Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/22 kur. 4-7
  • Kuna Wakati Ujao Gani kwa Vita?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuna Wakati Ujao Gani kwa Vita?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wazo la Kwamba Vita Huleta Hasara
  • Jitihada za Ulimwenguni Pote za Kuleta Amani
  • Hali ya Vita vya Wakati Ujao
  • Tatizo Ni Nini?
  • Umoja wa Mataifa—Njia Bora Zaidi?
    Amkeni!—1992
  • Ni Nani Awezaye Kuleta Amani Yenye Kudumu?
    Amkeni!—1996
  • Mwisho wa Vita Vyote—Je! Unaweza Kufikiwa?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Mipango ya Mwanadamu kwa Ajili ya Usalama wa Kimataifa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/22 kur. 4-7

Kuna Wakati Ujao Gani kwa Vita?

“VITA imekuwa zoea katika muda wa miaka 4000 ya majaribio na ya kupigana tena na tena,” akasema mwanahistoria wa kijeshi John Keegan. Je, zoea hilo litakomeshwa? Idadi ya watu wasiohesabika wameuawa vitani. Nishati nyingi na mali nyingi isivyo kawaida zimeendeleza vita. Kwa milenia nyingi, watu wenye akili wamejikakamua kuvumbua njia mpya na bora za kuua na kuharibu. Je, wanadamu hudhihirisha juhudi ileile katika kuendeleza amani? La hasha! Lakini, wengi kwa hadhari husababu kwamba kuna msingi fulani wa kutazamia mema.

Wazo la Kwamba Vita Huleta Hasara

Tumaini hilo hutegemea itikadi ya kwamba watu waliostaarabika hawaioni vita tena kama zamani. Imeripotiwa kwamba mpiganaji wa kabila la Mongol, Genghis Khan, alisema hivi katika karne ya 13: “Furaha hutokana na kuwashinda maadui wako, kuwatimua mbio, kupora mali zao, kuwakatisha tamaa, kubaka wake na binti zao.”

Hakuna mtu awezaye kuwazia kiongozi wa nchi akisema maneno kama hayo leo! Kitabu A History of Warfare chataarifu: “Leo haiwezekani mahali popote ulimwenguni kupata watu wanaounga mkono kauli ya kwamba vita ni utendaji halali wakiwa na sababu za kutosha na zilizo thabiti.” Vita havionwi tena na wengi kuwa jambo la kawaida, la kiasili, tukufu, au la adili. Mauaji ya vita vya karne ya 20 yamewaacha wanadamu wakiwa na hofu na chuki kuelekea madhara ya vita. Mwandishi mmoja alisababu kwamba chuki hii kuelekea jeuri imefanya nchi nyingi zifutilie mbali adhabu ya kifo na imeondoa chuki kuelekea wale wanaokataa kushiriki katika shughuli za kijeshi.

Chuki kuelekea uchinjaji si sababu pekee ambayo imebadili mitazamo. Pia kuna jambo muhimu la kujilinda. Silaha za kisasa ziwe za kinyuklia au za kawaida zina uwezo mkubwa wa kuharibu hivi kwamba, vita vyovyote baina ya mataifa yenye uwezo leo vyaweza kutokeza hatari ya kuangamizana. Kuanzisha vita vikuu ni kichaa, ni kujiangamiza. Wengi hudokeza kwamba usadikisho huo umezuia vita ya nyuklia kwa zaidi ya miaka 50.

Kuna sababu nyingine inayowafanya watu fulani wawe na maoni tofauti kuhusu wakati ujao. Vita vikuu huonwa kuwa vinaleta hasara si kwa sababu tu ya uharibifu wa mali bali kwa sababu havileti faida yoyote. Hoja ya kiuchumi dhidi ya vita vikuu ni hii: Mataifa tajiri na yenye uwezo ulimwenguni hunufaika sana kutokana na ushirikiano wa kiuchumi. Faida za kimwili zinazofurahiwa na mataifa haya wakati wa amani haziwezi kulinganishwa na faida zozote ziwezazo kuletwa na vita. Hivyo, kuna sababu nzuri kwa mataifa yenye uwezo kudumisha amani na mataifa mengine yenye uwezo. Isitoshe, yanafaidika yanaposhirikiana na mataifa mengine yenye uwezo ili kukomesha mapambano baina ya mataifa yenye uwezo mdogo ambayo yanatisha hali ya kiuchumi.

Jitihada za Ulimwenguni Pote za Kuleta Amani

Tamaa ya kukomesha vita inadhihirishwa kwenye dibaji ya mkataba wa Umoja wa Mataifa. Inasema juu ya azimio la mataifa yanachama “la kuokoa vizazi vijavyo kutokana na baa la vita, ambavyo mara mbili katika wakati wetu [pamoja na vita vya ulimwengu viwili] vimeletea wanadamu huzuni isiyoelezeka.” Azimio hilo la kuokoa vizazi vijavyo kutokana na vita lilionyeshwa na wazo la usalama wa pamoja—wazo la kwamba mataifa yapaswa kuungana dhidi ya taifa lolote linaloonwa kuwa lenye uchokozi. Hivyo, endapo taifa lolote litafikiria kuanza vita, litashambuliwa na jamii ya kimataifa.

Japo wazo hilo ni sahili na la kiakili, kulitekeleza kumekuwa jambo tofauti. Kichapo The Encyclopædia Britannica chataarifu: “Ijapokuwa usalama wa pamoja, kwa njia fulani mbalimbali, ulitimiza fungu muhimu katika Agano la Ushirika wa Mataifa na japo ni sehemu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, umeshindwa kabisa katika visa vyote viwili. Kwa sababu ya kukosekana kwa serikali ya kimataifa yenye uwezo wa kutatua kabisa masuala haya, mataifa yameshindwa kuafikiana juu ya uelewevu wazi wa uchokozi, hayatendi kupatana na kanuni ya kwamba uchokozi kutoka kwa taifa lolote lile unapaswa kuzuiwa bila kujali ni taifa jipi, na, kwa hiyo, hayajafaulu kuanzisha kikosi cha kimataifa cha usalama wa pamoja kilichozingatiwa kwenye Mkataba huo.”

Hata hivyo, wazo la kubuni shirika kuu la kimataifa la kudumisha amani lilikuwa jambo jipya katika shughuli za binadamu. Kwa watu wengi wanaotamani sana amani, askari-jeshi wa kudumisha amani wa UM, akiwa na kofia ya buluu, anaashiria tumaini. Watu hawa wana maoni sawa na mwandishi wa habari aliyeunga mkono “wazo la askari-jeshi wa amani, anayetumwa kwenye eneo lenye vita, si kupigana, bali kudumisha amani, si kupambana na maadui, bali kusaidia rafiki.”

Kwa miongo mingi Vita Baridi vimegawanya UM katika pande mbili zenye uwezo, kila upande ukinuia kuzuia utendaji wowote wa upande mwingine. Japo kumalizika kwa Vita Baridi hakujakomesha mapambano, kutotumainiana, na shaka kati ya mataifa, wengi wanaamini kwamba hali ya kisiasa iliyopo inaandalia UM fursa bora ya kutekeleza wajibu wake.

Mambo mengine ambayo yametokea katika karne ya 20 yanawapa tumaini wale wanaotamani sana amani. Kwa kielelezo, mradi wa upatanishi wa kimataifa ni kusuluhisha mapambano kwa njia ya amani. Msaada wa fadhila husaidia mataifa kupatanisha mataifa mengine na husaidia watu waliosambaratishwa na vita. Kudumisha amani na kutoa msaada wa fadhila zimekuwa sehemu ya sera ya ugenini. Wale wanaoendeleza amani wanaheshimiwa.

Hali ya Vita vya Wakati Ujao

Lakini, ni lazima hali yoyote ya kutazamia mema, isawazishwe na mambo halisi ya kuhofisha. Vita Baridi ilipokoma mnamo 1989, wengi walikuwa na uhakika wa kuwapo kwa mfumo wa ulimwengu wenye amani. Hata hivyo, vita viliendelea. Katika miaka saba iliyofuata, kulikuwa na takriban mapambano makali 101 yaliyoendelea sehemu mbalimbali. Mengi ya mapambano hayo hayakuwa vita kati ya mataifa bali vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mapambano hayo yalikuwa kati ya vikundi vyenye kuzozana vinavyotumia silaha za kawaida. Katika Rwanda, kwa mfano, watu wengi waliuawa kwa upanga.

Mara nyingi, miji na vijiji vimekuwa viwanja vya kisasa vya vita, na hakuna tofauti kubwa kati ya wapiganaji na raia. Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kudumisha Amani, Michael Harbottle, aliandika: “Huenda ilikuwa rahisi kidogo kutambua visababishi vya mapambano hapo kale, ilhali leo visababishi vya mapambano ni tata zaidi na haviwezi kutatuliwa kwa urahisi. Jeuri inayotukia katika mapambano haya ni isiyoaminika na isiyofaa kabisa. Raia wakazi huwa katika hatari ya kupigwa risasi sawa na wapiganaji.” Hakuna tumaini lolote kwamba mapambano haya yanayohusisha silaha za kawaida yatakoma.

Wakati uleule, katika nchi tajiri za ulimwengu, utengenezaji wa silaha za kisasa unaendelea kwa kasi. Sensa—ziwe zimetegwa hewani, angani, baharini, au ardhini—huwezesha jeshi la kisasa kuona upesi zaidi na waziwazi zaidi kuliko wakati mwingineo wowote, hata katika maeneo yasiyo wazi, kama misitu. Mara baada ya sensa kutambua mahali ilipo shabaha, makombora, topido, au mabomu yanayoongozwa na leza huweza kuilipua—mara nyingi pasipo kukosea. Kadiri tekinolojia mpya zinavyoendelea kuboreshwa na kukamilishwa, ndivyo “vita vya masafa marefu” vinavyoelekea kuwa halisi, jeshi laweza kuona kila kitu, kulipua kila kitu, na kuharibu vifaa vingi vya adui.

Tunapozingatia uwezekano wa kuzuka kwa vita wakati ujao, hatupaswi kusahau kuwapo kwa silaha za nyuklia zenye kutisha. Gazeti The Futurist latabiri: “Ueneaji mkubwa wa silaha za atomi huzidisha uwezekano wa kwamba kutakuwapo na vita moja au zaidi vya atomi katika miaka 30 ijayo. Kwa kuongezea, huenda silaha za atomi zikatumiwa na magaidi.”

Tatizo Ni Nini?

Ni jambo gani limevuruga jitihada za kuleta amani ulimwenguni pote? Jambo lililo wazi ni kwamba familia ya kibinadamu imefarakana. Wanadamu wamegawanyika katika mataifa na tamaduni ambazo zinatokeza kutotumainiana, chuki, au hofu kuelekea nyingine. Kuna kanuni, maoni, na miradi inayohitilafiana. Zaidi ya hayo, matumizi ya uwezo wa kijeshi yameonwa kwa milenia nyingi kuwa njia halali ya kutetea masilahi ya kitaifa. Baada ya kukiri hali hii, ripoti moja kutoka taasisi ya Strategic Studies Institute ya U.S. Army War College ilisema: “Kwa wengi, hii ilimaanisha kwamba amani ingeletwa tu na serikali ya ulimwengu.”

Watu fulani wamehisi kwamba huenda Umoja wa Mataifa ukawa ndiyo serikali hiyo. Lakini UM haukukusudiwa kamwe uwe serikali ya ulimwengu yenye uwezo unaozidi ule wa mataifa yanachama. Uwezo wake unaamuliwa na mataifa yanachama. Tuhuma na migogoro inaendelea kati ya mataifa haya, na uwezo ambao UM umepewa una mipaka. Kwa hiyo, badala ya kugeuza mfumo wa kimataifa, UM unashabihi mfumo huo.

Hata hivyo, amani ya ulimwenguni pote itaenea duniani kwa hakika. Makala ifuatayo inaonyesha jinsi jambo hilo litakavyotukia.

[Blabu katika ukurasa wa 5]

“NI LAZIMA WANADAMU WAKOMESHE VITA, LA SIVYO VITA VITAWAANGAMIZA WANADAMU.”—JOHN F. KENNEDY

[Picha katika ukurasa wa 7]

UM haujawa serikali ya ulimwengu

[Hisani]

UN photo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki