Wamakabayo Walikuwa Nani?
KWA watu wengi, kile kipindi cha Wamakabayo ni kama chanzo cha habari juu ya kipindi cha kati ya kukamilishwa kwa vitabu vya mwisho vya Maandiko ya Kiebrania, na kuja kwa Yesu Kristo. Sawasawa na vile habari fulani hufunuliwa wakati kifaa cha kunasa habari katika ndege kichunguzwapo baada ya ndege kuanguka, uelewevu fulani waweza kupatikana kwa kuchunguza kwa makini ule muhula wa Wamakabayo—muhula wa mpito na mabadiliko ya taifa la Kiyahudi.
Wamakabayo walikuwa nani? Waliathirije dini ya Kiyahudi kabla ya kuja kwa Mesiya aliyeahidiwa?—Danieli 9:25, 26.
Mweneo Wenye Nguvu wa Utamaduni wa Kigiriki
Aleksanda Mkubwa aliyashinda maeneo yote toka Ugiriki hadi India (336-323 K.W.K.). Ufalme wake wenye mweneo mkubwa, ulikuwa sababu moja ya kuenezwa kwa Utamaduni wa Kigiriki—lugha na ustaarabu wa Kigiriki. Maofisa wa Aleksanda na vikosi vyake waliwaoa wanawake wenyeji, wakitokeza mchangamano wa tamaduni za Kigiriki na za kigeni. Baada ya kifo cha Aleksanda, ufalme wake uligawanyika miongoni mwa majenerali wake. Kuanzia karne ya pili K.W.K., Antioko wa Tatu wa nasaba ya kifalme ya Ugiriki ya Seleukia katika Siria, aliitwaa Israeli kutoka mikononi mwa Watawala Wagiriki wa Misri. Utawala wa Kigiriki uliwaathirije Wayahudi katika Israeli?
Mwanahistoria mmoja aandika hivi: “Kwa kuwa Wayahudi hawangeepuka uhusiano wa karibu pamoja na majirani zao waliofuata Utamaduni wa Kigiriki, na kwa vile uhusiano wao pamoja na ndugu zao wa Kiyahudi walioishi mbali ulikuwa mdogo, hawangeweza kuepuka kutwaa Utamaduni wa Kigiriki na njia zao za kufikiri. . . . Kule kuwapo tu katika kipindi hicho cha Utamaduni wa Ugiriki, kulihusisha kutwaa Utamaduni wa Kigiriki!” Wayahudi walijipatia majina ya Kigiriki. Kwa viwango vyenye kutofautiana, walitwaa mila na mitindo ya mavazi ya Kigiriki. Ule uwezo wenye hila wa kuwafanya Wayahudi wafanane na Wagiriki, ulikuwa ukiongezeka.
Ufisadi wa Makuhani
Miongoni mwa Wayahudi, wale walioelekea kuvutwa sana na Utamaduni wa Kigiriki walikuwa makuhani. Kwa wengi wao, kukubali Utamaduni wa Kigiriki kulimaanisha kuruhusu dini ya Kiyahudi kusonga mbele pamoja na wakati. Yasoni (aliyeitwa Yoshua kwa Kiebrania) ni mmoja wa Wayahudi hao, ndugu ya kuhani mkuu Oniasi wa Tatu. Oniasi alipokuwa safarini Antiokia, Yasoni aliwahonga wenye mamlaka wa Ugiriki. Kwa nini? Ili kuwachochea wamchague yeye kuwa kuhani mkuu na kuchukua mahali pa Oniasi. Mtawala Mgiriki wa Seleukia Antioko Epifane (175-164 K.W.K) alikubali toleo hilo kwa vyepesi. Watawala wa Ugiriki hawakuwa wameingilia ukuhani mkuu wa dini ya Kiyahudi hapo awali lakini Antioko alihitaji fedha za kampeni ya kijeshi. Pia, alipendezwa kuwa na mtawala wa Kiyahudi ambaye angeendeleza Utamaduni wa Kigiriki. Kwa kujibu ombi la Yasoni, Antioko alilipa jiji la Yerusalemu cheo kilicholingana na kile cha jiji la Kigiriki (polis). Naye Yasoni akajenga ukumbi wa michezo ya mazoezi, ambapo vijana Wayahudi na hata makuhani, walishindana michezoni.
Hila ilitokeza hila. Miaka mitatu baadaye Menelau, ambaye haielekei alikuwa wa ukoo wa kikuhani alitoa hongo kubwa kuliko ile ya Yasoni, naye Yasoni akatoroka. Ili kumlipa Antioko, Menelau alichukua kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwenye hazina ya hekalu. Kwa kuwa Oniasi wa Tatu, (aliyekuwa uhamishoni Antiokia) alipinga jambo hilo, Menelau alipanga auawe.
Uvumi ulipoenea kwamba Antioko alikuwa amekufa, Yasoni alirudi Yerusalemu akiwa na wanaume elfu moja katika jitihada za kuchukua wadhifa wa kikuhani kutoka kwa Menelau. Lakini Antioko hakuwa amekufa. Aliposikia juu ya tendo la Yasoni na vurugu miongoni mwa Wayahudi za kukaidi sera za Utamaduni wa Kigiriki, Antioko alilipiza kisasi.
Antioko Achukua Hatua
Katika kitabu chake The Maccabees, Moshe Pearlman aandika hivi: “Ijapokuwa maandishi hayako wazi, yaelekea Antioko alikata maneno kwamba kuwapa Wayahudi uhuru mwingi wa kidini kulikuwa kosa la kisiasa. Kulingana naye, uasi huo uliokuwa wa karibuni zaidi katika Yerusalemu haukutokana na sababu halisi za kidini, bali ulitokana na hali ya kuwaunga mkono Wamisri iliyokuwa ikisitawi katika Yudea, na mawazo hayo ya kisiasa yalionyeshwa kwa njia yenye hatari, hasa kwa sababu Wayahudi peke yao miongoni mwa watu wote waliokuwa chini ya milki yake, ndio waliokuwa wameomba na kuruhusiwa kujitenga kwa njia kubwa kidini. . . . Yeye aliamua jambo hilo lingesimamishwa.”
Mwanasiasa na msomi Mwisraeli, Abba Eban, huelezea kwa muhtasari yaliyofuata: “Kwa mfuatano wa upesi-upesi wakati wa miaka ya 168 na 167 [K.W.K.], Wayahudi walichinjwa, Hekalu likaporwa na kuzoea dini ya Kiyahudi kukapigwa marufuku. Kifo kikawa adhabu kwa waliotahiriwa au kushika Sabato. Fedheha kubwa zaidi ilitokea Desemba mwaka wa 167, ambapo kwa amri ya Antioko, madhabahu ya Zeo ilisimamishwa ndani ya Hekalu, nao Wayahudi wakalazimika kutoa dhabihu za nyama ya nguruwe kwa mungu wa Kigiriki, ambayo kwa wazi haikuwa safi kulingana na sheria ya Kiyahudi.” Katika kipindi hiki, Menelau na Wayahudi wengine waliofuata Utamaduni wa Kigiriki, waliendelea na nyadhifa zao, wakitumikia katika hekalu lililokuwa najisi sasa.
Huku Wayahudi wengi wakiukubali Utamaduni wa Kigiriki, kundi jipya la watu waliojiita Wahasidimu—waliojionyesha kuwa watakatifu—walihimiza kushika sana Sheria ya Musa. Wakiwa sasa wamechukizwa na makuhani waliofuata Utamaduni wa Kigiriki, watu wa kawaida walijipatanisha zaidi na zaidi na Wahasidimu. Kipindi cha ufia-imani kikaingia, Wayahudi nchini kote wakalazimishwa ama kujipatanisha na desturi za kipagani na kutoa dhabihu, ama kufa. Vitabu vya Wamakabayo vyenye uasilia wenye shaka hutoa masimulizi mengi juu ya wanaume, wanawake, na watoto waliochagua kufa badala ya kuridhiana.
Wamakabayo Watenda kwa Kupinga
Matendo ya kupita kiasi ya Antioko yaliwachochea Wayahudi wengi wapiganie dini yao. Katika Modiʼin, kusini magharibi mwa Yerusalemu karibu na jiji la kisiku-hizi la Lod, kuhani aitwaye Matathiasi aliitwa kwenda katikati ya mji. Kwa kuwa Matathiasi aliheshimiwa na wenyeji wa mahali hapo, mwakilishi wa mfalme alijaribu kumshawishi ashiriki katika dhabihu za kipagani—kusudi ajiokoe mwenyewe na kuwawekea watu wengine wa kawaida mfano. Matathiasi alipokataa, Myahudi mwingine alijitokeza, tayari kuridhiana. Akijawa na ghadhabu, Matathiasi alichukua silaha na kumwua. Wakiduwazwa na tendo hilo la jeuri la mtu huyu mzee-mzee, askari Wagiriki walikawia kutenda. Kwa muda wa sekunde chache, Matathiasi akawa amemwua ofisa Mgiriki pia. Wana watano wa Matathiasi na wakaaji wa mji wakavishinda nguvu vikosi vya Kigiriki kabla havijaweza kujihami vyenyewe.
Matathiasi akasema kwa sauti kubwa hivi: ‘Yeyote yule mwenye juhudi kwa ajili ya Sheria na anifuate.’ Ili kuepuka kulipiziwa kisasi, yeye pamoja na wana wake walikimbilia milimani. Na habari za matendo yao zilipoenea, Wayahudi (kutia na Wahasidimu wengi) wakajiunga pamoja nao.
Matathiasi alimteua mwanaye Yuda kuwa mkuu wa shughuli za kijeshi. Labda kwa sababu ya uhodari wa Yuda wa kijeshi, akaitwa Makabayo, jina lililomaanisha “nyundo.” Matathiasi na wanawe waliitwa Wahasmonia, jina lililotwaliwa kutoka kwa mji wa Heshmoni au kutoka kwa babu aliyeitwa hivyo. (Yoshua 15:27) Kwa kuwa Yuda Makabayo alikuja kuwa mtu mashuhuri sana wakati wa kipindi cha uasi, hata hivyo, familia nzima ilikuja kuitwa Wamakabayo.
Hekalu Larudishwa
Wakati wa mwaka wa kwanza wa uasi, Matathiasi na wanawe waliweza kuunda jeshi dogo. Kwa pindi kadhaa, majeshi ya Kigiriki yalivamia vikundi vya wapiganaji Wahasidimu siku ya Sabato. Ijapokuwa wangeweza kujikinga, hawangeihalifu Sabato. Hivyo, kukawa na mauaji makubwa. Matathiasi—sasa akionwa kuwa mwenye mamlaka ya kidini—alitoa amri iliyowaruhusu Wayahudi kujikinga siku ya Sabato. Mbali na kuupa uasi nguvu mpya, amri hiyo iliandaa kigezo katika dini ya Kiyahudi cha kuwaruhusu viongozi wa kidini kupatanisha sheria ya Kiyahudi na hali zilizokuwa zikibadilika. Talmud huonyesha mwelekeo huo katika taarifa ya baadaye iliyosema: “Wataihalifu Sabato moja ili kutakasisha Sabato nyingi.”—Yoma 85b.
Baada ya kifo cha baba yake mzee-mzee, Yuda Makabayo akawa kiongozi asiyepingwa wa uasi huo. Akitambua hakuwa na uwezo wa kumshinda adui wake katika pigano la waziwazi, alibuni mbinu mpya, zinazofanana na namna ya vita vya kisiku-hizi vya kuvizia. Alivishambulia vikosi vya Antioko katika sehemu ambazo havingeweza kutumia njia zao za kawaida za kujikinga. Pigano moja baada ya jingine, Yuda alifanikiwa kuyashinda majeshi mengi zaidi kuliko yale yake.
Wakikabiliwa na ule ushindani wa ndani na mamlaka ya Roma yenye kukua, watawala wa Milki ya Seleukia, walipuuza kuidhinisha sheria ambazo zingewapinga Wayahudi. Hili lilimwezesha Yuda kuzidisha mashambulizi yake hadi kwenye malango ya Yerusalemu. Katika Desemba 165 K.W.K. (au labda 164 K.W.K.), yeye pamoja na vikosi vyake walilitwaa hekalu, wakavitakasa vifaa vyalo, na kulitoa wakfu tena—miaka mitatu kamili baada ya kuchafuliwa kwalo. Wayahudi hukumbuka tukio hili kila mwaka, wakati wa Hanuka, msherehekeo wa kutolewa wakfu.
Siasa Yatangulizwa Zaidi ya Utakatifu
Malengo ya uasi huo yalikuwa yametimizwa. Vizuizi juu ya kuzoea dini ya Kiyahudi vilikuwa vimeondolewa. Ibada na kutoa dhabihu hekaluni kulikuwa kumerudishwa. Wakiwa sasa wametosheka, Wahasidimu waliliacha jeshi la Yuda Makabayo na kurudi makwao nyumbani. Lakini Yuda alikuwa na mawazo mengine. Yeye alikuwa na jeshi lililozoezwa vizuri, basi mbona asilitumie kusimamisha taifa huru la Kiyahudi? Vichocheo vya kisiasa sasa vilichukua mahali pa zile sababu za kidini ambazo zilisababisha uasi. Hivyo mapambano yaliendelea.
Akitafuta kuungwa mkono katika vita vyake dhidi ya utawala wa Seleukia, Yuda Makabayo alifanya mapatano pamoja na Roma. Ijapokuwa aliuawa vitani katika 160 K.W.K., ndugu zake waliendeleza pigano. Yonathani, ndugu yake Yuda aliwashawishi watawala wa Seleukia wakubali kuchaguliwa kwake kuwa kuhani mkuu na mtawala katika Yudea, ingawa alikuwa bado chini ya enzi yao. Yonathani alipodanganywa, akatekwa, na kuuawa kutokana na njama ya Wasiria, ndugu yake Simeoni—wa mwisho kati ya ndugu watano wa Wamakabayo—akachukua uongozi. Chini ya utawala wa Simeoni, masalio ya mwisho ya utawala wa Seleukia yaliondolewa (katika 141 K.W.K.). Simeoni alifanya upya mapatano pamoja na Roma, nao uongozi wa Kiyahudi ukamkubali awe mtawala na kuhani mkuu. Nasaba ya kifalme iliyo huru ya Wahasmonia ilisimamishwa mikononi mwa Wamakabayo.
Wamakabayo walirudisha ibada kwenye hekalu kabla ya kuja kwa Mesiya. (Linganisha Yohana 1:41, 42; 2:13-17.) Lakini, sawa tu na vile imani ya watu katika ukuhani ilivyokuwa imevunjwa na vitendo vya makuhani walioukubali Utamaduni wa Kigiriki, ilitikiswa hata zaidi chini ya Wahasmonia. Kwa kweli, utawala wa makuhani wenye fikira za kisiasa badala ya utawala wa mfalme wa ukoo wa Daudi mwaminifu, haukuwaletea Wayahudi baraka za kweli.—2 Samueli 7:16; Zaburi 89:3, 4, 35, 36.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Matathiasi, baba ya Yuda Makabayo, alisema hivi kwa sauti kubwa: ‘Yeyote yule mwenye juhudi kwa ajili ya Sheria na anifuate’
[Hisani]
Mattathias appealing to the Jewish refugees/The Doré Bible Illustrations/Dover Publications