Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w03 1/15 uku. 21
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2022
  • Kula Viapo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Kiapo cha Kale Ambacho Ni Muhimu Leo
    Amkeni!—2004
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
w03 1/15 uku. 21

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Je, inapatana na Maandiko kwa Mkristo kushika Biblia na kuapa kwamba atasema ukweli mtupu mahakamani?

Kila mtu anapaswa kufanya uamuzi wake binafsi kuhusu jambo hilo. (Wagalatia 6:5) Hata hivyo, Biblia haikatazi mtu kuapa ili kusema ukweli mahakamani.

Kuapa ni zoea la zamani ambalo limeenea sana. Kwa mfano, zamani Wagiriki waliapa huku wakiwa wameinua mkono kuelekea mbinguni au wameshika madhabahu. Waroma nao waliapa huku wakiwa wameshika jiwe mkononi na kusema: “[Mungu] Jupiter na anitupe kama ninavyotupa jiwe hili wakati aokoapo jiji na ngome hii, iwapo nitasema uwongo kimakusudi.”—Kichapo Cyclopedia of Biblical, Theological, and Ecclesiastical Literature cha John McClintock na James Strong, Buku la 7, ukurasa wa 260.

Viapo hivyo vilionyesha kwamba mwanadamu anatambua kwamba kuna mungu anayeweza kuchunguza wanadamu na ambaye wanawajibika kwake. Tangu zamani, waabudu wa kweli wa Yehova walitambua kwamba yeye alijua waliyosema na waliyotenda. (Mithali 5:21; 15:3) Waliona kana kwamba wanaapa mbele za Mungu, au mbele zake akiwa Shahidi wao. Kwa mfano, Boazi, Daudi, Solomoni, na Sedekia walifanya hivyo. (Ruthu 3:13; 2 Samweli 3:35; 1 Wafalme 2:23, 24; Yeremia 38:16) Waabudu wa Mungu wa kweli pia waliwaruhusu wengine wawaweke chini ya kiapo. Abrahamu na Yesu Kristo waliwekwa chini ya kiapo.—Mwanzo 21:22-24; Mathayo 26:63, 64.

Wakati mwingine, mtu alitoa ishara fulani alipoapa mbele za Yehova. Abramu (Abrahamu) alimwambia mfalme wa Sodoma hivi: “Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.” (Mwanzo 14:22) Alipokuwa akizungumza na nabii Danieli, malaika mmoja ‘aliinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele.’ (Danieli 12:7) Hata Mungu anatajwa kuwa anainua mkono wake kwa njia ya mfano anapoapa.—Kumbukumbu la Torati 32:40; Isaya 62:8.

Maandiko hayakatazi kuapa. Hata hivyo, si lazima Mkristo aape ili kuthibitisha kila neno analosema. Yesu alisema: “Acheni tu neno lenu Ndiyo limaanishe Ndiyo, La yenu, La.” (Mathayo 5:33-37) Mwanafunzi Yakobo alitaja jambo kama hilo. Aliposema “komeni kuapa,” alikuwa akionya juu ya kuapa kuhusu mambo madogo-madogo. (Yakobo 5:12) Yesu na Yakobo hawakusema kwamba ni makosa kuapa kusema ukweli mahakamani.

Namna gani basi ikiwa Mkristo atahitajika kuapa mahakamani kwamba ushahidi wake ni wa kweli? Huenda akaona kwamba anaweza kuapa. La sivyo, anaweza kuruhusiwa atangaze rasmi kwamba hatasema uwongo.—Wagalatia 1:20.

Iwapo utaratibu wa mahakama unahusisha kuinua mkono au kushika Biblia wakati wa kuapa, basi Mkristo anaweza kuamua kufanya hivyo. Huenda akakumbuka mifano fulani ya Biblia ambapo kuapa kuliambatana na ishara fulani. Kwa Mkristo, jambo lililo muhimu zaidi ya kufanya ishara fulani wakati wa kuapa, ni kukumbuka kwamba anaapa mbele za Mungu ili kusema ukweli. Kiapo hicho ni jambo zito. Iwapo Mkristo anahisi kwamba anaweza na anapaswa kujibu swali analoulizwa baada ya kuapa, basi anapaswa kukumbuka kwamba aliapa kusema ukweli, ambao hapana shaka Mkristo angependa kuusema nyakati zote.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki