Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 6/15 kur. 3-5
  • Je, Sayari Dunia Itaangamizwa Kabisa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Sayari Dunia Itaangamizwa Kabisa?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ufafanuzi Ulio Wazi wa “Siku ya Maangamizi”
  • Usimamizi Mbaya wa Mwanadamu Warekebishwa
  • Inawezekana
  • Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?
    Amkeni!—1999
  • Mto Thames—Urithi wa Pekee wa Uingereza
    Amkeni!—2006
  • Je, Wanadamu Wataiharibu Dunia Kabisa?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Mungu Anaahidi Kwamba Dunia Yetu Itaokoka
    Amkeni!—2023
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 6/15 kur. 3-5

Je, Sayari Dunia Itaangamizwa Kabisa?

MWISHO wa karne ya 20 unakaribia, na karne ya 21 iko karibu kuanza. Katika hali hiyo, idadi inayoongezeka ya watu ambao kwa kawaida wangekazia uangalifu mdogo au kutokazia uangalifu wowote unabii mbalimbali wa maangamizo wanajiuliza kama tukio fulani lenye umaana wa kutikisa ulimwengu laweza kutokea karibuni.

Huenda ukawa umeona makala za magazeti juu ya jambo hilo—hata vitabu vizima ambavyo vimezungumzia habari hiyo. Kuhusu ujuzi wa yale yatakayotokea mwanzoni mwa karne ya 21, ni lazima tungoje tuone. Watu fulani husema kwamba kuufikia mwisho wa mwaka wa 2000 hutokeza tofauti ya mwaka mmoja tu (au dakika moja, kutoka mwaka wa 2000 hadi mwaka wa 2001) na yaelekea hautakuwa na matokeo makubwa. Jambo linalohangaisha zaidi watu wengi ni wakati ujao wa sayari yetu ulio mbali.

Unabii mmoja ambao siku hizi hukaziwa mara nyingi wasema kwamba kwenye pindi fulani—iwe ni katika wakati ujao wa karibu au wakati ujao ulio mbali—Dunia sayari yenyewe inakusudiwa kuangamizwa kabisa. Fikiria matabiri machache kama hayo yenye kuhuzunisha.

Katika kitabu chake The End of the World—The Science and Ethics of Human Extinction, kilichochapishwa mara ya kwanza mwaka wa 1996, mwandishi na mwana-falsafa, John Leslie, atoa njia tatu ambazo huenda uhai wa mwanadamu duniani ukaisha. Kwanza, yeye auliza hivi: “Je, vita ya nyuklia yenye kuenea pote ingeweza kumaanisha mwisho wa jamii ya kibinadamu?” Kisha aongeza kusema hivi: “Hali ambayo yawezekana zaidi kuwako . . . ingekuwa kutoweka kabisa kwa uhai kwa sababu ya matokeo ya mnururisho: kansa, kudhoofika kwa mfumo wa kinga hivi kwamba maradhi yenye kuambukiza yaenea pote, au kasoro nyingi za wakati wa kuzaliwa. Kungeweza pia kuwa na vifo vya vijiumbe muhimu kwa hali nzuri ya mazingira.” Uwezekano wa tatu ambao Bw. Leslie atokeza ni kwamba dunia yaweza kugongwa na nyotamkia au sayari ndogo: “Kwa habari ya hizo nyotamkia na sayari ndogo ambazo mizingo yake ni ya kiasi cha kwamba siku moja huenda zikagonga Dunia, yaonekana kunazo zipatazo elfu mbili, zikiwa na kipenyo cha kati ya kilometa moja hadi kilometa kumi. Pia bado kuna idadi ndogo zaidi (kukadiria kungekuwa jambo la kukisia tu) ya nyokamkia kubwa zaidi, na idadi kubwa zaidi ya nyingine ndogo zaidi.”

Ufafanuzi Ulio Wazi wa “Siku ya Maangamizi”

Au fikiria mwanasayansi mwingine, Paul Davies, profesa katika Chuo Kikuu cha Adelaide, Australia. Alifafanuliwa na gazeti la Washington Times kuwa “mwandikaji wa sayansi wa kimataifa aliye bora zaidi.” Katika mwaka wa 1994 aliandika kitabu The Last Three Minutes, ambacho kimeitwa “kielelezo asili cha vitabu vyote vya siku ya maangamizi.” Sura ya kwanza ya kitabu hicho inaitwa “Siku ya Maangamizi,” nayo yafafanua mpangilio wa kuwaziwa wa yale yawezayo kutukia kama nyotamkia ingegonga sayari Dunia. Soma sehemu ya ufafanuzi wake wenye kutia hofu sana:

“Sayari yatetemeka kwa nguvu sawa na mitetemeko ya dunia elfu kumi. Wimbi lenye kishindo la hewa iliyoondolewa mahali pake lapita kwa kasi juu ya uso wa tufe, likiharibu majengo yote, likiponda tikitiki kila kitu njiani mwake. Eneo lililo tambarare kuzunguka sehemu iliyogongwa lainuka kufanyiza milima ya mawe yaliyoyeyuka, yenye urefu wa kilometa kadhaa, kufanyizwa kwa hiyo kukitokeza kreta yenye upana wa kilometa 150 ambayo yaacha wazi sehemu za ndani za Dunia. . . . Safu kubwa mno ya mabaki ya mawe yatandaza katika angahewa, ikifunika jua kabisa lisionekane katika sayari yote. Sasa mahali pa nuru ya jua panachukuliwa na ule mng’ao mkali wenye kumetameta na wenye kuleta maafa ya mabilioni ya nyota zipitazo kwa kasi angani, ukichoma ardhi iliyo chini kwa joto lake lenye kuunguza, huku vitu vilivyoondolewa mahali pake vikianguka tena kwenye angahewa.”

Profesa Davies aendelea kuhusianisha mpangilio huo wa kuwaziwa na ule utabiri kwamba nyotamkia iitwayo Swift-Tuttle ingegonga dunia. Yeye aongeza kuonya kwamba, ingawa tukio kama hilo huenda lisitukie katika wakati ujao ulio karibu, katika maoni yake “karibuni au baadaye, Swift-Tuttle, au kitu kingine chenye kufanana nayo, kitaigonga Dunia.” Mkataa wake wategemea makadirio yadokezayo kwamba, vitu 10,000 vyenye kipenyo cha nusu kilometa au zaidi huzunguka Dunia katika mizingo yenye kupitana.

Je, unaamini kwamba matazamio kama hayo yenye kuogofya ni halisi? Idadi yenye kushangaza ya watu yaamini hivyo. Lakini wao hupuuza hangaiko lolote kwa kujipa moyo kwamba jambo hilo halitatukia katika wakati wao. Ingawa hivyo, kwa nini sayari Dunia iharibiwe—ama karibuni ama mileani nyingi kutoka sasa? Bila shaka, dunia yenyewe siyo chanzo kikuu cha taabu ipatayo wakazi wake, wawe binadamu au wanyama. Kinyume cha hilo, je, mwanadamu siye wa kulaumiwa kwa mengi ya matatizo ya karne hii ya 20 kutia na uwezekano wa ‘kuiangamiza dunia’ kabisa?—Ufunuo 11:18.

Usimamizi Mbaya wa Mwanadamu Warekebishwa

Vipi ule uwezekano zaidi kwamba mwanadamu mwenyewe huenda akaiangamiza au kuiharibu dunia kwa usimamizi wake mbaya na pupa? Ni wazi kwamba uharibifu mkubwa wa sehemu za dunia tayari umetokea kupitia ukataji-misitu kupita kiasi, uchafuzi wa angahewa usiozuiwa, na kuharibiwa kwa mito. Hali hiyo ilitolewa muhtasari kwa kufaa miaka ipatayo 25 iliyopita na waandishi Barbara Ward na René Dubos katika kitabu chao Only One Earth: “Maeneo matatu makubwa ya uchafuzi ambayo ni lazima tuyachunguze—hewa, maji, na udongo—bila shaka yafanyiza sehemu tatu muhimu kwa uhai katika sayari yetu.” Na hiyo hali haijabadilika kimsingi kuwa bora tangu wakati huo, je, imefanya hivyo?

Tunapofikiria uwezekano wa mwanadamu wa kuiangamiza au kuiharibu dunia kwa upumbavu wake mwenyewe, twaweza kutiwa moyo kwa kufikiria uwezo wa kustaajabisha wa sayari Dunia wa kujirudisha na kujirekebisha upya. Akifafanua uwezo huo wa kushangaza wa kujirudisha katika hali yake ya kawaida, René Dubos atoa maoni haya yenye kutia moyo katika kitabu kingine, The Resilience of Ecosystems:

“Watu wengi huhofu kwamba ufahamu kuhusu kudhoofika kwa mazingira umechelewa sana kuja kwa sababu madhara ambayo tayari yamefanyiwa mifumikolojia hayawezi kurekebishwa. Kwa maoni yangu, kutazamia mabaya huko hakuna msingi mzuri kwa sababu, mifumikolojia ina uwezo mkubwa mno wa kujirudisha katika hali yake ya kawaida kutoka katika madhara yenye kuipata.

“Mifumikolojia ina taratibu kadhaa za kujirekebisha. . . . Taratibu hizo huwezesha mifumikolojia kushinda matokeo ya mivurugo kwa kuanzisha tena tu usawaziko wa ikolojia hatua kwa hatua.”

Inawezekana

Kielelezo chenye kutokeza cha jambo hilo katika miaka ya majuzi ni kusafishwa hatua kwa hatua kwa Thames, mto wa London wenye kujulikana sana. Kitabu The Thames Transformed, kilichoandikwa na Jeffery Harrison na Peter Grant, hutoa habari za mafanikio hayo yenye kutokeza ambayo hudhihirisha yale yawezayo kutimizwa watu wafanyapo kazi pamoja kwa manufaa ya umma kwa ujumla. Dyuki wa jiji la Edinburg la Uingereza aliandika katika utangulizi wake kwenye kitabu hicho hivi: “Hatimaye hapa pana simulizi la mafanikio la kiwango kikubwa sana hivi kwamba lastahili kuchapishwa ijapokuwa huenda likawatia moyo watu fulani wadhani kwamba matatizo ya kuhifadhi mazingira kwa kweli si mabaya kama walivyosadikishwa. . . . Wote waweza kuwa na uhakika kutokana na mafanikio ambayo yamepatikana katika Thames. Habari njema ni kwamba inawezekana na mipango yao pia inaweza kufanikiwa.”

Katika sura “Usafishaji Mkubwa,” Harrison na Grant waandika kwa shauku kuhusu yale ambayo yamefanywa kwa mafanikio katika miaka 50 iliyopita: “Kwa mara ya kwanza ulimwenguni, mto uliokuwa umechafuliwa vibaya na wenye viwanda vingi umerekebishwa kwa kiwango kikubwa hivi kwamba ndege wa majini, na samaki wamerudi kwa wingi. Uhakika wa kwamba badiliko kama hilo limetokea kwa haraka hivyo, katika hali ambayo mwanzoni ilionekana isiyo na tumaini, watoa kitia-moyo hata kwa mhifadhi wanyama mwenye kutarajia mabaya zaidi.”

Kisha Harrison na Grant wafafanua hilo badiliko hivi: “Hali ya huo mto ilizidi kuharibika kadiri miaka ilivyopita, labda, pigo la mwisho likija wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili wakati ambapo karakana za kusafisha maji machafu na mabomba ya maji machafu yalipoharibika. Wakati wa miaka ya 1940 na 1950, hali ya Thames ilikuwa katika kiwango cha chini zaidi. Huo mto ulikuwa sawa na mtaro wa takataka ulio wazi; maji yalikuwa meusi, bila oksijeni, na wakati wa miezi ya kiangazi uvundo kutoka Thames ulisikika katika eneo kubwa. . . . Hatimaye samaki waliokuwako kwa wingi walikuwa wamefukuzwa, isipokuwa mikunga wachache walioweza kubaki hai kwa sababu ya uwezo wao wa kupumua moja kwa moja kutoka sehemu ya juu ya maji. Ndege wa maeneo ya ndani yaliyo mapana na wazi, yenye kujaa majengo kati ya London na Woolwich, walipungua wakabaki bata-mwitu na bata weupe wachache, nao walikuwa hai kwa sababu ya nafaka iliyomwagika kutoka katika gati za nafaka wala si kwa sababu ya ugavi wa chakula cha asili. . . . Basi ni nani angeliamini urekebishaji wenye kutazamisha ambao ulikuwa karibu kutokea? Katika muda wa miaka kumi maeneo hayohayo ya mto yasiyo na chochote yangebadilishwa na kuwa kimbilio la spishi nyingi za ndege wa majini, kutia na ndege wanaokuja kupisha majira ya baridi kali, ambao idadi yao hufika bata-mwitu 10,000 na vitwitwi 12,000.”

Bila shaka, hayo yafafanua badiliko moja tu katika sehemu ndogo moja ya tufe. Hata hivyo, twaweza kujifunza mengi kutokana na kielelezo hicho. Chaonyesha kwamba sayari Dunia haipasi kufikiriwa kwamba itaangamizwa kwa sababu ya usimamizi mbaya, pupa na kutojali kwa mwanadamu. Elimu ifaayo na jitihada yenye muungano kwa manufaa ya wanadamu kwa ujumla yaweza kusaidia dunia kurekebisha uharibifu wa ikolojia yake, mazingira, na uso wa nchi. Lakini vipi maangamizi yawezayo kutokana na kani zitokazo nje, kama vile nyotamkia au sayari ndogo zenye kuzunguka huku na kule?

Makala inayofuata ina jibu lenye kuridhisha kwa swali hilo lenye kutatanisha.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

Elimu na jitihada ya muungano yaweza kuisaidia dunia irekebishe hata uharibifu mkubwa sana ambao umefanywa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki