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu.”—Yohana 14:21, 23; 15:10.
20. Ni yapi baadhi ya mambo yatakayoonyesha ikiwa kwa kweli twampenda Yesu?
20 Alitupa amri zipi? Kwanza kabisa, tumwabudu Mungu wa kweli, Yehova, yeye peke yake. (Mathayo 4:10; Yohana 17:3) Kwa sababu ya fungu lake katika kusudi la Mungu, Yesu alifundisha pia kwamba lazima tudhihirishe imani kwake akiwa Mwana wa Mungu na kwamba lazima tuonyeshe hilo kwa kuepuka kazi za uovu na kwa kutembea katika nuru. (Yohana 3:16-21) Alitushauri tutafute kwanza Ufalme wa Mungu na uadilifu wake, tukitanguliza mambo hayo mbele ya mahitaji ya kimwili. (Mathayo 6:31-33) Aliamuru kwamba tupendane kama alivyotupenda. (Yohana 13:34; 1 Petro 1:22) Naye alitupa utume wa kuwa mashahidi kuhusu kusudi la Mungu, kama alivyokuwa. (Mathayo 24:14; 28:19, 20; Ufunuo 3:14) Ingawa hawakumwona Yesu kamwe, leo Mashahidi wa Yehova wapatao milioni tano wanasukumwa na upendo wa kweli kwake kutii amri hizo. Kutomwona kwao Yesu kibinafsi hakudhoofishi kwa njia yoyote azimio lao la kuwa watiifu. Wanakumbuka yale ambayo Bwana wao alimwambia mtume Tomasi: “Kwa sababu umeniona mimi je, umeamini? Wenye furaha ni wale ambao hawaoni na bado waamini.”—Yohana 20:29.
21. Tutanufaikaje kwa kuhudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo, utakaofanywa mwaka huu Jumapili, Machi 23?
21 Yatumainiwa kwamba utakuwa miongoni mwa wale ulimwenguni pote watakaokusanyika kwenye Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova Jumapili, Machi 23, 1997, baada ya machweo, ili kukumbuka wonyesho mkubwa zaidi sana wa upendo wa Mungu kwa wanadamu na kukumbuka kifo cha Mwana wake mwaminifu-mshikamanifu, Yesu Kristo. Yasemwayo na kufanywa kwenye pindi hiyo yapaswa kuongeza kina cha upendo kwa Yehova na Mwanaye na hivyo yakuze tamaa ya kushika amri za Mungu.—1 Yohana 5:3.
Ungejibuje?
◻ Walioandikiwa kitabu cha kwanza cha Petro walikujaje kumjua na kumpenda Yesu?
◻ Ni yapi baadhi ya mambo waliyosikia Wakristo wa mapema yanayokuvutia?
◻ Ni nini kuhusu roho aliyoonyesha Yesu ambacho huongeza kina cha upendo wako kwake?
◻ Kwa nini kumtegemea Mungu kwa unyenyekevu kwa Yesu ni kwa maana sana kwetu?
◻ Twaweza kuonyeshaje upendo wetu kwa Yesu Kristo?
[Picha katika ukurasa wa 16]
Twahisi tukivutwa kwa Yesu kwa sababu ya roho aliyoonyesha