Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w13 6/1 kur. 3-4
  • Ubaguzi Tatizo la Ulimwenguni Pote

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ubaguzi Tatizo la Ulimwenguni Pote
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • TATIZO LA KIBANAFSI
  • Ubaguzi Utakwisha Lini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Ubaguzi—Je, Umekuathiri?
    Amkeni!—2020
  • Je, Wewe ni Mhasiriwa wa Ubaguzi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Mwisho wa Ubaguzi
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
w13 6/1 kur. 3-4
[Picha katika ukurasa 3]

HABARI KUU: UBAGUZI UTAKWISHA LINI?

Ubaguzi Tatizo la Ulimwenguni Pote

JONATHAN, mwenye asili ya Korea, alizaliwa Marekani na alibaguliwa sana alipokuwa mtoto. Baada ya kuwa mtu mzima alitafuta mahali ambapo angeishi bila kubaguliwa kwa sababu ya sura, rangi, au jamii yake. Akawa daktari katika mji ulio kaskazini mwa jimbo la Alaska, Marekani, ambako watu wengi katika eneo hilo walikuwa na umbo kama lake. Alitumaini kwamba kwa kuishi katika eneo hilo lenye baridi kali angeepuka ubaguzi.

Siku moja, alikatishwa tamaa alipokuwa akimhudumia mwanamke fulani mwenye umri wa miaka 25. Mgonjwa huyo aliyekuwa amezimia alipoamka na kumtazama Jonathan usoni, alimtukana, na maneno yake yakaonyesha jinsi alivyowachukia Wakorea. Hali hiyo ilimuumiza Jonathan, kwa sababu licha ya jitihada zake, hakufaulu kuepuka kabisa kubaguliwa.

Kisa cha Jonathan kinaonyesha uhalisi wa mambo. Ubaguzi unapatikana kila mahali duniani. Inaonekana kwamba kila mahali penye watu pana ubaguzi.

Ingawa ubaguzi umeenea, watu wengi wanaupinga. Hilo linashangaza. Inawezekanaje jambo ambalo linachukiwa sana lienee hivyo? Kwa kweli, watu wengi wanaopinga ubaguzi, ni wabaguzi pia kwa njia fulani. Je, wewe pia uko hivyo?

UBAGUZI NI NINI?

Watafiti wana maoni yanayotofautiana kuhusu ubaguzi. Baadhi yao husema ubaguzi ni “mtazamo au hisia zisizofaa kuelekea mtu fulani kwa sababu mtu huyo ni mshiriki wa kikundi fulani.” Wengine husema mtazamo huo unasababishwa na “kutokuwa na habari za kutosha” na hivyo “kuwabagua watu wa kikundi fulani.” Vyovyote vile, mtu anaweza kubaguliwa kwa sababu ya jamii, uzito, jinsia, lugha, dini, au jambo lolote lililo tofauti.

TATIZO LA KIBANAFSI

Iwe tunatambua au la, ni vigumu kwetu kujua ikiwa tuna ubaguzi wa aina fulani katika mioyo yetu. Biblia inafafanua hali hiyo inaposema: “Moyo wa mtu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote.” (Yeremia 17:9, Biblia Habari Njema) Kwa hiyo, tunaweza kujidanganya kwa kufikiri kwamba hatuna ubaguzi hata kidogo. Au huenda tukasema tuna sababu za kuwabagua watu fulani.

[Picha katika ukurasa 4]

Ungefanya nini ikiwa ungekabili hali kama hii?

Ili kugundua kama tuna tatizo la ubaguzi, fikiria hali ifuatayo: Unatembea peke yako barabarani usiku. Vijana wawili ambao hujawahi kuwaona wanakukaribia. Wanaonekana wenye nguvu na mmoja wao ameshika kitu fulani.

Je, unafikiri kwamba watu hao ni hatari? Bila shaka, hilo litategemea mambo ambayo ulikabili wakati uliopita, lakini je, mambo uliyojionea yanapaswa kukusadikisha kwamba vijana hao ni hatari? Mara moja huenda ukajiuliza, vijana hao ni wa kabila au jamii gani? Jibu la swali hilo linaweza kufunua mtazamo wako. Huenda kwa njia fulani jibu lako likafichua jinsi ambavyo umeathiriwa na ubaguzi.

Tukiwa wanyoofu, tutagundua kwamba sote tuna kiwango fulani cha ubaguzi. Hata Biblia inaeleza kuhusu ubaguzi ambao umeenea sana inaposema: “Binadamu huangalia uzuri wa nje.” (1 Samweli 16:7, Biblia Habari Njema) Kwa kuwa sote tunaathiriwa na ubaguzi​—pamoja na matokeo yake mabaya​—je, kuna tumaini lolote kwamba tunaweza kuepuka ubaguzi kabisa? Je, kuna wakati ambapo hakutakuwa tena na ubaguzi?

UBAGUZI—TATIZO LA ULIMWENGUNI POTE

Kanada: “Licha ya kufuata sera zinazokubali watu wa namna zote na kuanzishwa kwa haki za kisheria na sera za kulinda haki za watu wa jamii mbalimbali, ubaguzi wa kijamii unaendelea kuwa tatizo kubwa.”​—Ripoti ya Shirika la Amnesty International kuhusu Kanada, 2012.

Ulaya: “Asilimia 48 ya watu Barani Ulaya wanaamini kwamba hakuna jitihada za kutosha za kuondoa ubaguzi katika nchi zao.”​—Ripoti ya Ulaya Kuhusu Ubaguzi, 2011.

Afrika: “Jeuri na ukandamizaji wa haki za wanawake unazidi kuongezeka katika nchi nyingi.”​—Ripoti ya Shirika la Amnesty International 2012.

Nepal: “Wahindi wanaodharauliwa huteseka kwa sababu ya ubaguzi wa kiuchumi, kijamii, na kitamaduni.”​—Ripoti ya Shirika la Human Rights Watch World, 2012.

Ulaya Mashariki: “Jamii ya Waromani wanaoishi Ulaya mashariki wanaonewa katika nchi za kigeni na kubaguliwa katika nchi zao, hakuna mwanasiasa anayetaka kusuluhisha matatizo yao.”​—Gazeti The Economist, la Septemba 4, 2010.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki