Je, Tunaweza Kukomesha Vita na Ukatili?
Watu hupigana kwa sababu mbalimbali. Baadhi yao hupigana kwa sababu za kisiasa, hali za kiuchumi, au mabadiliko ya kijamii. Wengine hupigana ili wadhibiti ardhi na maliasili zilizopo. Mara nyingi, vita husababishwa na tofauti za muda mrefu za kijamii au za kidini. Watu wanafanya niniili kukomesha mapiganona kuleta amani? Je,jitihada za wanadamuza kukomesha vita zinaweza kufanikiwa?
Drazen_/E+ via Getty Images
MAENDELEO YA KIUCHUMI
Lengo: Kuboresha hali ya maisha ya watu. Hilo linaweza kuondoa au kupunguza tatizo la kutokuwa na usawa wa kiuchumi, jambo linaloweza kuwa chanzo kikuu cha mapigano.
Kwa nini ni vigumu?: Serikali inalazimika kubadili matumizi ya pesa. Inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 2022, dola bilioni 34.1 za Marekani zilitumiwa ili kutafuta na kudumisha amani ulimwenguni pote. Hata hivyo, hicho kilikuwa kiasi kidogo sana cha pesa kinapolinganishwa na kiasi kikubwa kilichotumiwa ili kugharamia shughuli za kijeshi katika mwaka huohuo.
“Tunatumia pesa na mali nyingi sana kuwasaidia walioathiriwa na vita kuliko kuzuia vita na kutafuta amani.”—António Guterres, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Biblia inasema nini?: Serikali na mashirika ya ulimwengu yanaweza kuwasaidia maskini, lakini hayawezi kamwe kuondoa umaskini kikamili.—Kumbukumbu la Torati 15:11; Mathayo 26:11.
MAKUBALIANO YA AMANI
Lengo: Mazungumzo ya amani kuhusu hali iliyopo na kufanya makubaliano yatakayonufaisha pande zote mbili zinazohusika.
Kwa nini ni vigumu?: Wahusika wa upande mmoja au pande zote mbili huenda wakakataa kufanya makubaliano. Vilevile, makubaliano ya amani yaliyofanywa huvunjwa kwa urahisi.
“Makubaliano ya amani hayafanikiwi sikuzote. Makubaliano yaliyofanywa ili kukomesha vita huenda yakalemea upande mmoja na hivyo kuendeleza vita.”—Raymond F. Smith, Mwanadiplomasia wa Marekani.
Biblia inasema nini?: Watu wanapaswa ‘kutafuta amani.’ (Zaburi 34:14) Lakini leo watu wengi ni “wasio washikamanifu, . . . wasiotaka makubaliano yoyote, . . . wasaliti.” (2 Timotheo 3:1-4) Tabia kama hizo huwazuia wanasiasa wenye nia nzuri kusuluhisha mizozo.
KUPUNGUZA SILAHA ZA VITA
Lengo: Kupunguza au kuharibu silaha, hasa za nyuklia, za kemikali, na za kibiolojia.
Kwa nini ni vigumu?: Kwa kawaida, nchi nyingi haziwi tayari kupunguza silaha kwa sababu zinaogopa kupoteza mamlaka na uwezo wake wa kujilinda. Kuharibu silaha za vita hakusuluhishi sababu zinazofanya watu wapigane.
“Mapatano mengi ya kuharibu silaha na ahadi zilizotolewa mwishoni mwa vita baridi hazijatimizwa kutia ndani hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kupunguza hatari, uadui wa kimataifa, na hatimaye kuufanya ulimwengu uwe na uhusiano wa karibu na wenye usalama.”—“Kulinda Wakati Wetu Ujao: Ajenda ya Kupunguza Silaha za Vita.”
Biblia inasema nini?: Watu wanapaswa kutupa silaha na ‘kufua panga zao ziwe majembe ya plau.’ (Isaya 2:4) Hata hivyo, mengi zaidi yanahitajika kwa sababu ukatili huanzia moyoni mwa mtu.—Mathayo 15:19.
MATAIFA KUUNGANA ILI KUDUMISHA AMANI
Lengo: Mataifa kukubaliana kuchukua hatua za pamoja dhidi ya maadui. Inatazamiwa kwamba maadui hawataanzisha vita dhidi ya mataifa hayo kwa sababu hilo linamaanisha kupigana vita dhidi ya majeshi ya mataifa yaliyoungana.
Kwa nini ni vigumu?: Tishio la kulipiziwa kisasi na mataifa mengi haliwahakikishii watu kuwa na amani. Mara nyingi, mataifa hayashikamani na mapatano waliyofanya, wala hayakubaliani kuhusu hatua wanayopaswa kuchukua na wakati wa kuchukua hatua dhidi ya maadui.
“Ingawa mashirika ya Muungano wa Mataifa na Umoja wa Mataifa yamejitahidi sana kusaidia serikali kufanya miungano ya amani. . . miungano hiyo imeshindwa kuzuia kutokea kwa vita.”—“Encyclopedia Britannica.”
Biblia inasema nini?: Hali huwa nzuri zaidi watu wengi wanapofanya kazi pamoja kwa ushirikiano. (Mhubiri 4:12) Hata hivyo, hatuwezi kutegemea mashirika ya kibinadamu ili kupata amani na usalama wa kudumu. “Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa. Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka.”—Zaburi 146:3, 4, Biblia Habari Njema.
Licha ya jitihada zinazofanywa na mataifa mengi ili kuleta amani ulimwenguni, bado dunia inakumbwa na vita.