Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 11/1 kur. 28-29
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Kusalimu Bendera, Kupiga Kura, na Utumishi wa Kiraia
    “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu”
  • Kwa Nini Mashahidi wa Yehova Hawajihusishi na Siasa?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
  • “Wao Si Sehemu ya Ulimwengu”
    Mwabudu Mungu wa Pekee wa Kweli
  • Usitawi wa Muundo wa Tengenezo
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 11/1 kur. 28-29

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Mashahidi wa Yehova huonaje kupiga kura?

Kuna kanuni ambazo zimetajwa wazi katika Biblia zinazowawezesha watumishi wa Mungu wawe na maoni yanayofaa juu ya suala hili. Lakini, inaonekana hakuna kanuni inayopinga tendo lenyewe la kupiga kura. Kwa mfano, hakuna sababu inayozuia baraza la wakurugenzi wasipige kura ili kufikia maamuzi yanayohusu shirika lao. Mara nyingi makutaniko ya Mashahidi wa Yehova hufanya maamuzi kuhusu saa za mikutano na matumizi ya fedha za kutaniko kwa kupiga kura kwa njia ya kuinua mikono.

Lakini, namna gani kupiga kura katika uchaguzi wa kisiasa? Bila shaka, katika nchi fulani za kidemokrasia, asilimia 50 hivi ya watu hawaendi kupiga kura kwenye siku ya uchaguzi. Mashahidi wa Yehova hawaingilii haki za wengine za kupiga kura; wala hawafanyi kampeni yoyote ile ya kupinga uchaguzi wa kisiasa. Wao hustahi na kushirikiana na wenye mamlaka ambao wamechaguliwa katika uchaguzi kama huo. (Waroma 13:1-7) Kuhusu suala la kama wao wakiwa mmoja-mmoja watampigia kura mtu fulani anayegombea kiti katika uchaguzi, kila mmoja wa Mashahidi wa Yehova hufanya uamuzi unaotegemea dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia na uelewevu wake wa wajibu wake kwa Mungu na Taifa. (Mathayo 22:21; 1 Petro 3:16) Wanapofanya uamuzi huo wa kibinafsi, Mashahidi hufikiria mambo kadhaa.

Kwanza, Yesu Kristo alisema yafuatayo kuhusu wafuasi wake: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile mimi si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:14) Mashahidi wa Yehova huchukua kanuni hii kwa uzito. Kwa kuwa “wao si sehemu ya ulimwengu,” hawahusiki na masuala ya kisiasa ya ulimwengu.—Yohana 18:36.

Pili, mtume Paulo alijirejezea kuwa “balozi” anayemwakilisha Kristo kwa watu wa siku zake. (Waefeso 6:20; 2 Wakorintho 5:20) Mashahidi wa Yehova huamini kwamba Kristo Yesu sasa ametawazwa kuwa Mfalme wa Ufalme wa kimbingu wa Mungu, na wao, kama ilivyo na mabalozi, ni lazima watangaze jambo hilo kwa mataifa. (Mathayo 24:14; Ufunuo 11:15) Mabalozi hutazamiwa kuwa watu ambao hudumisha kutokuwamo na kuepuka kuingilia masuala ya ndani ya nchi walizotumwa. Wakiwa wawakilishi wa Ufalme wa kimbingu wa Mungu, Mashahidi wa Yehova huhisi kwamba wana wajibu kama huo wa kutoingilia masuala ya siasa ya nchi wanamoishi.

Jambo la tatu la kufikiria ni kwamba wale wanaoshiriki kumpigia mtu kura ili apate kiti huenda wakawajibika kwa matendo ya mtu huyo. (Linganisha 1 Timotheo 5:22, The New English Bible.) Ni lazima Wakristo wafikirie kwa makini kama wanataka kujitwika wajibu huo.

Jambo la nne ni kwamba Mashahidi wa Yehova huthamini sana muungano wao wa Kikristo. (Wakolosai 3:14) Dini zinapoingilia siasa, mara nyingi mgawanyiko hutokea baina ya waumini wake. Kwa kumwiga Yesu Kristo, Mashahidi wa Yehova huepuka kuingilia siasa na hivyo kudumisha muungano wao wa Kikristo.—Mathayo 12:25; Yohana 6:15; 18:36, 37.

