Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 1/22 kur. 24-27
  • Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuzunguka Katikati ya Vifusi vya Sayari
  • Kufunua Kreta, Milipuko, na Migongano
  • Mpangilio wa Misiba
  • Ni Nini Kinachopasa Kufanywa?
  • Miamba Inayoruka
    Amkeni!—1995
  • Nyotamkia Yagonga Sumbula!
    Amkeni!—1997
  • Ni Nini Kilicho Nyuma ya Sayari?
    Amkeni!—1999
  • Je, Msiba wa Anga Utaangamiza Ulimwengu Wetu?
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 1/22 kur. 24-27

Sayari Ndogo, Nyotamkia, na Dunia—Je, Ziko Katika Mwendo wa Kugongana?

‘Mapema asubuhi mnamo Juni 30, kitu kisicho cha kawaida kilionekana katika kijiji fulani huko Siberia. Juu angani, wakulima waliona kitu kilichong’aa kwa uangavu mwingi; kilikuwa na uangavu mwingi sana usioweza kutazamwa kwa macho. Chini kwenye anga, upande uleule kulipokuwa na kitu hiki chenye kung’aa, wingu dogo jeusi lilionekana. Kitu hicho kiangavu kilipokaribia kufika ardhini, kilionekana kuwa kimesagwa kuwa mavumbi. Mahali kilipoanguka, kulitokea wingu kubwa la moshi mweusi, na mlipuko mkubwa ulisikika, kana kwamba ulitokana na lundo kubwa la majabali. Majengo yalitikisika, na ndimi za miale zilizogawanyika zilijitokeza juu ya wingu hilo. Wanakijiji walikimbia barabarani wakiwa na hofu. Wanawake wazee walilia; kila mtu alifikiri mwisho wa ulimwengu umewadia.’—Muhtasari wa ripoti iliyochapishwa katika gazeti la habari la Sibir, Irkutsk, Urusi, mnamo Julai 2, 1908.

WANAKIJIJI hao hawakutambua hata kidogo kwamba kitu fulani kutoka mbinguni kilikuwa kimelipuka tu juu ya vichwa vyao. Leo, zaidi ya miaka 90 baadaye, mojawapo ya matabiri yasiyokuwa ya kawaida kuhusu mwisho wa sayari yetu yanahusisha msiba utakaosababishwa na sayari ndogo au nyotamkia. Maneno yanayoundwa kutokana na herufi za mwanzo kama vile NEO (vitu vinavyokaribia dunia) na PHO (vitu vinavyoweza kuwa hatari) yanasikika kuhusiana na utabiri wa uharibifu wa mwisho kuhusu kuharibiwa kwa dunia kwa kugongana na magimba ya kimbingu. Hollywood imejipatia faida kubwa sana kwa kuonyesha hofu hii katika sinema kama vile Deep Impact na Armageddon.

Lakini kuna uwezekano gani kwamba wewe au watoto wako mtaangamizwa na kimondo kutoka mbinguni? Je, utarajie ua wako uangukiwe na vipande vikubwa vya chuma na barafu hivi karibuni? Ikiwa unaishi karibu na pwani, je, nyumba yako itabomolewa na wimbi kubwa la maji yaliyojaa lenye kusababishwa na nyota ndogo inayozunguka-zunguka na kutumbukia baharini?

Kuzunguka Katikati ya Vifusi vya Sayari

Mfumo wetu wa jua haufanyizwi tu na jua, sayari tisa, na miezi ya sayari hizo. Nyotamkia (mkusanyiko wa barafu na vumbi), sayari ndogo, na meteroidi (hasa ni vipande vya sayari ndogo) pia zinazunguka ndani ya mfumo wa jua. Kwa muda mrefu wanasayansi wamejua kwamba dunia yaweza kushambuliwa kutoka angani. Tunahitaji tu kutazama sura ya mwezi jinsi ambavyo imeharibiwa ili kutambua kwamba tunaishi katika ujirani uliovurugika. Ikiwa angahewa halingekuwako na utaratibu wa kufanya upya uso wa dunia na mabamba na mmomonyoko, sayari yetu ingekuwa na mashimo kama mwezi.

Wanasayansi wanakadiria kwamba vimondo vipatavyo milioni 200 huonekana kwenye angahewa la dunia kila siku. Vitu vingi ambavyo huingia kwenye angahewa ni vidogo na huungua hata kabla havijaonekana. Hata hivyo, baadhi ya vitu hivi huokoka joto kali vinapoingia kwenye angahewa na mwendo wao hupunguzwa na msuguano wa hewa kufikia mwendo upatao kilometa 320 kwa saa. Mabaki yao hugonga ardhi yakiwa mawe kutoka kwenye nyota. Kwa kuwa vingi vyao huanguka kwenye bahari au mabara yasiyokuwa na watu, huwa vigumu kusababisha madhara kwa wanadamu. Inakadiriwa kwamba vitu vinavyoingia katika angahewa letu huongeza mamia ya tani kila siku kwa uzito wa dunia.

Kwa kuongezea, waastronomia wanakadiria kwamba huenda kukawa na sayari ndogo 2,000 hivi ambazo zina kipenyo cha kilometa moja ambazo ama huvuka ama hukaribia mzingo wa dunia. Wamegundua na kuchunguza mwendo wa sayari ndogo zipatazo 200 tu kati yao. Pia, inakadiriwa kuwa kuna sayari ndogo milioni moja zenye kipenyo kinachozidi meta 50 ambazo hutokeza hatari kwa kukaribia mzingo wa dunia yetu. Sayari ndogo zenye ukubwa huo zaweza kufika ardhini na kusababisha madhara. Nguvu hiyo ya kurusha sayari kwa kulinganisha ina megatoni kumi za nishati—inayotoshana na bomu kubwa la nyuklia. Ingawa angahewa la dunia laweza kutulinda kutokana na migongano midogo, haliwezi kuzuia migongano yenye megatoni kumi za nishati au zaidi. Watafiti fulani wanadai kwamba, kulingana na takwimu, tunaweza kutarajia mgongano wa nishati ya megatoni kumi kwa wastani wa karibu mara moja kwa karne moja. Kulingana na makadirio fulani, ili mgongano urudiwe tena wa vitu vyenye kipenyo cha karibu kilometa moja itakuwa mara moja katika miaka 100,000.

Kufunua Kreta, Milipuko, na Migongano

Si vigumu kuamini kwamba sayari yetu imegongwa na vitu vikubwa ambavyo vimeanguka kutoka angani wakati uliopita. Ithibati ya migongano hii yaweza kupatikana katika kreta zaidi ya 150 zilizogunduliwa ambazo zimetoboa uso wa dunia. Kreta nyingine huonekana waziwazi, nyingine zaweza kuonekana tu ukiwa kwenye ndege au kutoka kwa setilaiti, na bado nyingine zimefunikwa kwa muda mrefu au ziko kwenye sakafu ya bahari.

Kreta moja mashuhuri sana kati ya hizi, inayojulikana kuwa Chicxulub, ilitokeza kovu lenye kipenyo cha kilometa 180 kwenye uso wa dunia. Kreta hii iliyoko karibu na ncha ya Peninsula ya Yucatán, Mexico, ni kubwa sana na inaaminiwa kuwa eneo ambapo palitokea mgongano wa nyotamkia au sayari ndogo yenye upana wa kilometa kumi. Watu fulani wanadai kwamba mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyoanzishwa na mgongano huu yalisababisha kutoweka kwa dinosau na wanyama wengine wa bara na wa baharini.

Katika Arizona, Marekani, kipande cha chuma kilichotoka kwenye nyota kilitoboa Meteor Crater yenye kustaajabisha—shimo lenye upana upatao meta 1,200 na kina cha meta 200. Ni watu wangapi ambao wangekufa ikiwa kipande cha chuma kama hicho kingeangukia jiji? Wonyesho unaopendwa sana kwenye Jumba la Makumbusho la Marekani la Historia ya Asili, katika New York City, unaonyesha kwamba ikiwa kitu kama hicho kingeipiga Manhattan, mji huo uliojaa watu ungeharibiwa kabisa.

Mnamo Juni 30, 1908, sayari ndogo au kipande kikubwa cha nyotamkia kinachokadiriwa kuwa na upana unaopungua meta 100 kiliingia kwa mngurumo kwenye angahewa na kulipuka kilometa zipatazo kumi juu ya eneo lisilokuwa na watu wengi la Tunguska la Siberia, kama ilivyotajwa katika utangulizi. Mlipuko huo, uliokadiriwa kuwa wa megatoni 15, uliharibu eneo lenye kilometa mraba 2,000, ukiangusha miti, kuwasha mioto, na kuua kulungu. Ni watu wangapi ambao wangekufa iwapo mahali palipotokea mlipuko huo palikuwa eneo lenye watu wengi sana?

Mnamo Julai 1994, darubini-upeo duniani pote zilielekezwa kwa Sumbula huku vipande vya nyotamkia iitwayo Shoemaker-Levy 9 vikianguka kwa kishindo ndani ya sayari hiyo. Makovu ya muda yaliyotokezwa kwenye Sumbula yatakumbukwa daima na wale waliojionea migongano hiyo moja kwa moja. Wakitazama Sumbula ikigongwa mara kadhaa, watafiti na watu wa kawaida walistaajabia ni nini kingalitokea ikiwa, badala yake, dunia ndiyo ambayo ingaligongwa.

Mpangilio wa Misiba

Wakiwa na hofu, wanasayansi wamefikiria matokeo yenye kutisha ambayo yangesababishwa kwa sayari yetu na mgongano wa nyotamkia au wa sayari ndogo. Hivi ndivyo wanavyofikiri matokeo ya mara moja ya mgongano mkubwa yangekuwa. Kungekuwako mlipuko mkubwa wa mawe na vumbi. Vifusi vinavyoanguka vingetokeza manyunyu ya vipande vya nyota ambayo yangelifanya anga liwe moto kwelikweli na kuanzisha mioto kwenye misitu na mbuga za nyasi, ikiua wanyama wengi wa ardhini. Vumbi ambayo ingebaki ikielea juu ya angahewa kwa kipindi kirefu zaidi ingezuia nuru ya jua, ikisababisha halijoto iporomoke na kukomesha usanidinuru kwenye sehemu za chini zenye giza. Kukomeshwa kwa usanidinuru pia kungeongoza kwenye kukatizwa kwa mfuatano wa chakula wa baharini, kukisababisha vifo vya viumbe wengi wa majini. Kulingana na mpangilio huu, msiba wa kimazingira ungefikia kikomo kwa kunyesha mvua ya asidi ya tufeni pote na kuharibiwa kwa tabaka ya ozoni.

Iwapo sayari ndogo ya namna hiyo ingeanguka baharini, ingesababisha mawimbi ya maji yaliyojaa yenye uwezo mkubwa sana wa uharibifu. Mawimbi ya maji yangefikia mbali zaidi kutoka kwenye eneo la mgongano kuliko wimbi la kishindo la kwanza na yangetokeza uharibifu wenye kuenea katika maeneo ya pwani yaliyo umbali wa maelfu ya kilometa. Mwastronomia Jack Hills asema: “Mahali palipokuwa na majiji, pangekuwa tu na ardhi tambarare.”

Hata hivyo, mtu apaswa kuwa mwangalifu kuhusu madai hayo. Nyingi za nadharia hizo ni mambo ya kukisia tu. Bila shaka, hakuna mtu ameona au kuchunguza sayari ndogo ikigongana na dunia. Pia, vyombo vya habari vya leo vinavyotamani kusambaza habari zenye kushtua hutokeza upesi vichwa vya habari vyenye kushtua, vinavyotegemea habari isiyo kamili au hata isiyo sahihi. (Ona sanduku lililo juu.) Kwa kweli, inasemekana kwamba uwezekano wa kufa kutokana na kitu kinachoanguka kutoka angani ni mdogo sana kuliko uwezekano wa kufa katika aksidenti ya gari.

Ni Nini Kinachopasa Kufanywa?

Wataalamu wengi wanaamini kwamba hatua bora ya kuzuia msiba unaoletwa na nyotamkia au sayari ndogo inayokaribia ingekuwa ni kurusha roketi ili kuingilia kati mvamizi huyo na, angalau, kubadili mwendo wake. Ikiwa sayari hiyo ni ndogo na inagunduliwa miaka mingi kabla ya mgongano wake uliokisiwa, kuingilia kati huku kwaweza kutosha.

Hata hivyo, kwa kitu kikubwa zaidi kiwezacho kugongana na dunia, wanasayansi fulani wanapendekeza silaha za nyuklia zitumiwe. Katika kisa hicho, inaaminiwa kwamba mlipuko uliopangwa vizuri wa nyuklia ungedukua hiyo sayari ndogo kwenye eneo lililo salama, na kuizuia isigongane na dunia. Ukubwa wa hiyo sayari ndogo na kupakana kwake na dunia ungeamua ukubwa wa mlipuko wa nyuklia ambao ungehitajiwa.

Tatizo ni kwamba hakuna mojawapo ya hatua hizi za kujilinda iwezayo kuwa na matokeo bila onyo linalotolewa muda unaofaa kimbele. Vikundi vya waastronomia kama vile Spacewatch na Near Earth Asteroid Tracking vimejitolea kipekee kutafuta sayari ndogo. Watu wengi wanahisi kwamba mengi zaidi yahitaji kufanywa kuhusu jambo hili.

Kwa kukiri wazi, wanadamu wasiokamilika hawana ujuzi wa kutosha kuhusu mahali yalipo magimba haya ya kimbingu na miendo yao. Lakini hakuna uhitaji wa kuhangaika sana au kuwa na hofu inayopita kiasi juu ya vitisho vya kwamba wakati ujao wa uhai uliopo duniani upo hatarini. Uhakikisho ulio salama zaidi kwamba hakuna sayari ndogo au nyotamkia itakayowahi kuruhusiwa iharibu uhai wote uliopo duniani watoka kwa Muumba wa ulimwengu, Yehova Mungu.a Biblia inatuhakikishia hivi: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”—Zaburi 37:29; Isaya 45:18.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa mazungumzo zaidi juu ya maoni ya Biblia kuhusu habari hii, ona ukurasa wa 22-23 wa toleo la Amkeni! la Desemba 8, 1998.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Kisa cha 1997 XF11

Mnamo Machi 12, 1998, habari zenye kuogofya zilisambaa tufeni pote: Sayari ndogo yenye upana wa kilometa moja na nusu ilikuwa ikielekea duniani na ilipaswa kuwasili Oktoba 26, 2028 “siku ya Alhamisi.” Sayari ndogo iliyoitwa 1997 XF11, iligunduliwa Desemba 6, 1997, na mwastronomia Jim Scotti, wa kikundi cha Spacewatch cha Chuo Kikuu cha Arizona. Kwa kutumia data ya wakati uliopita na uchunguzi mpya zaidi, wanasayansi wanaoshirikiana na kituo cha Harvard-Smithsonian Center for Astrophysics walitoa habari ambayo ilitumiwa na watu fulani kutabiri kwamba mzingo wa hiyo sayari ndogo yaelekea ungeikadiria kuwa umbali wa kilometa 50,000 kutoka duniani—umbali mfupi sana kulingana na viwango vya waastronomia, au “bila uwezekano wa kukosa kugongana na dunia.” Misambazo ya televisheni ilijaa uigizaji wenye kuogofya wa sayari ndogo ikiigonga dunia. Kisha, hata kabla ya siku moja kwisha, hatari hiyo ilikuwa imetoweka. Data mpya na makisio mapya yalionyesha kwamba hiyo sayari ndogo ingekosa kuigonga dunia kwa umbali wa kilometa 1,000,000. Bado hiyo sayari ndogo ilikaribia dunia zaidi ya nyingine yoyote yenye ukubwa sawa iliyopata kuonekana awali, lakini ilikuwa kwenye umbali usio na hatari. Upesi vyombo vya habari vilichapisha vichwa vya habari kama vile “Sawa, kwa Hiyo Data Hizo Zilikuwa na Makosa Madogo Tu.”

[Picha katika ukurasa wa 26]

1. Nyotamkia ya Halley

2. Nyotamkia Ikeya-Seki

3. Sayari ndogo 951 Gaspra

4. Meteor Crater—shimo lenye upana upatao meta 1,200 na kina cha meta 200

[Hisani]

Courtesy of ROE/Anglo-Australian Observatory, photograph by David Malin

NASA photo

NASA/JPL/Caltech

Photo by D. J. Roddy and K. Zeller, U.S. Geological Survey

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

NASA photo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki