Nuru Yamalizia Enzi ya Giza
ULIMWENGU wa Yesu Kristo na mitume wake ulikuwa tofauti sana na ule wa nyakati za Maandiko ya Kiebrania. Wasomaji wa Biblia wasiojua hilo waweza kufikiria kwamba kulikuwa na mwendelezo wa kijamii na kidini toka nabii Malaki hadi mwandikaji wa Gospeli Mathayo, wakifikiria kidogo sana juu ya yale yaliyotokea katika ile miaka 400 iliyokuwa kati yao.
Malaki, kitabu cha mwisho cha Maandiko ya Kiebrania katika Biblia nyingi za kisasa, chamalizika mabaki wa Israeli wakiwa wamerudishwa kwao baada ya kufunguliwa kutoka utekwa katika Babiloni. (Yeremia 23:3) Wayahudi wenye kujitoa walitiwa moyo kuingoja siku ya Mungu ya hukumu atakapoondoa uovu ulimwenguni na kuleta Enzi ya Kimesiya. (Malaki 4:1, 2) Wakati uo huo, Uajemi ilitawala. Majeshi ya Uajemi yaliyokuwa Yuda yalidumisha amani na kutekeleza amri za kifalme kwa nguvu za kijeshi.—Linganisha Ezra 4:23.
Hata hivyo, mabara ya Biblia yalibadilika-badilika katika zile karne zote nne zilizofuata. Giza la kiroho na mvurugo ulianza kuingia. Mashariki ya Karibu ilijawa sana na jeuri, uharamia, udhalimu, mawazo ya kidini ya kishupavu, falsafa ya dhana, na mvurugo wa kitamaduni.
Mathayo, kitabu cha kwanza cha Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, kiliandikwa katika kipindi tofauti. Majeshi ya Roma yalitekeleza ile Pax Romana, au Amani ya Roma. Watu wenye kumwogopa Mungu walingojea kwa hamu kuja kwa Mesiya kuondoa mateseko, udhalimu, na umaskini, na kuangaza nuru katika maisha, ufanisi, na utulivu. (Linganisha Luka 1:67-79; 24:21; 2 Timotheo 1:10.) Ebu tuchunguze kwa ukaribu zaidi kani zenye nguvu zilizounda upya jamii ya Kiyahudi katika karne zilizotangulia kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Maisha ya Kiyahudi Katika Nyakati za Kiajemi
Kufuatia tangazo la Sairasi lililowafungua Wayahudi kutoka utekwa wa Kibabiloni katika 537 K.W.K., kikundi cha Wayahudi na washiriki wao Wasio Wayahudi kiliondoka Babilonia. Mabaki hao walioitikia kiroho walirudi katika eneo la majiji yaliyoharibiwa na bara lililofanywa ukiwa. Waedomu, Wafoinike, Wasamaria, makabila ya Kiarabu, na wengineo walikuwa wamepunguza eneo la Israeli ambalo wakati mmoja lilikuwa kubwa. Kile kilichosalia kutoka Yuda na Benjamini kilikuja kuwa mkoa wa Yuda katika jimbo la Uajemi lililoitwa Abar Nahara (Ng’ambo ya Mto).—Ezra 1:1-4; 2:64, 65.
Chini ya utawala wa Uajemi, Yuda ikaanza kupata “kipindi cha mpanuko na ukuzi wa idadi ya watu,” chasema The Cambridge History of Judaism. Chaendelea kusema hivi kuhusu Yerusalemu: “Wakulima na wapilgrimu walileta zawadi, Hekalu na jiji likawa tajiri, na utajiri walo ukavutia wafanyabiashara na mafundi.” Ingawa Waajemi waliruhusu sana serikali na dini ya hapo kufanya mambo, kodi ilikuwa kali sana na ilikuwa ilipwe kwa madini yenye thamani pekee.—Linganisha Nehemia 5:1-5, 15; 9:36, 37; 13:15, 16, 20.
Miaka ya mwisho ya Milki ya Uajemi ilikuwa nyakati zenye msukosuko sana, ikiwa na maasi ya maliwali. Wayahudi wengi walijihusisha katika uasi mmoja kwenye Pwani ya Mediterania nao walihamishwa mbali kaskazini, kwenda Hyrcania kwenye Bahari ya Kaspiani. Hata hivyo, sehemu kubwa zaidi ya Yuda inaonekana haikuathiriwa na adhabu ya Uajemi.
Enzi ya Kigiriki
Aleksanda Mkubwa aliirukia Mashariki ya Kati kama chui katika 332 K.W.K., lakini upendezi wa bidhaa za Kigiriki zilizoingizwa humo tayari ulimtangulia. (Danieli 7:6) Akitambua kwamba utamaduni wa Kigiriki ulikuwa na thamani ya kisiasa, alianza kugeuza mambo kimakusudi ili yafuate utamaduni wa Kigiriki katika milki yake iliyokuwa ikipanuka. Kigiriki kikawa lugha ya kimataifa. Utawala wa muda mfupi wa Aleksanda uliendeleza upendo wa mabishano, kupenda michezo sana, na uthamini wa umaridadi. Hatua kwa hatua, hata utamaduni wa Kiyahudi ukashindwa na utamaduni wa Kigiriki.
Baada ya kifo cha Aleksanda katika 323 K.W.K., waandamizi wake katika Siria na Misri walikuwa wa kwanza kutimiza mafungu ambayo nabii Danieli aliyaita “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini.” (Danieli 11:1-19) Wakati wa utawala wa “mfalme wa kusini,” wa Misri, Tolemi 2 Filadelfa (285-246 K.W.K.), Maandiko ya Kiebrania yalianza kutafsiriwa katika Kikoine, Kigiriki cha kawaida. Tafsiri hiyo ikaja kuitwa Septuagint. Mistari mingi ya kitabu hicho ilinukuliwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Lugha ya Kigiriki ikawa bora sana katika kuwasilisha tofauti ndogo-ndogo za maana zenye kuelimisha katika ulimwengu huo wenye kuvurugika uliokuwa gizani.
Baada ya Antioka 4 Epifane kuwa mfalme wa Siria na vilevile mtawala wa Palestina (175-164 K.W.K.), Dini ya Kiyahudi karibu iangamizwe kabisa na mnyanyaso uliodhaminiwa na serikali. Wayahudi walilazimishwa, wakitishwa kwa kifo, kumkana Yehova Mungu na kutoa dhabihu kwa miungu ya Kigiriki pekee. Mnamo Desemba 168 K.W.K., madhabahu ya kipagani ilijengwa juu ya madhabahu kuu ya Yehova kwenye hekalu la Yerusalemu, na dhabihu zilitolewa juu yayo kwa Zeo wa Olimpia. Watu waliopigwa na butaa lakini wenye moyo mkuu wa sehemu za mashambani walijiunga pamoja chini ya uongozi wa Yudasi Makabayo na kupigana vikali mpaka wakauteka Yerusalemu. Hilo hekalu liliwekwa wakfu tena kwa Mungu, na miaka mitatu kamili baada ya kuchafuliwa, dhabihu za kila siku zilianza kutolewa.
Katika kipindi kilichobaki cha enzi ya Kigiriki, wale wa jumuiya ya Yudea walitafuta kwa nguvu kupanua eneo lao lifikie mipaka yalo ya zamani. Nguvu zao mpya za kijeshi zilitumiwa kwa njia isiyo ya kimungu kwa kuwalazimisha majirani wao wapagani wageuzwe imani au wauawe. Lakini, bado nadharia ya kisiasa ya Kigiriki iliendelea kutawala majiji na miji.
Katika wakati huu, wagombea ukuhani wa cheo cha juu mara nyingi walikuwa wafisadi. Hila, mauaji, na ujanja wa kisiasa ulichafua mamlaka yao. Kadiri roho miongoni mwa Wayahudi ilivyozidi kuwa isiyo ya kimungu, ndivyo michezo ya Kigiriki ilivyozidi kupendwa. Ilishangaza kama nini kuona makuhani wachanga wakiacha kazi zao ili kushiriki katika michezo! Wanariadha wa Kiyahudi hata walikubali hali ya uchungu mno ya kurudishiwa ngovi wawe ‘wasiotahiri’ ili wasione aibu waliposhindana wakiwa uchi pamoja na Wasio Wayahudi.—Linganisha 1 Wakorintho 7:18.
Mabadiliko ya Kidini
Katika miaka ya mapema ya baada ya kutoka uhamishoni, Wayahudi waaminifu walikinza kuchanganywa kwa mawazo na falsafa za kipagani na dini ya kweli iliyofunuliwa katika Maandiko ya Kiebrania. Kitabu cha Esta, kilichoandikwa baada ya zaidi ya miaka 60 ya ushirikiano wa karibu pamoja na Uajemi, hakina dalili yoyote ya Uzoroastria. Isitoshe, hakuna uvutano wa dini hii ya Kiajemi upatikanao katika vitabu vya Ezra, Nehemia, au Malaki, vyote vikiwa viliandikwa mapema katika enzi ya Kiajemi (537-443 K.W.K.).
Hata hivyo, wasomi huamini kwamba katika sehemu ya mwisho ya enzi ya Kiajemi, Wayahudi wengi walianza kukubali baadhi ya maoni ya waabudu wa Ahura Mazda, mungu mkuu wa Waajemi. Hilo laonwa katika ushirikina wenye kupendwa na itikadi za Waesene. Maneno ya kawaida ya Kiebrania ya mbweha, viumbe vingine vya jangwa, na ndege wa usiku yakaja kushirikishwa katika akili za Kiyahudi na roho waovu na madubwana wa usiku wa hadithi za Kibabiloni na Kiajemi.
Wayahudi walianza kuyaona mawazo ya kipagani kwa njia tofauti. Mawazo ya mbingu, helo, nafsi, Neno (Logos), na hekima, yote yakawa na maana tofauti. Na ikiwa, kama ilivyofundishwa wakati huo, Mungu alikuwa mbali sana hivi kwamba hakuwasiliana na watu tena, yeye alihitaji wapatanishi. Wagiriki waliita roho hao wa upatanishi na utunzi daimoni. Baada ya kukubali wazo la kwamba daimoni (roho waovu) wangeweza kuwa wazuri au waovu, Wayahudi wakawa rahisi kudhibitiwa na roho waovu.
Badiliko zuri lilihusu ibada ya sehemu walizokuwako. Masinagogi yalitokea haraka-haraka yakawa sehemu za Wayahudi waliokuwa karibu za kukutania kwa ajili ya elimu na utumishi wa kidini. Haijulikani hasa ni lini, wapi na jinsi masinagogi ya Kiyahudi yalivyoanza. Kwa kuwa yalitimiza mahitaji ya Wayahudi ya ibada katika mabara ya mbali wakati hawangeweza kwenda hekaluni, yaaminiwa kwa ujumla ya kwamba masinagogi yalianzishwa katika nyakati za uhamishoni au baada ya uhamisho. Kwa njia ya maana, hayo yakawa sehemu nzuri kwa Yesu na mitume wake ‘kuzitangaza fadhili za Mungu, aliyewaita watu watoke gizani wakaingie katika nuru yake ya ajabu.’—1 Petro 2:9.
Dini ya Kiyahudi Ilikubali Mawazo Mbalimbali
Katika karne ya pili K.W.K., mawazo mbalimbali yalianza kutokea. Hayo hayakuwa matengenezo tofauti ya kidini. Badala ya hivyo, hayo yalikuwa mashirika madogo-madogo ya makuhani wa Kiyahudi, wanafalsafa, na wanasiasa waliotafuta kuvutia watu na kudhibiti taifa, wote wakiwa chini ya Dini ya Kiyahudi.
Masadukayo wenye kupenda siasa walikuwa hasa matajiri wa tabaka la juu, waliojulikana kwa werevu wao mwingi tangu uasi wa Hasmonia katikati ya karne ya pili K.W.K. Wengi wao walikuwa makuhani, ingawa wengine walikuwa wafanyabiashara na wamilikaji wa mashamba. Kufikia wakati Yesu alipozaliwa, Masadukayo wengi walipendelea utawala wa Waroma juu ya Palestina kwa sababu walifikiri huo ulikuwa thabiti zaidi na ulielekea kudumisha hali iyo hiyo ya mambo. (Linganisha Yohana 11:47, 48.) Wachache (Waherode) waliamini kwamba utawala wa familia ya Herode ungependelewa taifani. Kwa vyovyote vile, Masadukayo hawakutaka taifa hilo liongozwe na washupavu wa Kiyahudi au mtu yeyote ila makuhani wenye kudhibiti hekalu. Itikadi za Kisadukayo zilikuwa za kidesturi, zikitegemea hasa fasiri yao ya maandishi ya Musa, nazo zilionyesha upinzani wao kwa farakano lenye nguvu la Mafarisayo. (Matendo 23:6-8) Masadukayo walikataa unabii wa Maandiko ya Kiebrania wakiuona kuwa ni dhana. Wao walifundisha kwamba vitabu vya Biblia vya kihistoria, kishairi, na vya methali havikupuliziwa na si muhimu.
Mafarisayo waliibuka wakati wa enzi ya Kigiriki kwa kupinga vikali utamaduni wa Kigiriki wenye kupinga mambo ya Kiyahudi. Hata hivyo, kufikia siku ya Yesu, walikuwa wageuza watu imani na walimu wasiobadilikana, wenye kushika mapokeo sana, wenye kufuata sheria sana, na wenye kiburi, waliojaribu kudhibiti hilo taifa kupitia mafundisho ya sinagogi. Wao walitokana hasa na jamii ya tabaka ya kati nao waliwadharau watu wa kawaida. Yesu aliwaona Mafarisayo wengi kuwa wapenda pesa wenye ubinafsi na wakatili waliojaa unafiki. (Mathayo, sura 23) Wao walikubali Maandiko ya Kiebrania yote kulingana na maelezo yao wenyewe lakini wakayapa mapokeo yao ya mdomo uzito kama huo au kuyazidi. Walisema kwamba mapokeo yao yalikuwa “ua kuizingira Sheria.” Hata hivyo, badala ya kuwa ua, mapokeo yao yalitangua Neno la Mungu na kufadhaisha umma.—Mathayo 23:2-4; Marko 7:1, 9-13.
Waesene walikuwa waamini-mafumbo ambao yaonekana waliishi katika jumuiya chache zilizotawanyika. Walijiona kuwa mabaki wa kweli wa Israeli, wakingoja kwa utakato kumpokea Mesiya aliyeahidiwa. Waesene waliishi maisha ya utafakari ya kumcha Mungu na bila anasa na itikadi zao nyingi zilikuwa na mawazo ya Kiajemi na Kigiriki.
Wazalendo wenye bidii sana wa aina mbalimbali waliochochewa kidini na wenye ushupavu waliona mtu yeyote aliyejiingiza katika mambo ya utaifa wa Kiyahudi kuwa adui mkubwa wa kuuawa. Wao wamefananishwa na Wahasmonia nao walivutia hasa vijana wenye kutafuta msisimko na wenye kutaka mambo yafanywe kikamili. Wakionwa kuwa wauaji-magaidi au wapiganiaji ukombozi, wao walitumia mbinu za kuvizia ambazo zilifanya barabara za mashambani na sehemu za umma kuwa hatari na kuongezea wasiwasi uliokuwapo wakati huo.
Katika Misri, falsafa za Kigiriki zilisitawi miongoni mwa Wayahudi wa Aleksandria. Toka huko zikaenea Palestina na kwa Wayahudi waliotawanyika sana wa Diaspora. Wananadharia wa Kiyahudi walioandika Apokrifa na vitabu vingine visivyopuliziwa waliyaona maandishi ya Musa kuwa yasiyo wazi, na yenye mafumbo yasiyosisimua.
Kufikia wakati enzi ya Kiroma ilipofika, utamaduni wa Kigiriki ulikuwa umebadilisha Palestina kijamii, kisiasa na kifalsafa kwa njia ya kudumu. Dini ya Kibiblia ya Wayahudi ilikuwa imebadilishwa na Dini ya Kiyahudi, iliyokuwa mchanganyiko wa mawazo ya Kibabiloni, Kiajemi, na Kigiriki yaliyochanganyishwa kwa kadiri fulani na kweli ya Kimaandiko. Hata hivyo, Masadukayo, Mafarisayo, na Waesene walifanyiza chini ya asilimia 7 ya idadi ya taifa. Hapo katikati ya kani hizo zenye kupingana palikuwa umati mwingi wa watu wa Kiyahudi, waliokuwa “wamechunwa ngozi na kutupwa huku na huku kama kondoo wasio na mchungaji.”—Mathayo 9:36, NW.
Katika ulimwengu huo wenye giza akaingia Yesu Kristo. Mwaliko wake wenye kutoa uhakikisho ulifariji: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” (Mathayo 11:28) Ni jambo la kusisimua kama nini kumsikia akisema: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu”! (Yohana 8:12) Na ahadi yake yenye kuchangamsha moyo ilifurahisha kwelikweli: “Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”—Yohana 8:12.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Yesu alionyesha kwamba viongozi wa kidini wa Kiyahudi walikuwa katika giza la kiroho
[Picha katika ukurasa wa 28]
Sarafu yenye picha ya Antioka 4 (Epifane)
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.