Jambo la tano na la mwisho, kwa sababu hawaingilii siasa Mashahidi wa Yehova wana uhuru wa usemi wa kuwafikia watu wenye imani mbalimbali za kisiasa wakiwa na ujumbe muhimu wa Ufalme.—Waebrania 10:35.

Kwa sababu ya kanuni hizo za Kimaandiko ambazo zimetajwa, katika nchi nyingi Mashahidi wa Yehova hufanya uamuzi wa kibinafsi wasipige kura katika uchaguzi wa kisiasa, na uhuru wao wa kufanya uamuzi huo unaungwa mkono na sheria za nchi. Lakini namna gani ikiwa sheria inasema ni lazima wananchi wapige kura? Katika hali kama hiyo, kila Shahidi ana wajibu wa kufanya uamuzi unaotegemea dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia kuhusu namna ya kushughulikia hali hiyo. Mtu akiamua kwenda kwenye kituo cha kupigia kura, huo ni uamuzi wake. Kile anachofanya katika kituo cha kupigia kura ni kati yake na Muumba wake.

Toleo la Mnara wa Mlinzi la Novemba 15, 1950 (la Kiingereza), lilisema hivi kwenye ukurasa wa 445 na 446: “Mahali ambapo Kaisari analazimisha raia wapige kura . . . [Mashahidi] wanaweza kwenda kwenye uchaguzi na kuingia katika vituo vya kupigia kura. Hapo ndipo wanapotakikana kutia alama karatasi ya uchaguzi au kuandika msimamo wao. Wapiga kura hufanya jambo watakalo na karatasi zao za uchaguzi. Sasa hapa mbele ya Mungu ndipo mashahidi wake lazima watende kwa kupatana na amri zake na kwa kupatana na imani yao. Si daraka letu kuwaagiza jambo la kufanya na karatasi za uchaguzi.”

Namna gani ikiwa mume asiyeamini wa mke Mkristo anasisitiza kwamba aende kwenye uchaguzi? Yeye yuko chini ya mumewe, kama vile tu Wakristo walivyo chini ya mamlaka zilizo kubwa. (Waefeso 5:22; 1 Petro 2:13-17) Akitii mume wake na kwenda kwenye kituo cha kupigia kura, huo ni uamuzi wake wa kibinafsi. Asishutumiwe na mtu yeyote.—Linganisha Waroma 14:4.

Namna gani nchi ambamo sheria haishurutishi kupiga kura lakini kuna uhasama mkali sana dhidi ya wale ambao hawaendi kwenye kituo cha kupigia kura—labda hata wakiweza kupigwa? Au namna gani ikiwa watu mmoja-mmoja, ingawa kisheria hawawajibiki kupiga kura, wanaadhibiwa vikali kwa njia fulani wasipokwenda kwenye kituo cha kupigia kura? Katika hali hizo na nyingine zinazofanana na hizo, ni lazima Mkristo afanye uamuzi wake mwenyewe. “Kila mmoja atachukua mzigo wake mwenyewe.”—Wagalatia 6:5.

Huenda kuna watu wanaoweza kukwazika wanapoona kwamba wakati wa uchaguzi katika nchi yao, baadhi ya Mashahidi wa Yehova huenda kwenye kituo cha kupigia kura na wengine hawaendi. Wao waweza kusema, ‘Mashahidi wa Yehova hawafanyi mambo kwa upatano.’ Lakini watu wanapaswa kutambua kwamba katika mambo kama haya yanayohusu dhamiri ya mtu binafsi, ni lazima kila Mkristo afanye uamuzi wake mwenyewe mbele ya Yehova Mungu.—Waroma 14:12.

Mashahidi wa Yehova huchunga sana wahifadhi kutokuwamo kwao kwa Kikristo na uhuru wao wa usemi wanapofanya maamuzi yoyote yale ya kibinafsi katika hali tofauti-tofauti. Wao humtegemea Yehova Mungu katika mambo yote ili awaimarishe, awape hekima, na kuwasaidia waepuke kuridhiana imani yao kwa njia yoyote ile. Kwa njia hiyo wao huonyesha uhakika katika maneno ya mtunga-zaburi: “[Wewe] ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.”—Zaburi 31:3.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki