Wapiga-mbiu wa Ufalme Waripoti
Mpinzani wa Zamani Ajifunza Kweli
MENGI yameripotiwa katika habari kuhusu vita ya wenyewe kwa wenyewe katika Liberia. Watu makumi ya maelfu walikufa, na hata wengi zaidi walihamishwa. Licha ya magumu haya, watu wenye mioyo ya haki waliendelea kukubali kweli, kama jambo lililoonwa lifuatalo linavyoonyesha.
Kuanzia umri wa miaka kumi, James alielimishwa na Kanisa la Kilutheri. Baada ya kuwa mhariri wa gazeti la kanisa, alitumia cheo chake kuandika dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Alifanya hivyo ijapokuwa hakuwa amepata kukutana na mmoja wao.
Baada ya muda, James aliacha kuhariri gazeti la kanisa na akawa na mafanikio kuendesha hoteli yake mwenyewe. Siku moja alipokuwa akiketi katika sehemu ya mapokezi ya hoteli yake, dada wawili waliovalia vizuri walimtembelea. Alipoyaona mavazi yao nadhifu, aliwaalika waingie ndani. Lakini walipoeleza kusudi la ziara yao, yeye alisema hivi, “Nina shughuli sana sina nafasi ya kuongea.” Mashahidi hao walimtolea maandikisho ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, naye alikubali ili tu waende zao. Alipokea magazeti nyumbani kwake kwa miezi 12, lakini aliyaweka katika mfuko wa plastiki bila hata kuyafungua.
Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilikuwa imechacha, kwa hiyo James alifunga mkoba na pesa na vitu vyenye thamani ili kutoroka shambulizi la kwanza litokeapo. Asubuhi moja grunedi lililipuka nyuma ya mlango wake wa nyuma, kwa kushtuka akanyakua mkoba wake na kukimbia aokoe uhai wake. Akiungana na maelfu ya raia wenzake waliokuwa wakikimbia, ilimbidi apitie vituo kadhaa vya kukagulia. Huko, raia wasio na hatia mara nyingi walikuwa wakinyang’anywa mali zao na kuuawa bila sababu yoyote.
Akiwa mahali pa kwanza pa kukagulia, James aliulizwa maswali machache kisha akaambiwa afungue mkoba wake. Alipofanya hivyo, alitazama mkobani mwake na hakuweza kuamini macho yake. Alitishika sana alipoona kwamba mkoba aliobeba haukuwa ule uliokuwa na vitu vyake vyenye thamani. Kwa kushtuka alikuwa amebeba mkoba uliokuwa na magazeti ambayo yalikuwa hayajafunguliwa ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Hata hivyo, askari alipoona magazeti hayo na kusoma jina lake kwenye vibandiko, alisema hivi: “Ooh, wewe ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Hatuwatafuti nyinyi, twajua hamsemi uwongo.” Baada ya kuchukua magazeti machache kutoka mkobani, askari huyo alimwambia James aendelee na safari yake.
Jambo hilo lilitokea katika vituo tisa vya kukagulia, kwa kuwa makamanda wote walidhania kwamba James alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova nao wakamwacha aende bila kumdhuru. Sasa James alishukuru sana kwamba hakubeba vitu vyake vya thamani kwa sababu kutokana na aliyoona, kwa hakika angekuwa ameuawa kwa sababu ya mali zake.
Mwishowe, alipofika mahali pa kukagulia pa mwisho na penye kuogopwa zaidi, alichukizwa sana kuona idadi ya miili iliyokuwa imekufa chini. Akiwa na hofu, aliita jina la Yehova. Alisali kwamba ikiwa Mungu angemsaidia apite mahali hapa pa mauaji, angemtumikia katika maisha yake yote.
James aliwaonyesha askari mkoba wake, kwa mara nyingine tena wakasema: “Hatuwatafuti watu hawa.” Wakimgeukia, wakaongezea: “Mmoja wa ndugu zako huishi chini ya mlima huu. Nenda ukae naye.” Kufikia wakati huo maoni ya James kuhusu Mashahidi yalikuwa yamebadilika kabisa. Mara hiyo alimtafuta ndugu huyo, na mipango ikafanywa ya funzo la Biblia katika kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani.a
Siku chache baadaye, shambulizi fulani lilimlazimisha kutoroka mahali hapo. Wakati huo, James alikimbilia msituni akikamata kitabu chake Kuishi Milele tu! Alipokuwa peke yake kwa miezi 11 mbali na Mashahidi, alisoma kitabu chake chote mara tano. Mwishowe, alipoweza kurudi jijini, alianza kujifunza Biblia na Mashahidi naye akafanya maendeleo ya haraka. Muda mfupi baadaye, alibatizwa, naye sasa hutumikia kwa uaminifu pamoja na ndugu zake wa kiroho.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.yy