Kuteseka Kwingi Mno
“KWA sababu gani kuna kuteseka kote huku kwa watu mmoja-mmoja na kwa watu wote pamoja . . . ? Mungu apaswa kuwa udhihirisho halisi wa kusudi la uhai na bado kuna mengi mno yasiyo na maana katika ulimwengu huu, kuteseka kwingi mno kusiko na kusudi na dhambi zisizo na maana. Je, yawezekana kwamba Mungu yu jinsi Nietzsche alivyomshtaki kuwa: mwenye kupiga ubwana, mlaghai, mpunjaji, mfishaji?”—Kitabu On Being a Christian, kilichoandikwa na Hans Küng.
Waweza kuona kwamba Hans Küng mwanatheolojia Mkatoliki anatokeza tu tatizo linalowatatanisha wengi—kwa nini Mungu mwenye nguvu zote, mwenye upendo anaruhusu kuteseka kwingi mno? Je, hujawasikia watu wakiuliza swali kama hilo? Yeyote aliye na huruma hupatwa na kihoro kwa sababu ya yale ambayo Küng afafanua kuwa “mkondo usio na mwisho wa damu, wa jasho na machozi, wa umivu, wa sikitiko na hofu, wa upweke na kifo.” Kwa hakika, ni kama bubujiko, furiko la ogofyo na maumivu makali ambalo limeathiri vibaya maisha ya mamilioni ya watu katika historia yote.—Ayubu 14:1.
Imejawa na “Taabu na Ubatili”
Fikiria kuteseka kunakotokana na vita, umivu linalohisiwa si na wahasiriwa tu bali pia na walioachwa wakiwa na kihoro, kama vile wazazi na watu wa ukoo wa watoto wahasiriwa na wengine ambao wametendwa kinyama. “Kwa miaka 10 iliyopita,” likasema shirika la Msalaba Mwekundu majuzi, “watoto milioni 1.5 waliuawa katika mapambano ya kijeshi.” Huko Rwanda katika 1994, shirika la Msalaba Mwekundu laripoti, “mamia ya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto walikuwa wamechinjwa kinyama na kikamili.”
Pia tusipuuze umivu linalosababishwa na wapotovu wa kuwatumia vibaya watoto kingono. Mama mmoja mwenye kihoro, aliyesema kwamba mwana wake alijiua baada ya kutendwa vibaya na mfanyakazi wa kutunza watoto, alitaarifu hivi: “Mwanamume aliyemtumia vibaya mwana wangu . . . alimharibu yeye na idadi fulani ya wavulana wengine katika njia kamili zaidi, iliyopotoka zaidi iwezayo kuwaziwa.” Na vipi juu ya lile jinamizi la umivu linalohisiwa na wahasiriwa wa wauaji kimakusudi au wauaji wa mfululizo walio sugu, kama wale waliokamatwa Uingereza ambao “waliteka nyara watu, walibaka, walitesa na kuua kwa miaka 25 bila hofu ya kuadhibiwa”? Katika historia yote yaonekana hakujawa na mipaka ya yale ambayo wanaume na wanawake wametendeana katika njia ya umivu na kuteseka.—Mhubiri 4:1-3.
Kwa kuongezea kuna kule kuteseka kunakosababishwa na magonjwa ya kihisia-moyo na ya kimwili na lile umivu kali mno la kihoro linalokumba familia, wapendwa wanapokufa mapema maishani. Pia kuna maumivu makali yanayohisiwa na wahasiriwa wa njaa kuu au ile misiba mingine iitwayo kwa kawaida misiba asilia. Ni wachache watakaobisha taarifa ya Musa ya kwamba miaka yetu 70 au 80 imejawa na “taabu na ubatili.”—Zaburi 90:10.
Sehemu ya Ubuni wa Mungu?
Je, yawezekana, kama vile wengine wamedai, kwamba kuteseka huku kusikokoma ni sehemu ya ubuni wa Mungu usioweza kufahamika? Je, ni lazima tuteseke sasa ili tuthamini uhai ‘katika ulimwengu unaofuata’? Je, ni kweli kama vile mwanafalsafa Mfaransa Teilhard de Chardin alivyoamini, kwamba “kuteseka kunakoua na kuvunjavunja, ni kwa lazima kwa binadamu ili aishi na kuwa roho”? (The Religion of Teilhard de Chardin; italiki ni zetu.) Bila shaka la!
Je, mbuni mwenye ufikirio angeumba kimakusudi mazingira yenye kufisha kisha adai kuwa mwenye huruma alipowaokoa watu kutoka kwa matokeo yayo? La hasha! Kwa nini Mungu mwenye upendo afanye jambo kama hilo? Kwa hiyo, kwa nini Mungu anaruhusu kuteseka? Je, kuteseka kutapata kwisha? Makala ifuatayo itazungumzia maswali haya.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya WHO iliyopigwa na P. Almasy