Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 10/15 kur. 4-7
  • Jitihada ya Kuishi Muda Mrefu Zaidi Yaweza Kufanikiwaje?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jitihada ya Kuishi Muda Mrefu Zaidi Yaweza Kufanikiwaje?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matibabu ya Homoni na Elimu ya Chembe za Urithi—Je, Ni Sababu za Kuwa na Tumaini?
  • Je, Nanotechnology na Cryonics Zatokeza Suluhisho?
  • Twapaswa Kuweka Tumaini Letu Wapi?
  • Sababu Kuu Inayofanya Tuzeeke na Kufa
  • Tumaini la Kweli
  • Uhai Udumuo Milele Katika Dunia Paradiso
  • Kutafuta Chembe ya Urithi “Isiyokufa”
    Amkeni!—2000
  • Kwa Nini Sisi Huzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Jitihada za Kurefusha Maisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu Wote)—2019
  • Kwa Nini Tunazeeka na Kufa?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 10/15 kur. 4-7

Jitihada ya Kuishi Muda Mrefu Zaidi Yaweza Kufanikiwaje?

WATU wengine hutumaini kwamba katika milenia mpya mwanadamu atafanikiwa katika jitihada zake za kurefusha maisha. Dakt. Ronald Klatz ni mmoja wao. Yeye ni msimamizi wa shirika liitwalo American Academy of Anti-Aging Medicine, la matabibu na wanasayansi ambao wamejitolea kurefusha muda wa kuishi wa mwanadamu. Yeye na wenzake wanaazimia kuishi kwa muda mrefu zaidi. “Ninatarajia kuishi kwa angalau miaka 130,” asema Dakt. Klatz. “Tunaamini kwamba kuzeeka si jambo lisiloepukika. Sasa kuna tekinolojia iwezayo kupunguza, kukomesha na labda hata kutangua sana kudhoofika kimwili na maradhi ambayo sasa huitwa kuzeeka kwa kawaida.” Dakt. Klatz mwenyewe humeza vidonge 60 vya dawa kila siku katika jitihada za kurefusha maisha yake.

Matibabu ya Homoni na Elimu ya Chembe za Urithi—Je, Ni Sababu za Kuwa na Tumaini?

Matibabu ya kutumia homoni ni uwanja mmoja wa kitaaluma unaoleta matumaini. Majaribio ya kutumia homoni iitwayo DHEA huonekana kupunguza kuzeeka katika wanyama wa maabara.

Kuhusu homoni ya mimea iitwayo kinetin, gazeti la Sweden Aftonbladet lilimnukuu Dakt. Suresh Rattan, ambaye ni profesa katika Chuo Kikuu cha Aarhus, Denmark, akisema: “Majaribio tunayofanya kwenye maabara yanaonyesha kwamba chembe za ngozi ya mwanadamu zilizokuzwa ndani ya kinetin hazigeuki katika njia ile ya kawaida ambayo chembe hugeuka mtu anapozeeka. Chembe hizo hubaki zikiwa changa muda wote wa maisha yake.” Yasemekana kwamba muda wa kuishi wa wadudu waliotiwa homoni hiyo hurefushwa kwa asilimia 30 hadi 45.

Inasemekana kuwa matibabu ya kutumia homoni iitwayo melatonin yamerefusha muda wa kuishi wa panya kwa asilimia 25. Isitoshe, panya hao walionekana wachanga zaidi, wenye afya zaidi, na wenye nguvu zaidi.

Wale wanaotetea homoni ya ukuzi wa binadamu (hGH) hudai kwamba homoni hiyo hufanya mtu awe na ngozi nzuri, misuli mikubwa, hamu nyingi ya kufanya ngono, furaha zaidi, akili zaidi, na utendaji wa kemikali mwilini unakuwa kama wa kijana.

Wengi pia hutumainia elimu ya chembe za urithi. Wanasayansi wamefikia mkataa kwamba wakitumia chembe za urithi kwa ustadi, wanaweza kudhibiti muda wa kuishi wa minyoo. Kwa kweli, wamefanikiwa kurefusha mara sita muda wa kawaida wa kuishi wa baadhi ya minyoo. Jambo hilo limezusha matumaini ya kupata na kutumia kwa ustadi chembe kama hizo za urithi katika wanadamu. Gazeti la Time lilimnukuu Dakt. Siegfried Hekimi wa Chuo Kikuu cha McGill, Montreal, akisema: “Tukipata chembe zote za urithi ambazo huhusika na muda wa kuishi wa mwanadamu, labda tunaweza kupunguza utendaji wake kidogo tu, ili tuweze kurefusha maisha.”

Wanabiolojia wamejua kwa muda mrefu kwamba urefu wa sehemu ya mwisho ya chembeuzi, ile iitwayo telomere, hupungua kila wakati chembe inapojigawanya. Wakati telomere inapopoteza asilimia 20 ya urefu wake, uwezo wa chembe wa kujigawanya hukoma nayo hufa. Kimeng’enya maalum kiitwacho telomerase kinaweza kurudisha urefu kamili wa telomere hiyo, hivyo kikiiwezesha chembe hiyo kuendelea kujigawanya. Katika chembe nyingi, kimeng’enya hiki huzuiwa na hakitendi, lakini telomerase tendaji imeingizwa kwa mafanikio ndani ya chembe fulani, ikizifanya zikue na kujigawanya kwa wingi sana kuliko ilivyo kawaida.

Kwa mujibu wa watafiti, hilo hutokeza fursa zenye kusisimua za kupambana na maradhi yanayohusiana na kuzeeka. Namna gani kubadilisha chembe za mwili zinazofanyiza upya tishu ya mwili kwa chembe nyingine za aina hiyo ambazo zimepewa uwezo wa “kutoweza kufa” kwa kutumia telomerase tendaji? Dakt. William A. Haseltine asema: “Hilo ni wazo lililo wazi kabisa kuhusu hali ya kutoweza kufa kwa mwanadamu litakaloendelea kutumika polepole katika miaka 50 ijayo.”—The New York Times.

Je, Nanotechnology na Cryonics Zatokeza Suluhisho?

Mbinu ya nanotechnology, utaalamu wa sayansi unaohusu vitu vidogo sana (vinavyotoshana na sehemu moja kwa bilioni moja ya meta), pia inatoa matumaini. Wataalamu wa mambo hayo wanadai kwamba mashine ndogo sana zenye kompyuta, zilizo ndogo zaidi ya chembe, huenda zikabuniwa wakati ujao ili kufanya kazi ndani ya molekuli kwa kusudi la kurekebisha na kufanyiza upya chembe, tishu, na viungo vinavyozeeka. Kwenye kongamano moja la watu wanaopambana na hali ya kuzeeka, mtafiti mmoja alidokeza kwamba huenda matabibu wa karne ya 21 wakatumia mbinu ya nanotechnology kumfanya mwanadamu asiweze kufa.

Nayo mbinu ya cryonics ni utaratibu wa kugandisha miili ya wanadamu kwa matumaini kwamba sayansi itaweza kuzihuisha chembe zilizokufa, hivyo kuzirudisha kwenye uhai tena. Mwili wote, au ubongo pekee, unaweza kugandishwa. Mtu mmoja hata alitaka shuka ya kitanda igandishwe. Kwa nini shuka igandishwe? Hiyo shuka ilikuwa ya rafiki aliyepotea na ilikuwa na chembe za ngozi na nywele chache. Alitaka zigandishwe ili kumpa rafiki yake fursa ya kuishi tena ikiwa sayansi itafikia hatua ya kuunda watu upya kutokana na chembe kadhaa au hata chembe moja.

Twapaswa Kuweka Tumaini Letu Wapi?

Mwanadamu ana tamaa ya asili ya kuishi wala si kufa. Hivyo, maendeleo ya kisayansi katika nyanja hizo hushangiliwa kwa moyo nayo huambatana na matumaini makubwa. Lakini, kufikia sasa hakuna uthibitisho kamili kwamba DHEA, kinetin, melatonin, hGH, au kitu kinginecho ambacho kinaweza kwa kweli kuzuia kuzeeka kwa wanadamu. Wanaotilia shaka huhofu kwamba kutumia telomerase katika chembe kutatokeza tu chembe ziwezazo kusababisha kansa. Nayo matumizi ya nanotechnology na cryonics ungali ni kama ubuni tu wa sayansi wala si mambo halisi.

Sayansi imesaidia, na bado yaweza kusaidia, wengine waishi muda mrefu zaidi na kuwa na afya nzuri zaidi, lakini haitaweza kamwe kumpa yeyote uhai wa milele. Kwa nini? Kwa wazi, sayansi ya kibinadamu haiwezi kabisa kueleza sababu kuu inayofanya tuzeeke na kufa.

Sababu Kuu Inayofanya Tuzeeke na Kufa

Wanasayansi wengi hukubali kwamba kuzeeka na kifo zaonekana kana kwamba zimewekwa kwa utaratibu fulani katika chembe zetu za urithi. Swali ni: Ni lini, jinsi gani, na kwa nini ziliingia katika kanuni zinazoongoza chembe zetu za urithi?

Biblia hutupa jibu sahili—ijapokuwa jibu hilo halitaji mambo ya chembe za urithi au DNA. Andiko la Waroma 5:12 lasema: “Hiyo ndiyo sababu, kama vile kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi.”

Mwanadamu wa kwanza, Adamu, alikuwa na matazamio ya kuishi milele. Mwili wake ulibuniwa ukiwa na uwezo uliohitajika ili kuishi na kufurahia uhai wa milele. Hata hivyo, uhai wa milele ulikuwa na masharti. Ilikuwa lazima Adamu atii na kushirikiana na Muumba wake, aliye Chanzo cha uhai, ili aishi daima dawamu.—Mwanzo 1:31; 2:15-17.

Adamu alichagua kutomtii Muumba. Ni kama Adamu alidai kwamba hali ya mwanadamu ni bora anapojitawala bila kumtegemea Mungu. Hivyo akafanya dhambi. Tangu wakati huo, hali ilikuwa kana kwamba kanuni zinazoongoza chembe zake za urithi zilibadilishwa. Badala ya kuwarithisha wazao wake uhai udumuo milele, Adamu aliwarithisha dhambi na kifo.—Mwanzo 3:6, 19; Waroma 6:23.

Tumaini la Kweli

Hata hivyo, hali hiyo haikukusudiwa idumu. Andiko la Waroma 8:20 lasema: “Viumbe vilitiishwa chini ya ubatili, si kwa mapenzi yavyo vyenyewe bali kupitia yeye aliyevitiisha hivyo, juu ya msingi wa tumaini.” Muumba wa mwanadamu, Yehova Mungu, aliwatiisha wanadamu chini ya kifo kwa sababu walifanya dhambi dhidi yake, lakini alipofanya hivyo, aliweka pia msingi wa tumaini.

Msingi huo ukajulikana kabisa Yesu Kristo alipokuja duniani. Andiko la Yohana 3:16 lasema: “Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu sana hivi kwamba akatoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele.” Lakini, kudhihirisha imani katika Yesu Kristo kwaweza kutuokoaje na kifo?

Ikiwa dhambi ndiyo husababisha kifo, basi ni lazima dhambi iondolewe kabla kifo hakijaondolewa. Mapema katika huduma ya Yesu akiwa Kristo, Yohana Mbatizaji alisema hivi: “Ona, Mwana-Kondoo wa Mungu ambaye huondolea mbali dhambi ya ulimwengu!” (Yohana 1:29) Yesu Kristo hakuwa na dhambi yoyote. Hivyo, hangepatwa na kifo, ambacho ndicho adhabu ya dhambi. Hata hivyo, aliruhusu wengine wamwue. Kwa nini? Kwa sababu kwa kufanya hivyo, alitoa bei iliyohitajiwa kwa ajili ya dhambi zetu.—Mathayo 20:28; 1 Petro 3:18.

Bei hiyo ikiwa imetolewa, iliwezekana kwa wote wanaodhihirisha imani katika Yesu waishi milele. Sayansi inaweza kusaidia kurefusha maisha yetu kwa kiasi kidogo sana, lakini kudhihirisha imani katika Yesu ndiyo njia hasa iongozayo kwenye uhai udumuo milele. Yesu alipata uhai huo mbinguni, nao mitume wake waaminifu na wengineo wataupata pia. Hata hivyo, kwa wengi wetu wanaodhihirisha imani katika Yesu, uhai udumuo milele utakuwa duniani, wakati Yehova Mungu atakaporudisha Paradiso ya kidunia.—Isaya 25:8; 1 Wakorintho 15:48, 49; 2 Wakorintho 5:1.

Uhai Udumuo Milele Katika Dunia Paradiso

Mtu mmoja aliuliza: “Ni watu wangapi watakaoona inafaa kuishi bila kulazimika kufa?” Je, kuishi bila kifo kutachosha? Biblia hutuhakikishia kwamba hakutachosha. “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.” (Mhubiri 3:11) Uumbaji wa Yehova Mungu ni mwingi na tata sana hivi kwamba utaendelea kutuvutia, kutuchochea, na kutufurahisha kwa muda ule tutakaoishi—hata milele.

Mtu mmoja aliyechunguza ndege aitwaye Siberian Jay alimtaja kuwa “[ndege] mwenye kupendeza asiye wa kawaida” na kudai kwamba kumchunguza ndege huyo kulikuwa mojawapo ya mambo yenye kufurahisha zaidi maishani mwake. Kadiri alivyozidi kumchunguza ndege huyo ndivyo alivyozidi kuvutiwa naye. Alisema kwamba hata baada ya miaka 18, uchunguzi wake hata haukuwa umekaribia kumalizika. Ikiwa aina moja ya ndege yaweza kuvutia, kuchochea, na kuendelea kumfanya mtu mwenye akili awe na furaha wakati wa miaka 18 ya uchunguzi wake wa makini, ebu wazia furaha na uradhi tuwezao kupata kwa kuchunguza uumbaji wote wa kidunia.

Ebu wazia nyanja za kisayansi zenye kupendeza ambazo zitapatikana kwa mtu asiyezuiwa na wakati. Ebu wazia sehemu zote zenye kupendeza za kutalii na pia watu wote wenye kupendeza tutakaokutana nao. Jaribu kufikiria fursa nyingi sana za kuwaza, kubuni na kutengeneza vitu. Tutakuwa na fursa nyingi sana za kusitawisha na kutumia uwezo wetu wa kubuni. Tufikiriapo wingi wa vitu vilivyoumbwa, ni wazi kwamba umilele ndio muda unaotosha kuzitumia kikamili fursa za maishani.

Biblia yaonyesha kwamba kupitia ufufuo, wafu pia wataishi milele. (Yohana 5:28, 29) Huenda mambo mengi ya historia yasiyo dhahiri yakawa wazi wakati ambapo wale waliohusika wataweza kutoa habari zote na kujibu maswali yetu. Ebu wazia jinsi wale wenye kufufuliwa watakavyoeleza kwa undani juu ya vipindi mbalimbali vya historia.—Matendo 24:15.

Unapotafakari kuhusu wakati huo, unaweza kutambua kwamba huenda Yobu mwenye kufufuliwa atataka kurekebisha maneno yapatikanayo kwenye andiko la Ayubu 14:1. Badala ya maneno hayo labda atadokeza: ‘Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, sasa huishi milele naye hujaa uradhi.’

Kwa wale wamtumainio Yehova na kudhihirisha imani katika Yesu, kurefusha maisha milele si ndoto tu. Karibuni jambo hilo litatukia hakika. Kuzeeka na kifo zitakoma. Hilo lapatana na andiko la Zaburi 68:20, lisemalo: “Njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.”—Ufunuo 21:3, 4.

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Maendeleo ambayo sayansi imefanya yameleta matumaini kuhusu uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu zaidi

[Picha katika ukurasa wa 7]

Umilele ndio muda unaotosha kuzitumia kikamili fursa za maisha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki