Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 9/1 kur. 22-23
  • Betheli Jiji la Wema na Ubaya

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Betheli Jiji la Wema na Ubaya
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Betheli Lawa Kitovu cha Uasi-Imani
  • Je, Hii Yaweza Kuwa Kazi-Maisha Inayokufaa Zaidi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Kutazama “Nyumba ya Mungu” kwa Uthamini
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Je, Waweza Kujitolea?
    Huduma Yetu ya Ufalme—2001
  • Watu Wote Wanaalikwa!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 9/1 kur. 22-23

Betheli Jiji la Wema na Ubaya

MAJIJI fulani huwa na sifa njema—au sifa mbaya—kwa sababu ya yale yatukiayo ndani yake. Hata hivyo, Betheli ni jiji lisilo la kawaida kwa kuwa lilijulikana kwa wema na vilevile kwa ubaya. Mzee wa ukoo Yakobo, aliliita jiji hilo Betheli, jina limaanishalo “Nyumba ya Mungu.” Lakini miaka elfu moja baadaye, nabii Hosea aliliita jiji hilo “Nyumba ya Madhara.” Jiji hilo lilibadilikaje likawa jiji la ubaya na kuacha kuwa jiji la wema? Na twaweza kujifunza nini kutokana na historia yake?

Kushirikishwa kwa Betheli na watu wa Mungu kulianza mwaka wa 1943 K.W.K. Abrahamu alipokuwa bado hai. Wakati huo jiji hilo liliitwa Luzu, jina lake la awali la Wakanaani. Jiji hilo lilikuwa kwenye kilima, kilometa zipatazo 17 kaskazini mwa Yerusalemu. Ebu wazia Abrahamu na Loti mpwa wake wa kiume wakiangalia nyanda za upande wa chini wa Bonde la Yordani wakiwa mahali pafaapo juu milimani karibu na Betheli. Kwa busara, Abrahamu alimfahamisha Loti tatizo la kugawa maeneo ya kulisha makundi yao akisema: “Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.”—Mwanzo 13:3-11.

Abrahamu hakusisitiza kuwa na haki ya kuchagua kwanza. Badala yake, alimruhusu huyo mwanamume mchanga achukue mahali palipokuwa bora zaidi. Tunaweza kuiga mtazamo mwema wa Abrahamu. Tunaweza kusuluhisha masuala yenye kuleta ugomvi kwa kuchukua hatua ya kwanza kuzungumza kwa utulivu na kutenda bila ubinafsi.—Waroma 12:18.

Miaka kadhaa baadaye wakati mjukuu wa Abrahamu Yakobo alipopiga kambi huko Luzu, aliota ndoto isiyo ya kawaida. Aliona “ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.” (Mwanzo 28:11-19; linganisha Yohana 1:51.) Ndoto hiyo ilikuwa na umuhimu fulani. Malaika ambao Yakobo aliona wangemhudumia katika kutimiza ahadi ambayo Mungu alimtolea kuhusu mbegu yake. Cheo cha Yehova kilichoinuliwa juu ya hiyo ngazi kilionyesha kwamba angewaongoza malaika hao katika kazi hiyo.

Uhakikisho huo wa utegemezo wa Mungu uligusa moyo wa Yakobo sana. Baada ya kuamka kutoka ndotoni, alipaita mahali hapo Betheli, yaani “Nyumba ya Mungu” na kuweka nadhiri hii kwa Yehova: “Katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”a (Mwanzo 28:20-22) Akitambua kwamba chochote alichokuwa nacho kilitoka kwa Mungu, alitamani kurudisha sehemu kubwa ikiwa ishara ya shukrani zake.

Leo pia malaika huhudumu kwa niaba ya Wakristo. (Zaburi 91:11; Waebrania 1:14) Wao pia wanaweza kuonyesha uthamini wao wa baraka zote walizopata kwa kuwa “tajiri kwa maonyesho mengi ya shukrani kwa Mungu.”—2 Wakorintho 9:11, 12.

Baada ya muda, wazao wa Yakobo walipata kuwa taifa. Yoshua kiongozi wao alimshinda mfalme mpagani wa Betheli karibu na mwanzo wa ushindi juu ya Kanaani. (Yoshua 12:16) Wakati wa Waamuzi, nabii wa kike Debora, aliishi karibu na Betheli naye aliwaeleza watu neno la Yehova. Samweli pia alizuru Betheli kwa ukawaida alipokuwa mwamuzi wa taifa la Israeli.—Waamuzi 4:4, 5; 1 Samweli 7:15, 16.

Betheli Lawa Kitovu cha Uasi-Imani

Kushirikishwa kwa Betheli na ibada safi kulikoma baada ya kugawanyika kwa Ufalme katika mwaka wa 997 K.W.K. Mfalme Yeroboamu alijenga Betheli liwe kitovu cha ibada ya ndama, ikidhaniwa kwamba ndama huyo alimwakilisha Yehova. (1 Wafalme 12:25-29) Hiyo ndiyo sababu, alipokuwa akitoa unabii wa kuharibiwa kwa Betheli, Hosea alilirejezea kuwa “Beth-Aveni,” yaani “Nyumba ya Madhara.”—Hosea 10:5, 8.

Ingawa Betheli lilikuwa limekuwa kitovu cha madhara ya kiroho, matukio yenye kuhusianishwa na jiji hilo yaliendelea kuandaa masomo muhimu. (Waroma 15:4) Somo moja kama hilo lahusu nabii asiyetajwa jina ambaye alitumwa kutoka Yuda kwenda Betheli ili akatabiri juu ya kuharibiwa kwa madhabahu na makuhani wake. Yehova pia alimwambia arudi Yuda—kilometa chache upande wa kusini—bila kula au kunywa. Nabii huyo alitoa unabii kwa ujasiri mbele ya Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akilaani madhabahu ya Betheli. Lakini nabii huyo alikosa kumtii Mungu kwa kula nyumbani mwa nabii mmoja mzee huko Betheli. Kwa nini? Huyo nabii mzee alidai isivyo kweli kwamba malaika wa Yehova alikuwa amemwagiza amkaribishe nabii mwenzake. Kutotii kwa huyo nabii kutoka Yuda kulifanya afe kabla ya wakati.—1 Wafalme 13:1-25.

Twapaswa kuitikiaje mwamini mwenzetu akidokeza kwamba tufanye jambo ambalo laonekana kuwa lenye kutilika shaka? Kumbuka kwamba hata shauri lenye nia nzuri laweza kuwa lenye madhara likiwa lenye kosa. (Linganisha Mathayo 16:21-23.) Kwa kutafuta mwongozo kutoka kwa Yehova kupitia sala na kujifunza Neno lake, tutaepuka kosa lenye kuleta msiba la nabii huyo asiyetajwa jina.—Mithali 19:21; 1 Yohana 4:1.

Miaka 150 baadaye, nabii Amosi pia alisafiri kwenda kaskazini kutoa unabii dhidi ya Betheli. Amosi aliwashutumu wasikilizaji wake wenye uhasama, kutia ndani kuhani Amazia, ambaye kwa kiburi alimwambia Amosi ‘aende zake, akimbilie nchi ya Yuda.’ Lakini kwa ujasiri Amosi alimwambia Amazia juu ya maafa ambayo yangepata nyumba ya huyo kuhani mwenyewe. (Amosi 5:4-6; 7:10-17) Kielelezo chake chatukumbusha kwamba Yehova anaweza kuwajasirisha wahudumu wake wanyenyekevu.—1 Wakorintho 1:26, 27.

Hatimaye, Yosia, Mfalme mwaminifu wa Yuda aliharibu ‘madhabahu iliyokuwako Betheli, akapateketeza mahali pa juu, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera.’ (2 Wafalme 23:15, 16) Wazee leo wanaweza kuiga kielelezo chake chema kwa kutekeleza kwa bidii maagizo ya Mungu na kuongoza katika kuliweka kutaniko likiwa safi.

Matukio hayo katika historia ya Betheli huonyesha dhahiri matokeo ya uadilifu na uovu, matokeo ya kumtii na kutomtii Yehova. Miaka kadhaa mapema, Musa alikuwa ameweka chaguo hili mbele ya taifa la Israeli: “Nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya.” (Kumbukumbu la Torati 30:15, 16) Kutafakari juu ya historia ya Betheli kutatusaidia kujitambulisha na “Nyumba ya Mungu,” mahali pa ibada ya kweli, badala ya kujitambulisha na “Nyumba ya Madhara.”

[Maelezo ya Chini]

a Yakobo na vilevile Abrahamu walitoa sehemu ya kumi kwa hiari.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Magofu yaliyo mahali Betheli ilipokuwa, ambapo Yeroboamu alianzisha kitovu cha ibada ya ndama

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki